Habari

WATAWALA WETU, VIFARU VILETE UMOJA SASA – MZIGO ULIDODA.

Tunahitaji majibu sahihi, hatutaki porojo na mizaha, hatutaki soni wala mihemuko.

Watawala mje mtwambie kwa vigezo na hoja kwa misimamo na uweledi iko wapi Zanzibar?

Walau tuanzie hii miaka mitano tu iliyopita kulifanywa jitihada kuwaunganisha wazanzibari kwa maslahi mapana ya vizazi vyetu tena kwa ridhaa ya wazanzibari wenyewe kuamua kuiendesha Zanzibar kwa umoja wao bila ubaguzi wala hiyana. Leo mtawala aliyeshikwa mkono kuliongoza jahazi hilo ndiye huyo huyo aliyelizamisha. Ni huyo huyo analeta mzaha tena mzaha rahisi wa kejeli na kebehi yeye anashangaa badala ya kutoa jibu eti anasema . “Wazanzibari hawakuipa ridhaa GNU” Ridhaa gani tena hiyo. Angejiuliza suala moja tu ” Kwa nini hawakuipa ridhaa ilihali ni yeye aliyepewa dhamana kuilinda? lengine angejiuliza ina maana Kumbe GNU inakataliwa kwa uchaguzi batili na si kwa kura ya maoni? MZIGO ULIODODA.

Ikiwa misingi ya haki inapuuzwa kunalazimisha batili ishinde tena kwa nguvu za dola unategemea nini? Hilo tuliache.

Turudi kwenye uchaguzi ulioitwa wa marudio kwa kiasi kile ilitosha kuonesha mtawala alivyodhamiria kuwa mzigo kwa wazanzibari.

Alikuwa radhi watu wauwawe ili kulinda maslahi yake. Hakuupa umuhimu mgogoro wa uchaguzi uliokuwepo, yeye aliona ni bora jamii igawike vipande vipande, watu wafarakane, wasusiane, wagome kushiriki uchaguzi wa marudio ulio batili na mwishowe kuwe na mazingira ya kutangazwa kuwa mtawala, MtaWala MZIGO ULIODODA. Hilo alilipenda na kulifurahia kuliko kutumia jitihada kuenge enga maridhiano kabla ya kuhalalisha huo uchaguzi batili.

Ni mtawala mzigo pekee atafurahia hili.Uchungu wa nchi na wananchi haumsumbuwi wanachotaka ni kuitwa wahaeshimiwa tu tena kwa gharama yeyote.

Sawa kama ni utawala wameupata na wengine wamekuwa wakubwa sasa jamii pana ndio imeambulia nini?

Si tunaona kususiana na utengano wa kijamii, chuki na ukimya wa uadui wenye kusubiri kulipizana visasi.

Kuna mwangwi mkubwa. Watawala wamekosa nguvu za kijamii na mshikamano wa watu. Wanatumia nguvu kubwa kuikubalisha jamii kile watawala wanachokisema na kukiamini.

Sasa ikiwa watawala mlitumia vifaru na bunduki na majeshi kutisha na hatimae kupata mazingira ya kuwa watawala na hamkujali kutumia busara ya kuelewana na kutatua sintofahamu hapo kabla mi mi NAWASHAURI LETENI TENA MIZINGA, VIFARU BUNDUKI na MAJESHI yaje yawaunganishe Wazanzibari.

Watawala wetu mjitafakari tena kama sio mzigo iliododa ni nini?

Kufanya hilba kwa njia zozote zile hakukubaliki na huu ujanja wa watawala kushika madaraka kwa hila kwa gharama za kuwatia wananchi na wazanzibari katika mifarakano linapaswa kulaaniwa na kila mzalendo. Tumerejeshwa tena nyuma sana kwa maslahi ya walafi wachache wasiojali maslahi mapana.

Iko wapi tena dhana ya maridhiano? iko wapi GNU? iko wapi Zanzibar?

Share: