Makala/Tahariri

CCM-Mtenda Akitendewa Hujiona Kaonewa Eh?

Mtenda akitendewa By Farell Jnr Foum

Wakati wa ufungwaji wa Baraza La Wawakilishi tarehe 13 August 2015, mualiko wa Makamo wa Kwanza wa Rais ulizuiwa na wawakilishi wa watawala. Wakambeza na kumdhihaki, alipotajwa jina lake na Spika kwa pamoja walizomea kuashiria faraja ya kumzuia kuingia barazani kama mualikwa. Hawakuuona ule utoto mpaka yalipowakuta? Alau Makamo wa kwanza alikuwa na haki ya kikatiba si ya kupanga panga ya kualikwa barazani lakini wakampinga. Walikurupuka hawakufahamu, yanayotokea sasa ni kama mzungo kuanzia kauli zao na matendo yao. Walizomea leo yamewakuta wanalialia, waliwaita mabwege leo yamewageukia. Qadar ya Mungu inapokuja huja na fedheha kwa wanaoichezea.

Sasa tazama ya jana jinsi nalo bunge lilivyokataa hadaa ya kuhalalisha uongozi uliomaliza muda kisheria lakini ukajificha katika tamthilia ya kutoapishwa kwa mwengine nae yalimkuta yale yale walioyaanza wenyewe wakati wa ufungwaji wa Baraza la Wawakilishi. Na yataendelea kila kukicha kwa kukosa “legitimacy” ya kuwaongoza watu kwa ridhaa yao. Cha kushangaza spika wetu wa Baraza nae alikuwapo, hivi maana hasa ya kuvunjwa Baraza ni ipi ikiwa wawakilishi wamemaliza muda wao na spika kung’ang’ania majoho ya chombo kisichokuwepo? Ukiuliza utazungushwa na karagosi wakufanye kama vile hazikutoshi huku mantik nzima ikiwa wazi kabisa juu ya uhadaifu wa kuficha ukweli.

Jengine la kushangaza na la kutia aibu kusikia ati Bunge tukufu limechangiwa fedha na wafanyabiashara na wadau wengine kufanya sherehe ya wabunge waliochaguliwa. Sijawahi kuona jinsi gani tunavyodharau na kubeza mamlaka kubwa za nchi hasa katika suala hili lenye kuonyesha wazi wazi kile kinachotambulika kama ni “conflict of interest”. Sasa tuliwahukumu vipi kina Tibaijuka na kesi hizi hizi za kuambatana kimaslahi lakini tukafumbia macho uhuni huu wa kuliangamiza bunge kwa kuruhusu michango ya wenye kutamani kuliweka bunge mikononi mwao na fedha hizi za milioni 270 zenye harufu kabisa ya msongamano wa kimaslahi?

Baya zaidi namna ya vyombo vyahabari na jamii nzima ilivyolipokea kama vile ni jambo la kawaida. Tena wanamsifu Rais kwa kuzipeleka fedha hizo ambazo hazikutakiwa kabisa kupokewa na bunge kimantik lakini yeye akaona ni vyema zikatumike kwengine badala ya anasa ya siku moja. Ninaloliona la ajabu kabisa ni namna gani mazingira yanavyojengwa kinyume na maadili na mantik na kupokewa mikono miwili na chombo kikuu cha kutunga sheria za nchi wakisahau kabisa mgongano wa kimaslahi baina ya wachangiaji na wapokeaji. Usishangae kabisa ukisikia kwamba ni uongozi wa bunge uliokwenda kuomba fedha hizo za anasa bila ya kutambua dhamana walionayo na watoaji haziwiani.

Share: