Habari

Wanaojistiri kwa Ramadhan, wataendelea hata ikimalizika?

June 14, 2018 – by Manager

Umeandikwa na Haji Nassor, PEMBA

SI haba wazanzibar wenzetu hasa wanawake, wanatambua thamani, heshima na ukubwa wa mwezi mtikufu wa Ramadhani, kwa kule kuuyasitiri maungo yao.

Kwa ndani ya mfungo huu wa Ramadhani, mwenye juba, lemba kubwa, kanzu pana, au vazi la kuziba uso umaarufu ninja, limekuwa livaliwa ili kuustiri mwili.

Kwangu mimi nasema hii ni faraja, na pengine kwa hawa wanaofanya hivyo, ndio wameshaelimika na kutokana kwenye ujinga, kwa huku kuyaficha maungo yao.

Suali ambalo limenileta mbele leo hii, ni kuwauliza hawa wanaostiri miili yao kwa kuvaa mitandio, majuba, vilemba vya heshima yalioambana na madira mapana, kwa lengo ya kuficha viongo wataendelea hata baada ya mwezi huu kumalizika?

Au wanaofanya hivi, aya zao za kujistiri pamoja na hadithi huwepo ndani ya mwezi mtukufu wa ramadhani pekee, na ukimalizika na hayo maelekezo na makatazo yao, ndio nayo yamefutika.

Maana kwa ndani ya mwezi huu mtukufu wa ramadhani, kila mwanamke, imekuwa ni vigumu kuiona ovyo pengine sura yake na hata yale maungo tuliozoea kuyapicga chabo, mwezi wa kula na mchana, sasa je hali hii itaendelea hata baada ya kumalizika Ramadhani.

Mbona kwa sasa kivazi cha baadhi ya wanawake hawa hasa wanaojua nini maana ya Ramadhani, kimekua kikivutia na pangine hata sasa kuwatofautisha kati yale wasiokuwa waumini wa dini ya kiislamu na wengine.

Ukipanda nao gari wanawake hawa kwa sasa, utajiuliza kama kuna Ijtimai pahala, au wanakwenda kufanya intaviuu ofisi ya Mufti, kumbe laa hasaha, ni kuupokea na kuusikindikiza mwezi ulioshuhwa Qur-an.

Inawezekana, vile vijilemba na vijitandio vya kuwarusha moyo wanaume, ambavyo huvaliwa kwa mwezi wa kula na mchana aidha vimeshatiwa moto au wameshapewa watoto wadogo, na pengine sasa wanawake hawa wa kizanzibar wameshamua kuvaa mavazi yanayokwenda na majina yao.

Kwa mfano katika kipindi cha kula mchana, vazi alilokuwa akivaa mtu mwenye jina kama la Jackline, Doyosis halikuwa na tofauti na analovaa mtu mwenye jina la Kul-thumu au Aishaa ambapo haya ni majina ya kiislamu kiitikadi.

Kwangu mimi nasema, inawezekana sasa kuwa wanazuoni wetu na masheikh, wameshafanikiwa alau kwa upande wa wanawake, kwamba wamesharejea kwenye mavazi yao ya asili yaliokuwa yakificha maungo.

Maana, wapo wanaosema hata ukitaka kuacha pombe, sigara na wizi basi mwezi huu mtukufu wa ramadhani ni mwafaka kufanya hivyo, na ndio pengine sasa vazi la wanawake wanalovaa mwezi huu, ndio moja kwa moja hadi maisha yao.

Kwa hali hii, hata wale wanaume wenye kuvaa surauali chini ya makalio, ummarufu mlengezo, bila shaka mjifunze sasa kutoka kwa wanawake, jinsi walivyojistiri ndani ya mawezi huu.

Na ikiwezekana baada ya mwezi huu kumalizika, kusiweko tena surauali mlegezo, wala kwa watu wazima wanawake kuvaa vilemba na mitandio ya watoto wao, ambayo honesha mashina ya maziwa wakitembea barabarani.

Kama hivyo ndivyo, sote tukumbe kuwa, hata baada ya kumalizika kwa mwezi huu mtukufu, bado aya, hadithi na Muumba ndio yule yule, acheni kuvaa vitandio vinayoonesha maumbile yenu.

Lakini hata wakuu wa kaya, bado mnawajibu wa kuhakikisha, suala la vazi la stara kwa wanawake na wanaume, linakuwa endelevu hata baada ya kuhitimishwa kwa kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Viongozi wetu wa dini, lazima muendelee na jukumu lenu la kuwaelezea waumini wenu, hasara za wasiofunika maungo yao, maana kwa kweli ni hatari jinsi maungo yanavyopigwa jua kama vile mwenyewe amerukwa na akili.

Kama hivyo ndivyo lazima kila mmoja, aseme na akili yake akijua kuwa, kama mwezi wa Ramadhani unavyoondoka, hata mimi, wewe, yule na wao wataondoka, je tunajipangaje.

Kila kitu kinawezekana iwapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake, kwa kufuata maelekezo na makatazo wa Muumba na huku akijua kuwa, iko siku ya malipo.

Pembatoday

Share: