Makala/Tahariri

Hawakamatiki… ng’o

Mwandishi Maalum,

NIACHENI niseme nilichokigundua. Katika kutaja na kutajwa, wanatajana. Wale wanasema, natajana menyewe ka menyewe. Yule profesa angejua anaowataja kama ni madume ya mbegu, asingethubutu.

Labda anawafahamu ila tu hawajui. Tuseme hajui kuwa hii nchi inao madume waliotimia? Ile kuwa ameagizwa na mwenyewe ndio kapata ujasiri wa kutaja na kuwataja madume, sio? Raha kama nini….

Miaka tisa iliyopita, ndani ya kazi hiihii ya kuwajaza habari wananchi, na kuwazindua watawala wasilale maana wenye nchi wako macho, tulichapisha habari iliyobebwa na neno moja tu – hawakamatiki.

Hili neno tuliliandika kwa herufi kubwa ili msomaji apate uzito unaostahili kuhusu kilichokusudiwa akielewe. HAWAKAMATIKI. Tulilenga kuonesha ugumu wa kuwakamata mafisadi. Walikuwepo madume ya mbegu kama hivi wanavotangazwa sasa na kamati maalum. Wale walionekana ndio wanaofisidi au kutafuna nchi kwa mgongo wa kuwa sirikalini na chini ya kwapa za watawala – CCM.

Nakumbuka Mabere Marando – Alhamdulillah, Mzee Marando shikamoo, nakusalimia na kukuombea Mola akuongezee afya na uzima uendelee kufikiria namna ya kuitoa jamhuri katika dhulma inayoendelezwa na chama chao kile ambacho unakipinga sana – alilitamka neno hilo “hawakamatiki.”

Gwiji wa sheria huyu na mmoja wa waasisi wa mageuzi nchini kutoka mfumo wa ukiritimba wa siasa za chama kimoja, Marando katika kujibu maswali ya MwanaHALISI, gazeti dogo lenye mdomo mpana, alitwambia watu waliotajwa na kambi ya upinzani kuhusika na ufisadi wa uchumi wa Watanzania, hawawezi kukamatwa.

Kwamba sirikali ya CCM haina ubavu, na ikitokea imewakamata, basi itashindwa kuwashitaki mahakamani. Sababu kubwa ni kwamba ni wenzao wala nchi, wanapewa nafasi ya kula bila ya kunawa. Mapato ya kutafuna kwao mali na raslimali za taifa, sehemu nzuri inatumika kuendesha siasa za chama chao. Hawakamatiki.

Wakikamatwa ni aibu na fedheha kwa chama chao, kwa sirikali yao, kwa maslahi yao. Wakikamatwa na kushitakiwa inamaana watakapokwenda kwenye kizimba watayasema wanayoyajua kuwa ndio mambo ya wenzao katika chama chao CCM.

Wakipafikiria hapo tu, wanaufyata. Fyatu. Wanagoma kukamata mafisadi na wafisidi nchi. Kwa utamaduni huo wa kulinda maslahi ya chama chao na kulindana wao kwa wao, ndio maana leo hii nchi inaendelea kumong’onyolewa mali moja baada ya nyengine kama vile wenye nchi wamelala na kufukiwa udongo ulio mzito wa kinongo.

Lahaula kufa hakuna breki. Ingekuwepo inayofaa kuzuia kifo, kingepita bila kuondoka na yeyote.

Ndo haya yaliyotokea Jumatatu hii kutokana na kamati ya Ikulu kutaja majina ya watu wanene-wanene. Mule katika orodha hamna jina dhaifu kama nilivyo mimi nawe unayesoma mistari.

Wanene watupu usipime. Wanasiasa tayari na wale watendaji wakishajisikia, wamechoka kama watendaji sirikalini, wanaingia siasani na kugombea ubunge kupitia chama chao hicho.

Nilijisikia raha kinara wa kamati ameamua kumwaga mboga. Lakini baada ya mboga kumwagwa ikaingia mchanga, hailiki tena, naendelea kumsubiri shujaa wa kupindua bati ya ugali (dona). Pindua pindu huu uji mgumu utapakae mchangani. Usilike. Nasubiri nione mmwaga dona. Maskhara nini!

Wanaweza kuhojiwa lakini weeee, sijui. Kuwashitaki? Shughuli hii ninaisubiri kwa urefu wake. Kwani naye si wa chama hicho? Yumo leo au alikuwemo tangu sheria inatungwa mjengoni? Nitaandika makala kurasa mbili kumpamba maashaallah.

Hili nisisahau. ‘Nampongeza’ ofisa wa tanrodi Pwani ambaye Jumatatu alikesheza wafanyakazi wakiziba pechi kwenye barabara ya Bagamoyo. Unajua why? Jumanne mtumbuaji mapunye alitarajiwa apite kwenda kufungua daraja la Ruvu ya Bagamoyo. Watu hawa visa vya wali wa maji!

chanzo:mwanahalisi

Share: