Habari

Winnie Mandela, tafsiri ya mnyama paka kugeuka chui

By Luqman Matolo
Saturday, April 14, 2018

Paka ni mnyama mpole na rafiki kwa binadamu na pia mlinzi wa nyumba dhidi ya panya na hata nyoka. Paka anapopigwa na binadamu hukimbia na hana kawaida ya kupambana na watu. Hata hivyo, inashauriwa usimpige paka ukiwa umefunga milango, maana ni hatari mno.

Inaelezwa kuwa unapofunga mlango, paka huona hana pa kukimbilia kujiokoa baada ya kipigo. Hapo akili yake humwambia kuwa kusudio ni kumuua. Kwa hiyo naye hufikiria njia ya kujiokoa na kifo. Ni hapo huona hakuna namna zaidi ya kupambana na anayempiga.

Kwamba paka hutuna na kubadilika kabisa na kuwa mithili ya chui. Kucha zake hurefuka na kama binadamu atachelewa kufungua mlango, anaweza kumrarua mithili ya chui. Hata watu wakitokea wakimuuliza amejeruhiwa na nani, wanaweza wasiamini wakiambiwa ni paka.

Simulizi hiyo tafsiri yake ni kwamba paka si muuaji, ila anayapenda mno maisha yake. Hivyo, inapotokea analiona jaribio la kumtoa uhai atakuwa tayari kufanya lolote ili kujinusuru.

Tafsiri ya jumla ni kwamba kila kiumbe kinapoona hatari mbele yake na kukawa hakuna mahali pa kukimbilia kujiokoa, moja kwa moja huwaza kuyalinda maisha yake.

Ushujaa wa Winnie Madikizela Mandela ambaye mwili wake unazikwa leo (Jumamosi, Aprili 14, 2018), unapatikana hapo.

Aliyekuwa mume wake, Nelson Mandela alipofungwa jela, akajikuta yeye ndiye mwenye kutakiwa kufanya kazi kuhudumia watoto wake wawili bila baba yao. Jumlisha na kuona mwanaume aliyempenda akiwa jela, ni hapo wazungu walimkoma.

Ni rahisi kuzungumza na kueleweka kwamba Mandela asingefungwa na kukaa jela miaka 27, pengine Winnie asingekuwa mwanamke jasiri, mkorofi na mwenye kuamini katika kulazimisha Serikali ya kikaburu itoe haki kwa watu weusi kuliko kwenda kidiplomasia.

Aliamini kwamba endapo makaburu wangeona ugumu wa kutawala, wangelazimika kuwapa haki watu weusi.

Ni sababu hiyo, Winnie alihamasisha vijana na kuunda vikundi vya kufanya ulipuaji, uchomaji matairi barabarani na kadhalika ili kukata mawasiliano na kuipa hasara serikali.

Historia ya machafuko ya Soweto, wakati mapambano ya watu weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, itakuwa na matege kama haitamtaja Winnie.

Ujasiri wa Winnie

Zipo sababu tatu ambazo unaweza kupatia kama utazijengea hoja kwamba ndizo zilizokuza ujasiri wa Winnie. Hata hivyo, utakosea kama hutakubali kuwa roho ya ujasiri na kutoogopa ilikuwamo ndani yake, lakini ikawa haijapata kichocheo. Kwa mantiki hiyo, mambo matatu nitakayoeleza yalimpa huo moto.

Sababu ya kwanza ni weusi wake, kwa hiyo alikuwa mmoja wa watu wa jamii kubwa ya waliokuwa wakibaguliwa kutokana na rangi yao.

Hapo ndipo kwenye mwanzo wa yote ambayo Winnie aliyafanya. Hakuna binadamu anaweza kuridhika kubaguliwa. Mbaya zaidi kubaguliwa kwenye nchi yake.

Ipo sababu ya pili, ni kitendo cha mume wake, Nelson Mandela kufungwa jela. Watu ambao alikuwa akiwachukia kwa sababu ya jinsi ambavyo walikuwa wakiibagua jamii yao ya watu weusi, waliingia ndani ya nyumba yake na kumweka jela mwanaume aliyempenda.

Sababu ya tatu ipo kwa wanaye wawili – Zenani na Zindzi. Winnie alijikuta katikati ya mzigo mzito wa kulea watoto wake mwenyewe baada ya baba yao kuwa jela.

Unapoweka maeneo hayo matatu kwa pamoja, unapata picha ni kiasi gani Winnie aliguswa pabaya kiasi cha kufanya ‘mizuka’ iliyokuwa imelala iamke.

Winnie aliona viongozi waandamizi wa ANC, waliokuwa nje, walikuwa wanatumia njia ndefu kudai uhuru. Viongozi wa ANC walikuwa na sera ya kutaka makaburu wawape uhuru watu weusi wa Afrika Kusini kwa njia ya Amani.

Wakati Winnie aliamini kwamba kuwapelekesha na kuwanyima pumzi ya kutawala kwa nafasi, kungewafanya wasalimu amri haraka.

Eneo lingine ambalo Winnie alitofautiana na viongozi waandamizi wa ANC ni mawazo ya kujenga taifa baada ya kuwashinda makaburu.

Viongozi wa ANC walitaka taifa lenye utawala wenye kuheshimu na kutoa haki sawa kwa raia wa rangi zote, wakati Winnie alitamani tofauti.

Winnie alikuwa na hisia za kutaka watu weusi wamiliki nchi kwa upendeleo mkubwa ili kuwafanya wazungu wayaone na kuyahisi machungu ambayo watu weusi waliyapitia kipindi chote cha utawala wa makaburu na sera za ubaguzi wa rangi.

Lakini, Viongozi wa ANC, hasa Nelson Mandela, waliona kuwabagua Wazungu ingekuwa kuendeleza ubaguzi.

Winnie na vijana

Winnie aliona njia rahisi ya kufanikisha mitazamo yake ni kuwekeza kwa vijana. Aliwajaza hasira na chuki dhidi ya makaburu, vilevile aliwatengeneza kuwa na mtazamo kwamba bila mapambano haki isingepatikana.

Zaidi, Winnie aliwajenga vijana kuamini kuwa kwa mawe na petroli wangewashinda polisi wa Serikali ya makaburu wenye bunduki.

Ilikuwa kawaida kwa Winnie kukamatwa na kuwekwa kizuizini na serikali ya makaburu. Aliteswa na kuzuiwa kutoka nje ya nyumba yake.

Aliwekwa chini ya uangalizi. Kuna wakati alifungwa katika jela aliyotengwa peke yake kwa zaidi ya mwaka mmoja na kupigwa marufuku kujumuika na watu mijini.

Hata hivyo, Winnie aliporejea Soweto, alikusanya vijana na kuwapa moto. Akauambia umati mkubwa kwamba wanaweza kuwashinda makaburu bila bunduki.

Alisema: “Hatuna bunduki, tuna mawe peke tu, maboksi ya viberiti na petroli. Kwa pamoja, mkono kwa mkono na viberiti vyetu, petroli na kuchoma moto matairi ya magari, tutaweza kuikomboa nchi hii.”

Katika kuhamasisha vijana, Winnie aliweza kujipambanua kuwa Mwakilishi wa Mandela aliyekuwa jela.

Upande wa pili Winnie kila alipomtembelea Mandela katika gereza la Robben Island, alipotumikia miaka 19, alimshawishi kuamini katika nguvu ya vijana. Zaidi, aliwafanya vijana wawe wanamiminika kumtembelea gerezani.

Zaidi, Mandela alikutana na vijana waliokamatwa na polisi katika operesheni zilizoongozwa na Winnie kwenye gereza hilo.

Hata mwaka 1982, Mandela alipohamishiwa Gereza la Pollsmoor alikokaa miaka sita kisha mwaka 1988 Gereza la Victor Verster miaka miwili, kote huko aliona wafungwa vijana walioshiriki harakati za Winnie.

Ni hivyo, Mandela aliiona kazi kubwa ya Winnie akiwa gerezani. Aliuona ujasiri wake alipomtembelea na kuzungumza naye.

Alikubali harakati zake alipowafanya vijana wawe na utaratibu wa kumtembelea Robben Island, nyakati za mapambano makali bila dirisha la mazungumzo dhidi ya serikali ya makaburu.

Winnie ni binadamu

Jambo lisilopingika ni kwamba Winnie ni shujaa wa Afrika Kusini. Vurugu zake za kulipua maeneo mbalimbali na kuchoma matairi ya magari kwa moto na kutengeneza milipuko ya petroli mitaani, kwa kiasi kikubwa ziliwafanya makaburu waone ugumu wa kuitawala Afrika Kusini bila kuwapa haki stahili watu weusi.

Hata Rais wa mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, Frederik de Klerk, aliporidhia mazungumzo na kwenda kwenye uchaguzi uliowapa watu weusi uhuru wa kweli, ilikuwa ni baada ya kujionea misukosuko mingi ya kutawala.

Ndani ya nchi Winnie na watu wake walikuwa moto na kwenye jumuiya za kimataifa kulikuwa na presha kubwa, hasa baada ya nchi nyingi za Magharibi kuanza kutambua kilio cha raia weusi wa Afrika Kusini.

Kutokana shinikizo la pande zote mbili, makaburu waliona hakuna namna ya kukwepa kutoa haki iliyopiganiwa.

Upande wa pili, Winnie anayo makosa yake kama binadamu. Kubwa ambalo limebaki kuwa doa lenye kuchafua ushujaa wake wa kutetea uhuru na haki za watu weusi wa Afrika Kusini ni kifo cha mvulana mwenye umri wa miaka 14, Stompie Moeketsi aliyeuawa mwaka 1989. Stompie alitekwa, akateswa na kuuawa na vijana wa Winnie.

Ilielezwa kwamba Winnie ndiye aliagiza Stompie auawe. Stompie alikuwa mmoja wa wapigania uhuru na haki za jamii kubwa ya watu weusi akiwa na umri mdogo mno.

Hata hivyo, timu ya Winnie ilimtuhumu kuwa shushushu, kwamba alikuwa anaungana na wanaharakati na kuvujisha siri kwa polisi wa makaburu ambao walijua mipango yao mingi. Winnie alishtakiwa kwa mauaji ya Stompie.

Ubinadamu mwingine wa Winnie unaonekana kwenye ndoa yake na Mandela. Mwaka 1990 Mandela alipoachiwa huru, walikuwa watu wenye furaha mno. Miaka miwili baadaye kila kitu kilibadilika, Mandela alipotangaza kuvunjika kwa mapenzi yao.

Vyombo vya habari vikaeleza kuwa sababu ya Mandela kuvunja ndoa na Winnie ni baada ya kugundua mkewe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mwanasheria Dali Mpofu.

Ripoti nyingine zikasema Winnie alijihusisha kimapenzi na vijana wadogo. Mwaka 1996 ndoa baina ya Mandela na Winnie, ilivunjwa rasmi kwa talaka.

Winnie alikuwa First Lady wa Afrika Kusini kuanzia mwaka 1994 pale Mandela alipoapishwa kuwa rais mpaka mwaka 1996 talaka ilipotoka rasmi.

Mandela alipomuoa Graca Machel mwaka 1998, Winnie alikuwa mchangamfu kwa mwanamke huyo aliyechukua nafasi yake. Na alibaki kuwa sehemu ya familia.

Winnie ameigizwa uhusika wake kwenye filamu mbalimbali na wasanii tofauti. Filamu ya Mandela and de Klerk (mwigizaji ni Tina Clifford), Mrs Mandela (Sophie Okenedo), Winnie Mandela (Jennifer Hudson) na nyingine.

Aprili 2, mwaka huu ukawa mwisho wa maisha ya Winnie duniani akiwa na umri wa miaka 81 na anazikwa leo (Jumamosi, Aprili 14, 2018), mjini Johannesburg.

Utility
Nukuu ya Winnie kwa Mandela

“Nilikuwa na kipindi kifupi cha kumpenda Mandela kabla hajafungwa jela. Kipindi hicho kimefanya nimpende mpaka mwisho.”

“Tungeishi muda mrefu labda ningeyaona makosa yake, labda ningemchukia. Muda mchache tulioishi ulikuwa wa kumpenda tu na nilimpenda mpaka kifo chake,” Winnie.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Share: