Habari

Waziri aagiza matangazo ZBC yarudishwe

Na Kauthar Abdalla
WAZIRI wa Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk ametoa agizo kwa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), kushirikiana na uongozi wa Wizara kulitatua tatizo linalokikabili kituo cha kurushia matangazo Bungi.
Akizungumza na viongozi na mafundi wa shirika hilo katika ziara maalum iliyofanyika Bungi kujua sababu zilizopelekea kutosikika kwa matangazo ya shirika hilo la umma kwa muda mrefu sasa, Waziri Mbarouk alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanafaidika na haki yao ya msingi ya kupata habari kwa wakati.
Alisema ni jambo lisilo la kawaida kuona kwamba redio ya umma inashindwa kuendesha matangazo yake kutokana na kushindwa na gharama za kifedha za kutengeneza kifaa kilichoharibika.
Aidha alisema kutokuwa na masafa ya uhakika ni tatizo kwa serikali pamoja na wananchi hivyo kuwe na mpango kazi madhubuti kati ya viongozi wa shirika na Wizara ili kuona tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.
Alisema endapo tatizo lililopo katika kituo hicho litakuchukua muda kutengenezwa kunaweza kukasababisha athari kubwa kwa serikali na wananchi.

Nae Fundi Mkuu wa wa ZBC Redio, Ali Aboud Talib, alisema tatizo lililopo katika kituo cha Bungi linahitaji gharama kubwa hadi kukamilika kwake ambapo kwa hatua za mwanzo zinahitajika zaidi ya shilingi milioni nne.
Alisema chanzo cha kutokuwa na masafa ya uhakika ya kusikika kwa shirika hilo ni kuharibika ‘radio frequency cable’ yenye urefu wa mita 150 inayounganisha baina ya mnara na mitambo ya kurushia hewani.
Alisema kuharibika kwa cable hiyo pia kumetokana na kuchakaa sana kwani ilianza kutumika tokea ilipokuwepo Chumbuni na baadae kuhamishiwa Bungi.
Sambamba na hayo alisema licha ya kuwa kituo cha Bungi kina kasoro kadhaa lakini bado uwezo wa shirika wa kuweza kuzitatua kasoro zilizopo ni mdogo mno.
Zanzinews
Share: