Makala/Tahariri

Hawajaelewa maana ya madaraka

Na Juma Duni Haji

KAZI kubwa ya elimu ni kumtayarisha binaadamu awe bora zaidi. Kama chuma hutengenezwa gari basi binaadamu hutengenezwa kuwa daktari wa kutibu binaadamu wengine, au hutengeneza gari, simu, dawa na nyumba.

Binaadamu huyu hubadilika na kuwa tafauti na yule ambae ajuacho ni kubeba au kulima kwa kutumia kijembe kongoroka. Mtu anapotoka shule katika daraja yoyote ile huwa ameendelezwa ili kuendeleza vitu vingine vitakavyomrahisishia maisha. Huhitaji malipo zaidi kwa kazi aliyoifanya wakati akitayarishwa.

Kiuzalishaji, huyu ni bora zaidi kuliko yule wa fungu la mwanzo, ingawa wote ni binaadamu. Kilichofanya apelekwe kusoma ni kumjengea uwezo ili atengeneze vitu vya kumrahisishia maisha. Binaadamu aliyesoma anautajiri wa nguvukazi na nguvuakili.

Msingi mkuu unaowezesha kutafautisha nchi moja na nyingine, ni uwezo mkubwa wa wananchi kulingana na walivyoendelezwa kielimu. Kinachofanya nchi ionekane tajiri kuliko nyingine si wingi au ukubwa wa raslimali, wala si wingi wa watu tu. Bali kiasi gani watu wake wameelimika au wameendelezwa.

Japan, Singapore na hata Hong Kong ni nchi za visiwa vidogo visivyokuwa na maliasili nyingi. Ila kwa sababu ya kuwa na watu walioendelezwa kielimu, zimekuwa tajiri na zinazojitosheleza kwa kila kitu. Tanzania ni nchi kubwa na yenye kila aina ya maliasili lakini ni masikini wa kutupwa ku­linganisha na nyingi duniani.

Hoja mpya ya mwelekeo wa kuondoa umaskini lazima itazamwe katika muono huo wa uwezo wa binaadamu na kiasi gani wamethaminiwa na kuwezeshwa ili kumiliki mazingira yao kwa urahisi.

Utafiti wa kiuchumi uliofanywa na Benki ya Dunia unaeleza kuwa wakati Tanganyika inapata uhuru mwaka 1961, au pale Ghana kama vile ilivyokuwa Tanganyika nayo ilipokuwa huru mwaka 1959, Pato lake la Taifa (GDP) lilikuwa sawasawa na la Singapore au Malaysia. Leo miaka 50 baadae, Singapore na Malaysia ambazo hazina dhahabu wala ardhi ya kutosha, zinaitwa nchi mpya zilizoendelea na kuwekwa kundi la nchi za dunia ya pili.

Tanganyika na Ghana zimerudi miaka 50 nyuma. Wao wamethamini watu wao na kuwajenga kimaarifa. Utajiri wa raslimaliwatu ndio mtaji mkubwa kwao. Tanganyika na sasa Ghana si nchi masikini, ila watu wake, ndivyo inavyobainishwa na jarida la Benki ya Dunia. Kipimo kikubwa cha kujua kiwango cha nchi kuendelea, ni namna gani raslimaliwatu yake imeendelezwa.

Benki ya Dunia ilifanya utafiti huo miaka ya 1990 na kugundua kuwa matumizi ya pato la taifa kwa kila mwananchi kwenye elimu ni makubwa kwa nchi tajiri kuliko zile masikini. Kila panapotumika fedha nyingi katika kuwaendeleza watu kielimu, ndivyo nchi hupimwa kiutajiri. Utajiri wa pili wa binaadamu ni uwezo wake wa kujifunza na kuyatawala mazingira.

Utajiri wa aina ya tatu ya mwanaadamu ni mahusiano. Tumejifunza kuwa binaadamu anamhitaji binaadamu. Yupo kwasababu mwingine yupo na ataendelea au kuangamia kutegemea mahusiano yao.

Watu wasiosoma taaluma ya nadharia, mara zote huwa wengi na hubakishwa daraja la wakosefu wa elimu hiyo. Hao huhitaji kuthaminiwa si kwa sababu wamekosa elimu ya nadharia inayotumika kupima kiwango cha mtu kuelimika. Linabidi lithaminiwe kwa sababu lina nguvukazi na linamiliki elimu ya kuishi ambavyo huhitajiwa na kundi dogo lililoshiba nadharia na linalotawala.

Lakini jamii yoyote haikamiliki kama hakuna mustakabali mwema wa makundi haya mawili –kundi kosefu wa elimu ya nadharia linalobaki kutawaliwa, na lile lililoelimika, kumiliki utajiri wa dola na linalotawala. Unaweza kuwa umesoma nadharia na kuendelezwa kwa kiwango cha juu, lakini ukawa dhaifu na kudharau binaadamu wa kundi la kwanza.

Kwa hivyo kuna aina ya tatu ya utajiri wa mwanaadamu ambao ndio kiungo muhimu kinachowezesha yule wa kundi la kwanza na yule wa pili waweze kuendelea na hivyo kuendeleza nchi. Utajiri huu ni aina ya utamaduni na mfumo wa maisha unaojenga uhusiano wa binaadamu mmoja na mwengine katika jamii ile. Aliyesoma nadharia pamoja na uwezo wake wote alionao, lazima ampate yule mwenye elimu ya kuishi au mwenzake aliyesoma fani nyingine ili waweze kufanikisha kurahisisha maisha yao.

Maana binaadamu hawezi kuwa binaadamu kama hakuna binaadamu mwengine. Kwa maana nyingine ni jinsi gani jamii ya binaadamu katika taifa wanavyoshirikiana katika kubadili mazingira yao na nani ana mamlaka ya mazingira hayo. Kama alivyoona Karl Marx, hiki ndicho hujenga mustakbali mwema au mbaya kati ya makundi hayo na kuzaa msongamano wa maslahi wa kudumu kati ya makundi mbalimbali.

Mfumo gani wa utawala uliopo katika nchi hiyo ndio kiungo muhimu kinachowezesha maendeleo ya watu wa makundi mawili hayo, kufanikiwa au kushindwa kuendelea au kujiendeleza.

Maendeleo yanahusu bi­naadamu siyo vitu. Maendeleo hutegemea zaidi uwezo wa watu kuyamudu mazingira yao, nguzo kuu ya mafanikio ikiwa ni elimu. Kuthaminiana kwao hutegemea mfumo waliowekewa kiutawala. Unakubali kuwa wanahaki sawa na wanawajibu sawa kushiriki kuyabadilisha mazingira yao ili yawatumikie? Wote ni utajiri na wote ni neema. Penye neema pana wema. Wema ni matunda ya haki sawa kwa wote na ndio utajirisho.

Swali gumu ambalo linahitaji jibu ni kwa jinsi gani wema hujengwa katika jamii? Wema na uovu ni taaluma inayoambatana na imani ya dini. Watanzania wanazo dini wanazoabudu. Kinachofurahisha ni kwamba dini zote na vitabu vyote vitakatifu vinafundisha masuala mawili makubwa ya msingi wa maisha ya kila siku duniani. Vyote vinahimiza kufanya wema na kuacha uovu. Elimu ya kuishi na ile ya nadharia inatiliwa mkazo hapo.

Ni vyema watawala kuhimiza umuhimu wa haki za bi­naadamu lakini ni lazima pia kuruhusu elimu hiyo kutolewa ndani ya mfumo wenyewe wa elimu au nje ya mfumo chini ya msaada wa watawala wenyewe. Wema na uovu umejikita pale kundi moja la jamii linapokuwa na nguvu kubwa za maamuzi dhidi ya jingine. Kwa hivyo ni muhimu elimu ikazingatia kuelimisha wanafunzi ubaya na uzuri wa utajiri wa aina tatu hizo na umuhimu wa kujenga utamaduni mpya wa kufanyiana wema.

Elimu ni ukombozi

Vipimo na vigezo hivyo vya maendeleo havitaweza kufanikiwa kama wananchi hawakuelimishwa. Kama kuendelea ni kuwa na elimu ya mazingira yanayowatawala basi wanahitaji elimu itakayowakomboa na sio elimu ya kikasuku inayosifu nadharia pekee na ya kujisifia katika kujenga uhasama na matusi. Iwe elimu itakayomwezesha mwananchi kuyatawala mazingira yake. Ndio ukombozi kwake. Jee ni elimu gani basi itafaa?

Kwa mfano ni mfumo gani wa elimu au ni elimu ya aina gani itawezesha wananchi kutawala mazingira yao? Maana hatuna budi kujiuliza tunaishi ili tusome au tunasoma ili tuishi? Hapa ndipo uamuzi wa aina ya elimu unapohitaji maamuzi ya msingi, maana kule Pemba jamii ya Wakojani wanaishi kwa kutegemea uvuvi.

Kijana wa kikojani asiyeingia darasani, akaishi kwa kufuatana na wazazi baharini hadi akitimia miaka 11, atakuwa ameelimika kuhusu kuvua samaki. Ataishi na anauwezo wa kuyatawala mazingira ya kijijini kwao. Lakini kijana mwenzake wa kikojani aliyetumia miaka yake 11 darasani na kufeli, hataweza kwenda baharini na kuvua, lazima kwanza asomeshwe kama yule mwenzake ambaye hakukaa darasani.

Huyu anaishi bila elimu ya kuishi hata kama amekwenda shule kwa sababu hawezi kuyatawala mazingira yake na kuishi. Yule wa kwanza ana elimu ya kuishi hata kama hakwenda skuli. Elimu ya nadharia pekee haitawasaidia masikini. Panahitajika elimu shule na elimu ya maisha ya kijijini itolewe kwa mizania.

Chukua mfano wa wanafunzi wa Mkoa wa Mwanza ambako ufugaji na kilimo cha pamba dio shughuli kuu ya kiuchumi. Wanahitaji elimu itakayowasaidia kutekeleza shughuli hiyo kwa ufanisi.

Pamoja na umuhimu wa elimu ya nadharia ya kumaliza vidato vya juu na kupata shahada, mkazo uelekezwe katika maana mpya ya kumjengea mwananchi uwezo wa kuyatawala mazingira yake. Ulaya kwa sababu ya baridi kali, wanafundishana njia za kuhimili athari za baridi kali. Lakini Afrika elimu juu ya kujikinga na kupata malaria ni muhimu zaidi kuliko kuepuka joto kali wakati wa kiangazi.

Kuendelea kunahitaji watu waliohuru na walioelimika. Watu waendelezwe sio vitu. Watawala hawajafahamu maana ya madaraka na mamlaka. Wanadhani ni kutesa, kuonea, kutisha na kukandamiza raia.

Tagsslider
Share: