Makala/Tahariri

Aliyozungumza Mzee Moyo

Na Farrell Foum
#TeamZanzibar

Wiki hii gumzo kubwa liko kwa hadithi ya Mzee Moyo na namna ya matokeo ya uchaguzi yalivyotolewa akiwa yeye shuhuda wa aliyoyaona na kuyafanyia kazi. Wengi wetu tuna pupa ya kuhukumu na kutotazama mazingira halisi na mapambano ya kifikra yaliopo na yaliodumu kwa takriban miaka 20 ya uhai wa siasa za vyama vingi. Ninaamini kwa dhati yangu kwamba Mzee Moyo si wa kutupiwa lawama kwa alichokifanya bali wa kupongezwa kwa kuepusha mauaji makubwa na vurugu kubwa visiwani wakati tayari tukishafungua kurasa mpya za maelewano. Wengi wetu ni kizazi kisichojuwa hasa athari ya mapinduzi na nini hasa kilitokea katika kipindi hicho, uzee wa Babu yetu Mzee Moyo umempa hekima na busara kubwa kwa kuwa miongoni mwa wachache waliosukuma gurudumu la kuwepo kwa mazingira ya mafahamiano baina yetu hata tukaweza kujivunia serikali ya umoja wetu. Kwa wapenda amani ushindi wa mgombea mmoja ambao unasukumwa makusudi kuwa ni chanzo cha vurugu mpya haikuwa ni mwanzo mzuri baada ya makubaliano yaliohakikisha kila chama kitashiriki katika uundwaji wa serikali ya umoja wetu.

Nawatazama wanaombeza Dr Karume kwa kuzuia fujo na mauaji ambayo kiukweli amri yake huwa mbali na uwezo wa nafasi ya Rais wa Zanzibar. Hata haya ya mwaka 2000 mamlaka yaliohusika na mauaji ya raia hayakuwa kutoka Zanzibar, mengine yaliotokea hata aliekuwa Makamo wa Rais wa wakati ule hakuwa na taarifa nayo wala mamlaka nayo zaidi ya shuhuda alieumizwa na makubwa yaliotokea. Kwangu kwa hili pekee Dr Karume anazidi heshima anayostahili kwa kuweza kwanza kutuvusha katika siasa za uhasama baina yetu kwa kukubali mashirikiano na kuzika tafauti zetu zilizoturejesha na kuwa chanzo cha kudumaa kwa maendeleo yetu. Pili kwa kuwa na “vision” ya kuona mbali zaidi na kuegemea katika nusra badala ya hamasa ambayo ni changa na iliohitaji zaidi kuimarishwa kwa misingi ya kushirikiana baina ya vyama na kulifanya suala la mshindi kutokuwa zito kwa vile sote kwa pamoja tuwe washindi wa kukataa fujo iliokuwa ikipandikizwa na kuvunja “legacy” yake ya kuliegemeza jahazi katika bandari kwa salama.

Naomba tutazame kwa undani laiti Maalim Hamad, angeliyakataa matokeo na kupuuza ushauri wa Mzee Moyo na Edi Riyami leo hii tungekuwa wapi? Tusigeuke samaki na tukawa rahisi wa kusahau kwanza “lesson” ya Mapinduzi na maisha ya watu yalivyotoweka kwa nguvu na chuki za kupandikizana. Fikirini laiti kama serikali wakati ule baada ya uhuru ingewezekana kuundwa kwa kushirikiana na ASP na kuepusha Mapinduzi tungelikuwa wapi hii leo? Fikirini hizi chuki zilizochangia umwagaji wa damu wa wananchi wasio na hatia kupitia mikono ilio nje ya uwezo wa mamlaka zetu zingeliweza kuzuiliwa kwa Hizbu na ASP kushirikiana katika uundwaji wa serikali tungelikuwa wapi hii leo? Historia ya nchi yetu na mazingira tulionayo hadi hii leo ni vyema kutumia akili zaidi badala ya ubishi ambao hatima yake ni vifo kwa wasio na hatia na mbaya zaidi hata yale makubaliano ya mashirikiano baina yetu yasingekuwa yakisimama hasa kwa vile wenye itikadi kali ndio wangeliweza kubadili na kubeba mwelekeo wa siasa za kukomoana zaidi na kuturudisha nyuma.

Nguvu zilizotumika kupinga wahafidhina waliokuwa hawasikii wala hawaoni kuyakubali maelewano zilihitajika ili kuhakikisha jahazi linasonga mbele na serikali ya umoja inaundwa. Tunaweza kudharau nafasi ya serikali hii ya umoja na hali ya sasa ilivyo lakini tukumbuke kwamba huko nyuma tulipotoka hakukuwa na “alternative” nyengine yoyote na kama tungelikuwa vipofu wa kutoona mbele leo hii tungelikuwa pabaya zaidi. Ninachokiona mimi ni kwamba Maalim Hamad alipewa heshima tu ya kuambiwa ukweli na kupewa nafasi ya kusukuma zaidi mbele “struggle” ya wanamageuzi katika mazingira ya amani zaidi huku akijijenga zaidi akiwa ndani ya “system” ya uongozi kuliko nje katika barabara huku akibeba mgongoni lawama za kukataa sulhu ya kudumu yenye faida kubwa zaidi.
Niwakumbushe hasa wanamageuzi waliomeza hii ndoana ya wahafidhina kwamba ushindi wa 2010 haukuwa ushindi wa yoyote zaidi ya wazanzibari wote. Kuimeza ndoana ya wahafidhina hii leo ni kuwapa nafasi ya kuturejesha nyuma zaidi wakiwa na lengo lile lile la wagawe na uwatawale zaidi. Sisi si wa kulalamika na kuwatusi waliojiri kugeuza hasad kuwa kheri bali wa kuwapigia makofi kwa jitihada zao huku tukijiimarisha zaidi na kwa nguvu zote kuhakikisha kwanza hatutegeki katika madema ya shari zao na pili tunasoma kutoka miaka 20 ya “struggle” zetu kuhakikisha ushindi wa wanamageuzi unakuwa mkubwa zaidi na kuwafanya wasio tutakia kheri kukosa nguvu za hujuma baina yetu. Hili litafanyika pale tu tutapokuwa tayari kusonga mbele na kujiimarisha kwa mikakati ya umoja, amani na utulivu kwa thamani yoyote tutayoiona.

Kwa nini vita vikubwa viwekweze kwa serikali ya umoja? Sababu kubwa ni moja kuu, hii ndio silaha nzito ya umoja wetu na ndio nguzo imara ya mabadiliko tuyatakayo. Tazama wanaowekeza fitna miongoni mwetu kwa kushadidia ubaya kwa walioiokoa Zanzibar katika machafuko lakini wakasahau lililo na uzito zaidi kwamba hivi lipi kosa kubwa baina ya alieshinda akaepusha machafuko na yule alieshindwa na kuvaa joho kwa nguvu zote bila ya kujali athari na uhalali wa kinachotokea? Tungewauliza wazee wa Hizbu waliofikiri mapinduzi yasingewezekana laiti wangelikuwa na nafasi kama ilivyokuwa ya mwaka 2010 wangelirudi nyuma kuepusha janga la mauaji makubwa na kukosa kila kitu kwa takriban miaka hamsini?
Tuwapongeze wote waliowezesha kuepusha madhara makubwa kwa wananchi visiwani na kuwaweka kati wahafidhina waliofikiri matangazo ya ushindi ni ndoana ya kuwamaliza wanamageuzi. Tuwapongeze waliothubutu kukataa ushindi kwa khofu ya madhara kwa wananchi wake na kurudisha nyuma gurumu la maendeleo tunaloliona likisonga mbele kila pembe ya visiwa hivi. Tuwapigie makofi na kuwapa moyo wale wote walioona mbali kwa kuuweka utu na ubinadaamu kwanza kuliko hamasa ya ushindi wa kutangazwa ambao usingeweza kutoa mafanikio ya uongozi tuutakao. Tuwadharau wale wote wanaofikiri fitna zao zitaweza kuturudisha nyuma katika azma ya mabadiliko yatayoleta haki, usawa na heshima katika safu za uongozi wetu na katika mabadiliko ya mfumo wa muungano tuutakao.
Masimulizi ya Mzee Moyo ni wakati muafaka kuyaweka wazi ili wananchi wawajuwe walio na uchu wa madaraka na walio tayari kwa lolote kuzima nuru ya mabadiliko na demokrasia inayohitajika nchini. Ni uzinduo kwa wale wenye hisia kwamba ahadi mulizoziweka muzitimize na kuwatendea haki wananchi na viongozi walioweka maslahi ya wananchi kwanza badala ya matumbo na kibri cha matumizi ya nguvu. Ni uzinduo kwa wananchi juu ya jitihada kubwa zilizozaa matunda tunayoyaona leo na utulivu mkubwa uliowajenga mara dufu wanamageuzi kwa kutoa kidogo ili kushinda kikubwa zaidi katika jina la amani na utulivu. Na uzinduo kwa wanaofikiri wataendelea kuwafitinisha wananchi wakati ongezeko la umma ni kubwa mara dufu ya mwaka 2010, na umoja wetu, upendo wa nchi yetu pamoja azma ya mabadiliko ya kweli ndio yatayotuwezesha kushinda ghilba zote mwaka 2010. Kumbukeni tulipo sasa na umma uliojitokeza kuunga mkono mabadiliko tuyatakayo tusingeweza bila ya kukubali matokeo yaliotuamsha wengi na kuona ukweli ulipo. Umoja wetu ndio nguzo pekee ya kutuvusha katika mabadiliko ya utulivu.

Tagsslider
Share: