Habari

ZURA yaruhusu ushindani bei ya mafuta

June 8, 2018

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imesema kampuni za mafuta zinaruhusiwa kuuza mafuta kwa bei ya ushindani, alimuradi tu hazivuki bei elekezi inayotangazwa na mamlaka hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa ZURA, Haji Kali Haji, alisema hayo katika taarifa yake kwa umma kuhusu bei elekezi za mafuta zitakazotumika kuanzia Juni 8 mwaka huu.

Hata hivyo, alisema kutokana na wananchi wa Zanzibar na waislamu kuwa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani na kukaribia sikukuu ya Eid el Fitri, bei za mafuta zilizotumika mwezi Mei zitaendelea kutumia kwa mwezi Juni.

Alisema lita ya petrol itaendelea kuuzwa kwa shilingi 2,255, dizeli shilingi 2,250, mafuta ya taa shilingi 1,740, mafuta ya meli (banka) shilingi 2,078 na mafuta ya ndege (Jet-A1) yataendelea kuuzwa kwa shilingi 1810.21.

Alisema bei zilizotangazwa ndio halali na zitaanza kutumika kuanzia leo lakini kama kampuni inataka kuuza mafuta kwa bei ya chini inaruhusiwa kufanya hivyo kwa sababu itasaidia kuongeza ushindani.

Zanzibarleo

Share: