Makala/Tahariri

2016 talaka zilitolewa kwa kasi Z’bar

Muhammed Khami -0774848800

Ndoa ni makubali makubaliano ya baina ya pande mbili kati ya mume na mke kwa lengo la kujenga familia moja.Kwenye maisha ya ndoa kuna mazuri na mabaya ambayo huwakabili wanandoa hao.

Visiwani Zanzibar kutengana kwa wanadoa kwenye familia nyingi inaonekana ni changamoto kubwa kwa watoto na Mama wa familia hizo.Talaka ni kuvunjika kwa makubalino ya kindoa kati ya mke na mume waliokubalina kwa hiari zao na kupata baraka za wazazi wa pande zote mbili.

Inaelezwa kuwa suala la kuvunjika kwa ndoa ni kigenzo kikubwa na kuparaganyika kwa familia nyingi hivi sasa na hufanya watoto kukosa malezi yalio bora kutoka kwa wazazi wao.

Kisiwani Unguja suala la talaka linaedelea kushamiri siku hadi siku kutokana na familia nyingi kutengana huku baadhi yao wakieleza sababu mbali mbali za kutengana huko.

Kuthibitisha hili mwandishi wa makala hii alifika hadi Mahakama ya Kaadhi Kwerekwe Mjini Unguja kuona hali halisi ya takuimu ipoje kwa suala la talaka kwa wanandoa.

Karani mkuu wa Mahakama hio Bwana Haji Hassan Haji alisema katika kipindi cha miaka minne na miezi mitatu yaani kuanzia mwaka 2012 hadi miezi mitatu ya kwanza 2016), jumla ya kesi 2,841 za kudai kuvunja ndoa zilipokelewa mahakamani hapo.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa takuimu hii idadi inayoonekana ni kubwa kulinganisha na kesi za kutafuta msaada wa matunzo ya watoto ambazo katika kipindi hicho zilikuwa 268.

Akitoa mchanganuo wa kesi hizo za kudai talaka kwa kila mwaka, karani huyo alisema, mnamo mwaka 2012, jumla ya kesi 647 zilipokelewa, ambapo zilizohusu watoto zilikuwa 52.

Mwaka 2013, idadi ya kesi za kudai kuvunja ndoa iliongezeka na kufikia 785, wakati madai ya matunzo kwa watoto au haki ya kuishi nao yalikuwa 88.

Haji alisema, kwa mwaka 2014, jumla ya kesi 666 za talaka na 62 za watoto ziliwasilishwa katika mahakama hiyo, wakati mwaka 2015, kesi za kudaiana talaka zilikuwa 568 na za matunzo ya watoto zilifikia 55.

Bila shaka ukubwa wa tatizo la kutaka kuvunja ndoa unaonekana kuzidi kuongezeka visiwani hapa, kwani karani huyo alisema katika miezi mitatu tu ya kwanza ya mwaka huu wa 2016, (Januari, Febuari na Machi), tayari kesi 175 za talaka zimeripotiwa kulinganisha na 11 za matunzo kwa watoto.

Khadija Sleiman Said wa Maungani Zanzibar alisema aliishi kwenye ndoa na mume wake kwa muda wa miaka 7 huku akiwa na watoto wa watatu lakini hafla bila ya kujua kosa lake aliachwa na mume wake pamoja na kumtaka aondoke na watoto wote kwenye nyumba hio huku akishindwa kuelewa ni vipi ataweza kuwahudumia watoto hao wadogo waliohitaji mahitaji mbali mbali kama watoto wengine.

Alisema hakua na budi na kukubaliana na hali hio na akaamua kurudi nyumbani kwao kuishi na wazazi wake ingawa ilimuia vigumu kutokana na hali ya maisha kuwa duni kwenye familia yake.

Alisema awali aliishi kwenye ndoa hio kwa amani na upendo lakini hafla aliekua mume wake alibadilika na kuanza tabia za kumpiga na kumfukuza kila mara kabla ya maamuzi ya kumuacha.

Nae Mwanshamba Said Haroud wa Mitondooni Mjini Magharib Unguja alisema pia aliishi kwenye ndoa kwa miezi sita tu tokea kuolewa kwake na badae kuachika huku aliekua mume wake akieleza sababu kadhaa za kumuacha ikiwa ni pamoja na alichokidai ugumu wa maisha.

Alieleza kwamba kabla kuolewa kwake mwanaume huyo alimshawishi sana na kuamini kuwa angeweza kuishi maisha mazuri ya ndoa jambo ambalo lilitokea kuwa kama ndoto kutokana na hali alioikuta kweye ndoa.

‘’Wanaume wengine wana maneno mazuri wanapokuja kukuchumbia unaamini haraka sana kuhisi huyu ni mwanaume lakini ah wapi leo najutia kwanini nilikubali kuolewa na mwanamke asiekua na dira’’alieleza kwa mamasikitiko Mwanshamba.

Gazeti hili likiwa katika ofisi ya kadhi Vuga Mjini hapa lilishuhudia makundi ya kina Mama na wanaume kadhaa waliofika hapo wengi wao wakiwa na kesi za ndoa kama ilivo kawaida.

Baadhi ya wanandoa walikua wakigombana nje ya Mahakama hio huku kila mmoja akieleza hisia zake kwa mwenzake baada ya kufika kuskilizwa kwa kesi zao.

Baadhi ya kina Mama hao kwa nyakati tofauti walisikika wakisema Mahakama hio imekua na tabia ya kulimbikiza kesi bila ya kuzitolea hukumu kwa maamuzi huku wanandoa wakiendelea kuteseka kwenye ndoa zao kwa kusubiria maamuzi ya Mahakama hio maalumu inayohusika na wanandoa.

Juma Haroub Saidi kijana anaeishi kwenye ndoa kwa miaka kumi sasa anaeleza kuwa ndoa ni maisha mazuri kwa wanandoa wenyewe iwapo watakuwa tayari kuishi kwa utulivu na amani bila ya kulazimishana vitu wasivyokua na uwezo navyo.

Alibainisha kutokana na hali halisi ya baadhi ya wanandoa wengi miongoni mwa familia kujaribu kuiga kutoka kwa mashoga zao au marafiki zao ni sababu kubwa zinazopelekea kuongezeka kwa wingi talaka kwa wanandoa.

Mwanafunzi wa darasala tisa skuli mjini hapa aliekataa kutajwa jina lake kwenye makala hii alisema kutengana kwa wazazi wake kunamkosesha amani pia kupunguza ari ya kusoma kila anapofikiria ugumu wa maisha unaomfanya Mama yake kuhangaika peke yake bila ya msaada wa yoyote ule.

‘’Nakumbuka niliamshwa kutoka usingizini na Mama yangu huku akilia sikuweza kujua kwa haraka analilia nini kwa vile nilikua natoka usingizini aliniambia niamke tuondoke Baba ametufukuza’’alieleza mtoto huyo huku machozi yakimtoka.

Ni mwaka wa pili sasa tokea Babake kuachana na Mama yake hajawahi kupata msaada wowote hule kutoka kwa baba yake mzazi jambo ambalo linamsikitisha sana na kukosa mapenzi na mzazi wake huyo.

Kwa upande wake Kaadhi mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji Khamis amekiri uwepo wa ongezo wa takala kwa wanadoa visiwani hapa huku akisema miongoni mwa sababu hizo ni ukosefu wa uvumilivu katika ndoa nyingi.

Alibainisha kuwa maisha ya zamani na sasa ni tofauti sana kwa wanandoa kwa vile zamaani wanandoa wengi waliheshimu taratibu za ndoa na kukubali kuwa wavumilivu katika maisha.

Lakini pia hakusita hapo alieleza zipo baadhi ya familia za wanandoa nazo pia huchangia kwa kiasi kikubwa kuvunjika kwa ndoa kutokana na kuwalazimisha watoto wao kuolewa na waume wasiopenda.

Akizungumzia kuhusu ukosefu wa maadili kwa wanandoa alisema nalo ni miongoni mwa sababu ambazo hupelekea ukosefu wa uwelewa wa kina kwa wanandoa wenyewe pia aligusia suala la utandawazi ni miongoni mwa changamoto za ndoa nyingi hivi sasa.

‘’Utaona wanandoa wegi sasa wanaiga tamaduni za nje na kutaka mambo yalio chini ya uwezo wa waume zao jambo ambalo limekua changamoto kwa ndoa nyingi visiwani hapa’’alieleza Kaadhi huyo.

Aidha kaadhi huyo akitolea ufafanuzi kuhusu mrundikano wa keshi kwenye Mahakama yake alisema wanachokifanya wao kama Mahakama ni taratibu za kuskiliza kesi kisheria hawawezi kutolea majibu kwenye kesi za ndoa kama watu wanavofikiria .

‘’Unajua mwandishi watu wanadhani kesi hizi ni rahisi unaweza kuja leo na kesho kesi ikaamuliwa ,hatuwezi kufanya hivyo kesi za ndoa zinahitaji kuskilizwa pande zote mbili bila ya kuacha upande wowote hule na kisha kutolea maamuzi’’ alifafanua zaidi.

Aliendelea kwa kutoa wito kwa wanandoa na wale wote wanatoka kuingia kwenye ndoa kujidhatiti kabla ya kufanya maamuzi hayo wakijua kuwa ndoa inahitaji uvumilivu mkubwa.

Katika kuhakikisha suala la haki za wanawake linapatiwa ufumbuzi kwenye maeneo mbali mbali visiwani hapa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA)tawi la Zanzibar halikukaa kimya linaedelea kutoa elimu za haki za msingi kwa kina Mama ili kuweza kupambana na vitendo vya unyanyasaji ikiwemo kupewa talaka na kukosesha watoto haki zao za msingi ikiwemo elimu bora.

Sasa imefika wakati jamii jamii kupaza sauti zetu kutambua kuwa mwananmke ni sehemu ya maisha yetu na Mama wa Taifa letu tuna kila sababu ya kumtunza mwanamke kwa maisha bora ya leo na kesho.

Share: