Makala/Tahariri

Demokrasia ya Afrika ni uhuni mtupu!

Julius Mtariro,

Pamoja na tafsiri nyingi zilizowahi kutolewa na kufundishwa, utekelezaji wa dhana ya demokrasia hapa Afrika una tafsiri maalumu kutoka kwa vyama vilivyokaa madarakani muda mrefu au wakuu wa nchi waliosalia madarakani kwa muda mrefu.

Wengi wetu walipokuwa shule za msingi na sekondari walisikia na kulijua neno demokrasia kwa mara ya kwanza likitajwa na kupewa maana zake. Moja ya maana za demokrasia ni “utawala wa watu kwa ajili ya wao wenyewe…” na tena maana nyingine ni “utawala unaowekwa na watu kwa kufuata misingi waliokubaliana”.

Pamoja na tafsiri nyingi zilizowahi kutolewa na kufundishwa, utekelezaji wa dhana ya demokrasia hapa Afrika una tafsiri maalumu kutoka kwa vyama vilivyokaa madarakani muda mrefu au wakuu wa nchi waliosalia madarakani kwa muda mrefu.

Kuna demokrasia mbili Afrika, ile ya watawala na ya watawaliwa. Ya watawala haitabiriki na inakuwapo pale wanaposhinda uchaguzi kupitia njia mbalimbali na hasa kwa msaada wa vyombo vya dola, mabavu, rushwa, vitisho, mifumo ya uongozi ya kiupendeleo na tume za uchaguzi zinazoongozwa na wao wenyewe. Demokrasia hii ya watawala imeonekana Zanzibar kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 watawala walipoona Maalim Seif Sharif Hamad anaelekea kushinda uchaguzi wakazuia kwa nguvu matokeo yasiendelee kutangazwa na kisha yakafutwa na ‘mtu’ mwenye dhamana ya kuisimamia tume kwa kufuata kanuni za uchaguzi, sheria na katiba ambavyo hata mara moja havimpi yeye au tume nzima mamlaka ya kufuta matokeo ya jumla ya uchaguzi na ambayo yamethibitishwa na ngazi za wasimamizi wa uchaguzi.

Matokeo yaleyale yaliyomzuia Maalim Seif kuwa rais wa Zanzibar ndiyo yakampaisha Rais John Magufuli kutangazwa kuwa Rais wa Tanzania.

Kidemokrasia (Demokrasia ya Tanzania) kwa tafsiri ya dola na chama kinachoongoza dola ni pale ambapo wagombea wa CCM wangelikuwa wanaongoza wote, pia bila aibu aliposhindwa mmoja wakashindwa kujibaraguza ilimradi wazuie matokeo yote ya Zanzibar kwa chaguzi zote (urais wa Jamhuri na ule wa Zanzibar) na kwa hivyo uchaguzi wa marudio unaokwenda kufanyika Zanzibar (huku vyama vyenye nguvu kama CUF vikiwa vimeususia) ungelifanyika kwa nafasi zote za urais wa Jamhuri na ule wa Zanzibar.

Ndiyo kusema hadi leo wakati fukuto la Zanzibar linaendelea, Rais mstaafu Jakaya Kikwete angepaswa kuwa madarakani huku John Magufuli (aliyekuwa anaongoza kura za urais wa Jamhuri wakati matokeo ya Zanzibar yanafutwa) akisubiri apigiwe kura upya Zanzibar kabla ya kutangazwa mshindi wa jumla wa uchaguzi wote.

Kwa vyama vilivyoongoza Afrika muda mrefu demokrasia ni jambo la upande mmoja, ni jambo la wao wanataka kupata nini, ni jambo la wanachokipata kinawatosha kiasi gani! Watawala wa Afrika huitafsiri demokrasia yao na kuilazimisha ikubalike hivyo ilivyo kwa kadri watakavyoamua na hapo ndipo bara hili linakwama.

Kwenye shule zetu watoto wanaendelea kufundishwa demokrasia ni uamuzi wa wananchi na wengine wanadhani jambo hilo ni dhahiri, kwenye utekelezaji demokrasia ya Kiafrika ni tofauti na kile kinachofundishwa na labda kinachofanywa na wenye demokrasia wenyewe, huko nchi za Magharibi.

Mwalimu Kitila Mkumbo (Profesa) mara kadhaa amepata kuandika juu ya “dhana ya demokrasia ya Afrika” na amekuwa akihoji ikiwa kuna haja ya Afrika kuendelea na demokrasia hiyo ya maigizo badala ya kukaa chini na kuamua moja na hata kuanzisha demokrasia ya Afrika na kuijulisha dunia “hii ndiyo demokrasia yetu!” Kitila anaongelea dhana pana ya unafiki mkubwa unaofanywa na viongozi wa Afrika kuanzia kwenye ngazi ya chama kimoja kimoja (kilichoshika dola na visivyoshika dola) na ngazi ya nchi ambapo vyama vyote hukutana na kushindana ili kimoja kipate ushindi wa jumla.

Hii ni wiki ambayo nchini Uganda kumekuwa na gumzo la Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni na wakati wananchi wa kawaida wanaimba mabadiliko wayatakayo, vyombo vya dola na rais aliyeko madarakani, Yoweri Museveni wanasimamia kile wanachokiamini kama “ni lazima Museveni aendelee kutawala”.

Katika wiki ya mwisho ya uchaguzi, kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, alikamatwa na kushikiliwa mara tatu.

Mara ya mwisho ni siku ya uchaguzi yenyewe tena akiwa katika mizunguko ya kufuatilia mienendo ya uchaguzi. Kiongozi mwingine wa upinzani, Amama Mbabazi naye aliwekwa jela ya nyumbani kwake siku ya uchaguzi.

Haya yote yakifanywa na majeshi ya Uganda yakishirikiana na walinda usalama wengine, hii ndiyo demokrasia ya Afrika.

Museveni hana mpango wa kuondoka madarakani na kwake yeye na wanaonufaika moja kwa moja na utawala wake ‘demokrasia sahihi ni yeye kutawala!”

Ukihamia pale Burundi utakumbana na matatizo makubwa, Pierre Nkurunziza amekatalia madarakani, alifanya uchaguzi wa upande moja akajihalalisha kuendelea kuwa mtawala wa Burundi.

Kwa Nkurunzinza, tafsiri ya demokrasia ni yeye kuendelea kuitawala Burundi.

Mamia ya watu waliouawa kwenye machafuko yaliyoongozwa na vyombo vya dola ili kuwanyamazisha wapinzani wa Nkurunziza, hakujali, kwake demokrasia ni “kusalia madarakani” hata kama watu wanakufa!

Majirani zetu Wanyarwanda wanapita kwenye yaleyale, Rais Paul Kagame anaamini hakuna Mnyarwanda mwenye uwezo wa kuongoza nchi hiyo, amekaa madarakani miongo miwili na bado yumo tu, yeye tu! Vyama vilivyosajiliwa pale Rwanda vinafanya kazi kama wakimbizi.

mwananchi

Share: