Habari

Zanzibar ‘mguu mbele mguu nyuma’ hadi lini?.

El-Battawi
Jumapili, Novemba 19, 2017

WAKATI wa mjadala wa katiba mpya mwaka 2013/14, niliwahi kumsikia akijibu swali, Abubakar Khamis Bakari (Waziri wa Sheria na Katiba wa Serikali ya Umoja wa Kifaifa – SUK), kutoka kwa mjumbe mmoja wa Baraza la Wawakilishi, kuhusu uhalali wa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.

Abubakar, katika kujibu swali hilo kuhusu uhalali wa Muungano wa Tanzania, alisema: “Inawezekana hakuna nyaraka za kutosheleza na kuridhisha kuthibitisha uhalali wa Muungano wa Tanzania.”

“Lakini kwa taratibu za kisheria, jambo lolote LIKIZOELEKA KWA MUDA MREFU linakubalika ndani ya jamii, japo kuwepo kwa jambo hilo kuna utata na hivyo ndivyo ilivyo kwa muungano wetu,” alisema Abubakar na kuongeza:

“Ili kupata muungano halali wa maridhiano kwa watu wa Zanzibar na kwa watu Tanganyika, lazima kuwepo na mabadiliko makubwa ya katiba, itakayoweka wazi masuala yote muhimu ya muungano.”

Majibu ya Abubakar, yalikuja kufuatia swali la msingi lililoulizwa kuhusu utata uliyopo kwamba, hakuna nyaraka sahihi zinazoeleza kwa uwazi uhali wa muungaano na masharti yake.

Na kwanini nyaraka za muungano hazijawahi kuonekana, hata zinapohitajika na penye ulazima wa kuonekana, hazionekani au hazioneshwi kama kweli zipo?.

Dk Amani Abeid Karume, wakati mmoja aliwahi kunukuliwa akisema kwamba, amekaa Ikulu ya Zanzibar kwa miaka 10, hakuwahi kuziona nyaraka za muungano.

Ingawa baadaye naye, Dk Shein alinukuliwa akisema nyaraka za muungano ziko Ikulu ya Zanzibar, ndani ya makabati. Kwa kauli hizi mbili, hatujui tumuamini nani!.

Inapoelezwa kuwa akina Dk Shein na Profesa Mbarawa na wenzao wengine kuwa si Wazanzibari, inawezekana inaelezwa  hivyo kutokana wao wenyewe kushindwa kutetea maslahi ya Zanzibar.

Abubakar, kasema kuwa jambo lolote likiwepo kwa muda mrefu (likizoeleka) ndani ya jamii linakubalika na kuonekana kuwa ni halali ni la kweli, japo sivyo ilivyo.

Kwa uzoefu huo, ndiyo unawasaidia akina Dk Shein na Profesa Mbarawa, kuonakana Wazanzibari, ilhali sivyo. Je, wao-wenyewe wanautaka Uzanzibari?. Kwa sababu ya vitendo vyao havikuelekea kuwa na maslahi kwa Wazanzibari waliyowengi.

Hata hivyo, sidhani kuwa ni sahihi kuwa kiongozi wa Zanzibar, akashindwa kulinda maslahi ya Wazanzibari. Wanatumia nguvu kubwa ili Zanzibar, iendelee kutawali na Tanganyika. Hilo ndilo linalotiashaka na Uzanzibari wao.

Pengine, wanaamini maslahi yao yanalindwa na Tanganyika. Kwa hivyo, Zanzibar hata ikimezwa yote poteleambali, habari hawana,  wala haiwaumi. Maddam maslahi yao yako salama.

Watu kama Mzee Moyo (Hassan Nassor) na Shaaban Khamis Mloo na baadhi ya wenzao wengine NASABA zao ni kutoka Tanganyika lakini wame-‘declare’ kwa uwazi katika kulinda maslahi ya Zanzibar.

Mzee Moyo, anaposimama kwenye jukwaa anasema ‘Zanzibaaa kwanzaa.’ Ndiyo sababu wanakubalika Zanzibar, Uzanzibari wao hauna shaka. Hata iwe wazee wao wametoka Tanganyika, wao wanasimamia maslahi ya Zanzibar. Mzee Moyo ndiyo sababu ya kufukuzwa CCM.

Mwanzoni mwa miaka 1980, Aboud Jumbe, Rais wa Zanzibar awamu ya ll (Mwenyezi Mungu amsamehe dhambi zake, huko aliko), alijenga nyumba ya kuishi Kigamboni, Mjimwema Dar es Salaam, akaipa jina ‘MTU-KWAO’.

Nyerere (Julius Kambarage), baada ya kusikia taarifa za nyumba ya Jumbe ya Kigamboni, kuwa inaitwa ‘mtu-kwao’ alimwita, alimwambia jina la nyumba yake linatoa taswira mbaya kisiasa, hasa kwa Wazanzibari wenye misimamo mikali juu ya viongozi wa Zanzibar, na kuhusu Muungano.

Pomaja na kwamba Mzee Jumbe, alipokuwa katika madaraka hakuonekana kuwa na maslahi na Tanganyika. Kosa moja kubwa alilofanya ni kukiua ASP (Afro Shirazi Party), kitendo ambacho kafukiwa kaburini, kinamsononesha moyoni.

Mansour Yussuf Himid, Kada wa Chama cha Wananchi (CUF), nilimsikia katika mkutano mmoja uliyofanyika jioni kwenye eneo la nyumba za Michenzani, Unguja. Mansour anasema:

“Mimi muwarabu kweli kweli, kwa sababu nimetoka ndani ya mifupa na damu ya waarabu na hilo siwezi kulikanuka kwa sababu wazee wangu, nikimaanisha mama yangu ni muwarabu.”

“Lakini mimi najinasibu kwa nguvu zangu zote kuwa ni Mzanzibari kindakindaki, mbali ya kuwa nimezaliwa Zanzibar, lakini naipenda Zanzibar, nawapenda Wazanzibari na Wazanzibari kwangu ni daraja la kwanza.”

Maslahi ya Zanzibar, iwe mafuta, gesi, karafuu au raslimali nyingine za nchi hii mbele ya macho yangu ni mali ya Wazanzibari na yatawanufaisha Wazanzibari popote walipo ndani ya Zanzibar, Unguja na Pemba,” alisema Mansour.

Alisema: “Mimi ni muwarabu lakini ifahamike uwarabu wangu mnaposafiri kwenda nchi za arabuni, unaishia Chumbe au ‘Airport’ ya Kiembasamaki, nikifika uwanja wa ndege wa Muscat, ‘passport’ yangu ni ya rangi ya kijani.”

“Wala sijawahi kuinua mdomo wangu kuitetea nchi yoyote ya arabuni kwa sababu mimi najinasibu ni Mzanzibari na nitasimama pamoja na Wazanzibari wezangu katika suala lolote linalohusu nchi yetu,” alisema Mansour.

Pia, niliwahi kumsikia wakati mmoja Eddy Riyami anasema kuwa ni jambo la kushangaza kuwa Kiongozi wa Zanzibar, lakini kila kukicha anatetea maslahi ya Tanganyika.

Watawala wa zamani wa kifalme wa Zanzibar watatu nawakumbuka, Sayyid Khalifa, Sayyid Abdullah na Sayyid Jamshid ambao asili yao ni kutoka nchini Oman. Lakini katika awamu zote walizokaa kwenye madaraka wakiwa viongozi wa Zanzibar, walionesha mapenzi kwa Wazanzibari, si kwa raia wa Oman.

Kwa mfano: Ukikutana na Sayyid Jamshid mkazungumza, anazungumzia Zanzibar, hazungumzi mambo ya Oman kwa sababu Zanzibar ndiyo kwao alikozaliwa, ndiyo kwenye kaburi za wazee wake wote, baba yake, mama yake, babu zake na bibi zake na jamaa zake wengine. Zanzibar ndiyo kwenye kitovu chake. Viongozi wa sasa wa Zanzibar, utata mtupu, kuhusu nasaba zao.

Profesa Mbarawa, ndani ya Bunge Dodoma, anamsulubu Saada Mkuya, Mzanzibari kisa kasema ajira zote za TTCL upande wa Zanzibar, wapewe Wazanzibari. Hapo kosa la Saada, liko wapi?.

Anamsulubu kwa sababu kawatetea Wazanzibari, hakuwatetea Watanganyika. Kwani Saada Mkuya ni Mtanganyika au ndani ya bunge anawawakilisha Watanganyika?.

Halafu, anatokea mtu anazuia kulalamika kuwa Profesa Mbarawa na Dk Shein ni Wazanzibari kwa kuwa hatujaona vyeti vyao vya kuzaliwa. Cheti cha kuzaliwa si hoja, wala si shani!.

Profesa Mbarawa ametutukana na ametutukania wazee wetu wa Pemba vijijini kufuatia mfano wake ndani ya bunge alioutoa katika maelezo yake kuhusu madai ya Saada Mkuya.

Mzamzibari wa kweli ni yule anayewaoneahuruma, anayewapenda na kuwaheshimu Wazanzibari wenzie. Mzamzibari wa kuwaangamiza Wazanzibari, huyo ni adui wa Wazanzibari.

Sikubaliani nao, wanaoifananiza kauli ya Saada Mkuya, kuhusu ajira za TTCL kuwa ni kauli inayofaa kutolewa kwa mfano wa dharau na kejeli kwa Wapemba wa vijijini au watu wa kijiweni Darajani, Unguja. Maneno ya Profesa Mbarawa ni matusi kwa Wazanzibari wote.

Mohamed Hamed Seif Al Rumhy ni Waziri wa Oman wa Petrol na Gas, kazaliwa Mbuguwani, Mkoani kasoma Skuli ya Uweleni, Mkoani. Kwa ufupi, kazaliwa, kakulia na kasoma Mkoani, baada ya kuhamia Oman, anawatumikia raia wa Oman, kilillahi, wala hana habari tena ya Mkoani au ya Pemba.

Na hivyo ndiyo inavyotakiwa, huwezi kuwa kiongozi wa Oman, maslahi ya Waoman, raslimali zao zikawanufaisha Wadubai au Waabu-Dhabi au watu wengine wasiyokuwa wa Oman. Hilo haliwezekani.

Na kwa mifano hiyo ndipo tunapowapinga watawala wa sasa wa Zanzibar, wanakosa uchungu juu ya Zanzibar. Linapotokea suala la kuingamiza Zanzibar, hawasimami na Wazanibari kulipinga kwa pamoja.

Wanaonekana kusimama upande wa maadui dhidi ya Zanzibar, hawaungani na Wazanzibari wenzao katika kulisimamia kwa maslahi ya Zanzibar. Mfano ni wakati wa Bunge Maalum la Katiba. Hali iliyojitokeza.

Wakati viongozi wa Chama cha CUF, wanapodai Mamlaka Kamili ya Zanzibar, kwa maslahi ya Wazanzibari wote, wa leo, wa kesho na wa keshokutwa. Kwa maslahi ya sasa na kwa maslahi ya baadaye ya watoto, wajukuu, vitukuu na vilembwe, Dk Shein kama Nahodha Mkuu wa Wazanzibari na wenzake wengine, wanasimama kidete kuipeleka Zanziabr, Tanganyika. Ndiyo maana Uzanzibari wao, umejaa dosari.

Viongozi na wananchi wote kwa pamoja wanapaswa kusimamia maslahi ya nchi yao, huku akizingatia kuna vizazi mbele yake vitakuja vitahitaji kuwa na nchi yao.

Maandaliza ya ukombozi wa nchi kama Zanzibar, inayoelekea kumezwa yanatakiwa kuwaunganisha Wazanzibari wote kuwa pamoja, ili kuinusuru Zanzibar, isitokomee na kuwa ya Watanganyika.

Miaka 53 tangu mapinduzi, Zanzibar inadidimia katika kupoteza utaifa wake, inapoteza mamlaka yake. Zanzibar, hainonooki imekuwa nchi fukara na fakiri kwa sababu ya watawala FEKI, mamluki wanaoletwa kutoka Tanganyika.

Saada Mkuya, Mbunge kutoka Zanzibar, anashauri na kutetea katika bunge maslahi ya Wazanzibari, Profesa Mbaraka anamsulubu kwa maneno ya dharau na kashifa dhidi ya wazee wetu wa Pemba, waliyotuzaa. Hilo tabaan haikubaliki.

Hatuamini kuwa Profesa Mbarawa ni Mpemba, hakuna Mpemba anaweza kuwadharau wa-Pemba wenzie ‘Mtu Kwao.’ Profesa Mbarawa ni Mtwana wa Bara Tanganyika. Ndipo tunapata ile maana ya ‘Mdharau Kwao Mtwana.’

Kuhusu suala la uchumi: Kwani Zanzibar, inakabiliwa na tatizo la uchumi tu?. Zanzibar inakabiliwa na matatizo mengi na hasa tatizo kubwa ni la utawala uliyopo?.

Utawala ndiyo unaofanya nchi kuwa na uchumi nzuri, unaonawirika siku baada ya siku au vyenginevyo, utawala ukiwa mbaya haiwezekanai kuwa na uchumi imara unaostawi.

Utawala unaozingatia ‘haki za binadamu/utawala wa sheria’ utawala uliyobobea katika misingi ya demokrasia, mfumo imara wa utawala, mfumo imara wa bunge na mahakama na vyombo vya kusimamia sheria, huo ndiyo utawala unaweza kujenga uchumi nzuri na kufanyamaisha ya wananchi kuwa bora.

Kwa Zanzibar, ukiondoa tatizo la utawala uliyopo kuwa ni mbovu na usiyosikiliza madai ya wananchi wake yaani vipa umbele vyao kuna matatizo ya chuki za kisiasa zinazotengenezwa na mamlaka za utawala kwa lengo maalum na kwa makusudi.

Kuna suala la kisiasa, kuna suala la uchumi/biashra na suala la ustawi wa nchi yaani suala la maisha ya wananchi wa kawaida na ustawi wa jamii kwa jumla. Matatizo yote hayo yanabaraka za utawala.

Mwezi wa Februari 1984, Serikali ya awamu ya tatu ilipoanza chini ya Ali Hassan Mwinyi (Rais wa Zanzibar), Maalim Seif Sharif Hamad (Waziri Kiongozi) Zanzibar, Unguja na Pemba maisha ya wananchi yalikuwa katika hali mbaya.

Nchi ilikuwa haina hata chakula. Hospitali zilikosa dawa zilikosa na huduma za kitabibu, huku hakukuwa na huduma za nje za afya na maduka ya dawa.

Maisha ya watu yalikuwa magumu. Biashara za kawaida zilisuasua au zilikufa kabisa, hata za kuuza muhogo wa kuchoma na maandazi, zilipotea. Nchi ilikuwa inaelekea kudamirika.

Miezi mitatu ya kwanza tangu serikali ya awamu ya tatu kushika hatamu, sura ya mji wa Zanzibar, ilianza kubadilika taratibu kadiri siku zilivyokwenda. Serikali ikafungua milango, watu wakaanza kufanyabiashra.

Biashara zote zilianza kuibuka. Biashara za maduka, mbali maduka ya chakula, maduka ya nguo maduka ya vifaa vya kujengea, biashara ya gari za abiria kwa manispaa ya Unguja mjini (daladala). Na miji yote Pemba, usafiri ukawa rahisi.

Ni mwaka huo, ambao wananchi wa Zanzibar, walianza kujenga nyumba za matofali na bati, nyumba nzuri angalau kuweza kuishi binadamu na kustirika, bila kuvujiwa.

Wazanzibari wafanyabiashara wakaanza kusafiri nje na kuleta nchini aina zote za bidhaa na nguo. Zanzibar, ikawa ndiyo soko kuu la biashara ndani na nje ya Tanzania. Biashara ya vioski vya kuuza chips/mishakaki na urojo ikaenea.

Nchi ikanawirika ndani ya miezi mitatu, nchi ikaonekana kuwa na utawala bora uliyofuata sheria na demokrasia, uliyozingatia haki za binadamu. Japo mfumo wa siasa ulikuwa wa chama kimoja, uliridhisha sana.

Watu walitulia, baadhi ya watu waliyokuwa wamehama, au niseme waliyokuwa wamekimbia shida za maisha walirejea haraka wakaishi kwa furaha.

Maisha ya wananchi wa Zanzibar, yalibadilika na watu wakanza kumiliki milo mitatu kwa siku. Nyuso za watu zikajaa furaha, tabasamu na bashasha.

Utamaduni na Hulka za Kizanzibari, vikarejeshwa kwa haraka na kuimarika. Ngoma za asili ikiwemo vikundi vya taarabu zikafufuka.

Kikundi kipya cha taarab kilianzishwa, (East African Melody) ambacho awali kilikuwako Dubai, wakahamia Unguja, chini ya Haji Momamed (Mwenyezi Mungu amsamehe dhambi zake). Ngoma za Bale kutoka nchini Guinea na aina ya utamaduni wa kigeni, vikafutwa, vikapotea.

Viongozi walijikita kuwatumikia wananchi, walionesha kwa wananchi imani, huruma na unyenyekevu kwa dhati. Na wananchi walijisikia kuwa wamo ndani ya nchi yao, waliamini wana serikali inayowathamini.

Kwa ufupi, hali za watu zilinonooka kwa muda mfupi. Hakukuwa na kauli za viongozi za kejeli, ubaguzi na vitisho. Zanzibar, ilikuwa kama ile aliyoisema Sitti binti Saad: ‘UNGUJA NI NJEMA ATAKAYE AJE’

Chakula kiliagizwa haraka haraka na kwa wingi. Biashara ya nguo ilinawiri, ule mtindo wa watu kuvaa nguo sare ulitoweka. Watu walianza kuvaa nguo tofauti kila mtu kwa uwezo wake. Wazanzibari, walisahau kabisa dhiki na ubaya wa watawala wa awamu zilizopita.

Mitaa ya Darajani kuelekea Kiponda, ilibadilika kwa kulifunguliwa maduka makubwa ya nguo na manukato. Duka la kwanza kubwa lilipewa jina la DUBAI, lilikuwepo Kiponda.

Mitaa ya Shangani kuelekea Darajani kwa kukatishia Hurumzi na Kwa Saleh-Madawa, yote ilikuwa imesheheni maduka ya nguo. Maduka yakuuza dagaa na tumbaku katika mitaa wa Mbuyuni, Mchangani na Mlandege, taratibu yalitoweka.

Kupata mlango wa biashara katika mitaa hiyo ilikuwa ni kimbembe. Ilikuwa haiwezekani kupata mlango wa kufanya biashara bila kutoa kilemba, tena kuanzia mamilioni ya shingi.

Shughuli za biashara hazikuwa na bugudha za TRA/ZRA na upuuzi mwingine, kama ilivyosasa. Wafanyabiashara kutoka nje ya Zanzibar, kama Tanganyika, Burundi na Comoro, walifika kwa misururu kufuata biashara.

Serikali ilionekana kudhibiti na kuwa katika ustawi nzuri wa uchumi wake. Wafanyakazi wa serikali walifanyakazi kwa nidhamu sana. Wananchi waliishi bila ubaguzi, bila chuki na dharau na bila vitisho.

Polisi na vikosi vya SMZ, vilifanyakazi zao kwa kufuata sheria na uadilifu. Vikosi vya usalama havikuonekana kiholela, kuwasumbua wananchi mitaani, hasa majira ya usiku kama ilivyo siku hizi.

Kwa ufupi, Zanzibar ilikuwa imeshaelekea kurejea ile Zanzibar ya KALE, kabla ya Januari 12, 1964. Kuondoka tu kwa Ali Hassan Mwinyi na Maalim Seif, Zanzibar ikajikuta katika hali tete.

Wapemba wakafukuzwa kazi na Maskulini na Vyuoni, wakavunjiwa nyumba zao. Sheikh Kurwa,  Mpemba wa Msingini, Chake Chake, akahamishiwa Tabora, Tanganyika. Kwa sababu alikuwa hakubaliani na siasa za Dk Salmin.

Kila siku zikienda mbele Wazanzibari, wanapandikizwa chuki. Hali mbayo inachangia nchi kudumaa katika hali ya umasikini na ufukara.

Namaliza kwa suala la uchumi: Zanzibar kwa udogo wake na kwa uchache wa wananchi wake, inaweza kujiendesha vizuri tu kiuchumi bila kuyumba kutokana na raslimali zake. Zanzibar, inahitaji uongozi bora, na mifumo mizuri ya kiutawala.

Zanzibar, viongozi wake siku ambayo wataamua kuachana na siasa uchwara za Tanganyika, siasa za chuki, uonevu na ubaguzi na kujikita katika kujenga nchi yao, wataondokana na hali mbaya ya maisha inayowakabili.

Hilo limo katika mikono ya watawala. Watawala wakibadilika nia zao wakawa wazuri kwa wananchi, nchi itaondokana na balaa zote pamoja na umasikini, itasonga mbele. Viongozi Wakuu wa Zanzibar, waachane na undumilakuwili, ili wananchi waishi kwa furaha..

Tagsslider
Share: