Habari

Zanzibar hoi kidato cha sita

Thursday, July 17, 2014
Na Andrew Chale

WAKATI watahiniwa 38,905 sawa na asilimia 95.98 ya waliofanya mtihani wa kidato cha sita 2014 wakifaulu, Zanzibar imeangukia pua kwa kutoingiza shule hata moja kumi bora, badala yake shule zake nne zimekuwa kati ya kumi za mwisho.

Kati ya watahiniwa waliofaulu, wasichana ni 12,080 sawa na asilimia 97.66 na wavulana 26,825 sawa na asilimia 95.25.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), watahiniwa 41,968 waliandikishwa kufanya mtihani huo, lakini waliofanya ni 40,695, kati yao wa shule ni 35,418 na wa kujitegemea ni 5,277.

Akitangaza matokeo hayo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema kuwa watahiniwa wa shule waliofaulu ni 34,645 wakati idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 4,260.

Kuhusu ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja ya watahiniwa wa shule, alisema inaonyesha kuwa 30,225 wamefaulu katika madaraja I-III, wakiwemo wasichana 9,954 na wavulana 20,271.

Katika mtiririko huo, daraja la kwanza, wavulana ni 2,232, wasichana 1,541. Daraja la pili, wavulana ni 6,179, wasichana 3,452. Daraja la tatu, wavulana ni 11,860 na wasichana 16,821. Daraja la nne, wavulana ni 3,474, wasichana 946 huku daraja sifuri wavulana wakiwa 524 na wasichana 88.

Dk. Msonde alizitaja shule 10 bora kuwa ni Igowole ya Iringa, Feza Boys’ (Dar), Kisimiri (Arusha), Iwawa (Njombe), Kibaha (Pwani), Marian Girls (Pwani), Nangwa (Manyara), Uwata (Mbeya), Kibondo (Kigoma) na Kawawa (Iringa).

Shule kumi za mwisho katika ufaulu huo ni Ben Bella ya Unguja, Fidel Castro (Pemba), Tambaza (Dar), Muheza (Tanga), Mazizini (Unguja), Mtwara Technical (Mtwara), Iyunga Technical (Mbeya), Al-Falaah Muslim (Unguja), Kaliua (Tabora), na Osward Mang’ombe (Mara).

Dk. Msonde alisema kuwa ufaulu wa masomo kwa watahiniwa wa shule kwa masomo yote 14 ya msingi umepanda kulinganishwa na mwaka 2013.

Kwamba mwaka huu, ufaulu wa juu kabisa ni ule wa somo la Kiswahili ambalo asilimia 99.88 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Ufaulu katika masomo ya Sayansi (Fizikia, Kemia, Biolojia na Hesabu), umeendelea kuimarika kwa kulinganisha na ufaulu wa masomo hayo mwaka 2013.
Watahiniwa kumi bora

Dk. Msonde alisema watahiniwa waliofanya vizuri zaidi wamepatikana kwa kuangalia wastani wa alama (point), (GPA), kwenye masomo yatahasusi (combination), pamoja na wastani wa alama za jumla walizopata.

Aliwataja watahiniwa kumi bora hao kwa masomo ya sayansi kitaifa kuwa ni Isaack Shayo (St. Joseph Cathedral – Dar), Doris Noah (Marian Girls – Pwani), Innocent Yusufu (Feza Boys’ – Dar), Placid Pius (Moshi – Kilimanjaro), Benni Shayo (Ilboru – Arusha), na Abubakar Juma (Mzumbe – Moro).

Wengine ni Mwaminimungu Christopher (Tabora Boys – Tabora), Chigulu Japhaly (Mzumbe – Moro), Husein Parpia (Al-Muntazir Islamic Seminary – Dar) na Ramadhani Msangi (Feza Boys – Dar).

Matokeo ya ualimu

DK. Msonde, alitangaza matokeo ya ualimu akisema yamegawanyika makundi ya mtihani wa ualimu wa daraja la ‘A’, stashahada ya ualimu wa sekondari na stashahada ya ualimu ufundi.
Alisema kuwa watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani wa daraja ‘A’ ni 10,827, wasichana wakiwa 4,093 na wavulana 6,734.

Kwa mujibu wa Dk. Msonde, watahiniwa 10,695 wa ualimu daraja ‘A’ wamefaulu, stashahada ya ualimu 4,161 na diploma ya ualimu ufundi walifaulu wote watatu.

Chanzo : Tanzania Daima

Share: