Habari

wanaume Pemba kuwasaidia wanawake kugombea uongozi

MAKALA: wanaume Pemba kuwasaidia wanawake kugombea uongozi

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA

“TUTAFANYA kila njia kuhakikisha tunawashawishi wanawake kuingia majimboni, kugombea uongozi”, hizo ni kauli zilizowatoka wanaume 10 mara baada ya kupatiwa mafunzo ya umuhimu wa uongozi kwa mwanamke.

Ni mafunzo yaliyoamsha hisia za akina baba hao mpaka kufikia kuanzishwa Tume ya Wanaume Mawakala wa Mabadiliko ambayo itaingia ndani ya jamii kutoa elimu itakayowasaidia kuwatoa kwenye dhana mbaya ya kuwa mwanamke hawezi kuongoza.

Katika kutekeleza wajibu huo, wanaume hao wanasema watahakikisha wanaibua wanawake wenye vipaji vya kugombea na kuwatoa hofu ya kusimama na kutetea haki zao.

Wakati wananchi wa Zanzibar wanaadhimisha siku ya wanawake dunia kote kila ifikipo Machi 8 ya kila mwaka, tayari wanaume kisiwani Pemba wamesimama kidete kuhakikisha haki zote za wanawake zinalindwa na kutekelezwa ipasavyo.

Kwa nini wasimae kidete kuhakikisha wanawake wanapatiwa haki zao? Mohamed Hassan Ali ambae ni Mwenyekiti kutoka Asasi za kiraia Pemba akiwa miongoni mwa wanaume hao 10 anaeleza……

“Ni kwa sababu watahakikisha kero za jamii zinatatuka, ili kuleta mabadiliko na maendeleo endelevu katika nchi”

Anaeleza kuwa, suala la elimu ni muhimu kwa jamii, hivyo watachukua juhudi kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa uongozi kwa wanawake.

Anasema ili ifikapo mwaka 2020 wanawak na hasa wenye uwezo wa kuingia majimboni, wahamasike kugombea nafasi za uongozi ikiwa kuanzia udiwani hadi ubunge.

“Tunatarajia mabadiliko makubwa, kwani tunakwenda kuondoa ile dhana potofu ya kuwa, mwanamke hafai kuwa kiongozi, hii itasaidia sana”, anafahamisha.

Anaeleza kuwa, ni vyema kwa vyama vya siasa kuweka sera maalumu itakayowawezesha wanawake kujiamini na kuwa na uthubutu wa kuchukua fomu na kugombea.

Amour Rashid Ali kutoka Jumuia ya Maendeleo ya Vijana Pemba, anaeleza kuwa, watawajengea uthubutu wanawake waweze kusimama imara na kutoa maamuzi yaliyo sahihi.

“Igawa kuna mila na desturi za jamii zinawakwaza akina mama, lakini tutashirikiana katika kumjengea uwezo wa kujiamini, ili ahamasike kuingia kwenye uongozi”, alisema.

Siku ya wanawake inalenga kuondosha ubaguzi, kutokomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi yao pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa huduma za kimaendeleo.

Timu hiyo ya wanaume wa 10 wa kazi, inakusudia kuondosha aina zote za ubaguzi na dhana potofu dhidi ya wanawake hasa katika suala la uongozi na kuhakikisha wanagombea nafasi za uongozi, ambazo ni haki yao ya msingi kisheria.

“Tutawahamasisha wanawake kugombea nafasi hizi za uongozi, tutahakikisha hawadhalilishwi na hawanyanyaswi kwa njia yoyote ile, kwani hiyo ni haki yao kisheria”, anasema Saleh Nassor Juma Katibu wa CUF Wilaya ya Chake Chake.

Tukiwa katika wiki hii ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani kote, hapa utagundua kuwa, mwanamke anayo thamani kubwa ndani ya jamii, maana kwenye dini mfano ya kiislamu hakubaguliwa juu ya dhana ya uongozi.

Achia mbali kuwa kiongozi wan chi, hapo sasa lakini kwa nafasi kama za ubunge, uwakilishi na udiwani mwanamke anayo nafasi sawa kama alivyo mwanamme, cha msingi na kwa wote wasitoke nje ya sheria za dini.

Suleiman Massoud Said kutoka Kituo cha Walimu wa Skuli za Maandalizi Pemba (MECP-Z) anasema, ataitumia elimu hiyo aliyoipata katika mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) ofisi ya Zanzibar, kwa kuwashajihisha wanawake waingie kwenye uongozi.

“Katika kituo chetu tunapotoa mafunzo tuna kiwango kikubwa cha wanawake, hivyo nitatumia nafasi hii kumuamsha mwanamke, ili apate haki yake ya msingi ya kugombea”, anafafanua.

Omar Mjaka Ali ambae ni mbunge mstaafu CCM, naeleza kuwa, anazo njia mbali mbali za kuwahamasisha wanawake, kugombea ikiwa ni pamoja na mikutano ya ana kwa ana juu ya umuhimu wa mwanamke kushiriki katika nafasi ya uongozi tena bila ya kudhalilishwa.

“Ni muhimu sana kwa mwanamke kugombea nafasi za uongozi, hivyo tutawawezesha, ili wakubali kwa maendeleo endelevu”, anaeleza.

Anasema kuwa, atatumia waandishi na vyombo vya habari kuelimisha, kwani wao ni kioo cha jamii na wenye kufikisha ujumbe kwa haraka na kuwafikia jamii nzima.

Wakati haya yakifanyika, kisiwa cha Pemba kwa mwaka huu, kimepata neema kubwa ya kuwa na mgeni mashahuri Mke wa rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Ishara hii, ni tosha kwamba wanaume au wanawake wanaowadharau wenzao, sio pahala pake, maana kila mmoja ana nafasi sawa na mwenzake kwenye kusaka haki.

Khalfan Amour Mohamed kutoka Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu wa Akili Pemba (ZAPDD) anasema, katika kuhakikisha wanawashajiisha wanawake kugombea nafasi za uongozi watatoa taaluma kwa viongozi wa Jumuiy hiyo, ili kuielimisha jamii kupata uelewa.

“Kwa kweli elimu hii tuliyopewa na wenzetu wa TAMWA imetusaidia sana, kwani tumeelewa wajibu wa mwanamke kisheria”, anasifu.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kusini Pemba Hafidh Abdalla Said anasema, chama hicho kitasaidia akina mama wanashiriki katika nafasi za uongozi nao waonekane wanaweza.

Anaeleza kuwa, kuna baadhi ya wanawake wana vipaji ingawa wanakosa fursa hizo na kusema kuwa watasimamia kuhakikisha wanagombea kwa wingi ifikapo 2020.

“Katika katiba yetu tumeweka asilimia 80 ya wanawake kushiriki katika shughuli za kijamii, hivyo tutajitahidi kuwahamasisha pia wagombee”, anafahamisha.

Katibu wa Jumuiya ya Maimamu Pemba Yussuf Abdalla Ramadhan anasema, watapita kwenye madrasa zote za wanawake Pemba kuelimisha juu ya umuhimu wa kuingia katika nafasi za uongozi kwa mwanamke.

“Tutahakikisha kila msikiti unaitisha mihadhara kuelimisha hili, kwani ni jambo zuri na lenye manufaa kwetu, hata madaktari wa kuzalisha tutapata wanawake endapo atakuwepo kiongozi mwanamke anaetetea”, anasema Katibu huyo.

Anafahamisha kuwa, kwa mujibu wa dini ya kiislamu mwanamke ana nafasi kubwa katika jamii, hivyo ushirikiano wa pamoja unahitajika kuijengea jamii uelewa juu ya dhana nzima ya uongozi kwa mwanamke, ili wahamasike kuingia katika uongozi.

Isack Maganyo Nzilamoshi ambae ni kiongozi wa Kanisa la RGC Makangale Wilaya ya Micheweni aliihakikishia TAMWA kushirikiana pamoja katika kuelimisha waumini wao na kuwashajihisha wanawake kugombea nafasi za uongozi.

“Nitaelimisha viongozi wenzangu, pia tutatumia fursa hii kuelimisha waumini wetu, ili na wao waelewe na wapate hamasa ya kugombea”, anaeleza.

Wakati dunia inaadhimisha siku ya Wanawake, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania-Zanzibar (TAMWA) kimeanza kuunda timu ya Wanaume Mawakala wa Mabadiliko kisiwani Pemba, kwa ajili ya kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa nafasi ya uongozi kwa wanawake.

Asha Mussa Omar ambae ni Mratibu TAMWA Pemba anasema, Timu hiyo imeundwa kwa kuwashirikisha viongozi kutoka Jumuia mbali mbali na Asasi za kiraia, kwenda kuihamasisha jamii, ili wanawake waitumie fursa ya kuingia majimboni kugombea nafasi za uongozi.

Mratibu anaeleza, viongozi wanawake ni muhimu na wanamchango mkubwa ndani ya jamii, kwani kuna mambo yanawalenga wao moja kwa moja ambayo hushindwa kuyatetea.

“Hivyo timu hiyo itaingia ndani ya jamii kuielimisha na kuishawishi, itaondoa yale mawazo waliyonayo wanajamii na kuleta mabadiliko kwa maendeleo endelevu”, anafahamisha.

Anasema, kuadhimishwa siku ya wanawake duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo.

“Pamoja na kuelezea jitihada mbali mbali zilizofanywa na Serikali na wadau mbali mbali katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao, familia, jamii na Taifa kwa ujumla”, anafafanua.

Siti Habib Ali ambae ni Afisa Mipango kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa waandishi wa habari, kuhusu Usawa wa Kijinsia katika masuala ya Uongozi anasema, nchi yeyote inayofuata mfumo wa demokrasia na utawala bora, suala la ushiriki wa wanawake na wanaume katika nyanja za kisiasa ni muhimu.

“Mwaka 1995 idadi ya ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi ilikuwa ndogo, mwaka 2010 ilikuwa ni asilimia 36, lakini mwaka 2015 idadi imeongezeka zaidi kwani wanawake 33 wameingia kwenye uongozi, hivyo tumefikia hatua nzuri sana, lakini waandishi muzidishe bidii kuelimisha, ili wajitokeze kwa wingi”, anafafanua.

Kwa mujibu wa mtandao wa ‘Channel five’ umeeleza kuwa, chimbuko la kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga mazingira duni ya kazi.

Waandamaji hao, walilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira, ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa ukilinganisha na wanaume.

Kwa kuzingatia hali hiyo, Umoja wa Mataifa baada kuanzishwa mwaka 1945 uliridhia kuwa, tarehe 8 Machi ya kila mwaka iwe ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani kote.

Uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuanzisha Siku ya Wanawake Duniani ulitokana na ukweli kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo maalumu na wa kipekee.

Lengo kuu la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kutoa fursa kwa jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa, kikanda na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na uwezeshaji wanawake.

Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa haki za wanawake kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa zinapatikana na zinalindwa.

MWISHO.

PembaToday

Share: