Habari

Yaliopita si-ndwele tugange yaliopo na yajayo..

By Padri Privatus Karugendo
Jumatano, Machi 21, 2018

Babu zetu walikuwa na busara kubwa. Kama tungeendeleza busara hizi, tungekuwa mbali kama taifa. Misemo yote tuliyonayo kwenye lugha ya kiswahili na lugha nyingine za kikabila, inaonyesha busara kubwa.

Inaonyesha jinsi mababu zetu walivyokuwa na falsafa ya maisha. Falsafa hii ilitoa mwelekeo wa maisha kwa kila mtu ndani ya jamii.

Busara hizi ziliongoza maisha na siasa za wakati ule. Ipo misemo mingi yenye mafundisho, lakini kwa leo nimechagua mmoja. Msemo huu wa ‘yaliyopita si-ndwele’, unafanana na ule wa ‘kufanya kosa si-kosa, kosa ni kurudia kosa.’ Na ‘mavi ya zamani hayanuki.’

Busara na hekima iliyondani ya misemo hii ni kwamba, yale yaliyopita hayawezi kumsaidia mtu leo au kesho. Au kosa lililofanyika kwa makusudi yaani kwa kujuwa au kwa kutokujuwa, likirudiwa ndiyo ubaya wa kosa hilo unapodhihirika.

Kwao, mambo ya maana ni yale ya leo, lakini ya maana zaidi ni ya kesho. Ni lazima mtu kuangalia mbele. Kuangalia ya kesho. Mfano, mtu anaangalia familia yake inaishi vipi leo, inakula nini leo, na je, kesho itakula nini?

Hivyo hivyo, mtu anaiangalia jamii yake leo na kesho, mtu analiangalia taifa lake leo na kesho. Ni lazima mtu kuangalia kwamba kama unakula leo na kesho utakula. Kama wewe hutakuwepo, wale watakaokuwepo watakula.

Kwa njia hii mtu anaweza kuiangalia familia yake miaka 50 au 100 ijayo, hivyo hivyo kwa jamii na taifa zima. Mfumo wa kuganga yaliyopo na yajayo, ni mfumo wa matumaini na imani.

Ni mfumo ambao nchi zilizoendelea zinautumia. Lakini, pia ni mfumo ambao babu zetu waliutumia, kabla ya kuvamiwa na wakoloni.

Kuendelea kwa familia, kuendelea kwa ukoo na kuendelea kwa falme mbalimbali ni kitu ambacho mababu zetu walitilia maanani.

Kuna hoja ya wataalamu wengine, inayopingana na mfumo huu kidogo, hoja hii inasema kwamba mwanadamu anaendelea kwa kuangalia yale ya jana. Kwamba yale ya jana ndiyo yanayompatia nguvu na uwezo wa kupiga hatua.

Maana yake ni kwamba daima mwanadamu katika maisha yake anatembea kinyumenyume. Yaliyopita yanakuwa mbele ya macho yake, na yeye anatembea kuelekea asikokujua. Imani na matumaini ya kupiga hatua yanatokana na historia inayokuwa mbele yake.

Kama ni utumwa, anauchukia na kupiga hatua kuelekea uhuru kwa uangalifu mkubwa ili na yeye asiwafanye wengine watumwa;

kama ni ukoloni, anauchukia na kupiga hatua kuelekea uhuru kwa uangalifu mkubwa ili na yeye asiwatawale watu wengine; kama ni ufisadi vilevile ili na yeye asigeuke fisadi.

Kama alikuwa na mwendo wa kinyonga, anajitahidi kuwa na kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Kama alikuwa wa uvivu wa kufanya kazi anahamasika kwa wito wa Hapa Kazi Tu, anaanza kufanya kazi kwa bidii na kusonga mbele.

Ingawa siipingi sana hoja hii, kwa leo nisingependa kuijadili. Leo nitabakia kwa ile ya “yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo”.

Nafikri kwa hali ya Tanzania, hoja hii inatufaa sana. Viongozi wetu wakikubali kusikia hili, ni lazima tutasonga mbele kwa kasi. Tugange yaliyopo na yale yanayokuja mbele yetu.

Teknolojia ina kuja kwa kasi, utandawazi unatandaa kwa kasi ya kutisha, nchi yetu inakuwa soko la mataifa mengine, ni lazima kujipanga.

Tunaweza kuendelea kwa kukubali kuwa soko au na sisi kuzalisha na kuuza kwenye masoko mengine. China inakuja kwa kasi kwa kila kitu hadi mfumo wake wa sasa wa viongozi kutawala milele.

Tumejipanga vipi kupambana au kutembea na kasi hii mpya? Haya ndiyo ya kuganga yajayo kwa nguvu zote na si yale yaliyopita.

Tumefanya mengi, mazuri na mabaya kama jamii. Tumepitia historia ndefu kama taifa. Pamoja na historia yetu, bado Watanzania walio wengi ni maskini; bado hatujapata maendeleo ya kujivunia. Bado tunaomba misaada, bado tunashindwa kulinda na kusimamia raslimali za nchi yetu.

Bado elimu haitoshi, ingawa namba ya Watanzania waliomaliza darasa la saba inaongezeka mwaka hadi mwaka, na kwa msaada wa sekondari za kata, namba ya waliomaliza sekondari itaongezeka, bado kuna wanaopata elimu hii wakashindwa kuandika hata majina yao na kuzungumza sentensi ya Kiingereza;

Bado hatuna hata uwezo wa kujenga vyoo, tunasubiri misaada kutoka nje; bado hatuna uwezo wa kutengeneza barabara zetu; bado hatuna uwezo wa kuendesha maisha yetu wenyewe mpaka tupate misaada kutoka nje ya nchi.

Kama nilivyosema hapo juu, kuna mazuri na mabaya. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba tumeshindwa kabisa kujenga jamii inayojivuna, inayojiamini, inayoweka mbele maslahi ya Taifa.

Hata hivyo bado hatujachelewa, ndio maana ninasema yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yale yajayo. Baadhi yetu tunabaki kulaumu makosa ya nyuma, tunawalaumu viongozi waliopita badala ya kubuni mbinu mpya za kujenga jamii iliyo imara.

Kwa bahati mbaya, siasa zetu zimebaki kuyashughulikia yaliyopita. Tunapoteza muda, nguvu na raslimali nyingi kushughulikia yaliyopita. Tunapoteza muda mwingi kuwashawishi wapinzani kuingia chama tawala.

Wabunge na madiwani wanahama kwa kasi na tunatumia fedha nyingi kurudia uchaguzi. Tunaingiza taifa kwenye hasara kubwa kwa kuyashughulikia yale yaliyopita.

Wale wote wanaoitwa mafisadi, na wengine wako gerezani wakitunzwa kwa fedha zetu, wakati wao wana fedha nyingi na wanaweza kuchangia maendeleo ya taifa letu.

Lakini, wapo wanakula, wanatunzwa na akili zao zimedumazwa kule gerezani, badala ya kuwatumia na kuwakumbusha kuyaweka nyuma yaliyopita ili tugange yaliyopo na yale yanayokuja kesho.

Hawa tunaowaita mafisadi ni watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na wa kufanya biashara. Kinachohitajika ni kuwabadilisha na kuwaelekeza ili badala ya kuangalia maisha yao tu, waangalie maendeleo ya taifa nzima.

Kama tunataka kuganga yaliyopita, basi yatusaidie kujifunza na kusonga mbele. Ni lazima Watanzania wote kushiriki kulijenga taifa letu. Hata mafisadi, wakielekezwa vizuri watashiriki kulijenga taifa.

Ni lazima tuelekee siasa za kisasa, siasa za kisayansi. Ni muhimu kuangalia sifa na uwezo wa mtu zaidi ya kuangalia itikadi na chama chake cha siasa.

Dunia inabadilika na kila mtu sasa hivi anapambana kuliendeleza taifa lake na kuingia katika ushindani wa kuzalisha, kusambaza na kuuza. Hatuwezi kufanikiwa tukibaki kuganga yaliyopita.

Nimekuwa nikiongea juu ya jambo hili miaka yote. Kwamba ni lazima tujenge jamii yetu kwanza. Ni lazima tujenge jamii yenye kujiamini na kulitanguliza taifa. Mfano mzuri ni Marekani.

Kila anayepata nafasi ya kuitawala Marekani, kitu cha kwanza ni lazima asimamie wazo la msingi kwamba Amerika ni taifa lenye nguvu duniani, ni lazima alinde uchumi wa Marekani na ni lazima alinde uhai wa kila raia wa Marekani.

Ni lazima ahakikishe Amerika, ina chakula cha kutosha kwa miaka 50 au zaidi, ni lazima ahakikishe nchi ina mafuta ya kutosha, ina madini ya kutosha, ina maji ya kutosha, ina nishati ya kutosha. Haya ni ya lazima kwa kila chama cha siasa kinachoingia madarakani.

Pamoja na makosa yetu ya nyuma, ambayo mimi ninasema yamepita, sisi kama Watanzania tuna kitu gani cha kusimamia na kulinda kwa nguvu zetu zote? Tunalinda uchumi wetu? Tuna mafuta ya kutosha?. Tuna madini ya kutosha? Tuna nishati ya kutosha? Tuna chakula cha Kutosha?.

Je, tunalinda uhai wa raia wetu, vipi mauaji ya albino, mauaji ya vikongwe, vifo visivyokuwa vya lazima kama ajali ya MV Bukoba, ajali za barabarani, akina mama wanaokufa wakijifungua, watoto wanaokufa kwa malaria nakadhalika – ni matukio yanayotia shaka na kuacha alama ya kuuliza?.

Kama watu wanaanza kulikimbia taifa letu, kama tunavyosikia kwenye vyombo vya habari kwamba wengine wameanza kuomba ukimbizi wa kisiasa kwenye nchi za nje.

Watu wanapotea na hawaonekani tena, watu wanashambuliwa kwa risasi mchana kweupe, maiti zinakutwa kwenye viroba. Ni lazima tujiulize juu ya kuulinda uhai wa raia.

Hata kama ni mtu mmoja au wawili, uhai ni uhai, hakuna uhai ulio bora kuliko mwingine. Kila uhai ni lazima kulindwa kwa gharama yoyote ile.

Je, ni yapi tuliyokubaliana kuyalinda kwa nguvu zote, kuyalinda kwa umoja wetu?. Hata chama gani cha siasa kikiingia madarakani, tunahakikisha kinalinda yale tuliyokubaliana? Viongozi waje na kupita, serikali zije na kupita, lakini mambo muhimu na ya msingi katika jamii yetu yalindwe na kutunzwa.

Ni lazima tukubaliane wazi na iandikwe kwenye katiba yetu kwamba hakuna mwenye madaraka ya kuondoa uhai wa mwenzake, kwamba ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda na kutetea uhai wa watu wote, uhai wa viumbe vyote na kuyatunza mazingira yanayomzunguka.

Atakayetenda kinyume awajibishwe hata kama ni kiongozi wa nchi. Maadili bora ya watoto wetu na watu wetu yalindwe na kutunzwa.

Je, mipango yetu inalenga Tanzania ya miaka 100 ijayo? Maisha mazuri ya Wamarekani wa leo, yalitengenezwa na Wamarekani walioishi zaidi ya miaka 200 iliyopita. Na Wamarekani wa leo wanaandaa maisha mazuri ya vizazi vya miaka 300 ijayo.

Rais Obama alisema atahakikisha Amerika inakuwa nzuri kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Hivyo ndivyo na sisi tunapaswa kufanya. Taifa letu kwanza, mengine ya wataisoma namba baadaye.

Jinsi tunavyobuni na kuanzisha mambo mapya kama magazeti, redio, runinga, barabara za juu, reli ya kisasa nk, hivyohivyo tubuni mbinu za kujenga jamii yetu.

Ni lazima kwa pamoja tushikamane na kusema yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Tanzania yenye neema inawezekana kama tukishikamana na kulitanguliza taifa letu na kama tukipanga mipango ya miaka mingi ijayo.

Tukibaki kwenye visasi na kukumbuka hata waliotusukuma kidogo huko nyuma au waliotutukana na kutunyima tonge la ugali, tutabaki palepale tukinyonya kidole.

Kwa pamoja tuangalie mipango ya mbele, tuelimishane, tuelekezane, tushirikishane na kushikamana. Tutoe mawazo yetu na kuheshimu mawazo ya wengine, tukiwa na nia moja ya kuijenga jamii yenye kujiamini. Kwa pamoja, tuseme yaliyopita si-ndwele, tugange yaliyopo na yajayo.

Ni msemo mashuhuri wa WAHENGA: ‘Iliyopita si-ndwele tugange lijalo’ Watanzania wamebugi sana katika miaka mitano hii. Ila, ‘kufanya kosa si kosa, kosa ni kurudia kosa.’ Ni jukumu la CCM na Watanzania wengine wapenda amani ya kweli na umoja, 2020 kuepuka kurudia kosa, tusifanye makosa ya 2015.

Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere alisema hakuna maendeleo bila uhuru wa wananchi: “Ukitaka kuleta maendeleo lazima wananchi wawe huru ndani ya nchi yao. Watembee kwa uhuru bila ya hofu, waseme…wazungumze bila woga, bila hofu na bila vitisho.”

Padri Privatus Karugendo
+255 754633122
pkarugendo@yahoo.com

Tagsslider
Share: