Habari

Wanasaisa watakiwa kumaliza mgogoro wa Zanzibar

Na Salma Said,

Taasisi zisizokuwa za kiserikali nne zimekutana na kutoa tamko lao wakiwataka viongozi wa siasa kumaliza mkwamo wa kisiasa uliopo ambao unazidi kuwaathiri wananchi kisaikilojia.

Taasisi zilizotoa tamkono pamoja na Zanzibar Interfaith Center, Mtandao wa Kidunia wa Dini kwa Watoto (GNRC), Mwamvuli wa Asasi za Kiraia Zanzibar (ANGOZA), na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Bwawani Mjini Zanzibar, Mratibu wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Zanzibar Mzuri Issa Ali alisema wananchi wa Zanzibar wanakabiliwa na matatizo makubwa hivi sasa kiuchumi na kisaikolojia hivyo kuna kila sababu ya kutatuliwa matatizo yaliyopo.

“Hali ya Zanzibar sio nzuri na inahitaji kushughulikiwa haraka kwani inawaumiza wananchi kisaikolojia lakini pia mfumko wa bei umepanda kupita kiasi hali ya uchumi ni mbaya sana wananchi walinunua vyakula wakaweka ndani kama akiba na kwa hali hii ilivyo hatujui hali itakuwaje” alisema Mzuri.

Katika tamko wa Asasi hizo pia zinawashauri viongozi wa siasa nchini kuwa makini zaidi katika kumaliza mgogoro wa kisiasa unaendelea Zanzibar na kutatua mgogoro huo kwa njia ya amani na kwa haraka zaidi.

Mkwamo wa kisiasa Zanzibar umeanza Octoba 28 baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha kutoka tangazo la kufuta matokeo yote ya uchaguzi ambapo tayari majimbo 31 yalishatangazwa na tume hiyo.

Katika tamko la wana asasi hizo amesema wao kama Asasi za kiraia wameona jinsi uchaguzi ulivyofanyika kwa uhuru na amani na tum ehiyo kuanza kutoa matokeo kama kawaida ya sheria za uchaguzi zinavyoeleza lakini walishangazwa kusikia tangazo la kusitishwa kwa kusikia matokeo hayo yamefutwa.

“Kufuatia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi nchi imeachwa katika ombwe kubwa la kisiasa na hali ya taharuki na wasiwasi mkubwa hii ni kutokana na matakwa ya utawala bora yanayohimizwa uwazi ushirikishwaji wananchi katika mambo yanayohusu nchi yao” alisema Mzuri.

Mzuri alisema zinawashauri wanasiasa wakuu waweke utaratibu wa kuwapa wananchi mrejesho wa vikao vyao vya ndani ili kuondosha hali ya wasiwasi iliyotanda kuhusiana na hatma ya Zanzibar kisiasa.

“Tunawakumbusha viongozi wa siasa kuwa wananchi wanaathirika sana na hali hii ya sintafaham kijamii na kiuchumi pia kuiacha hali hii iendelee kwa muda mrefu inaweza pia kuhatarisha amani ya nchi na hivyo wananchi kuathirika zaidi” alisema Mzuri.

Aidha Asasi hizo zimewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa ustahamilivu wao muda wote huu na kuwaomba waendelee na moyo huo huo wa kusubiri na kuachana na ushawishi wowote ambao utaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Akizungumza katika mkutano huo Mwakilishi wa Mtandao wa Kidunia wa Dini kwa Watoto (GNRC), Lulu Abdallah Omar amesema wanafunzi wengi wameathirika kisaikolojia na baadhi yao wameshindwa kufanya mitihani yao kutokana na wazazi wao kuwakataza wasitokea kwenda kufanya mitihani.

“Wiki moja baada ya uchaguzi ndio kulikuwa na mitihani ya taifa kwa hivyo kuna baadhi ya wanafunzi walishindwa kufanya mitihani yao kwa sababu baadhi ya wazazi waliwazuwia watoto wao wasitoke nje wakiogopa baada ya kusikia nje hakutokeki wazee wakaingia na khofu” alisema Lulu.

Mratibu wa Mafunzo kutoka Zanzibar Interfaith Center, Lusungu Mbilinyi aliwaomba wana habari kuacha kushabikia taarifa ambazo zitaweza kusababisha maafa kwani baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika taarifa ambazo hazifuati maadili na zinalenga kuchafua hali ya amani nchini.

“Waandishi wa habari ni watu muhimu wa kusaidia kutuliza hali mnaposhabikia na kuandika taarifa zinazotolewa na viongozi nyinyi ndio mnaohatarisha amani ya nchi hii kwa hivyo ni jukumu lenu kuchuja na kupima ipi taarifa ya kuiandika na ipi taarifa ya kuiwacha kwa sababu bila ya nyinyi matamko yanayotolewa ni bure tu kama hayajatangazwa” alisema Mbilinyi.

Mwalimu Hassan Ali kutoka Mwamvuli wa Asasi za Kiraia Zanzibar (ANGOZA), amesema hali iliyopo katika visiwa vya Unguja na Pemba hivi sasa inamsikitisha na kumhuzunisha kila mtu na iwapo itaendelea inaweza kuleta athari kubwa kwa wananchi hasa kiuchumi kutokana na kuwa siku chache baada ya kutokea hali hii wananchi wamekuwa wakikabiliwa na maisha magumu.

“Tunawaomba viongozi wetu walichukulie jambo hili kwa urahisi athari zake ni kubwa wananchi wanahitaji kupata amani na wanahitaji kumalizwa jambo hili kwa njia za kidiplomasia bila ya athari na machafuko, hali ya uchumi imekuwa mbaya na athari hizi zinawakumba zaidi wananchi masikini” alisema Mwalimu Hassan.

Hii ni mara ya pili kwa jumuiya zisizo za kiserikali kutoa tamko lao kufuatia kufutwa kwa matokea ya uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba 25 mwaka huu na kufutwa na Mwneyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha Octoba 28 uamuzi ambao umelalamikiwa na wadau mbali mbali wakiwemo wanasheria maarufu hapa Zanzibar.

Awali Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kilitoa kauli yake ya kumtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi afikirie kwa kina uamuzi wake kwa kuwa unakwenda kinyume na sharia na katiba za nchi kwa kuwa Mwneyekiti huyo hana mamlaka kisheria kufuta matokeo ya uchaguzi ambayo wananchi wametumia haki yao kidemokrasia kuchagua kiongozi wanayemtaka kuwaongoza.

Rais wa ZLS Awadh Ali Said alisema kilichofanywa na Mwenyekiti wa ZEC ni uvunjifu wa sharia na katiba na kukiuka jukumu alilopewa kama Mwneyekiti na kuingilia jambo ambalo hana mamlaka nalo, Naye kwa upande wake Omar Ali Said alisema uchaguzi kutokan an akuwa Jecha hana mamlaka bado matokeo ya uchaguzi yanaweza kuendelea kutangazwa na kumtaja aliyeshinda ili hatua ya pili ya kumuapisha iendelee.

Watu wengine ambao wamechangia kwa nyakati tofauti kupitia vyombo vya habari ni Mwanasheria Fatma Amani Karume na aliekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud Othman ambao wanasema kilichofanyika ni kuvunjwa kwa katiba jambo ambalo ni baya kabisa katika nchi ambayo inajisifu inafuata demokrasia na utawala bora.

Hadi sasa ni Mwanasheria pekee, Hamid Bwezeleni ndiye aliyeonekana kuunga mkono upande wa serikali kwamba kilichofanyika ni sahihi na tume imetenda haki kufuta matokeo kwa kuwa uchaguzi ulikuwa na kasoro mbali mbali.

Tagsslider
Share: