Habari

WAZIRI AMUOMBA RADHI MAALIM SEIF

Khatib Suleiman HabariLeo Zanzibar

WAZIRI wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk ameomba radhi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kwa matamshi ya kumdhalilisha yaliyofanywa na Shirika la Utangazaji la Zanzibar, ZBC.

Waziri Mbarouk, alikiri kuwepo kwa kauli na vitendo vya kumdhalilisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kwa watangazaji wa Shirika la ZBC ambao kwa makusudi walishindwa kumpa heshima kiongozi huyo wa pili wa juu katika uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa.

Waziri alilazimika kutoa ufafanuzi huo kutokana na Mwakilishi wa Wawi, Pemba Saleh Nassor Juma (CUF) kulalamika kwamba wafanyakazi wa ZBC, upande wa televisheni wakati wanaposoma taarifa ya habari hawampi heshima yake ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kumtaja ‘Mheshimiwa au Maalim’ na badala yake wanamkata kwa kumwita ‘Seif Sharif Hamad’.

Alisema kufanya hivyo, kunatoa picha yenye tafsiri nyingi ndani ya akili ya binadamu: “Mbali ya kumvunjia heshima Maalim Seif…kuna imani za ubaguzi na chuki na kusababisha mkanganyiko kwa jamii na hasa kwa vijana wadogo kuweza kupotosha mila na silka zetu,” alisema Mwakilishi Saleh.

Mwakilishi huyo alisema baadhi ya viongozi wakuu wanatamkwa kwa kutajwa vyeo vyao ambapo kwa upande wa Rais wa Zanzibar, anatajwa kwa cheo chake cha Dk au Mheshimiwa, wakati Makamu wa Pili wa Rais, anatajwa kwa jina la Balozi: “Kwanini kwa Maalim Seif…kinakosekana hicho?,” alihoji Mwakilishi.

Akijibu kauli hiyo, Waziri Mbarouk alisema wamebaini kuwepo kwa vitendo vya kumdhalilisha Makamu wa Kwanza wa Rais, vinavyofanywa na WATENDAJI wa Shirika hilo. Waziri alisema kuwa tayari wamechukua hatua na wamemuomba radhi Kiongozi huyo:

“Mheshimiwa tumebaini kuwepo kwa vitendo vya kumdhalilisha kwa makusudi Makamu wa Kwanza wa Rais vinavyofanywa na watendaji wa Wizara wa Shirika la Utangazaji la ZBC…tayari nimemuomba radhi Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad,” alisema Waziri Mbarouk.

Waziri huyo alisema kwamba tayari watendaji wa Wizara hiyo, akiwemo Katibu Mkuu wamekemea vitendo vya udhalilishaji, vinavyofanywa na ZBC, dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais:

“Watendaji wa Wizara…pamoja na Katibu Mkuu tumekemea vitendo vya kumdhalilisha Makamu wa Kwanza…udhalilishaji ambao haulete taswira nzuri katika silka na mila za Wazanzibari katika kuweka heshima kwa mtu aliyekuzidi umri akiwemo kiongozi wa nchi,” alisisitiza Waziri huyo.

Aidha, Waziri alisema ameandika barua ya onyo kwa watendaji wa Wizara wanaohusika na udhalilishaji huo, kuhusu kutunza nidhamu kwa viongozi kwa kuwataja kwa mujibu wa vyeo vyao ama katika utaratibu wa kumjengea heshima yake, kila mmoja.

Awali, Waziri Mbarouk alisema kwamba Shirika hilo lipo katika mchakato wa mageuzi makubwa kwa lengo la kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake.

Alisema baada ya kazi ya kutiwa saini kwa sheria ya kuanzishwa kwa Shirika hilo, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kumteua Mwenyekiti, pamoja na wajumbe wa Bodi wa Shirika.

Katika kikao hicho, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha makadirio, mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2013/2014..

Share: