Makala/Tahariri

Hata Mheshimiwa Pinda nae anautamani urais

Na Farrell Foum jnr

Hata Mheshimiwa Pinda nae anautamani urais wa Tanzania. Nafikiri kwanza angejitathmini akiwa Waziri Mkuu nini hasa legacy yake?

Binafsi naona ni mmoja wa Mawaziri wakuu waliochangia kutufikisha hapa tulipo kwa kukosa umakini wa kauli zake. Umakini wa nafasi kubwa ya kiutawala nchini unahitaji hekima, busara na pia umakini wa mazungumzo na kauli kwa unaowaongoza.

Top 3 ya kauli zake:
1. Zanzibar si nchi ( kwa mara ya kwanza waziri mkuu asie na mamlaka yoyote visiwani akitamka bila ya kufahamu athari ya maneno yake tena ndani ya bunge, matokeo yake ni mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ya 2010).

2. Wapigwe tu, tumechoka nao. (Ndani ya bunge linalolinda katiba ya nchi na wananchi, akitoa fursa kwa kutothamini umuhimu wa sheria na mamlaka ya utowaji wa adhabu ni kwa mahakama pekee).

3. Tungelijuwa mapema, tungeleta kwanza kura ya maoni kuwauliza wananchi idadi ya serikali. Akienda kinyume kabisa na ukweli wa kwamba hili lilipigiwa kelele sana na akawa na uziwi wa kutoshaurika.

Hizi kauli zinamfanya kwanza kukosa hekima, busara na uwezo wa kutazama mazingira ya nchi anayoiongoza. Kigezo muhimu sana kwa rais mtarajiwa hasa katika nchi ilioundwa kutokana na muungano ambao bado una controversies nyingi katika muundo wake. Mazingira ya muungano yanahitaji kiongozi aliemadhubuti na mwenye kujifahamu kwa kauli zake na hisia za wadau wa muungano mzima, mwenye uwezo wa kutuunganisha na kutusikiliza.

Vile vile kuna khofu kubwa ya nchi kuwa katika mfumo wa matumizi ya nguvu kwa wananchi pale watapopinga matashi ya utawala wake. Aliposema wapige tu, tumechoka nao hakuonyesha ukomavu wa kisiasa na wa uongozi hasa tukizingatia kazi ya vikosi vya usalama ni ulinzi wa wananchi na utulizwaji wa ghasia. Amri ya namna hii isio na kikomo cha matumizi ya nguvu kwa raia yanaweza kuifanya nchi kurudi katika kipindi cha nyuma cha khofu na mfadhaiko.

Na mwisho haonekani kama ni mtu mwenye msimamo na anachokiamini, ndio maana sasa anakiri ni vyema angeliwasikiliza wananchi pale walipodai maoni ya mfumo wa serikali ngapi badala ya mparaganyo waliouwongoza. Ukweli umakini wa waziri mkuu ni mdogo sana, na kutokana na hapa taifa lilipofika tunahitaji mtu mwenye upeo mkubwa wa busara na mwenye kufahamu hali halisi ya nchi ilivyo.

Vitendo
Bado muda wake aliokalia nafasi ya uwaziri mkuu haujatoa mafanikio ya kiutendaji yenye msukumo wa maendeleo ya wananchi. Na nafikiri ni waziri mkuu wa kwanza alietishiwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani nae ndani ya bunge tena kutoka pande zote za vyama. Ikiwa wabunge wamefikia hadi ya kutaka kumtosa kwa nguvu nafasi yake, sijui mwenyewe anajitathmini vipi hasa ajihisi anauwezo wa kugombea nafasi kubwa ya nchi zetu. Wengi walitamani mabadiliko ya Waziri Mkuu baada ya reshuffle ya baraza la mawaziri.

Mfano mwengine ni kauli za Lukuvi ambae alikuwa akimuakilisha Waziri Mkuu katika hotuba yake iliokuwa bila unethical na ni msingi wa machafuko ya upatikanaji wa katiba mpya. Kusema tu kwamba maneno ya Lukuvi ni yake binafsi haionyeshi kama waziri mkuu anaithamini nafasi yake bila ya kukaripia na kupinga nafasi yake kuingizwa katika matatizo yaliojitokeza. Kwa vyovyote Lukuvi ni msimamizi wa wizara ya Waziri mkuu, na zipo dalili zinazoonyesha mind set zinazofanana kati ya waziri na waziri mkuu. Wote wamekosa vigezo vya nafasi kuu ya nchi hasa katika mazingira ya sasa.

Ufanisi
Ni vigumu sana kutambua ufanisi wa Mheshimiwa Pinda ukilinganisha na waliomtangulia. Kwa hali ilivyo sasa tunahitaji Rais mwenye ufahamu mkubwa na mwenye ari ya kuzaliwa ya ufanisi wa hali ya juu katika kuhuisha maendeleo ya nchi. Tunahitaji mwenye mentality ya Sokoine, hekima na busara za warioba, upole wa Salim Ahmed Salim, ucheshi wa Mzee Mwinyi na haiba ya ihsani katika nafasi ya ukuu wa serikali ya muungano.

Fikra mpya
Tunahitaji uongozi utakaokuwa fresh na wa fikra mpya isiotokana na mfadhaiko wa safu kuu ya sasa ili kuweza kuleta mapinduzi mapya ya kifikra mahsusi kwa ajili ya maendeleo. Binafsi sifikirii kwamba ujana kwa hali ilivyo ya sasa ni kigezo kikuu cha mabadiliko tunayoyahitaji. Tunahitaji kiongoZi wa wote, sawa na kinachoitwa kama ni “war time leader” kwa vile taifa lipo katika mpasuko na hekima, ujasiri, uelewa pamoja na busara zinahitajika kwa uongozi utaoweza kuturudisha katika safu ya uadilifu, uaminifu na utukufu wa nchi tuipendayo.

Uadilifu
Taifa linahitaji kiongozi muadilifu na mwenye kuaminika kwa wananchi wake. Lakini uadilifu pekee bila ya upevu wa uwajibikaji, ufanisi pamoja na utendaji wa hali ya juu hauwezi kuwa ndio sifa pekee ya kiongozi tumtakaye. Uadilifu si wa mali tu na amali pia kwa vile uongozi unahitaji nguvu na mawazo mapya yenye kubeba utendaji na ufanisi ikiwa lengo ni legacy mpya ya maendeleo na mafahamiano.

Mapatano
Tunahitaji kiongoZi anaekubalika na kila upande kimaadili, kiamali, kiuwajibikaji na kiihsani. Mtu ambae hatakubali kuburuzwa na yeyote badala ya matashi ya nchi na wananchi wake. Mtu ambae hatakuwa tayari kutazama manifesto ya chama chake pekee bali atakaeweza kuunda serikali ya vipaji yenye kubeba technocrats badala ya wanasiasa wanaotokana na ufuasi wa itikadi moja pekee. Tunahitaji safu ya juu ya wazee wenye busara, haki, uadilifu na wanaokubalika na jamii kuleta makubaliano na amani ya kila upande. Vile vile vijana wenye uwezo, ujuzi na uzoefu katika kusukuma maendeleo katika wizara, idara na mamlaka wanaziongoza.

Tunahitaji safu ya pamoja ya kujenga msingi imara wa kuhakikisha siasa zinakaa kando kwa miaka mitano ili maendeleo yaweze kushika hatamu na wananchi waweze kufaidi mapinduzi mapya ya fikra badala ya nguvu kubwa na kauli za ubabe kwa wanaoteleza.

Mawazo yangu binafsi ni kwamba Mheshimiwa Pinda kashindwa kuiongoza nchi hivi sasa akiwa Waziri Mkuu na hawezi kuwa kiongozi atakaeweza kutuvusha katika miaka mitano inayokuja.

Tagsslider
Share: