Makala/Tahariri

Kwa nini serikali idhaniye siku zote ndiyo yenye haki?

Ahmed Rajab

Na Ahmed Rajab

PANAWEZA pakawa utawala mbovu unaoendeshwa na watu ambao wao wenyewe si lazima wawe wabaya. Huenda labda wakawa wazembe au watu wasio na uelewa mkubwa wa mambo ya utawala bora. Lakini si watu wenye hulka ovu.

Jambo lililo baya zaidi na linalokirihisha ni kuwa na utawala ulio mbovu unaoendeshwa na watawala ambao wenyewe ni watu wabaya, washari na wakorofi. Watawala wenye nafsi zilizoroa uovu.

Watawala wa sampuli hiyo, wenye kuchusha na makuruhi, huwa na tabia ya kutaka kumshughulikia yeyote yule mwenye kuwakosoa. Huwatisha na haraka huwachukulia hatua. Huwa hawaoni raha ila ulimwengu mzima unapokuwa unawashuhudia wanapochukua hatua hizo za kuwadhalilisha wananchi wenzao.

Sio tu kwamba watawala wa aina hiyo huwa wanajiona kuwa ni wababe au wanafanya mambo kibabe lakini hufanya mambo kana kwamba hakuna tofauti baina yao na majambazi.

Siku moja mwandishi wa Kiingereza, Thomas Love Peacock, alikuwa akiandika riwaya yake fupi iitwayo “The Misfortunes of Elphin” (Misiba ya Elphin) aliyoichapisha mwaka 1829.

Alipokuwa akiiandika riwaya hiyo, Peacock alitafuta neno muwafaka la Kiingereza lenye kuelezea utawala au serikali inayoendeshwa na wakorofi na waovu.

Hao ni watu wabaya kabisa katika jamii. Wabaya kwa vitimbi vyao, wabaya kwa uovu wao na wabaya kwa uchafu wao. Ni wabaya kwa kila tafsiri uijuayo ya ubaya.

Peacock hakulipata neno lenye kuuelezea utawala wa aina hiyo. Akakaa, akafikiri na akaibuka na neno “kakistocracy” lenye kutokana na neno la Kigiriki “kakistos” lenye maana ya “-baya zaidi”.

Kwa Kiswahili tunaweza kusema kuwa utawala wa “kakistoskrasi” ni utawala wa watu wabaya, watu waovu. Ni utawala wenye kwenda kinyume na mfumo wa “kidemokrasi” na huendeshwa na watu wasiofaa kutawala.

Hebu tutafakari kidogo na tujiulize maswali mawili matatu. Ikiwa watu wasiostahili kutawala ndio wenye kutawala, kwa sababu mfumo wa utawala ni wa kakistoskrasia na si wa kidemokrasia, basi jamii ndio iyamezee maovu yao na ijifanye kama hakuna lililotokea?

Kufanya hivyo ndio kuiheshimu Katiba au kuisaliti Katiba?

Ikiwa Rais anaonesha dalili za kupenda kuendesha mambo kinguvunguvu ni haki kumuelezea kuwa ni dikteta ili aweze kujirudi? Na ikiwa wakuu kadhaa wa serikali yake nao pia wanajitia kumuiga ni sawa kuielezea serikali yake kuwa ni ya kidikteta?

Au ni bora kujitia uungwana na kumyamazia bila ya kumkosoa?

Viongozi wenye kumuitikia Rais kwa “hewala Bwana” kila anapotangaza uamuzi mpya bila ya kumtanabahisha anapokosea au kumzuia anapoteleza huwa wanamsaidia kuitawala nchi ipasavyo au huwa wanamsaidia ajitose yeye na nchi yake?

Katika mfumo wa kidemokrasia ukosoaji dhidi ya udikteta huhitajika na huhimizwa kwa nguvu. Huhimizwa kwa sababu ukosoaji wa namna hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kwamba nchi inaendeshwa kwa kufuata kanuni na misingi ya utawala wa bora.

Wakosoaji huwa si mashujaa tu bali katika ushujaa wao huonesha kuwa wao ni wazalendo na kwamba uzalendo wao ndio unaowahamasisha wawe wakosoaji.

Lakini wanaotawala katika mfumo wa “kakistoskrasi” wanauona ukosaji aina hiyo kuwa ni usaliti. Ndio maana mtu kama Tundu Lissu saa zote huingia matatani. Huonekana kuwa hana haki ya kusema kweli anayoiona.

Serikali imekuwa ikimfanyia kila hila Tundu Lissu lakini kila mara huibuka mshindi kwa sababu anazijua haki zake na namna ya kuzitetea. Ilijaribu kumzuia hata asichaguliwe kuwa rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) lakini ilishindwa.

Kwa mujibu wa Serikali, maneno na vitendo vya Lissu na wengine wenye muelekeo kama wake ni usaliti. Kwa upande mwingine, inachosema Serikali ndiyo haki, ndiyo kweli. Pasiwepo na wa kubisha. Hapa ndipo Tanzania ilipofika 2017.

Hali inayowakuta Watanzania siku hizi haiwabinyi na kuwabana wapinzani peke yao. Fimbo ya usaliti hawapigwi wao tu. Wanaweza wakapigwa nayo hata wabunge wa chama kinachotawala wanapoikiuka mipaka waliyowekewa.

Mwenyekiti wao, kwa mfano, anaweza akakutana na wapinzani wakati wowote autakao lakini mwanachama mwingine wa chama chake akifanya afanyavyo yeye huwa ni msaliti.

Watawala wana wajibu wa kuwaheshimu wanaowatawala. Lakini hivi sivyo wafanyavyo watawala wetu. Wao hawadhani kwamba kuna yeyote mwenye haki ya kuheshimiwa ila wao. Hawaamini kwamba mara nyingi wananchi wenzao, wakiwa pamoja na wapinzani, ndio huwa katika haki.

Iwapo watawala hawaoneshi unyenyekevu kwa wananchi wanaowatawala, hasa wale wasiokubaliana nao kisiasa, ndio waachiwe waendelee vivyo hivyo bila ya kujitokeza wa kuwakumbusha kwamba wanafurutu ada na kwamba haya hayastahiki katika karne ya 21?

Hapa ndipo panapozuka suala la umuhimu wa kuwa na taasisi za kuweza kuwadhibiti watawala wenye kuamini kuwa wao tu ndio wenye haki na kwamba kazi yao ni kuwadhibiti wananchi wanaojaribu kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuwakosoa.

La kusikitisha Bunge la Tanzania kwa lilivyo sasa haliwezi kuuzuia utawala wa kimabavu unapozidi kuonesha meno yake ya kutisha. Huenda lisiwe na uwezo wa kumzuia Rais lakini lina nguvu za kutosha za kuweza kuizuia serikali yake isiweze kutawala kwa njia zinazoonekana kuwa ni za kimabavu.

Mengi yamekuwa yakisemwa mitaani karibuni kumhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye hivi ninavyoandika makala haya Jumatatu asubuhi kulikuwa na tetesi kwamba huenda akatumbuliwa na Rais John Pombe Magufuli. Hata hivyo, inaonesha amenusurika kwani Rais amempongeza, amemkinga na kumwambia aendelee “kuchapa kazi”.

Pengine baadhi ya simulizi zinazomhusu Makonda zimetiwa chumvi kidogo. Lakini hata zikiwa na chembe tu ya ukweli kuendelea kumsitiri kwa kumvisha joho la heshima ya cheo chake huenda kukamvimbisha kichwa na kumsababisha aendelee kufanya mambo yasiyofaa. Miongoni mwayo ni kuutumia wadhifa wake kuwa kama jukwaa la kuwadhalilisha waliomkosa.

Hulka yake Makonda inatia wasiwasi. Inamfanya mtu ajiulize maswali mengi si kumhusu yeye mwenyewe tu bali hata kumkuhusu yule aliyempa wadhifa alio nao na anayeendelea kumtetea.

Inasikitisha kwamba mpaka sasa ninapoyaandika makala haya, Magufuli hakumkanya au hata kumpa nasaha ya haja ya kutokiuka maadili ya uongozi. Linalosikitisha zaidi ni kwamba hakuna kiongozi yeyote wa ngazi ya juu, tukimuacha Nape Nnauye, waziri wa habari, aliyeonesha kuingiwa na wasiwasi na namna Makonda anavyojifanyia mambo.

Swali kuu ni kwa nini hakuna anayeweza kumgusa Makonda juu ya kwamba kuna shutuma nyingi dhidi yake na ushahidi ulio bayana kuwa haendeshi mambo kwa mujibu wa maadili ya utawala wa kikatiba? Tumesikia namna alivyokuwa akiwashughulikia wakuu wa wizara ya ardhi, wilayani Kinondoni, jinsi alivyokuwa akiwakemea, jinsi alivyokuwa akivimbisha musuli na kuonesha kibri.

Waziri Nnauye ameunda Tume ya watu watano kumchunguza Makonda kwa shutuma za kuzivamia ofisi na studio za Clouds Media Group usiku wa Machi 17 akiwa na askari wenye silaha. Inasemekana kwamba lengo lake lilikuwa ni kushinikiza habari aitakayo irushwe katika kipindi cha Shilawadu.

Kama ni kweli hiyo ni dhambi kubwa ya kuuingilia uhuru wa habari na ndio maana Nnauye ameshtuka kiasi cha kumfanya aunde tume maalum ya kuichunguza kadhia hiyo.

Lakini Magufuli anasema kuwa yote hayo ni mambo yasiyo na msingi. Ubaya wa mambo ni kwamba Magufuli ana ugonjwa wa kujiona kwamba yeye ni yeye na hakuna amshindaye katika uongozi na kwamba ana haki ya kufanya atakalo. Ndio maana hazisikii kelele za wenye kutaka Makonda awajibishwe.

Si bure kwamba chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sasa kimetangaza rasmi kuwa na mgogoro naye Makonda.

Siku hizi mtu yeyote yule mwenye kuwakosoa watawala na hususan kwa namna wanavyotawala husingiziwa kuwa ni msaliti.

Watawala wanalitaka taifa zima liwe linawaunga mkono. Liwe linawashangilia na kuwachezea ngoma japokuwa wayafanyao ni karaha na ni yenye kuwafedhehesha wao pamoja na taifa.

Wao wanahisi kwamba maana ya uzalendo ni kuwa mtiifu kwa kiongozi badala ya kuwa mtiifu kwa taifa kwa kuyapigania maslahi yake na kuutetea uungwana wake.

Nathubutu kusema kwamba hata kuiasi serikali, hususan iliyo katika mfumo wa “kakistoskrasi”, huenda kukawa ni kitendo cha kizalendo. Kwani uzalendo ni nini? Uzalendo ni kuwa na mahaba na nchi yako; ni upendo wa nchi na kujitolea au kujisabilia kwa ajili ya nchi hiyo.

Si dhambi bali ni haki ya raia kuiasi serikali pale raia anapohisi kwamba serikali inajifanyia mambo ya ovyo na kwamba inakwenda kinyume na misingi ya Katiba. Ndiyo maana Tanzania inahitaji iwe na Tundu Lissu zaidi ya huyu mmoja iliye naye.

Yeye ni tunu ya taifa na si upinzani tu bali hata Serikali, ingelikuwa makini, ingepaswa kujivunia kuwa na mtu kama huyu katika jamii.

Ni mwanaharakati msomi, mwanasheria aliyebobea katika fani yake, mwenye kupigiwa mfano kwa uwezo wake wa kuvichambua vifungu vya sheria anapokuwa anatetea haki na utawala bora.

Share: