Habari

Wataka Katiba ya Tanganyika kwanza

Longido.Serikali imeshauriwa kuanza mchakato wa kuunda Katiba ya Serikali ya Tanganyika ili iweze kuendana na matakwa ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakizungumza katika semina ya mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Arusha iliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi na Maendeleo cha MS-TCDC na Mtandao wa taasisi zisizo la kiserikali mkoani Arusha (ANGONET), watendaji wa mashirika hayo walibainisha kuwa ili Jamhuri ya Muungano iwepo ni muhimu kurejea Serikali ya Tanganyika.

“Huwezi kuwa na Katiba ya Muungano, wa Serikali ya Zanzibar bila kuwa na Serikali ya Pili, hivyo ni muhimu sasa kuanza mchakato ya kuandikwa Katiba ya Tanganyika,” alisema Elibariki Malley.

Malley ambaye pia ni Diwani wa Arusha, alisema ni vyema sasa wakati mchakato wa Katiba Mpya umeanza, zianze taratibu za haraka kupata Katiba ya Tanganyika ambayo itakuwa ni tofauti na Katiba ya Jamhuri,” alisema

Akitoa mada juu ya katiba katika semina hiyo, Mkufunzi Mshiriki wa Chuo cha MS-TCDC, Mwanasheria, Anna Mghwira alisema kuwa katika rasimu ya Katiba Mpya, Tanganyika haikutajwa wazi bali imetajwa Tanzania Bara.

Mwananchi

Share: