Habari

Zanzibar waipiga TRA mkwara

01 Feb, 2012, Na Mwinyi Sadallah

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imetangaza kuwatimua kazi watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kanda ya Zanzibar kutokana na kushirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi na kuikosesha serikali mapato.

Hayo yalitangazwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yusuph Mzee, katika mkutano wa dharura na uongozi wa TRA, uliofanyika makao makuu ya wizara hiyo, Vuga, mjini hapa.

Alisema hatua hiyo italazimika kuchukuliwa baada ya kesi tatu za ukwepaji kodi kubainika katika kipindi cha Januari, mwaka huu, katika Bandari ya Malindi, Wete na Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume.

Alisema SMZ imegundua kuwa kuna vitendo vya makusudi vya ukwepaji wa kodi vinavyofanywa na wafanyabiashara wakishirikiana na maafisa wa TRA Zanzibar.

“Msidhani kwa kuwa ninyi ni waajiriwa wa Serikali ya Muungano, basi SMZ haiwezi kuwafukuza kazi, msijidanganye, tuna uwezo huo na ustahimilivu sasa basi, nitawafukuza halafu nimwone kiongozi gani wa Jamhuri ya Muungano atakayewarejesha tena,” alisema Mzee.

Alisema Januari 23, meli ya MV. Safina Alshahejaan iliyokuwa ikitokea India na kupitia Mombasa nchini Kenya, iliteremsha tani 375 za sukari katika Bandari ya Malindi, sawa na magunia 10,000 ya kilo 50 kila moja, lakini ni magunia 4,000 tu ndiyo yaliyolipiwa kodi.

Waziri Omar alisema sukari hiyo imeingizwa Zanzibar na kampuni ya Ms Sasco Tanzania Ltd na kusema lazima ilipe faini ya dola 10,000 za Marekani na kodi zote ambazo walipaswa kulipa.

Aliongeza kuwa ukwepaji wa kodi umefanywa kwa makusudi na maafisa wa TRA, kwa manufaa yao binafsi wakati Zanzibar inakabiliwa na matatizo mbalimbali ya kiuchumi.

Alisema kesi nyingine kama hiyo, imetokea katika Bandari ya Wete visiwani Pemba baada ya magunia 13,000 yenye ujazo wa kilo 50 kila moja, lakini magunia 7,000 pekee ndio yaliyolipiwa kodi.

“Kama mmezoea kuchezea chezea viongozi, mimi sio wa kuchezewa, hasa katika masuala ya ulipaji wa kodi, kabla ya mimi kufukuzwa na Rais, nitaanza kuwafukuza ninyi kwanza, kwa sababu Rais ameahidi kuwaletea wananchi maendeleo na hawezi kutekeleza bila ya kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato,” alisema.

Aliongeza: “Na jambo la kusikitisha ni kuwa muda wote huu mnakusanya Shilingi  bilioni sita kwa mwezi, isipokuwa Desemba mlikusanya Shilingi bilioni nane, mmeshindwa kufikia hata nusu ya mapato yanayokusanywa na Bodi ya Mapato Zanzibar ambao wanakusanya Sh. bilioni 13 kwa mwezi,” alisema Mzee.

Alisema Serikali imegundua mizigo inateremshwa siku za mapumziko ya mwisho wa wiki, kwa vile huwa hakuna watendaji na wafanyabiashara hupunguza kwa makusudi kiwango cha mzigo walichoingiza licha ya nyaraka za usafirishaji mzigo kutofautina na malipo wanayolipia kutoa mzigo.

Alisema maafisa wote waliohusika watachunguzwa na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

“Serikali imewapangia mishahara mizuri ili mtekeleze vyema wajibu wenu, watumishi wa TRA mnashika nafasi ya pili kati ya wafanyakazi wa Serikali wanaolipwa mishahara mikubwa,” alisema.

Alisema SMZ imegundua wafanyabiashara wamekuwa wakiteremsha shehena za mizigo katika Bandari ya Mombasa, Kenya na kuingiza katika Bandari ya Wete, Pemba ikiwa nusu nusu (loose cargo) na kwa kushirikiana na maafisa wa TRA wanafanya udanganyifu kwa kupunguza uzito wa mzigo.

Aidha, alisema katika uwanja wa ndege, watu wamekuwa wakiingia na bidhaa mbalimbali zikiwemo simu za mikononi, hasa zilizotumika bila ya kulipia ushuru na kuwaathiri wafanyabiashara wengine wanaoingiza bidhaa hizo kwa njia halali.

Mara baada ya taarifa hiyo ya kashfa ya ukwepaji kodi, Waziri Omar alimtaka Naibu Kamishna wa TRA Kanda ya Zanzibar, Mcha Hassan, kuwaeleza waandishi wa habari sakata zima la ukwepaji kodi na waliohusika na hatua zilizochukuliwa hadi sasa.

Hassan alisema Kampuni ya Ms Sasco, ilishapewa adhabu ya kulipa Sh. milioni 3.9, kiwango ambacho kilipingwa na Waziri na kumtaka arudi tena akatoe adhabu ya dola 10,000 za Marekani kama sheria inavyoelekeza na kuwasilisha kwake ripoti ya matukio yote.

Alisema kesi ya Bandari ya Malindi na Wete inaendelea kushughulikiwa kwa kuzingatia taratibu za kisheria lakini alisema hadi jana hakuna mfanyakazi yeyote ambaye alisimamishwa kazi kutokana na sakata hilo.

“Hakuna aliyesimamishwa kazi, tunaendelea kushughulikia haya mambo kwa kufuata taratibu,” alisema Kamishna huyo.

Kesi za ukwepaji kodi Zanzibar, ni za kwanza kujitokeza tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya saba, ambayo imedhamiria kuziba mianya yote ya ukwepaji wa kodi hasa misamaha ya kodi ambayo imekuwa ikitumika Zanzibar kunufaisha wafanyabiashara badala ya wananchi.

CHANZO: NIPASHE
Share: