Makala/Tahariri

Kichaka cha dhulma – Ardhi yote haiwezi kuwa mali ya Serikali

M.Ibrahim,

DK. SHEIN IKIWA MHE. MUFTI SHEIKH KABI HAKWAMBII, BASI SISI TUNAKUKUMBUSHA.

Imekuwa ni kawaida hapa Zanzibar, ukitaka uwaudhi viongozi wa Serikali basi watajie mambo ya dini.

Na hii ndivyo ilivyo mtu yeyote anae fanya mambo yanayo mchukiza Allah (S.W) mara zote huwa hapendi kusikia maovu yake yakitajwa, na hata inapotokezea akaweka channel ya TV au Radio akakuta kuna mawaidha yanayo husiana na uovu anao ufanya, basi huiondoa channel hiyo haraka sana ili asisikie.
Kumbe anaidanganya nafsi yake,kwani ikiwa yeye anajitoa fahamu basi yuko ambae hasahau na atamlipa kwa Mujibu ya Matendo yake.

Ndio maana leo huu kuna viongozi wengi wa Serikali unapowaambia wanavyo fanya ni dhulma waogope Akhera, kwa ujasiri kabisa wanakwambia Akhera ni mbali wacha kwanza tule maisha, huku wakijua wazi kwamba wanavyo fanya sivyo, na iko siku watakutana na Mola wao na watalipwa kwa mjibu ya matendo yao maovu wanayo yafanya.

Ajabu wababe hao wanapo karibiwa na umauti, khofu ya matendo yao huwa juu kwani wanajua wazi kwamba wana mwisho mbaya, lakini kwa vile bado wanapumua basi wao hawana haja ya mawaidha. Hufanya wapendavyo ilimradi mkono uende kinywani hawajali halali wala kharamu na wanakuwa wakali unapo wakumbusha kuhusu kumcha Mwenyezi Mungu (S.W)

Kutokana na ususuavu wa moyo na kujidanganya kwao, ndio wanakujana Msemo “SERIKALI HAINA DINI” Bila shaka ni kwamba Serikali haitoingia Peponi wala Motoni. Watakao ingia humo ni watu na Majini.

Sisi tujuavyo “SERIKALI NI JINA LA KINADHARIA” Ki ukweli hasa “SERIKALI NI WATU” na watu wana dini na wataadhibiwa kwa mujibu wa matendo yao hiki kisingizio cha Serikali kinacho tumiwa na wanadamu kuwafanyia watu dhulma, Mungu hakiangalii hasa. Anacho kiangalia ni matendo ya kila mmoja wetu.

Hivyo neno “SERIKALI” Lisitumike vibaya ikawa ndio kisingizio cha”KIKUNDI” cha watu kumdanganya Mwenyezi Mungu kwa kuwafanyia watu dhulma huku wakidhania kwamba kupitia neno Serikali watasalimika na uovu wanao utenda, hilo wasahau. Mwenyezi Mungu hadanganywi bali wanadanganya nafsi zao.

Hakuna malaika anae pelekwa kuandika amali za Serikali ila kila mmoja wetu anapelekewa Malaika wanao andika matendo yao hata yawe na udogo kiasi gani. Hivyo kutumia neno “SERIKALI” kama ni kivuli cha kufanyia maovu mbele ya Allah (S.W) ni kazi bure.

KWA LEO MADA YANGU INAANZIA HAPA.

DK. SHEIN KUSEMA KWAMBA ARDHI YOTE NI MALI YA SERIKALI, HII NI DHULMA WALA HUNA AMALI UTAKAZO WEZA KUWALIPA WANAO DHULUMIWA.

Kwa yeyote mwenye kumuogopa Mungu awe DK. Shein au kiongozi yeyote Serikalini,wawe Wabunge au Wawakilishi wakumbuke kwamba wamebeba dhima mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kufumbia macho jambo linalokwenda kinyume na dini ya kiislamu, huku wakijifanya wacha mungu wakubwa sijui wanamdanganya nani.

Nashangaa hakuna muwakilishi wa CCM wala wa CUF aliye wahi kusimama akapinga kauli hii, kwani kwa hakika kauli hii iko kinyume na dini ya kiislamu na wanao itekeleza ni waislamu. Hapa ndipo tunapoona neno “SERIKALI” Linapo tumika kuvunja amri ya Mwenyezi Mungu huku wavunjaji wakijiona wamekwepa adhabu ya Allah kwani itakayo tiwa motoni ni Serikali na sio wao.

Ni vizuri viongozi wetu wakakubali kukosolewa, Ardhi yote haiwezi kuwa mali ya Serikali, kwani kuna Ardhi ambayo inamilikiwa na wananchi ki uhalali kama wanavyo miliki mali nyengine. Juzi nimesikitika sana na kukatishwa tamaa na DK. Shein alipo kwenda kuweka jiwe la Msingi Nyamanzi kwenye mradi unaojengwa nyumba za kisasa.

Dk. Shein alisema kuwa Ardhi yote ni mali ya Serikali, na Serikali ndio yenye mamlaka ya kuhaulisha matumizi ya ardhi kwa malengo mbali mbali na iwapo Serikali itahitaji kuitumia ardhi inalazimika kutoa fidia za mali za wananchi zilizopo kwenye eneo hilo kama vile nyumba na vipando vya miti vya kudumu.

Ikumbukwe kwamba kuna watu wanamiliki ardhi yenye thamani kubwa na haina nyumba wala vipando, Jee! Mtu kama huyu unapo mchukulia Ardhi yake hujamdhulumu?

Tunaiomba Serikali itangaze kuwa Adhi ambayo “haina mwenyewe” hiyo ni mali ya Serikali na endapo Serikali itaamua kuchukuwa ardhi ya mtu, basi mwenye adhi hiyo atalipwa kwa mujibu wa ukubwa na fidia inayo endana na thamani ya ardhi hiyo, kwani kuna ardhi zina thamani kubwa kuliko nyumba na vipando.

Ama kuhusu Serikali kukodisha Ardhi yoyote kwa wageni hilo halina tatizo, lakini baada ya wamiliki kulipwa fidia ya Ardhi yao na sio vipando au nyumba hiyo ni dhulma na kesho Akhera mtakuwa hamna jinsi mtatakiwa mrejeshe haki za watu.

DK. Shein wewe mda huu ndiye unae chunga haki za watu, kesho Akhera wapambe wako wote watakukimbia Utakwenda ulizwa na utatakiwa umlipe kile aliye dhulumiwa katika utawala wako.Jee! Amali hizo unazo?

Piga hesabuza amali zako toa haki za watu angalia utabakisha kipi kitakacho kunusuru usiingie Motoni. Ukikuta huna basi Muogope Allah hakika iko siku utarejea kwake amali zako zigawiwe kwa kila aliye dhulumiwa hapo ndipo utagundua kwamba umefilisika tena kufilisika kuliko kubaya kabisa. Kumbuka ardhi ni mali kama mali nyengine haiwezekani Serikali ichukuwe mali za watu kwa njia ya batwil.

Kwa vyovyote vile Ardhi ya watu inapaswa kulipiwa fidia kwani ndio sheria ya kiislamu inavyo elekeza, Kumbuka ikiwa “SERIKALI HAINA DINI” Basi watu wana dini hamna ujanja. Dhulma ni dhulma tu.

Nikukumbushe DK. Shein na Serikali kwa ujumla kwamba “ARDHI NI MALI YA MWENYEZI MUNGU” lakini yeye mwenyewe amewamilikisha waja wake, na umiliki huo atautambua mpaka kesho Akhera, iweje Serikali iwanyang’anye?
Namalizia kwa kusema:-..

!!!” Wema hauozi. Dhambi haisahauliki. Allah Mlipaji hafi. Fanya unalotaka unavyotenda ndivyo utakavyolipwa.

Ardhi yote haiwezi kuwa mali ya Serikali, hiyo ni dhulma tena hakuna dhulma kubwa kama kudhulumu ardhi za watu.

Tagsslider
Share: