Habari

Zanzibar Diaspora waandamana Umoja wa Mataifa

Na Mwandishi wetu Washington

Ikiwa imepita karibuni miezi miwili tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wa vyombo vya utendaji kukaribia kupata sura kamili kwa upande wa Bara, hali bado ni tete kwa upande wa Visiwani, na hadi leo bado matokeo ya uchaguzi hayajatangazwa.
Hali hiyo imepelekea mtafaruku wa kisiasa visiwani Zanzibar, na juhudi za nje na ndani zimekuwa zikiendelea katika kuupatia ufumbuzi mzozo huo.

Katika muqtadha wa juhudi hizo, Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA), mnamo tarehe 18 mwezi huu ilifanya maandamano kwenye viunga vya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Akizungumza kwenye maandamano hayo, Mwenyekiti wa ZADIA Bwana Omar Haji Ali, alisema kuwa maandamano hayo yanakuja katika juhudi za Jumuiya hiyo za kutafuta uingiliaji kati wa jamii ya kimataifa katika kuukwamua mgando wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Bwana Omar H. Ali alisema kuwa wapenda amani wote ulimwenguni ikiwemo jumuiya yake walishangazwa na kushtushwa na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ya kuufuta uchaguzi wote Visiwani humo.

“Wazanzibari, Watanzania na wapenda amani wote ulimwenguni ikiwemo Jumuiya yetu walishtushwa na kushangazwa na tangazo lisilokuwa la kisheria la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bwana Jecha S. Jecha la kufutwa Uchaguzi wa Zanzibar” alisema Bwana Ali na kuongeza kuwa Wataalamu wote wa Kisheria waliuelezea uamuzi huo kuwa hauna mashiko ya Kisheria.

Akimnukuu Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Cha Zanzibar Bwana Awadha Said Ali, mwenyekiti wa ZADIA alisema: “Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 119 (10), ili maamuzi ya ZEC yawe sahihi, ni lazima pawepo na kikao cha Tume hiyo, chini ya Uenyekiti wa Mwenyekiti wa Tume au Naibu wake, pamoja na wajumbe wasiopungua wanne”. “lakini hilo halikufanyika”, alisisitiza Bwana Ali.

“Maelezo hayo yanatiliwa nguvu na maelezo ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bwana Othman Masoud Othman ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika marekebisho ya Sheria na kanuni za Uchaguzi za Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi ya 1984” , alifafanua Bwana Ali.

Aidha, alisema kwamba maandamno hayo pia yana lengo la kumkumbusha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-moon ili kufuatilita zaidi hali inavyoendelea Visiwani Zanzibar.

“Katibu Mkuu wa Umaja wa Mataifa aliwapongeza viongozi na wananchi wa Watanzania kwa kufanikisha zoezi la uchaguzi kwa njia za amani.

Wakati huo huo alielezea wasiwasi wake juu ya hali ilivyo Zanzibar, na kuwataka wadau wote kujizuia kuchukua hatua zozote zinazoweza kupelekea uvunjifu wa amani”, alidokeza Bwana Ali. Alisema kuwa, Wazanzibari wengi wameitikia wito huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hata hivyo matukio ya hapa na pale ya uvunjaji wa amani yamekuwa yakiripotiwa.

“Moja kati ya matukio hayo ni yale yaliyotokea usiku wa kuamkia tarehe 13 mwezi huu, ambapo makundi ya watu wenye silaha za moto na za kijadi yalivamia maeneo kadhaa katika Mji wa Zanzibar na kusababisha hasara kubwa za mali”.

Halkadhalika Bwana Ali alinukuu baaadhi ya vipengele vya Mkataba wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, akisema kuwa hali inavyoendelea huko Zanzibar hivi sasa inakwenda kinyume na Mkataba huo, ikiwemo kuweko kwa wanajeshi mitaani, kitendo ambacho kinatia khofu raia na kuzorotesha harakati zao za kiuchumi.

Alitahadharisha kuwa iwapo hatua za mapema hazitochukuliwa, basi kuna hatari ya Ulimwengu kukabiliwa na janga la kiutu huko Zanzibar, kwani tayari kumekuweko na mfumko mkubwa wa bei za bidhaa muhimu hususan za chakula na kufikia zaidi ya 10% katika kipindi cha mwezi mmoja kufuatia Uchaguzi Mkuu Zanzibar.

Aliongeza kuwa “Wananchi wa Zanzibar wameshindwa kutekeleza haki yao kwa zaidi ya nusu karne sasa. Wakati umefika sasa kwa ulimwengu kuchukua jukumu lake kivitendo ili kuhakikisha kuwa sauti za Wazanzibari zinasikilizwa na kuheshimiwa”

Itafaa kukumbusha kuwa mnamo tarehe 21 mwezi uliopita, ZADIA iliandaa maandamano kama hayo kwenye Ikulu ya Marekani ya kumtaka Rais Barack Obama wa nchi hiyo kutekeleza ahadi yake aliyoitoa kwenye hotuba yake katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika jijini Adis Ababa, Ethiopia, mapema mwaka huu.

“Katika hotuba yake hiyo, Rais Obama alisema ‘.. pale ambapo raia hawawezi kutekeleza haki zao, basi ulimwengu una jukumu la kukemea. Na Marekani itafanya hivyo, hata kama wakati mwengine itakuwa inauma”

Tayari serikali ya Marekani imesitisha baadhi ya misaada yake kwa Tanzania, zikiwemo fedha za Changamoto za Milenia mpaka pale serikali ya nchi hiyo itakapoutatua mgogoro wa kisiasa Visiwani Zanzibar.

Kufuatia maandamano hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo alidokeza kuwa, iwapo hali itaendelea kubakia kama ilivyo, basi ZADIA itaelekea kwenye Umoja wa Mataifa. Katika maelezo yake kwenye maandamano ya jijini New York, Kiongozi wa Zadia alielezea kushangazwa kwake na sifa kemkem alizojichotea Rais mpya wa Tanzania kwa mwanzo mzuri wa Urais wake.

“Rais mpya wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amejizolea sifa nyingi kutoka kila pembe ya Dunia kwa mwanzo mzuri wa Urais wake, lakini linapokuja swala la mzozo wa kisiasa Zanzibar, amekaa kimya na hajachukua hatua yoyote” alisisitiza Bwana Ali.

Katika maandamano hayo yaliyowashirikisha pia wapenda amani na demokrasia kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni, waandamanaji walibeba mabango yaliyokuwa na maneno kama vile “Mshindi wa uchaguzi atangazwe”, “maamuzi ya Wazanzibari yaheshimiwe”, “bila haki hakuna amani’, “tunahitaji mabadiliko”, “Wazanzibari wamechoshwa na ukandamizaji”, na mengineyo.

Aidha, waandamanaji hao walisikika wakipiga walipiga makelele wakidai “tunataka matokeo yetu ya uchaguzi..”Itakumbukwa kuwa, wananchi wa Zanzibar walipiga kura mnamo tarehe 25 Oktoba mwaka huu, lakini Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bwana Jecha Salum Jecha akatangaza kufutwa kwa uchaguzi huo Mkuu visiwani humo, kitendo ambacho wataalamu wa Sheria wamesema kuwa kinakwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar.

Wachambuzi wanaona kuwa hatua hiyo ya Bwana Jecha ilikuja wakati asilimia kubwa ya matokeo yaliyokuwa yametangazwa yalikuwa yanampa ushindi mgombea wa urais wa Zanzibar kutoka chama cha upinzani cha Wananchi (CUF) Maliim Seif Shariff Hamad.

Kitendo cha kufutwa kwa uchaguzi huo ambao wachunguzi wa nje na ndani waliulezea kuwa ulikuwa wa haki na huru, kimezua mtafaruku wa kisiasa visiwani Zanzibar, na juhudi za ndani na nje zimekuwa zikifanyika ili kumaliza mgogoro wa kisiasa visiwani humo.

Kwa muda wa wiki kadhaa hivi sasa mazungumzo yamekuwa yakiendelea katika Ikulu ya Zanzibar kwa kuwashirikisaha Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohammed Shein, Makamo wake wa kwanza Balozi Ali Seif Idd na Makamio wa Pili ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.

Mazungumzo hayo ya siri pia yamewashirikisha Marais wastaafu wa Zanzibar, Bwana Ali Hassan Mwinyi, Dkt Salmin Amour na Dkt Aman Abeid Karume.

Usiri wa mazungumzo hayo umezaa tetesi kadha wa kadha katika mitandao ya kijamii, na kupelekea kuzaliwa kwa msimati mpya wa siasa za mitaani ujulikaonao kwa jina la “Drips”. Maandamano ya ZADIA ni katika juhudi za hivi karibuni kabisa za kimataifa za kusaka suluhu za mgogoro huo kwa njia za amani.

Kufuatia maandamno hayo, Mwenyekiti wa ZADIA aliwashukuru wale wote walioshiriki kwa kuitakia kheri Zanzibar, na karamu maalum ya chakula cha Mchana iliandaliwa kwa ajili ya washiriki wa maandamano hayo.

zanzibaryetu

picha zaidi

Tagsslider
Share: