Makala/Tahariri

Kushambuliwa kwa CUF

KUSHAMBULIWA WAFUASI WA CUF: SUBIRA INA MIPAKA

Na: Mwandishi Maalum

Katika hali tunayoweza kuiita ya kutisha iliyotokana na Uharamia wa kundi linalosadikiwa kuwa la ‘janjaweed’, wafuasi kadhaa wa CUF wameshambuliwa na kujeruhiwa vibaya wakiwa njiani kutokea katika mkutano huko Makunduchi.
Pamoja na ubaya wa tukio lenyewe, nasema matukio kama haya kutoka kwa makundi yanayosadikiwa kuwa chini ya Chama tawala, yamekuwa ya kawaida sana dhidi ya CUF. Tangu chama cha CUF kusajiliwa rasmi mwaka 1992, watu kadhaa wamepoteza maisha na wengine kubakia na ulemavu wa kudumu kutokana na adhabu ya vyombo vya dola na vikundi vya kiharamia vilivyo chini yake.
Cha kushangaza zaidi, yanapotokea matukio kama haya hakuna hatua yoyote inayochukuliwa; si kwa upande wa CUF wala Serikali. Hii inanipa taswira ya kuanza tena kuihakiki nafasi ya binaadamu kwa watawala wetu na kwa viongozi wetu wa chama cha CUF pia. Laiti siogopi kukumbusha machungu yaliyowahi kutokezea, basi ningetaja mfululizo wa matukio ambayo wana CUF wamekuwa wakifanyiwa hakuna lolote lililofanyika.

Tukio la juzi, limeongeza tu idadi ya matukio kadhaa ya kiharamia wanayofanyiwa wananchi wasio hatia na makundi hayo maovu yanayosimama kwenye mwavuli wa dola. Kwa bahati mbaya, wanaohusika na matukio hayo wanajulikana kwa majina na wanapokaa.

Kwa mfano, matukio ya juzi yalitekelezwa katika mpango nzima ulioandaliwa na watu wanaojulikana. Gari lililotumika ni gari la mtu maarufu ambaye kwa jina anaitwa BHAA STYLE. Ndani ya gari hilo, walikuwemo vijana wengi waliokuwa wamevaa fulana za njano ambao waliwashambulia watu hao wasio na hatia.

Ikiwa gari liliotumika inajulikana, kwa nini mmiliki wa gari hakushikiliwa kwa mahojiano? Jeshi la polisi limechukua hatua gani juu ya tukio hili? Nani katika viongozi wa Serikali ukitoa yule wa CUF, katoa kauli juu ya matukio kama haya? Jawabu ni hakuna. Ukiuliza kwa nini iwe hivi. Majibu yanayotoka ndani ya chama cha CUF yanakuwa ni yale yale tuliyozoea kuyasikia tangu mwaka 1992 – ‘tuwe na subira!’, ‘hatulipizi kisasi’!

Kauli kama hizi sio mbaya kwa kweli kwani hata Bwana Mungu anazifurahia sana lakini… nasema lakini inategemea na hali na mazingira yalivyo. Uzoefu wa miaka 20 ya CUF, unaonyesha kuwa wahujumu na maharamia wanaoenga kuwadhuru wanachama wa CUF wamekuwa wakiuchukulia udhaifu wa kauli kama hizi za viongozi, ili kupata wepesi wa kufanya Uharamia wao. Na ndivyo hivi kila siku wanazidi kufanya tena na tena!

Mwaka 2005, tulishuhudia janjaweed Unguja, wakiwabaka wanawake nje chochoroni. Sisi wengi wetu tupatao maelfu, tukitishwa na kupelekwa mbio na kikundi hicho kidogo cha vijana waliokata tamaa na maisha na kuwaacha dada zetu hao wakifanyiwa uharamia huo hadharani. Kuna wanaume kadhaa waliobakwa na kupitiwa kinyume na maumbile. Wachilia mbali waliojeruhiwa vikali na wanamgambo hao. Sisi kama sisi, CUF tulichukua hatua gani?

Kosa lisipotolewa hukumu, ikaadhibiwa hupata uhalali. Likaselelea, na likawa mazoea. Na ndio kama hivi tunavyoona leo. Kila ukaribiapo uchaguzi, vijana hawa huwezeshwa kuja kutia adabu wafuasi wa CUF wakiamini hawatafanywa lolote. Tabia ya kosa, huzaa kosa. Vijana hawa wanapofanikiwa kututisha katika hatua ya kampeni, nasi tukatishika tusiwachukulie hatua, ndipo hawa hawa wanapojitokeza siku ya uchaguzi, wakapiga kura mara elfu kila mmoja. Kisha wasitosheke, wakarudi tena usiku kuiba kura! CUF tunabakia tukikariri uradi wetu wa ‘tuwe na subira na tusilipize kisasi’ ambao hata mungu kwa hali ilivyo sasa haoneshei kuwa anauridhia.

Nguvu ya vikundi kama hivi hapa Unguja imetokana sana na woga wa wafuasi wa CUF na viongozi wao hapo. Kama kuna mtu anayebisha juu ya hili, natoa mfano hai. Mwaka 2005, vijana wa janjaweed, walipelekwa Pemba kufanya uharamia kama waufanyao Unguja. Haukutimia mwezi, walikimbia wote wakaja zao Unguja. Nini kiliwakimbiza Pemba? Nini hasa
Jibu liko wazi. Kwa miaka mingi kule Pemba vikipelekwa vikosi vya kuwahiliki wananchi. Tukianzia na ‘Melody’ wale FFU wa mwaka 1995. Wananchi wa Pemba walipoona wanaonewa kila siku na chama hakitoi kauli yeyote, wala si serikali haijali, wakaamua kujichukulia hatua mikononi mwao. Na hiki ndicho kilichowakimbiza janjaweed Pemba miaka ya 2005. Tangu Pemba waamke na kuanza kujitetea, matukio ya kiharamia kama haya dhidi yao, yamepungua au tuseme hakuna.
Lakini kwa vile Unguja, tumeshikana na neno subira huku tukiumizwa na kudhulumiwa kila siku, basi sidhani kama kuna popote tutakapofika zaidi ya kuzidi kupata maumivu ya majeraha ya mashambulizi ya vikosi kila uchao. Kwa vile wahalifu wa jambo hili wanapewa kichwa na wenye uwezo na kauli, na wale ambao wanafanyiwa wanaonekana kustahamili kila siku, basi sidhanii kama haya yatakwisha.

Na ikiwa hali kama hii itaendelea, na bila shaka inaendelea, ushauri wangu kwa wana CUF ni kuwa wanapokwenda mikutanoni, ipo haja wavae mahelmet na nguo za chuma.
Kufanya hivi kutawapunguzia majanga yatokanayo na janjaweed. Ama kuhusu vitendo vya kuwabaka wanawake wanatoka mikutanoni, ushauri pia ni mwepesi sana, ni kuvalia ‘kufuli’ za chuma na funguo za kufuli hizo zikaachwa nyumbani mpaka watu watakaporudi mkutanoni kwani bila hivyo, wanachama na wafuasi wa CUF watakuwa wahanga wa janjaweed na bahati mbaya, hakuna hata wa kuwatetea!

Pamoja na hayo namalizia kwa kutoa ushauri kuwa ingawa subira ni njema, ifike siku iwe na mipaka. Ingawa tumesema hatulipizi kisasi, tuna haki ya kujitetea na kujihami. Sawa tusilipize kisasi, lakini TUJIHAMI watatumaliza!

Tagsslider
Share: