Habari

Z’bar sasa ijielekeze katika Mapinduzi ya kiuchumi

Jumanne,Januari13 2015 saa 16:14 PM

Wazanzibari jana waliadhimisha kumbukumbu ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa nderemo, vifijo na shamrashamra za kila aina. Siku hiyo hakika ni ya kukumbukwa, kwani miaka 51 iliyopita wananchi wa Zanzibar waliuangusha utawala dhalimu wa Kisultani uliokuwa ukiwakandamiza na kuwadhalilisha kwa miongo mingi katika nchi yao wenyewe.

Tunatoa pongezi za dhati kwa Wazanzibari na Watanzania wote kwa jumla kwa kuadhimisha siku hiyo muhimu katika historia ya pande zote mbili za Muungano. Tunawapongeza pia kwa kudumisha amani na udugu miongoni mwa wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa miaka yote hiyo 51, kwani tunafahamu kwamba safari ndefu ya miaka 51 aliyoianzisha mwasisi wa taifa hilo, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, haikuwa rahisi. Kumekuwapo changamoto nyingi za hapa na pale kiasi cha wakati mwingine kutishia umoja wa kitaifa wa Wazanzibari.

Yote hayo yalikuwa mapito. Jambo muhimu hivi sasa ni Wazanzibari wenyewe kujadili jinsi ya kusonga mbele na kuhakikisha hawarudii makosa ambayo yalisababisha matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na kugharimu maisha ya baadhi ya wananchi. Sisi wa Mwananchi tunaiona siku hiyo kama fursa pekee ya kutafakari Wazanzibari walikotoka, walipo na wanakokwenda, kwa maana ya kila mmoja wao kujiuliza ametoa mchango gani katika kulinda matunda ya Mapinduzi hayo katika miaka yote hiyo 51.

Pia ni wakati wa watawala waliopo sasa kubaini changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii ambazo zimewakwaza Wazanzibari kusonga mbele kimaendeleo kiasi cha kuwafanya baadhi yao kuishi maisha ya umaskini na ufukara uliopitiliza. Hotuba zilizotolewa na viongozi wakuu wa Zanzibar jana zilitoa kila aina ya matumaini kwa wananchi katika nyanja zote za ustawi wa jamii. Lakini kama ambavyo wananchi wamekuwa wakishuhudia, ahadi nyingi zinazotolewa katika hotuba za viongozi katika kumbukumbu za Mapinduzi zinazosherehekewa kila mwaka zimekuwa za kisiasa zaidi kutokana na kutofuatiwa na utekelezaji.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inayoundwa na vyama vya CCM na CUF imesaidia kuitoa Zanzibar katika maangamizi yatokanayo na siasa za chuki na visasi, kwani ndizo zimekuwa chanzo cha vurugu na machafuko visiwani humo. Hilo ni jambo la kujivunia. Kinachosubiriwa sasa ni vyama hivyo kujumuisha sera zake za kiuchumi ili kujenga uchumi wa Zanzibar, ambao umedumaa na kusababisha sekta nyingi, ikiwamo ya utalii kudidimia. Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ya Novemba mwaka jana imesema Zanzibar ilikuwa na nakisi ya Sh1.7 bilioni katika bajeti yake kutokana na kiwango cha ukusanyaji kodi kuporomoka kwa asilimia 13.3 mwezi uliotangulia.

Kama lengo la Mapinduzi lilikuwa ni kuwakomboa wanyonge kutoka katika minyororo na utumwa chini ya utawala wa Kisultani, lazima viongozi wahakikishe lengo hilo linafikiwa kwa kukuza uchumi. Kwa jinsi hali ilivyo Zanzibar, yanahitajika Mapinduzi ya kiuchumi ambayo utekelezaji wake utaleta nafuu kwa maisha ya Wazanzibari kwa sasa na siku zijazo. Mapinduzi hayo yamwezeshe kila Mzanzibari kuishi maisha bora yanayolingana na thamani ya utu wake. Hii inawezekana iwapo tu viongozi katika SUK wataweka kando itikadi zao za kisiasa na kutumikia wananchi bila ubaguzi. Safari ya kujenga uchumi wa Zanzibar ni ndefu, lakini kama wahenga walivyosema, safari ya maili 100 huanza na hatua moja.

Mwananchi

Share: