Habari

WAPINZANI WAFUNIKA

Na Thobias Mwanakatwe
Kakobe aibuka na kumtahadharisha Rais Kikwete Lipumba: Vijana anzeni kufanya mazoezi ya viungo Mbowe: Tukiwa Waoga, Katiba itahodhiwa na CCM Mbatia: Katiba Mpya haitatokana na ubabe wa watawala
KASI ya wapinzani kufanikisha mkakati wa kuushirikisha umma mpana katika mchakato wa Katiba Mpya, umewaweka pamoja maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam, wakisema `kimbilio’ pekee lipo kwa Rais Jakaya Kikwete.

Wapinzani kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, wamesema pamoja na mafanikio ya mkutano wa jana, wameandaa maandamano sehemu kubwa ya nchi, yatakayofanyika Oktoba 10, mwaka huu.

Moja ya malengo yake ni kumtaka Rais Kikwete, asisaini muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ya Katiba ya mwaka 2013, uliopitishwa hivi karibuni bungeni.

Katika mkutano wa jana, vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema, ‘vilizindua’ harakati hizo kwenye viwanja vya Jangwani na kutangaza kuwa havitashiriki Bunge la Katiba Novemba mwaka huu wala muswada wa Sheria ya Maoni ya Katiba.

Vimesema hatua hiyo itafikiwa ikiwa Rais Kikwete atausaini muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uliopitishwa na wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema.

Mkutano wa jana ulihutubiwa na wenyeviti, makatibu na wabunge wa vyama hivyo, viongozi wa dini 16 akiwamo Askofu Mkuu wa the Full Gospel Bible Fellowish, Zachary Kakobe.

Mbowe, aliwataka watu kuondokana na uoga katika kudai Katiba yenye maslahi kwa nchi na raia wote, vinginevyo itabaki kuhodhiwa na watawala wa CCM.

“Katiba ya nchi ni zaidi ya vyama vya siasa, ndiyo maana tumeamua kushirikiana katika hili, nchini kwetu hivi sasa kuna migogoro ya kidini kati ya waislamu na wakristo, wafugaji na wakulima, sababu ni Katiba ambayo ina majeraha,”alisema .

Kuhusu maandamano ya `nchi nzima’, Mbowe alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, alijulishwa katika kikao chake na viongozi wa vyama hivyo juzi, hivyo hawatakwenda kuomba kibali polisi bali kutoa taarifa kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uliopitishwa katika mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni, ulilenga `kuichakachua’ Katiba Mpya.

“Hatutakubali Katiba inayotaka kuwalinda mafisadi, vijana sasa hivi mmeshaona sera ya CCM ya piga inavyoanza kutekelezwa bungeni, wabunge wamepigwa, wakati wa vijana kufanya mazoezi ya viungo umefika…uchakachuaji huu hatuutaki ,” alisema.

Alisema madai yao ya msingi ni Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba kutowashirikisha Wazanzibar katika kutoa maoni kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria hiyo, hivyo kuwa mfano wa dharau wakati Zanzibar ni nchi.

“Viongozi wa CCM wamemdhalilisha hata Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ambaye walimwita Dodoma kutoa ushahidi kwamba Wazanzibar walishirikishwa katika mchakato wa Katiba,” alisema.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, Balozi Idd alikubali bila kujua kama kuna vifungu vitano vimeongezwa katika muswada ambavyo viongozi wa Zanzibar hawakupewa. Profesa Lipumba alisema kama muswada huo utasainiwa na kuwa sheria kamili, CUF kama ilivyo kwa ‘vyama washirika’ wake, haitashiriki mchakato wa Katiba Mpya.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema suala la Katiba ni la maridhiano na siyo la kibabe kama ambavyo watawala (CCM) wanataka kufanya.

Alisema, kinachotakiwa ni kwa serikali ya CCM kukubali kukaa meza moja na taasisi mbalimbali na vyama vya siasa, ili kufikia mwafaka wa suala hilo.

“Kuna nchi kama Syria kuna mgogoro mkubwa na Barack Obama (Rais wa Marekani) alipotaka kuishambulia nchi hiyo Putin (Rais wa Urusi) akasema hapana, tukae katika meza moja ili kuepusha vita ambavyo vingewaathiri wananchi wa Syria,”alisema.

Mbatia alisema viongozi wa serikali, CCM na wanachama wao, watambue kuwa chama hicho `kitayeyuka’ lakini Tanzania itabaki, hivyo ni lazima kutanguliza maslahi ya Taifa katika suala la Katiba Mpya.

Alimkosoa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, aliposema Rais Kikwete asiposaini muswada huo nchi itaingia katika mgogoro wa Katiba.

Mbatia alisema ni wazi kuwa Wassira hana uelewa mpana wa jambo hilo, kwani hadi hivi sasa nchi inakabiliwa na mgogoro wa Katiba kutokana na CCM kutaka kupora mchakato huo.

“CCM ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuongoza waone mchakato huu wa Katiba ni wa Watanzania wote na ili tusivuruge amani iliyopo tukae meza moja, tunataka kila fikra ya Mtanzania isikilizwe,”alisema.

Kwa upande wake Askofu Kakobe, ambaye aliingia uwanjani hapo saa 11:16 na kushangiliwa na umati wa watu, alisema kupitishwa kwa muswada huo kibabe, ni dalili za kuibua wasiwasi mkubwa nchini.

Askofu Kakobe, alisema tangu mwanzo viongozi wa CCM waliikataa Katiba Mpya, lakini Rais Kikwete, alishinikiza kuwapo kwake huku baadhi ya viongozi wa chama hicho wakikataa.

Alisema sasa Rais Kikwete, anakabiliwa na mtihani mwingine anapotakiwa asisaini muswada uliopitishwa na wabunge wa CCM na Mrema wa TLP na kwamba ikiwa atausaini, itajulikana kwamba azma yake ya awali ilikuwa ‘danganya toto’. Askofu Kakobe alimtahadharisha Rais Kikwete, kutosaini muswada huo ili kuendeleza imani ya umma kwake.

Mbunge wa Mkanyageni (CUF). Habib Mnyaa, alisema kwa sasa Bunge haliko vizuri kwani kuna mkono wa serikali na ndiyo maana Zanzibar inadhalilishwa kwa mambo mengi ikiwamo kutoshirikishwa katika suala hilo.

Alisema ndani ya serikali ya awamu ya nne kuna viongozi wakiwamo mawaziri ambao wanafanya hujuma dhidi ya Zanzibar. Mbunge wa Singida, Tundu Lisu alisema Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba ambaye yeye ni mjumbe haikwenda Zanzibar kupata maoni ya wananchi.

Mkutano huo ni matokeo ya Bunge kudaiwa ‘kuwabeba’ wabunge wa CCM na kutosikiliza hoja za upinzani wakati wa mjadala wa muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.

Hali hiyo ilifikia hatua ya kuibuka vurugu bungeni, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwaamuru askari wa Bunge kuwatoa kwa nguvu wabunge wa upinzani, wakiongozwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Mbowe.

Hali hiyo iliyohitimishwa kwa wabunge wa upinzani kulisusia Bunge, ilisababisha vurugu na ambapo Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi `Sugu’ anadaiwa kumtwanga askari mmoja kiasi cha kuhojiwa na polisi mkoani Dodoma.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Share: