Habari

Wazanzibar Wanaharakati amkeni tena tusemee mambo yetu

Jecha alitutenda. Wengi bado inawajia kwenye ndoto zao. Kama vile wakiona ukuti wakidhani ni nyoka. Leo Bwana Rais asherehekea mwaka mmoja tokea atangazwe mshindi kwenye uchaguzi uliokosa upinzani.

Bado Wazanzibari hasa wanaharakati wameendelea kugubikwa na giza hili la ujecha. Ikiwa Mwaka mmoja na miezi mitano tokea matokeo ya ushindi wa CUF, na Bwana Jecha kutulaza, bado hatujaamka.

Wako Wanaharakati waliozinduka lakini kwa upande mwengine, wameelekea Tanganyika kuwasaidia ndugu zao wa huko kuwatetea na kuwasemea mambo yao.

Vipi haya ya petu nani wa kutusemea? Ni sisi wenyewe lazima turudi kwenye line. Hakuna wa kutusemea isipokuwa ni kuzinduka kuona mwangaza unachomoza na kuendelea kujipanga.

Sehemu tatu sasa hivi zinahitaji kuwafanyiwa harakati badala ya mbili tulizozowea. Sehemu hizo ni:

1. Muungano (kama kawaida), lakini kutokana na Mtawala kujitia punguwani hatari ya kufifiliza imekuwa kubwa zaidi. Sasa hivi anajitia hamnazo kama vile hakuna Nchi ya Zanzibar, fedha za world Bank, Zanzibar haimo. Uteuzi wa viongozi wa serikali Wazanzibari na Waislam hawamo. Tunahitaji harakati

2. Kutetea ushindi wa wananchi 25 October 2015. Bado eneo hili liko wazi, hakuna harakati za kutosha zilizofanyika. Wengi wa wanaharakati wanadhani ule ulikuwa ushindi wa Maalim pekee hivyo yeye ndio mwenye jukumu la kuutetea. Hapana,ule ilikuwa ushindi wa wananchi hivyo ni jukumu la kila mmoja kuutetea. Hivyo harakati zinahitajika kwa haraka na kiasi kikubwa.

3. Mgogoro wa CUF. Ifahamike kuwa Chama cha CUF ndio mtetezi, platform, na sauti ya Wazanzibari. Haina maana kwamba ndugu zetu wa Tanganyika hawamo, kiuhalisia Zanzibar hakuna mbadala tofauti na Tanganyika. Hivyo tunahitaji harakati katika eneo hili ili kuirudisha CUF kwenye jukwaa kuliko ilivyo kuwa 1995. Irudi ikiwa na mbinu, mikakati, na malengo mapya.

Wazanzibari wanaharakati sasa hivi wamevutika kwa yale yanayotokea Tanganyika. Turudini jamani, sio mbaya, kutoa msaada lakini tusijisahau kwa haya ya kwetu.

Share: