Habari

Zipo dalili za kuwepo mafuta, gesi Zanzibar

AUGUST 6, 2018 BY ZANZIBARIYETU

MKURUGENZI Muendeshaji wa Mamlaka ya Uthibiti, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia (ZPRA), Omar Zubeir amesema upo uwezekano mkubwa katika visiwa vya Unguja na Pemba kuwepo kwa nishati ya mafuta na gesi asilia.

Alisema hilo limebainika katika utafiti unaoendelea ndani ya visiwa hivyo, ambapo kwa upande wa kisiwa cha Unguja utafiti wa nchi kavu umekamilika huku kisiwani Pemba ukiwa unaendelea.

Alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Forodhani mjini hapa.

Kuhusu uchimbaji na shughuli nyengine zilizobaki alisema, zitaanza rasmi baada ya kuingia mkataba na kampuni husika na kwamba mkataba huo unaitwa “Production sharing agreement” (PSA).

Alisema utafiti ulianza rasmini Machi mwaka 2017 kwa kurusha ndege ya uchunguzi angani baadae likaendelea zoezi la mtetemo baharini lililofanyika Oktoba 28 hadi Novemba 28 mwaka huo ambapo jumla ya mistari 66 yenye urefu wa kilomita 2,886.

Alisema katika maeneo ya nchi kavu zoezi hilo lilifanyika kisiwa cha Unguja Febuari 2018 na kukamilika mwezi Mei, 2018 kwa utafiti wa mistari 12 yenye urefu wa kilomita 380.

Aidha alisema, zoezi hilo linaendelea kufanyika katika kisiwa cha Pemba kuanzia Julai 18 mwaka 2018 ambapo jumla ya mistari 14 yenye urefu wa kilomita 309 unategemea kufanyiwa utafiti huo.

Aidha alihimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika suala zima la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesiasili nchini, pamoja na kuiamini serikali yao kwani hakutokua na usiri katika suala hilo hasa ikizingatiwa ni rasilimali ya Zanzibar.

Sambamba na hilo alisema, ZPRA itaendelea kutoa taarifa sahihi kupitia vyombo vya serikali pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya hatua zinazoendelea kuhusiana na zoezi la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gezi asilia.

Chanzo: Zanzibar Leo

Share: