Habari

Wanasiasa wakongwe: Acheni kupotosha chimbuko la Muungano‏

Nasaha za Mihangwa
Joseph Mihangwa
Toleo la 239
16 May 2012

MENGI yamesemwa na kuandikwa juu ya chimbuko na kufikiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 1964; lakini yote yenye kukinzana.

Tumefika mahali tukakata tamaa kuendelea kudadisi ukweli na kuacha kila mmoja wetu ajikite na kile anachoambiwa na kuamini namna Muungano huu ulivyofikiwa. Wapo wanaodai kwamba Muungano huu ni matokeo na udugu wa miongo na hata karne nyingi wa wananchi wa nchi hizi mbili; na kwamba Rais wa awamu ya kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipendekeza kwa Rais wa awamu kama hiyo wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, naye akakubali sawia, kuunganisha nchi zao, akitaka Muungano imara wenye Serikali moja, lakini Nyerere akashikilia kuundwa kwa Muungano wenye Serikali mbili – Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.

Wapo pia wanaodai kwamba, Muungano huo ni shinikizo la mataifa makubwa ya Magharibi, enzi hizo za vita baridi, yaliyotaka, Zanzibar imezwe kwenye tumbo kubwa la Shirikisho la Afrika Mashariki kuepusha isikamatwe na kambi ya Ukomunisti wa nchi za Mashariki. Na pale Shirikisho hilo liliposhindwa kuanza, Mwalimu Nyerere, kwa msaada wa Marekani na Uingereza, aligeuka hima kuitia Zanzibar ndani ya tumbo la Tanganyika kwa njia ya Muungano tata.

Lakini imeelezwa pia kwamba, kwa muda mrefu, na hata kabla ya uhuru, Nyerere alikuwa na wasiwasi juu ya Visiwa vya Unguja na Pemba kuwa karibu mno na Tanganyika. Aliwahi kunukuliwa akisema:
“Kama ningekuwa na uwezo wa kukivuta kisiwa kile mpaka katikati ya Bahari ya Hindi, ningefanya hivyo….. Nadhani moja ya matatizo makubwa ya Tanganyika katika siku za mbele litakuwa Zanzibar. Kwa kweli sitanii; ni rahisi sana kuingiliwa na nchi za nje. Nina wasiwasi [Zanzibar] itatuletea matatizo makubwa”.

Je, hii inaweza kuwa moja ya sababu kwa Nyerere kutaka kuitia Zanzibar ndani ya tumbo la Tanganyika, baada ya mchakato wa Shirikisho la Afrika Mashariki kushindwa?. Kuna ukweli gani baadaye, kwa matamshi ya Waziri wa Ulinzi na Mambo ya kigeni wa Tanganyika na kipenzi cha Nyerere cha wakati huo, Oscar Kambona, kuhusu sababu za Tanganyika na Zanzibar kuungana, aliposema: “Wasiwasi wetu wa kwanza ulikuwa kuongezeka kwa Ukomunisti Visiwani (ukisimamiwa na kuunganishwa na Abdulrahman Mohamed Babu, kiongozi wa zamani wa Umma Party na baadhi ya makada wa ASP); na pili, hofu ya mataifa makubwa kujitumbukiza Zanzibar enzi hizo za vita baridi, kati ya nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani na Uingereza kwa upande mmoja, na Urusi na China kwa upande wa pili”?

Kuthibitisha hayo, Kambona alibainisha kuwa, mvutano wa mataifa makubwa tayari ulikuwa umeikumba Congo (sasa DRC) hadi kusababisha kuuawa kwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Congo, Patrice Lumumba. Na tayari, Yule Balozi jasusi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) aliyesimamia machafuko nchini Congo, Frank Carlucci, alikuwa amehamishiwa Zanzibar kuongoza machafuko kama hayo, kwa kile kilichoitwa mapambano dhidi ya Ukomunisti Visiwani.

Kwa mantiki hii, wapo wanaodai kuwa tatizo lilikuwa ni jinsi ya kuitenga Zanzibar na nchi za Kikomunisti, na hapo hapo Zanzibar isitumike na nchi za Magharibi kwa faida za nchi hizo.
Kwa hili, Nyerere alinukuliwa wakati mmoja akisema: “China Kisiwani, na Marekani wanasema ninapambana na Wakomunisti; tayari tuna Vietnam katika Afrika, na mimi sitakubali kamwe kuwa na hali hiyo”, akimaanisha kuwa hakutaka kuona Zanzibar ikigeuzwa kitovu cha migogoro Afrika Mashariki.

Inadaiwa pia kuwa, Karume alitia sahihi Mkataba wa Muungano bila kuelewa aina na mfumo wa Muungano aliokuwa akiingia. Na baada ya kubaini kwamba Muungano alioingia si ule aliokuwa akifikiria, aligeuka jeuri, kila mara akitishia kuuvunja akiufananisha na koti kwamba “ukiona linakubana au kukutia jasho, unalivua kwa hiari yako”.

Kuna ukweli gani kwa hili? Kati ya dhana hizi mbili, ya vita baridi na ya undugu wa zamani, ipi iliyozaa Muungano? Wanasiasa wote wakongwe ni wa dhana ile ya kwanza; lakini wasomi na wanazuoni walio wengi ni wa dhana ya pili. Kundi lipi lenye ushahidi usiohojika, kuweza kuthibitisha dhana yake?

Kwa hiyo, tunapoelekea kwenye mchakato wa kupata Katiba mpya nchini, ambapo suala la Muungano na kero zinazoambatana nao zinatikisa mustakabali wa Taifa, ni vyema tukadadisi na kupata ukweli wa jambo hili, utakaosaidia kupata Katiba makini isiyokuwa na ubabaishaji juu ya Muungano. Tuachane na wanasiasa maslahi, wanaotaka tuamini kwamba Muungano ni “fumbo la imani” ili wao waendelee kunufaika kwa “tufani” wanayozua kila mara, na kujifanya wao “masiya” wa kero za Muungano wenye kuabudiwa. Fuatana nami katika mfululizo wa makala haya kupata majibu ya maswali haya.

Muungano Shinikizo la mataifa makubwa?
Tangu mwanzo, katu Nyerere hakuwa na wazo la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Yeye pamoja na Marais wenzake wa Kenya na Uganda, walipigania Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC) kwa ridhaa kubwa ya nchi za Magharibi. Hili linathibitishwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe kwenye taarifa yake kwa Mkutano wa nchi huru za Afrika, mjini Addis Ababa, mwaka 1960, aliposema: “Wengi wetu tunakubali bila ubishi kwamba Shirikisho la nchi za Afrika Mashariki litakuwa jambo jema. Tunasema kwa uhakika kwamba, mipaka inayozigawa nchi zetu hatukuiweka sisi, bali iliwekwa na mabeberu; na hivyo tusiruhusu itumike dhidi ya umoja wetu….. Lazima tuwatake wakoloni si kutoa uhuru tu wa Tanganyika, kisha Kenya, na Uganda na hatimaye Zanzibar, bali tudai uhuru wa Afrika Mashariki kama jamii moja ya kisiasa”.
Kwa mujibu wa Nyerere, muungano wa aina ya shirikisho la kisiasa kwa nchi zote tatu za Afrika Mashariki kuunda jamii moja ya kisiasa (single political unit), ulikuwa bora zaidi kuliko muungano mwingine wa aina yoyote.

Miaka mitatu baadaye, Juni 5, 1963, viongozi wa nchi hizo tatu walikutana mjini Nairobi, kuendeleza mchakato, kuona Shirikisho la Afrika Mashariki linaundwa walitoa tamko lenye nguvu juu ya kuundwa kwa Shirikisho hilo wakisema: “Sisi Viongozi wa watu wa nchi zetu, tunaaazimia kuunda Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki. Mkutano wetu wa leo unaongozwa na dhamira ya Umoja wa Afrika, na si ubinafsi na maslahi ya kikanda… Hii ni siku yetu ya vitendo kwa kuongozwa na maadili, tukiamini katika umoja na uhuru ambao tumesumbukia na kujitoa mhanga kwa mengi” (soma: A Declaration of Federation by Governments of East Africa, Kumb. Na. 13/931/63 DDT/1/1, na kuchapishwa kuwa kijitabu na Wizara ya Habari, Tanganyika, 1964).

Zanzibar, ambayo ilikuwa bado kwenye mchakato wa kupata uhuru miezi minne baadaye, Desemba 10, 1963, haikuwamo katika tamko hili, lakini ilipewa nafasi ya kujiunga itakapopata uhuru, na hivyo Azimio hilo lilisema: “Ingawa Zanzibar haikuwakilishwa katika kikao hiki, tunaweka wazi kuwa, nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu katika Mkutano wetu wa kuunda Shirikisho. Na mara Zanzibar itakapofanya chaguzi zake mwezi ujao (Julai 1963), Serikali yake itaalikwa kushiriki kwenye Tume inayoshughulikia uundaji wa Shirikisho, na kwenye taasisi yoyote itakayoundwa katika mipango yetu ya kuunda Shirikisho”.

Mpaka hapo, Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa championi na mwanaharakati kiongozi wa kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, hakuwa na ndoto wala kuonyesha dhamira ya kuunda Muungano wa nchi yake na Zanzibar, mbali na azima pekee kuona Zanzibar inajiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki.
Aidha, wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, 1964, viongozi wa Tanganyika, Kenya na Uganda walikuwa mjini Nairobi wakihudhuria Mkutano wa Shirikisho la Afrika Mashariki tarajiwa, na Zanzibar ilikuwa na mwakilishi.

Ilifika mahali kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar, Marais Jomo Kenyatta wa Kenya, na Milton Obote wa Uganda, wakajitoa kwenye mchakato wa Shirikisho, huku Kenyatta akidai kwamba hakuwa tayari kupiga magoti kwa Nyerere. Kwa jinsi hii, mchakato wa Shirikisho la Afrika Mashariki ukafa; Nyerere akaachwa njia panda, azima yake ya kuona Shirikisho la Afrika Mashariki likiundwa ikayoyoma.
Hapa tutue kidogo na tujiulize: Je, kama Shirikisho la Afrika Mashariki lingefanikiwa, Muungano wa Tanzania, ambao wanasiasa wengi wanatuambia ni wazo la zama kabla na baada ya uhuru, ungetoka wapi? Na hili wazo jipya (baada ya juhudi za kuunda Shirikisho kushindwa) la Muungano wa nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar, lilitoka wapi, na lilianzaje?

Nyerere abuni Muungano mpya
Mapema Februari 1964, huku akiwa amekata tamaa juu ya uwezekano wa kuundwa Shirikisho la Afrika Mashariki, Mwalimu Nyerere alimwita Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Roland Brown, akamwagiza amfanyie “kazi ya siri bila mtu mwingine yoyote kujua”. Kazi hiyo ilikuwa ni kuandaa Mkataba (Hati ya) wa Muungano wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Hatimaye, asubuhi ya Aprili 22, 1964, Mwalimu alitua Zanzibar akiwa na Hati hiyo mkononi iliyoandaliwa kwa lugha ya Kiingereza, kisha akamwomba Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aisome na kutafakari, na (pengine) akiridhika, aitie sahihi.
Karume aliiangalia Hati hiyo; na bila kupoteza muda alichukua kalamu; na wawili hao wakatia sahihi zao; wakishuhudiwa na Oscar Kambona (Tanganyika) na Abdullah Kassim Hanga (Zanzibar) na wengine waliokuwapo. Mwalimu alirejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ukawa umezaliwa.

Siku mbili kabla ya kutiwa sahihi Mkataba wa Muungano, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Wolfango Dourado, alipewa “likizo” ya siku saba ya lazima, na badala yake aliitwa Mwanasheria kutoka Uganda, Dan Wadada Nabudere, kumshauri Karume juu ya pendekezo la Muungano.
Haijafahamika bado ni kwa nini Karume alifanya hivyo, na matokeo yake akatia sahihi Hati ambayo aliilalamikia baadaye, kwamba amechengwa juu ya Muundo wa Muungano.

Hati hiyo waliyotia sahihi Marais hao wawili ilikuja kujulikana kama “Hati (Mkataba) ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”. Siku tatu baadaye, Aprili 25, Mabunge ya nchi hizo mbili yaliridhia makubaliano hayo na kuwa Sheria ya Muungano.

Aprili 26, 1964 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitangazwa rasmi, umma ukazizima kwa furaha iliyochanganyika na hofu na mashaka, huku wengi wasiweze kuamini kilichotokea; na wengine wakiuliza: ni lini mtoto huyo aliyezaliwa (Muungano) alitungiwa mimba?.

Mazingira na mikakati iliyowezesha kuundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilizua maswali lukuki, mengi hayajapata jibu hadi sasa, na mengine yanaendelea kuwa kiota cha migogoro ya Muungano hadi leo. Siku za baadaye, Nyerere alinukuliwa akisema kwamba, alitoa pendekezo la Muungano kwa Karume (kimzaha mzaha) wakati Karume alipomtembelea Mwalimu kuzungumzia suala la “Field Marshal” John Okello, naye Karume alikubaliana na wazo la Mwalimu papo kwa papo, na akapendekeza sawia Mwalimu awe Rais wa Muungano huo.

Wengi wanakubali kwamba, kulikuwa na usiri mkubwa kati ya Nyerere na Karume juu ya suala la Muungano. Kama kuna watu walioshirikishwa mwanzoni, basi watakuwa ni Rashidi Kawawa na Oscar Kambona kwa upande wa Tanganyika; Abdallah Kassim Hanga na Salim Rashid, kwa upande wa Zanzibar.

Je, Muungano huo ni matokeo ya juhudi za hiari za waasisi wake kama baadhi ya watu wanavyodai, au ni matokeo ya shinikizo kutoka nje?.
……….. Itaendelea toleo lijalo.

Share: