Habari

Z’bar kuadhimisha siku ya madola

March 10, 2018

NA KHAMISUU ABDALLAH

CHAMA cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola na Chama cha Wabunge wanawake wa Mabunge ya jumuiya hiyo matawi ya Zanzibar, wanakusudia kuadhimisha siku ya Jumuiya ya Madola, ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 12 ya kila mwaka.

Akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Mwenyekiti wa chama hicho, Simai Mohammed Said, alisema katika maadhimisho hayo wameandaa bunge la vijana Zanzibar litakalowashirikisha wabunge 50 wenye umri usiozidi miaka 30 ambao wanatoka katika mabaraza ya vijana ya Unguja na Pemba.

Alisema, kuanzishwa kwa bunge la vijana ni maazimio maalum ya mabunge ya Jumuiya ya Madola kuhakikisha kila bunge linaanzisha bunge la vijana kwa ajili ya kuchukua mawazo, fikra na uwezo wa kujenga hoja kutoka kwa wabunge waliokuwepo kwenda kwa vijana ambao ndio sehemu kubwa katika jamii.

Aidha, alisema bunge hilo litazungumzia masuala ya demokrasia ya kibunge na utawala bora na mambo mengine yatafanyika ikiwemo hati za kuwasilisha mezani, hoja binafsi, muswaada wa serikali unaogusa elimu ambao lengo lake kubwa ni kuimarisha elimu ya Zanzibar na hoja binafsi ya ushiriki wa vijana katika uchumi.

Aidha, alisema Baraza la Wawakilishi Zanzibar limekuwa likiandaa bunge la vijana tokea mwaka 2013 ikiwa na lengo la kuandaa jukwaa maridhawa la kuwandaa vijana kuwa viongozi bora katika kujenga hoja, kujadili kwa nidhamu, kushirikiana, kufahamu na kufuata taratibu za kibunge.

Alisema bunge hilo ni muendelezo wa azimio la chama hicho kuwalenga vijana na kuwajengea uwezo wa kujenga hoja, kuilinda na kuitetea hoja wanayoijenga.

Hata hivyo, alisema kabla ya kilele hicho, Machi 10 hadi 11 kutakuwa na mazoezi ya pamoja ambapo vijana hao watafuzwa masuala ya kanuni za kibunge na utaratibu wa majadiliano utakaoambatana na uchaguzi wa viongozi mbalimbali watakaoliendesha bunge hilo.

Alifahamisha kupitia ujumbe wa mwaka huu wa siku ya Jumuiya ya Madola unaosema “Kuelekea hatma ya pamoja” wanatarajia kupata mambo mbalimbali ikiwemo kuongeza uelewa wa vijana kuhusiana na mada na masuala yatakayojadiliwa na kuwajengea vijana moyo wa kizalendo, kushirikiana, stadi za uongozi na kujiamini.

Zanzibarleo

Share: