Makala/TahaririZanzibar Daima

Kama Zanzibar haiwezi kuchangia Serikali Tatu, Tanzania Bara inachangiaje kwenye Serikali Mbili?

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Salmin Awadh Salmin, alisema hivi karibuni kwamba Zanzibar haitakuwa na uwezo wa kuchangia uendeshaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kama muundo wake utakuwa wa Serikali Tatu.

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa jimbo la Magomeni (CCM), “Zanzibar haiwezi kuchangia hata kwa asilimia 10“. Hayo aliyazungumza kwenye semina ya Wabunge wa Muungano na Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar mjini Dodoma Jumatatu ya tarehe 11 Novemba, 2013. Hoja yake kubwa ni kwamba Zanzibar ina uchumi mdogo na, kwa hivyo, mfumo wa sasa wa serikali mbili ndio unaofaa katika kuudumisha Muungano.

Nimekuwa mbunge kwa mwaka wa nane huu, nikiwakilisha maslahi ya Zanzibar kwenye bunge la Muungano, na lazima niseme kauli ya mtunga sheria mwenzangu huyu, Mzanzibari mwenzangu, ilinikirihisha. Wakati mwengine anasimama mtu kutokea upande wako wa nchi, analisema neno, unatamani uingie chini ya meza kukimbia aibu na fedheha. Huu ulikuwa ni wakati mmojawapo kwangu.

Riziki OmarHoja ya Mheshimiwa Awadhi ina mapungufu mengi. Mojawapo ni ikiwa kama hicho anachokisema ni cha kweli, basi kwa nini asipendekeze serikali moja tu kabisa, maana kwa vyovyote vile Zanzibar inatakiwa ichangie kwenye mfumo huu wa sasa uliopo, na kama haitaweza kuchangia wakati huo, haiwezi kuchangia sasa pia. Hii ni kuuambia upande wa pili wa Muungano kwamba umekuwa ukiibeba Zanzibar siku zote na sasa uendelee kuibeba milele.

Asichokieleza, na pengine asichokielewa Mheshimiwa huyu, ni kwamba hata katika mfumo wa sasa wa Muungano ambao yeye na chama chake wanautetea, Tanzania Bara haipo na hivyo haichangii kitu kwenye Muungano wenyewe. Iliyopo ni Zanzibar na ndiyo pekee inayochangia.

Inawezekana ikawa kauli hii ni ngumu kuielewa lakini maelezo yake yamo kwenye mapungufu makubwa ya kikatiba na kimuundo katika mfumo wa sasa wa Muungano, na ndio maana ni lazima kuubadilisha na kwenda kwenye huo wa Serikali Tatu, ambao yeye anatumia hoja hiyo dhaifu kuupinga. Nitafafanua.

Katiba ya sasa ya Muungano haina sehemu yoyote inayotaja matumizi ya Tanzania Bara kama Tanzania Bara ndani ya Muungano au angalau matumizi kwa mambo yasiyo ya Muungano kuhusiana na ‘Tanzania Bara’. Badala yake ina Vifungu Na. 133 mpaka 144 ambavyo vinahusika na Mambo ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano na ambavyo vinaashiria kuwepo kwa Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano tu.

Hiki ni kizungumkuti kilichomo kwenye Katiba yetu na ambacho kinaonesha sura halisi ya Muungano wetu. Kwamba Katiba inaelezea wazi kuwapo kwa Serikali ya Zanzibar na pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo ina madaraka ya kushughulikia mambo yote ndani ya, kwa Jamhuri ya Muungano na yote mengine ndani ya, na, kwa Tanzania Bara, lakini haiitengi Tanzania Bara katika matumizi na, hivyo, mchango wake kwa Muungano.

Dhamana hizi mbili kwa Serikali ya Muungano zimeleta mtafaruku na suitafahamu kubwa. Hii ni pamoja na Mgawanyo wa Mapato, Mahkama ya Katiba, Mahkama ya Rufaa kwa Tanzania, orodha ya mambo ya Muungano na Mwenendo wa Mabaraza ya Sheria.

Tuchukulie mfano na ukweli huu: kuna mfuko mkuu kwa Jamhuri ya Muungano ambao unaingiza mapato yote au pesa zote kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Hapa tafsiri safi na isiyo na mashaka ni kwamba mfuko huu unapaswa kutumiwa kwa mambo ya Muungano tu, kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba.

Lakini, Tanzania Bara haina mfuko mkuu kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano yanayohusu Tanzania Bara tu, ingawa Zanzibar inao mfuko wake mkuu kwa mambo yasiyohusu Muungano, yanayohusu Zanzibar tu. Sasa kwa nini matumizi ya Tanzania Bara kwa mambo yasiyo ya Muungano yagharamiwe na mfuko mkuu wa Jamhuri ya Muungano?

Kuna upungufu mwengine. Nao ni kuhusu Akaunti ya Pamoja ya Fedha. Kifungu cha 133 cha Katiba kinazungumzia Akaunti ya Fedha ya Pamoja ya Jamhuri ya Muungano, ambapo zitatiwa fedha kutoka michango ya serikali mbili kwa viwango vitavyowekwa na Tume ya Pamoja ya Fedha.

Kwa hiyo, kikatiba ni Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambazo zina wajibu wa kuchangia huduma na uendelezaji wa Muungano. Tanzania Bara haichangii kitu na wala haiwajibiki kuchangia kwa mujibu wa Katiba.

Ni hapa ndipo sasa unapoona kwamba kumbe kulitakiwa kuwepo na Serikali ya Tatu ya Tanzania Bara, maana ilivyopaswa hasa iwe ni hivi: suala la mapato lihusishe Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara.

Hadi hilo litakapokuwa, Zanzibar pekee ndiyo itakayosalia kuwa mchangiaji wa uendeshaji wa Muungano. Na hivyo ndiyo inayoibeba Tanzania Bara kisheria na si kinyume chake. Serikali Tatu nazije, ili kila mmoja atoe kwa mujibu wa apokeacho.

Zanzibardaima

Share: