Habari

Wanne wafa kwa mvua Zanzibar, nyumba zaharibiwa

By Haji Mtumwa – Mwananchi
Sunday, May 27, 2018

Mvua zinazoendelea kunyesha Zanzibar, zimesababisha athari mbalimbali ikiwamo vifo vya watoto wanne huku maelfu ya wananchi nyumba zao zikibomoka na kujaa maji.

Taarifa hiyo iliyotolewa juzi na kamati ya kukabiliana na maafa Zanzibar imetoa tahadhari kwa wananchi, hasa wanaoishi mabondeni.

Akizungumzia athari hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame alisema mvua hizo zimesababisha vifo vya watoto wanne, nyumba kujaa maji, baadhi kubomoka kuta na miundombinu kuharibika.

Alisema kamati za maafa za wilaya na shehia zimebaini kuwa nyumba zilizoathirika zaidi ni zile zilizojengwa mabondeni. Hata hivyo, haikuelezwa kuhusu vifo vya watoto wanne waliyotajwa ni kutoka maeneo gani ya Unguja na Pemba.

Makame alisema wamebaini nyumba 2,619 zimeharibiwa kutokana na mvua na upepo mkali na kati ya nyumba hizo, 2,575 zipo Unguja na 44 Pemba. Alisema katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja kuna nyumba 2,097 zilizoathiriwa.

Alifafanua kuwa Wilaya ya Mjini zipo nyumba 654, Magharibi ‘A’ 281 na Wilaya ya Magharibi ‘B’ nyumba 1,162.

Alisema Mkoa wa Kaskazini Unguja, nyumba 62 zimeathirika kati ya hizo nyumba 20 zipo Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na 42 zipo Wilaya ya Kaskazini ‘B’.

Kwa upande wa Kisiwa cha Pemba, alisema nyumba 23 zimeathirika katika Mkoa wa Kusini; 15 zipo Wilaya ya Mkoani na nyumba nane Chake Chake.

“Kaskazini Pemba, nyumba 21 zimeathiriwa kati ya hizo nyumba 11 zipo Wilaya ya Wete na nyumba tisa Wilaya ya Micheweni,” alisema Makame.

Alifafanua kuwa kati ya nyumba zote zilizoathiriwa na mvua Unguja na Pemba, nyumba 1,021 wakazi wake wamehama kutokana na kujaa maji huku nyumba 460 zikiingia maji na nyingine 1,138 zikiwa zimeangukiwa na miti.

Makame alitaja maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hizo kuwa ni Shehia ya Mtoni Kidatu, Mwera, Kibweni, Sebleni, Sablani Kwawazee, Mtumwajeni, Tomondo, Ziwa maboga, Mwanakwerekwe, Fuoni Jangamizini na Chaani Masingini.

Maeneo mengine ni Chaani Kubwa, Kibeni, Matetema, Kazole, Shehia za Michamvu, Bwejuu, Chwaka, Ukongoroni na Mchangani.

Kwa upande wa Pemba ni Ngwachani, Gando, Wete Kipangani, Ole Uwandani, Ziwani, Shumba Viamboni na Tondooni, Tasini Pemba.

Share: