Habari

Wazanzibari watakiwa kuungana kudai na kutetea maslahi ya taifa lao

Salma Said,

Wazanzibari wametakiwa kuungana katika kutetea maslahi ya nchi yao wakati wa mchakato wa katiba mpya ikiwa njia mojawapo ya kuhakkikisha madai yao yanakubaliwa. Wakihutubia kwa nyakati tofauti katika muhadhara wa kiislam uliofanyika msikiti wa Mbuyuni Unguja jana, Sheikh Mussa Juma wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam, ambaye aliwahi kukamatwa na kuzusha sokomoko kubwa nchini, alisema bila mshikamano hakuna litakalokuwa hivyo amewahimiza Wazanzibari kushirikiana pamoja kupinga dhulma dhidi ya nchi yao pamoja na kuietete Zanzibar.

Sheikh Mussa alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tangu ulipobuniwa umekuwa ni wenye mashaka kwa wazanzibari “Sisi tunataka nchi yetu tumechoka na katika hili tunaomba tusiondolewe kwenye lengo letu maana kuna watu wanataka kuua hoja ya msingi ya dai la Wazanzibari”

Alisema mfumo wa muundo wa Muungano wa sasa haufai na ndio chanzo cha matatizo yote ambayo dawa yake sio kuongeza idadi ya Serikali ni kuweka mfumo mpya utakaowezesha Zanzibar kuwa na Mamlaka yake kama Taifa.

“Muungano huu msingi wake ni mbovu na hilo hatuaanza kulisema sisi watu wa Uamsho, limesemwa siku nyingi tena na wataalam waliobobea,tunaomba Wazanzibari kwa umoja wetu tushirikiane kurejesha nchi yetu katika Mamlaka yake “ Alisema Sheikh Mussa.

Kauli mbiu katika mikutano hiyo ni “Tuachwe Tupumuwe” imekuwa ikipendwa na kupata umaarufu siku hadi siku ambapo sasa vijana wengi wa Kizanzibari wameweka kuwa miito ya simu zao za mkononi.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na watu wengi, Sheikh Mussa ambaye wiki mbili zilizopita alikamatwa kwa madai ya kufanya mkusanyiko usiokuwa halali, aliwasimulia visa na mikasa ya Vyuo vya Mafunzo(Magereza) ambako alishangaa kupata mapokezi makubwa kutoka kwa wafungwa waliowapa heshima kubwa ndani ya Gereza.

“Jamani waislamu,tumepelekwa Gerezani, kule tulipoingia tu, tukapokewa kwa furaha na waislamu wenzetu waliokuwa wamefungwa,wakatueleza kuwa pamoja na wao wamo Jela,lakini wanaunga mkono harakati zetu na kututaka tusiogope jambo lolote hadi Zanzibar inakuwa na Mamlaka yake” Alisema Sheikh Mussa.

Kwa upande wake, Naibu Amiri wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam,Sheikh Azan Khalid alisema shutuma zinazoelekezwa kwa Jumuiya hiyo sio za kweli na zimekuwa zikipikwa kwa nia ya kuipaka matope zenye lengo la kuwatoa katika dhamira yao.

Sheikh Azan alisema kamwe mikutano yao haitasita hadi hapo kitakapoeleweka kwa Zanzibar kuwa na Mamlaka yake kwani Muungano ni jambo la khiyari na sio kulazimishana. Alisema Wazanzibari wakijitegemea wataweza kupiga hatua za maendeleo.

Alisema kwamba vitendo vya uchomaji wa makanisa ni mambo ambayo wanaamini hayafanywi na waislamu bali kuna mpango maalum uliondaliwa kuviza harakati za madai ya wazanzibari katika muungano na kulitaka Jeshi la Polisi kuunda Tume maalum kuchunguza matukio hayo.

Sheikh Azan alisema kwamba Jumuiya yao imekuwa ikiandamwa kipindi kirefu tangu kuanzishwa kwake akitolea mfano mwaka 2004 walipotaka kufanya maandamano Polisi ilikubali kwa kutoa kibali rasmi,lakini siku mbili kabla ya kufanyika kwa maandamano hayo baadhi ya Masheikh wa Jumuiya hiyo walianza kukamatwa kwa visingizio mbalimbali.

“Haya yanayotokea sasa ya sisi kusingiziwa kuwa tumevuruga amani si mageni haya yameandaliwa yalianza siku nyingi ,lakini jambo la kushangaza hapa kulichomwa kuran tukufu hakuna kiongozi aliyekemea,lakini leo yamechomwa makanisa kila kiongozi anasema” Alisema Sheikh Azan.

Alisema sehemu kubwa ya makanisa yaliyochomwa hayakuwa na hati miliki kutoka kwa Mamlaka zinazohusika kwani hapo mwanzo zilikuwa ni makaazi ya kawaida,lakini wakayageuza kuwa makanisa,licha ya kuomba kwa kipindi kirefu,Serikali haikuwa imewapa.

“Nikuchekesheni naambiwa hivi juzi mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd ameagiza makanisa yote yasiyokuwa na hati miliki yapewe haraka…naambiwa jana katuma ujumbe kwa watu wa ardhi kwenda kuwahimiza hao ndio viongozi wetu “ Alisema Sheikh Azan.

Tagsslider
Share: