Habari

ZBC yashauriwa kutumia nyimbo za kale kutoa elimu

August 28, 2018

NA KHAMISUU ABDALLAH

WIZARA ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) limeshauriwa kutumia nyimbo za zamani zenye kutoa mafunzo ili kuwarejesha vijana katika mila, silka na utamaduni wa nchi yao.

Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi,Omar Seif Abeid, alitoa ushauri huo wakati akichangia taarifa ya utekelezaji wa malengo na majukumu ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika Ukumbi wa Wizara hiyo Kikwajuni.

Alisema, ikiwa shirika hilo litarejesha utaratibu wa upigaji wa nyimbo hizo katika vyombo vyake vya habari, basi vijana wataweza kubadilika na kuacha kuiga tamaduni za nchi za kigeni.

“Utamaduni, silka na mila za kizanzibari zinapotea kwa kasi katika zama hizi kutokana na vijana wetu kuiga tamaduni za kigeni na kuacha tamaduni zao za asili, lakini tukiweza kurejesha nyimbo zetu zile na vijana wakiweza kuzisikia basi naamini wanaweza kubadilika,” alisema.

Mbali na hayo aliipongeza kamisheni ya utalii kwa kuanzisha mfumo wa kutangaza utalii kupitia michezo mbalimbali.

Zanzibarleo

Share: