Habari

Wasomi, wanasiasa wataka uchaguzi tu wapingana na Ponda

Aurea Semtowe na Kelvin Matandiko – Mwananchi
Jumatatu, Novemba 26, 2018

Kauli ya katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda kuwa kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 kwa Katiba na Tume ya Uchaguzi ya sasa ni hatari na kushauri kuuahirisha, imeibua moto kila kona.

Wanasiasa na wasomi waliozungumza na Gazeti la Mwananchi jana (Jumapili, Novemba 25) wamepinga hoja ya Sheikh Ponda na kutaka uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa katiba ila muundo wa Tume ya Uchaguzi ndio utazamwe upya.

Kauli za wasomi na wanasiasa hao ni kubainisha kuwa hoja ya Ponda inaweza kutumiwa na chama tawala, CCM kuendelea kubaki madarakani.

Sheikh Ponda alitoa kauli hiyo Ijumaa, Novemba 23 katika mahojiano maalumu na Gazeti la Mwananchi, kipindi ambacho kumekuwa na mjadala wa katiba na tume huru ya uchaguzi hasa baada ya Rais John Magufuli kusema serikali haijatenga fedha kwa ajili ya katiba.

Pia, kwa nyakati tofauti, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa katiba mpya.

Mchakato wa katiba mpya ulioasisiwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011, uliishia kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo licha ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa, hadi sasa haijapigiwa kura ya maoni.

Katibu Mkuu wa Chama cha AFP, Rashid Rai alisema pamoja na udhaifu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kusitisha uchaguzi ni kuhalalisha CCM iendelee kuongoza hadi katiba mpya itakapopatikana.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muhabi alisema haikubaliki kusitisha uchaguzi huo na badala yake bunge litumike kufanya marekebisho ya vipengele katika katiba ili ipatikane tume huru ya uchaguzi.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisita kuonyesha upande wowote katika mtazamo huo, akisema Sheikh Ponda ametumia uhuru wake kutoa maoni: “Waache watu wahoji, ni uhuru wao kutoa maoni, mie sina maoni katika hilo.”

Aliyekuwa mgombea urais wa CCK katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Dk Godfrey Malisa alisema si sahihi kusitisha uchaguzi, kwamba wapenda demokrasia waungane kushinikiza upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi kabla ya uchaguzi huo.

“Lakini ikishindikana kufanyika maboresho ya kupata tume basi hoja ya Sheikh Ponda itakuwa na mashiko kwa hapo baadaye,” alisema Malisa.

Katibu Mwenezi wa Ada Tadea, Felix Makuwa alisema suala la katiba mpya ni kupoteza fedha za Watanzania na muda wa kuendelea na masuala mengine ya kitaifa.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema katiba ni hitaji la lazima lisilohitaji utashi wa wanasiasa na endapo hakutakuwa na marekebisho ya mfumo wa tume ya uchaguzi, hali itakuwa mbaya zaidi katika uchaguzi mkuu ujao.

“Mabadiliko ya katiba hususan kwenye mfumo wa tume ya uchaguzi ndiyo suluhu ya kuondoa vurugu zisijitokeze uchaguzi ujao, bila hatua hiyo tunahitaji busara ya hali ya juu sana kutuvusha eneo hilo vinginevyo tutaingia kwenye matatizo,” alisema Dk Mashinji.

Hata hivyo, Dk Mashinji alisema kusitisha uchaguzi mkuu ujao ni jambo lisilowezekana kwa kuwa lipo kikatiba.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa NCCR, Samwel Ruhuza alisema hoja ya Sheikh Ponda ni mtego usiokubalika kwa vyama vya siasa vya upinzani.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema suala la kuahirisha uchaguzi kwa ajili ya kutokuwepo kwa katiba mpya ni gumu kutokea labda Rais Magufuli aridhie kuwa hadi katiba itakapopatikana.

“Kwetu sisi ni ngumu kufanya hivyo, tutaahirisha uchaguzi mara ngapi kushinikiza katiba mpya ikiwa kiongozi wa nchi amegoma kutoa hela ya kugharamia mchakato huo, hatuna la kufanya zaidi ya kusubiri mpaka pale atakapofanya hivyo,” alisema Profesa Shumbusho.

Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sheriff alisema kwa mujibu wa katiba iliyopo ni ngumu kuahirisha uchaguzi, lakini serikali inapaswa kuzingatia upatikanaji wake pamoja na tume huru ya uchaguzi.

“Wananchi waliotoa maoni yao hayajasikilizwa na matokeo yake zoezi hili lilikuja kukwama ukingoni,” alisema Profesa Sheriff na kuongeza:

“Sijui vipi tutaweza lakini kama serikali yenyewe haikuwa tayari ni ngumu kwetu kuamua kitu na Watanzania wataona kama maoni yao yamepuuzwa.”

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala aliunga mkono hoja ya Sheikh Ponda, akisema kwa katiba ya sasa na tume ya uchaguzi, uchaguzi ujao hautakuwa wa haki.

Share: