Habari

Zanzibar wawekwa kitimoto Dodoma

Dodoma.Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) juzi jioni walipata wakati mgumu katika kikao cha ndani cha wabunge wa chama hicho wakituhumiwa kwa ‘usaliti wa Muungano’.

Kilichowaponza wajumbe hao ni kupitisha mabadiliko ya Katiba mwaka 2010 yanayoitaja Zanzibar kuwa ni nchi na hivyo kuvunja Katiba ya Muungano na kitendo cha baraza hilo kupendekeza Serikali tatu mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kikao hicho kilifanyika muda mfupi baada ya Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba akieleza kuwa changamoto kubwa za Serikali mbili ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, uliotokana na Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Katika hotuba yake, Jaji Warioba alisema pia kuwa baraza hilo lilipendekeza mfumo wa Serikali tatu kutokana na maelezo kuwa linataka Zanzibar huru, Tanganyika huru na Serikali ya Muungano huru na kila chombo kuwa na mamlaka yanayotambuliwa.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, zinaeleza kuwa wabunge wa CCM hasa wa Bara walielekeza lawama kwa viongozi wa Zanzibar hasa Baraza la Wawakilishi kutokana na kuwasaliti.

Chanzo chetu kimemtaja mmoja wa wazungumzaji, Christopher Ole Sendeka kwamba alieleza kwa uchungu kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Zanzibar ni usaliti mkubwa kwa Serikali ya Muungano.

“Sendeka aliongea kwa uchungu kuhusu Zanzibar kuvunja Katiba ya Muungano na alisema lazima chama kichukue hatua ili kunusuru Muungano,” alisema mjumbe mmoja wa kikao hicho.

Alipoulizwa kuhusu kauli hizo, Sendeka hakukanusha wala kukubali, bali alisema hayo ni masuala ya kikao cha ndani na hawezi kuyazungumzia.

Mbunge mwingine aliyetajwa kuzungumza ni Silivester Mabumba wa Jimbo la Dole, ambaye alieleza wazi kuwa ni vyema kuacha unafiki kuwa mnataka Serikali mbili wakati kuna mabadiliko ambayo mmepitisha kuwa Zanzibar ni nchi. Hata hivyo, Spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi, Pandu Amir Kificho baada ya kushambuliwa alieleza kutofautiana na kile ambacho kimeelezwa katika hotuba ya Jaji Warioba.

Kificho, licha ya kukiri kuwa mmoja wa waliosaini taarifa ya baraza hilo, alisema bado msimamo wa baraza ulikuwa ni Serikali mbili. Kauli hiyo ilithibitishwa jana baada ya kufafanua katika kituo kimoja cha televisheni kuwa msimamo wa baraza haujawahi kuwa ni Serikali tatu.

Baada ya lawama nyingi, inadaiwa wajumbe hao, walifikia azimio la kuandaa utaratibu wa kufanyia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar kupitia kura ya maoni.

“Tumewaambia waone uwezekano wa kuifanyia marekebisho Katiba yao kama ukipitishwa muundo wa Serikali mbili,” alisema mjumbe mmoja.

Wawakilishi CUF wapinga

Hata hivyo, akizungumza na mwananchi jana, Ismail Jussa, ambaye ni mwakilishi kutoka CUF, alisema wamesikia maazimio ya kikao cha CCM lakini hawatakubali Katiba kufanyiwa marekebisho.

Jussa alisema mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, yalifuata sheria na kanuni na siyo rahisi kubadilishwa kama viongozi wa CCM wanavyofikiri.

Naye Mbunge wa Ole (CUF), Mohamed Mbaruku alisema iwapo CCM ikishinikiza kufanyika mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, suala hilo watalifikisha mahakamani.

“Tumepata taarifa ya kikao chao, lakini tunawaonya wasilete vurugu Zanzibar. Makubalino ya mabadiliko ya Katiba ni sehemu ya mwafaka wetu, sasa wakileta hoja zao tutafika mahakamani,” alisema Mbaruku.

Hotuba ya Warioba yawatibua

Kinachoonekana wazi ni kuwa hotuba ya Jaji Joseph Warioba imelivuruga baraza hilo hasa baada ya kueleza kwamba kiini cha tume kupendekeza Muungano uwe wa Serikali tatu ni pamoja na maoni ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kificho jana alikana maoni hayo ya kutaka serikali tatu na kwamba kilichoelezwa na Jaji Warioba siyo tafsiri sahihi ya mapendekezo yao.

“Hii inaonyesha kwamba Tume yenyewe ilishakuwa na mwelekeo wa serikali tatu kwa sababu kama alivyoeleza Jaji Warioba kwamba walitafsiri maoni yetu kuwa ni yenye kuhitaji serikali tatu, na wakati mwingine, tafsiri inaweza kukupa maana tofauti na maana halisi,” alieleza Kificho alipohojiwa na TBC1.

Kificho alisema baraza hilo linaundwa na wawakilishi kutoka vyama mbalimbali – CCM na CUF na msimamo wa CCM ni serikali mbili na hana uhakika kwa upande wa CUF, ingawa anadhani ni msimamo wa serikali tatu. Hivyo ni vigumu kudai Baraza la Wawakilishi limepeleka mapendekezo yenye msimamo mmoja.

Maoni ya Kificho yalipingwa na Mwakilishi Rufai Said Rufai aliyesema kuwa alichosema Jaji Warioba ndicho kilichomaanishwa na baraza.“Ingawa sikuwa mjumbe katika Kamati ya Uongozi, kwa nafasi yangu ya uwakilishi, naafikiana kuwa maoni yaliyosomwa na Jaji Warioba bungeni ndiyo haswa tuliyopeleka na jinsi alivyoyatafsiri ndivyo tulivyomaanisha,” alieleza Said.

“Unaweza vipi kukana kudai serikali tatu, wakati unatoa maoni yanayodai kuwapo kwa mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano yaliyowekwa wazi maeneo, uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya kila mamlaka? Wanaokataa, wanakataa wanachokubali,” alifafanua Said.

Mjumbe mwingine ambaye yumo kwenye Kamati ya Uongozi, Abdallah Juma Abdallah alisema anayekana kauli ya Jaji Warioba hana akili na anajikanyaga.

Imeandikwa na Sharon Sauwa na Mussa Juma.

mwananchi

Tagsslider
Share: