Habari

Wasimamizi mashamba ya mikarafuu kuramba 391m/-

September 13, 2018

NA MWANAJUMA MMANGA

SHILINGI milioni 391 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kifuta jasho kwa wasimamizi wa mashamba ya serikali ya mikarafuu.

Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi, wa Pemba Sihaba Haji Vuai, aliyasema hayo wakati akizunguzma na mwandishi wa gazeti hili huko Wizara ya Kilimo, Maliasili na Uvuvi Maruhubi.

Alisema fedha hizo zitatumika kwa wakulima 835 ambao walifanyiwa uhakiki juu ya usimamizi wa mashamba hayo.

Aidha alisema awali walipanga kutumia shilingi 479,075,500 kwa kuwalipa wakulima 1,010, lakini kutokana na badhi ya wakulima kukosa sifa stahiki ya usimamizi wa mashamba hayo.

Alisema malipo ya wakulima hao tayari yameanza kutolewa kwa kuanzia Septemba 11 mwaka huu ambapo wakulima hupokea fedha hizo kwa kiwango tofauti.

Alisema hatua hiyo ni moja ya kuunga mkono juhudi za wasimamizi wa mashamba ya serikali ili nao wajione wanathaminiwa na serikali yao kupitia kibarua walichopewa.

Hata hivyo aliosema katika msimu wa mwaka 2017 walitarajia kukodisha mashamba 1525 ya heka na waliweza kukodisha mashamba 1452.

Alisema pamoja na juhudi mbalimbali walizozichukua katika kuona mashamba hayo yanaimarika zaidi, lakini kuna changamoto kubwa ya wananchi kutotoa mashirikiano katika kuibua na kuonoesha mashamba ya serikali.

Zanzibarleo

Share: