Habari

ZEC yakabidhi mwakilishi mteule cheti cha uthibitisho wa ushindi

October 29, 2018

NA IS-HAKA OMAR

MWAKILISHI mteule wa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande jana amekabidhiwa rasmi cheti cha udhibitisho wa ushindi kwa nafasi ya uwakilishi wa jimbo hilo.

Hafla hiyo imefanyika katika ofisi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wilaya ya mjini iliyopo Maisara na kuudhuriwa na viongozi na wanatendaji wandamizi Tume hiyo na CCM.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa cheti hicho, Mwakilishi huyo mteule, aliahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kwa kufuata miongozo na taratibu zote za kisheria kwa maslahi ya wananchi wote wa jimbo hilo.

Aliwashukuru wananchi na wanachama wa CCM wa jimbo hilo kwa kumpatia ridhaa ya kuongoza jimbo hilo kupitia utaratibu halali wa kidemokrasia.

“Nitawatumikia kwa uadilifu wananchi wote wa Jang’ombe bila ya ubaguzi wowote, kwani naamini bila nyinyi kuridhia kunipa nafasi hii nisingeweza kushinda katika mchakato huu wa kisiasa uliokuwa na ushindani mkubwa.

Alisema ameshakabidhiwa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 na kwamba huu ni wakati wa kutekeleza mpango kazi wa kutekeleza ahadi alizowaadi wananchi wa jimbo hilo wakati wa kampeni.

Kwa upande wake aliyekuwa Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Jang’ombe ambaye pia ni ofisa wa ZEC wilaya ya Mjini, Mwanapili Khamis Mohamed amemsisitiza kiongozi huyo kufanya kazi zake kwa majibu wa taratibu na kanuni za kisheria ili kutimiza matakwa ya wananchi waliomchagua.

Mwakilishi huyo ameshinda nafasi hiyo kwenye uchaguzi uliofanyika juzi ambapo alipata kura 6,581 sawa na asilimia 90.5 katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Jang’ombe.

Uchaguzi huyo uliovishirikisha vyama tisa, ulifanyika katika mazingira ya amani na kwamba hakukuripotiwa kujitokeza matukio ya uvunjifu wa sheria za uchaguzi na nchi kwa ujumla.

Zanzibarleo

Share: