Makala/Tahariri

Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Mlango wa Pili: Mirengo ya Kizalendo na Mapinduzi

Na Prof. Harith Alghassany
Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mapinduzi yalikuwa, kwa kiasi fulani ni kisasi dhidi ya utumwa, yaliofanywa na watu na kufanyiwa watu ambao hawahusiki na utumwa. —Yasmin Alibhai-Brown

Fikra ya uzalendo ya Pan-Africanism ambayo ilikuwa ikiongozwa na hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa kila asiye “Muafrika” ni mgeni Afrika na kwa hiyo asiyekuwa na asili yenye kutoka bara la Afrika basi ni mgeni Zanzibar hata kama alizaliwa na alikuwa na mizizi mirefu ndani ya nchi hiyo. Na aliyekuwa ana asili ya Kiafrika na hata kama hakuzaliwa na wala hana mizizi mirefu Zanzibar basi ana haki zaidi juu ya kuitawala Zanzibar kwa sababu ni “Muafrika.”

Neno “Afrika” linatokana na neno Ifriqiya, ambayo kihistoria ilikuwa ni jimbo la Kaskazini ya Afrika katika nchi ambayo leo inajulikana kwa jina la Tunisia. Ibn Khaldun, mwanafalsafa wa historia maarufu duniani na baba wa sayansi ya jamii (sociology) aliyeishi miaka 676 nyuma, anamtaja katika kitabu chake Mfalme wa zamani wa Yemen Afriqus b. Qays b. Sayfi, ambaye “aliishi wakati wa [Nabii] Musa au labda kidogo kabla yake” na kuwa wanahistoria wanajisemea kuwa ndie alieivamia “Ifriqiyah”.1 Ibn Khaldun hakuwa anashuku kuwepo kwa mfalme kutoka Yemen ambaye akijulikana kwa jina la “Afriqus” ambalo inawezekana sana likawa moja wapo wa asili ya jina la “Afrika.” Wako wenye kusema neno “Afrika” linatokana na lugha ya kienyeji ya Afrika ya Kaskazini iitwayo “Berber.”2 Lini bara la Afrika lilianza kujulikana kwa jina la “Afrika” ni jambo liloanzishwa na wakoloni wa kizungu na ni suala linahohitajia kuthibitishwa kwa ushahidi wa kiutafiti.

Fikra zilizozagaa ni kwamba Zanzibar ni ya Muafrika mweusi mwenye asili ya bara peke yake kuliko Muafrika mwingine yeyote hata kama amezalika huko Zanzibar kwa daraja nyingi. Fikra hii inatokana na fikra nyengine iliyokalishwa kwenye fikra za wengi yakuwa “Bara la Waafrika” ni Bara la watu weusi tu, na labda tuseme la Mungu Mweusi. Na watu weusi wenyewe ni wanaotokana na asili ya Kibantu na Wabantu wenyewe wawe hawana asili au uhusiano wa karibu na Waarabu.

Na mizizi ya “Waafrika ni Wabantu peke yao” inalitenga kundi kubwa la Waafrika wa Afrika ya Kaskazani, Ethiopia, Somalia, Djibouti, Eritrea, Mauritius, wazungu wa Afrika Kusini, au Zimbabwe, Kenya, pamoja na Mayahudi na Wahindi wazalendo wa Afrika, na makabila yote ya kibinaadamu ambayo yana chimbuko lao Afrika.

Hapana shaka yoyote kuwa Afrika imedhulumiwa na Waafrika weusi bado hawajachukuwa dhamana ya kushiriki kwa machifu na makabila yaliyoshiriki kuwatia utumwani Waafrika wenzao. Haya yameelezwa kwa ufasaha ndani ya kitabu Zanzibar: Kinyang’ayiro na Utumwa na mwaka 2009 kimetoka kitabu muhimu chenye kichwa cha maneno It’s Our Turn to Eat (Sasa ni Zamu Yetu Kula) ambacho kinaelezea kwa undani namna ufisadi ulivyokumbatiana na ukabila nchini Kenya.3

Historia yote na kharita (ramani) zenye kulionyesha bara la Afrika kabla halikupewa jina la “Afrika” huonekana kuwa haina maana. Kwa hiyo kharita za miaka ya 1860 na za nyuma sana kabla ya hapo, zenye kuonyesha eneo la Afrika Mashariki kuwa likijulikana kama ni “Ethiopia” au mwambao wa “Azania” au “Sudan” au “Zinjibar” huonekana ni dalili tosha za ushahidi wa ubeberu kabla ya “Waafrika” kujitawala baada ya Wazungu kulipa bara lote jina la “Afrika.”

Tawi la uafrika ni mtu mweusi lina mzizi mrefu katika kuyakana makabila mengine ya Kiafrika ambayo yaliwasili mwambao wa Afrika hata kabla ya kuwasili Wabantu Pwani ya Afrika ya Mashariki. Anaelezea Profesa Ibrahim Noor Shariff:

Kuna baadhi ya watu wanafikiri kuwa “Waafrika” wote ni “Wabantu” na kuwa kila asiyekuwa Mbantu ni mgeni Afrika Mashariki. Ukweli ni kuwa “Wabantu” ndio katika waliofika Afrika Mashariki, khasa sehemu za Pwani karibuni kabisa. Kwa mfano, “Wabantu” Wagiriama wamewasili “Giriama” Kenya kama miaka mia tatu iliyopita. (Soma kitabu cha chifu wao R. G. Ngala kiitwacho “Nchi na Desturi za Wagiriama.” E. A Literature Bureau. 1949. Ukurasa wa 2).4

Mohamed Said ni msomi wa kwanza kabisa aliyeweza kuweka mkono wake juu ya mpigo wa moyo wa propaganda ya TANU kuhusu suala la Ubantu na wasio Wabantu, yaani, Waislamu. Kwa mujibu wa Mohamed Said:

Katika mwaka 1955, kikundi cha TANU Bantu kiliundwa makhsusi kukabiliana na tatizo la udini kutokana na hisia za baadhi ya Waislam ndani ya TANU. Tangu kuundwa kwa TANU, kulikuwa na hisia ya kupinga Ukristo ndani ya chama. Tatizo hili la udini lilikuwa likichemka pole pole na chini kwa chini ndani ya TANU.

Ilikuwa kazi ya kikundi cha TANU Bantu kuwafichua na kuwapiga vita wanachama wa TANU waliokuwa na hisia kama hizo. Bantu ilifanikiwa sana katika hili hadi kudiriki kupiga marufuku mamkuzi ya Waislam ya “Asalaam Alaikum” (Amani iwe juu yako) baina ya Waislam kwa msingi kuwa ilikuwa inawabagua Wakristo na hivyo inawatenga…Mamkuzi yale ya Kiislam yalionekana kama yanakwenda kinyume na imani ya TANU na ilishauriwa kuwa “salaam aleikum” ipigwe marufuku isitumike. Ikiwa mathalan kwa kusahau Muislam mmoja atatoa salaam kwa Muislam mwenzake, kwa kawaida angejibiwa “Alaikum salaam” maana yake “Amani iwe juu yako pia.” Badala ya majibu haya mazuri, majibu yaliyobuniwa na Bantu yalikuwa—“Ahlan tabu” maana yake—“ah tabu tu!”5

Lengo la Bantu Pan-Africanism si kuutumikiya uhakika wa historia au kuwapenda Waafrika na kuwachukiya Waarabu, bali ni kulipuuza suala zima la makabila, tamaduni, na staarabu na dini ya Kiisilamu zilizokuwepo Afrika ya Mashariki kabla ya kuwasili kwa Wabantu na khasa kwa Ukristo kutoka Ulaya. Mgeni mmoja kutoka Umoja wa Mataifa aliyekwenda kuitembeleya taasisi ya kihistoria ya kitaifa iliopo Dar es Salaam, alisikitishwa sana kuona historia ya Waarabu Tanzania imeshirikishwa na kitu kimoja tu: utumwa. Wanahistoria na wataalamu wa ilimu ya athari (archaeology) wanashindana na kuukiuka au kuuficha ukweli wowote ule wenye kuonyesha kuwa hakujakuwepo makabila yasiyo ya Kibantu Afrika ya Mashariki kabla ya kuwasili kwa Wabantu.

Ile historia ndefu ya Bahari ya Hindi yenye kuiunganisha Afrika ya Mashariki na ya Kati na Bara Arabu, Uajemi, Bara Hindi, Uchina, Misri, n.k, huwa inaonekana haina maana kwa sababu haikidhi haja na hoja za kisiasa. Au kama itatambulikana itakuwa kujengea hoja kuwa ilikuwa historia ya kibeberu iliyokuwa na kituo chake Zanzibar. Marejeo ya historia ya Afrika ya Mashariki yaliyoandikwa na akina Ibn Battuta, au Muruj al-Dhahab wa Ma’adin al Jawhar cha Al-Masudi, au Kilwa Chronicles iliopo jumba la makumbusho la Uingereza, hayapitiwi na wasomi wengi wa Tanganyika waliojazwa na kujaa chuki dhidi ya makabila mengine yasiyo ya Kibantu ya Afrika ya Mashariki.

Katika utangulizi wa kitabu chao Mapambano ya Ukombozi Zanzibar, B.F. Mrina na W.T. Matokke wa Chuo Kikuu cha Chama, Kivukoni, wanafafanuwa kuwa: “Madhumuni ya kuandika kitabu hiki ni kujaribu kukusanya pamoja data kwa ajili ya kuweza kufundishia. Jitihada zilizofanywa zilikuwa na lengo la kupata maandishi ambayo yanaweza kutumiwa na walimu na wanafunzi katika Vyuo vya Chama Cha Mapinduzi.”6

Pia katika sifa iliyopewa kitabu na kampuni ya uchapaji, Tanzania Publishing House, ni hii propaganda bila ya kizoro ambayo nainukuu kwa urefu:

Historia ya Afrika ni hadithi ndefu ya mapambano ya wananchi wake dhidi ya ubeberu ili waishi katika ardhi yao kwa amani na ustawi. Visiwa vya Unguja na Pemba havikukwepa adha ya kuwa sehemu ya uwanja wa mapambano hayo na kwa vizazi vingi vimekuwamo katika harakati moja baada ya nyingine hadi Mapinduzi ya 1964 yaliyokatilia mbali minyonyoro ya ukoloni mkongwe na kuashiria maisha mapya. Mapambano ya Ukombozi Zanzibar ni kitabu cha kwanza kuchapishwa kinachofuatilia kwa undani safari ndefu ya wananchi wa Zanzibar kuelekea ukombozi tangu majilio ya kwanza ya wageni kwenye pwani ya Afrika Mashariki yapata miaka 2000 sasa….Ndugu Mrina na Ndugu Matokke wamefanya utafiti wa hali ya juu uliowawezesha kutalii sehemu nyingi za historia ya Zanzibar ambazo hazijaguswa na mwandishi mwingine yeyote. Matokeo yake ni kitabu cha lazima kwa wanafunzi wa historia na siasa katika ngazi zote.7

Bila ya kutowa ushahidi wa marejeo yoyote yale, Mrina na Matokke wanakiri kuwa “Pwani ya Afrika Mashariki ilikuwa imefikiwa na wageni kutoka sehemu za mashariki ya mbali yapata miaka 500 kabla ya kuzaliwa Kristo.”8 Katika safari yao ndefu ya “utafiti wa hali ya juu” Mrina na Matokke hawakutaka kujuwa nini kimeandikwa katika kitabu maarufu duniani The Periplus of the Erythrean Sea kilichoandikwa miaka 2000 iliyopita kuwepo kwenye pwani ya Afrika Mashariki kwa karne nyingi tawala za kifalme za Arabuni ya Kusini na kuwa Waarabu “walikuwa wameingiliana na kuowana na wenyeji na wakiifahamu pwani nzima na lugha zilizokuwa zikizungumzwa.”9

Mrina na Matokke hawakujali kuyapitia matokeo ya utafiti makini wa wanahistoria na mabingwa wa ilimu ya athari (archaeology) au hata Biblia yenye kumtaja Kush na watu wa kutoka ustaarabu wa Kikushi ambao wanaiunganisha Afrika Mashariki na Somalia, Ethiopia na Bara Arabu. Lakini hilo halikuwa lengo lao na ndio maana safari yao haikuwapeleka huko. Lengo lao lilikuwa kupiga siasa na kuziharibu akili za walimu na wanafunzi kutoka Zanzibar na Tanganyika.

Misafara ya masomo ya dhiki na dhuluma

Hadithi dhidi ya Waswahili na Waarabu ambazo hazitegemei aina yoyote ile ya ushahidi zimekithiri kama uyoga kunako vichwa na nyoyo zenye kuipa jina baya Dola ya Zanzibar ili ipatikane sababu ya kuiangusha au kuizuwia isije juu. Yako mambo mtu akisema hapohapo hutakiwa ushahidi na hoja mpaka msikilizaji aridhike na kuna mambo hayahitajii hata chembe moja ya ushahidi midamu makapi ya hoja yanaonekana.

Kwa mfano, R. K. Mwanjisi kwenye kijitabu chake Abeid Amani Karume utakuta ameandika kuwa:

Kuna mambo mengi sana ambayo yalitendeka nchini Unguja na Pemba na ambayo hayana budi yathibitishwe kwa ushahidi kamili, na kuandikwa kwa makini.

Kuna nyumba Unguja iitwayo “Mambo Msiige” ambayo baada ya kumalizika kujengwa wale Waafrika walioijenga waliuwawa wote ili wasiige maarifa ya ujenzi wa nyumba kama ile.

Yasemekana pia kuwa wake za Waarabu siku hiyo wakifurahi huwaambia mabwana zao “mie sijapata kuona mtoto anavyokaa tumboni mwa mwanamke, Mirengo ya Kizalendo na Mapinduzi nataka kuona hivi leo.” Basi bwana wa Kiarabu hutuma watumwa wake wamlete mama wa Kiafrika mja mzito na akapasuliwa tumbo kumwonyesha bibi mkubwa jinsi mtoto anavyokaa tumboni! Kisha maiti ya yule mjakazi wa Kiafrika ikatupwa shimoni!

Yasemekana kuwa wakati huo Mwarabu akitaka kuhakikisha ikiwa gobori lake lina nguvu humwambia mmoja wa watumishi wake apande mnazi. Akiisha fika juu yule “Bwana” alifyatua gobori lake, kisha “Mtumwa” akalia “Yallah” akaanguka chini na kufa. Kiisha yule Mwarabu akaja na kuipiga teke ile maiti na kusema “Ama, hivi kafa huyu!”

Inasemekana kuwa kuna Mwarabu mmoja alizaa mtoto na mtumwa wake Mwafrika. Jambo hili lilipojulikana yule Mwarabu akachukua kisu akamwua yule kijakazi wake na kumtumbukiza chooni!10

Hizo ni sumu kali ndani ya kijitabu ambacho lengo lake ni kuzielezeya habari za maisha ya Mzee Abeid Amani Karume kwa wasomaji ambao wanatakiwa wafahamu kuwa:

Unguja na Pemba imepita katika tanuri la moto wa utumwa, udanganyifu wa wafanya biashara na washika misahafu, utawala wa kigeni, ubaguzi wa rangi, utetezi, juhudi za uhuru, mapinduzi na ujamaa.11

Cha Mwanjisi ni kijitabu kidogo kilichotungwa kwa ajili ya wasomaji wa kawaida. Mambo yalizidi kuwa hatari wakati kasumba kama za Mwanjisi zilipoingizwa ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Zanzibar. Na hayo yalifanywa na Wazanzibari Waafrika Waislamu ambao walitekwa akili na hadithi za utumwa zisizokuwa na hata chembe moja ya uthibitisho. Angalau Mwanjisi alitahadharisha kuwa hadithi zake kuhusu ushenzi na mambo maovu kabisa ya Waarabu waliyowafanyiya Waafrika “hayana budi yathibitishwe kwa ushahidi kamili, na kuandikwa kwa makini.”

Akina Luteni Kanali Musa Maisara Kheri, mkuu wa uandishi na muandikaji wa utangulizi, Maalim Ubwa Mamboya Ismail, Mwenyekiti wa halmshauri ya uandishi wa kitabu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania, 1964–1974, Zanzibar na ndugu zao wengine wa Kiislamu walioshiriki kwenye uandishi wa kitabu hicho, hawakuiyona haja wala madhara ya kuitumiya sumu ya hadithi zisizo na uthi-bitisho wowote midam sumu hiyo iliwapa uhai wenye utukufu wa kidunia. Mafunzo ya dini ya Kiislamu na ule msemo wa Imam Ali usemao “Utukufu hupatikana kwa kumtumikia Muumba na mwenye kuutafuta kwa viumbe hatoupata” haukuwa na maana yoyote kwao.

Jambo la kupendeza lilikuwa kwamba mpaka mwaka 1974 kulikuwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Zanzibar. Zanzibar ikijilinda wenyewe. Mambo makubwa zaidi ni yale yenye kuwasononesha wale waliohusika katika kushiriki kuwauwa ndugu zao ambao leo wameshakuwa watu wazima na kesho kuna kukutana na Muumba wao. Kitabu hicho kiliandikwa chini ya uwenyekiti wa halmashauri ya uandishi wa kitabu chini ya uongozi wa Kanali Seif Bakari Omari, na Luteni Kanali Musa Maisara Kheri akiwa Mkuu wa Uandishi na muandikaji wa Utangulizi. Propaganda ya “misafara ya dhiki na dhuluma” inasema:

Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania Zanzibar katika kazi yake ya siasa hufanya misafara kila mwaka mara mbili kwa kuvizuru vituo vyote ambamo wakiteswa Waafrika katika zama za utawala wa kifalme na vibaraka vyao ili kuelewa wanakotoka kwa makusudi ya kunyanyua juu nguvu za kimapigano na kuwa na chuki kwa matendo hayo waloyofanyiwa wafanyakazi na wakulima. Halmashauri ya siasa baada ya kukaa na kuzingatia ilitoa mpango maalumu kwa vikosi vyote kupita sehemu zote ambazo masalio ya baadhi ya vitu ambavyo Waafrika wakiteswa…Vituo hivyo ni:—

1. Mkunazini – U.M.C.A.

2. Tumekuja

3. Maruhubi

4. Kijichi

5. Dunga jumba la mawe

BEIT – El AJAB [Beit alajaib – jumba la maajabu]

Hapo Forodhani Unguja lipo jumba kubwa la ghorofa tatu lililojengwa na mflame Baraghashi katika mwaka wa 1883 na mpaka hivi leo lipo bado.

Ujenzi wa jumba hili ulipoteza roho chungu nzima za Waafrika wasio na hatia. Ilikuwa ni desturi kwa mujibu wa itikadi za kiarabu—kuchinja kinyama kama mbuzi, au ngombe ili awe kinga kwa kila baya. Watawala wa kiarabu badala ya kuchinja vinyama wao waliwachinja Binadamu badala yake! Dhulma ilioje!!!

Katika sehemu zote hizo zilizokwisha elezwa ndio sehemu muhimu kwa historia ya Waafrika walimoteswa na ndizo sehemu muhimu. Kwa hivi sasa zinazo pitiwa na wanajeshi na kufahamishwa hali ya tawala za kisultani na vibaraka vyao walivyo watesa kikatili Waafrika katika nchi hii. Ili kuwafanya wanajeshi wa kimapinduzi wawe na chuki kubwa mioyoni mwao kwa wapinga maendeleo ya kimapinduzi.12

Kuwatia chuki wasomaji na wanajeshi kwa kutoa mifano ya unyama wa Waarabu dhidi ya Waafrika ambayo imetumiwa na Mwanjisi hata baada ya kutanabahisha kuwa “hayana budi yathibitishwe kwa ushahidi kamili, na kuandikwa kwa makini” ni kushiriki katika uovu wa kimsingi ambao unaonekana katika mifano yote ya mauwaji ya halaiki ya viwiliwili na ya saikolojiya baada ya kuwanyima watuhumiwa haki yao ya kuishi na kuishi bila ya khofu au huzuni.

Misafara ya dhiki na dhuluma ambayo tunayazungumziya hayana nguvu kwenye Zanzibar ya leo kama ilivyokuwa kwenye miaka iliyopita ingawa juhudi ya kuvipiga marufuku vitabu au vijitabu vyenye kuwatia sumu Waafrika dhidi ya Waarabu au Waarabu dhidi ya Waafrika bado haijafanyika kama inavyopasa kufanywa. Ipo haja kubwa ya kuandikwa vitabu na vijitabu vipya na vyombo vya habari kutoa ilimu yenye kusimama juu ya ushahidi wa hadithi za utumwa walioufanya Waarabu, Waafrika, Wazungu na Wahindi.

Hii leo, hamira za fitina za kubuni na zisokuwa na ushahidi wowote za utumwa wa Waarabu na ukombozi ulioletwa na Ukristo kuwaokoa Waafrika zinaendeleya kuwalisha na kuwakogesha watalii wanaolizuru Kanisa la Anglikan Mkunazini Zanzibar. Kwa shilingi elfu 3,500 (au dola 3 za Kimarekani) watembezaji watalii hao ambao wengi wao si Wazanzibari, hutowa darasa kwa kila mtalii anayefika hapo kuwa Waarabu wameleta vitu viwili vibaya Afrika: Uislamu na Utumwa. Kilele cha darasa hufikiwa pale mtalii anapoongozwa na kuonyeshwa alama ya duara dogo jeupe la jiwe la marmar liliopo ndani ya kanisa ambalo linamahanisha alama mbele ya meza panapotolewa dhabihu au kafara (altar) na panaposemekana kuwa ndipo palipokuwa pamesimama mti wa Mkunazi ambao Waarabu wakiwafunga watumwa wa biashara yao na kuwapiga viboko.

Kwa mujibu wa mwalimu wa watalii wa msafara wa dhiki na dhuluma, duara hilo jeupe limezungukwa na jiwe refu jengine la marmar lenye rangi nyekundunyekundu ambayo ni alama ya damu ya Waafrika iliyokuwa ikichururuzika kutoka na mipasuko ya viboko vya Waarabu (Waisilamu). Kinachosafirishwa kwenye akili ya mtalii ni namna gani wafuasi wa Nabii Issa (sala na salamu za Mwenye Enzi Mungu zimfikie) wamekuja kusimama kunako alama iliyokuja kuwakombowa Waafrika kutokana na biashara ya utumwa wa Waarabu (Waislamu) na kuupa kasi ufalme wa Yesu Afrika.

Watu wenye akili za kibiashara wametambuwa kuwa fitina za utumwa zinaweza kufanyiwa biashara juu ya migongo ya Waarabu na Waislamu na pengine hata bila ya kutambuwa kuwa kunajenga mazingira mapya ya chuki dhidi ya Waislamu wa Zanzibar na wa Tanganyika. Mkutano wa kimataifa ambao umeandaliwa na taasisi ya African Diaspora Heritage Trail ya Marekani, ulitangaziwa kufanyika Dar es Salaam na Zanzibar baina ya tarehe 25–30 Oktoba mwaka 2009. Anwani iliyotumiliwa kuutangaza mkutano huo ilikuwa ni “Utumwa wa Waarabu Afrika Mashariki” na sambamba na mkutano huo ni zinduo la “Msafara wa Pembe za Ndovu na Utumwa” ambao utaihusisha miji kadhaa na mwahala munamohusika na utumwa na ubakaji wa Waafrika weusi milioni tano!

Upande mmoja mkutano huo umejihalalisha kwa kushirikiana na Mradi wa Biashara ya Utumwa (Slave Trade Project) wa shirika la Umoja wa Mataifa (UN) UNESCO. Mradi huo una kitengo cha utumwa katika nchi za Kiarabu na za Kiislamu. Kwa upande mwengine, madhumuni khasa ya mkutano huo ni kukuza biashara ya utalii kwa kuihusisha na urathi au turathi ya utumwa. Mashirika ya utalii na usafiri yameangaza na yamegunduwa kuwa kuna mijipesa inasubiri kuokotwa kwenye njia ya misafara ya dhiki na dhuluma. Walichokisahau ambacho hakimo kwenye hisabu yao ni umuhimu wa kuweka misingi ya maadili (ethics) kwenye kulifanyiya biashara suala kama hili ambalo limeamuwa kwenye anwani ya mkutano kuwabebesha Waarabu na watalii mizigo ya hadithi za utumwa ambazo hazina uthibitisho wala mashiko ya kitaaluma.

Mkutano uliwalenga Waarabu dhidi ya Waafrika milioni tano na si kuhusu utumwa wa Afrika Mashariki au wa Bahari ya Hindi ambao utawahusisha baadhi ya Waarabu, baadhi ya makabila ya Kiafrika, Wazungu na Wahindi. Walitokeya wapi hao Waafrika milioni tano na walimalizikiya wapi na walinunuliwa na kupelekwa na nani na ndani ya vyombo vya nani si suala ambalo limo katika matangazo ya mkutano huo. Wako wanaoamini kuwa mkutano kama huo ni wa kupuuzwa kwa sababu wenye kuuandaa si watu wazito sana duniani. Wanachokoseya ni kuwa mambo ya biashara za kipropaganda hayahitaji wataalamu au utaalamu mkubwa. Mikutano kama hii ndiyo yenye kuivumbika sumu ya chuki dhidi ya kikundi fulani cha watu ambayo mwisho wake hugeuka kuwa ni biashara mbovu kwa alotaka kufanya pesa na zaidi juu ya waliolengwa kufitinishwa, kuuliwa, na kufanyiwa faida juu ya migongo ya mauti yao.13

Mrengo wa Umoja wa Kiafrika—Pan-Africanism

Kwa Zanzibar, siasa ya Pan-Africanism au Pan-Arabism ni mfano wa globu za taa ambazo hazina budi kuzimika kwa sababu ni taa za siasa zenye kuumurika upande mmoja wa jamii na kuuwacha upande wa pili ndani ya giza. Zanzibar ni jamii ya mchanganyiko kwa hiyo mirengo ya kisiasa yenye kuiwacha nje nusu ya jamii na matokeo yake ni kuraruka kwa jamii ambayo ilitakiwa kwa pamoja ilikamate guo la kuwapamba na kuwasitiri.

Siasa ya Pan-Arabism na Uislamu inakuja kuikusanya nusu ya pili ya jamii ya Zanzibar ambayo iliongozwa na chama cha “Hizbu” (Zanzibar Nationalist Party, ZNP) ambalo ni neno la Kiarabu lenye maana ya “chama” kwa Kiswahili. Mchango wa Chama Cha Wafanyakazi cha Tanganyika, Tanganyika Federation of Labour (TFL), ni sehemu muhimu ya historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndiyo chombo kikuu kilichoendesha Mapinduzi kutoka Tanganyika kwa kushirikiyana na TANU na wafuasi wa Chama cha Wafanyakazi cha Afro-Shirazi (Zanzibar and Pemba Federation of Labour (ZPFL)).

Pan-Africanism kama alivyoichambuwa Dkt. Saleh Al-Miskry katika tasnifu yake ya shahada ya udaktari wa falsafa Pan-Africanism and Nyerere in Tanzania ni harakati yenye kuungwa mkono na kikundi cha watu na si na nguvu za umma. Sababu kubwa anayoitowa Al-Miskry ni ule ukaribu uliopo baina ya thakafa, dini, na mila baina ya viongozi wa Pan-Africanism na thakafa, dini, na mila za Ulaya. Anaendelea Al-Miskry, “…pan-Africanists na mabeberu kutoka Ulaya walifanya kazi kwa pamoja wakati wa ukombozi dhidi ya ukoloni.”14

Hoja ya kibaguzi iliyotumika ni kuwa Waarabu kutoka kokote kule ni wageni Zanzibar na Mwambao wa Afrika Mashariki. Na si Waarabu peke yao, bali hata Washirazi pia. Ubaguzi huu unaonekana waziwazi katika barua ya Jumuiya ya Waafrika /African Association ya 1949 waliyomuwandikia Balozi wa Kiingereza Zanzibar na kwa Waziri wa Makoloni wa Uingereza isemayo:

Tunasikitika sana kuona kwamba Serikali imemteuwa Mshirazi, Mwasia kwa ajili ya kumtumiliya, badala ya Waafrika wa Zanzibar. Inaeleweka wazi kwamba Mshirazi ni Mwasia katika rekodi za Serikali ya Zanzibar. Tunaelewa kwamba tunanyimwa haki zetu za uraia na hii imewabakiza Waafrika katika hali ya kukata tamaa. Kwa jina la Demokrasi, Ukristo, na usawa wa Binadamu, tunapinga vikali hatua ya Serikali na tunaomba ufikirie na kutizama upya mwenendo huu wa ubaguzi, ukandamizaji, kunyimwa haki na kunyanyaswa katika nchi yetu.15

Hii ni ajabu kubwa sana kuwa Wakristo, wageni kutoka bara ndiyo wenye kudai haki kwa fujo kwa kumpinga mwenyeji Mshirazi na Muislamu mwenye mizizi Zanzibar kwa kutumia garasa la “Uafrika”!

Tatizo kubwa la Zanzibar ni mavuno ya mti wa udanganyifu na wa mrengo maalum wa kisiasa wenye kuongozwa na kikundi kidogo chenye kuiamini itikadi maalumu ya uzalendo wa Kiafrika (Pan-Africanism) ambayo inasisitiza kuwa Waarabu/Washirazi/Waswahili/Waislamu chini ya Jangwa la Sahara ni wageni na kuwa Zanzibar ni mlango mkongwe uliyouingiza ubeberu Afrika Mashariki na Kati na Ukristo ndiyo muokozi wake.

Kwa nchi kama Zanzibar ambayo ina mchanganyiko mkubwa wa watu wa kila asili, fikra ya umoja wa watu weusi peke yao ni fitina iliyovaa guo la udugu wa kibaguzi dhidi ya Waafrika wa makabila mengine. Fikra ya mrengo huu iko kinyume na ilimu ya asili ya binaadamu ambayo inatuonyesha wazi kuwa binaadamu wote wametoka Afrika kwenda majuu katika nyakati tafauti. Dalili ni kuna watu ambao wamelelewa na fitina maalum na ambao wamewatiya chuki za kidini na za kikabila wenziwao bila ya hata kuona kama iko haja ya kuupima ushahidi wa ukweli au uongo unaotapakazwa au kutafuta juhudi za kuuondowa kwa faida ya makabila na dini nyenginezo.

Kwa mujibu wa falsafa hiyo ya mrengo huo wenye kuweza kutafakhari kuwa “Afrika Kwetu” au “Tupendane Waafrika” ni wale Waafrika wenye asili ya kibara tu peke yao na wakati huohuo kuuficha ukweli kuwa hayati Mwalimu Nyerere asingeliweza kuwa kiongozi wa Tanganyika African Association (TAA), na baadaye wa Tanganyika African National Union (TANU) bila ya kwanza kuungwa mkono na wazee mashuhuri wa Dar es Salaam, wakiwemo wenye asili na makabila tafauti, yakiwemo ndani yake makabila ya Kibantu wenye kuifuata dini ya Kiislamu.

Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi wa Kiafrika mwenye sifa kubwa duniani na kupendwa sana Tanganyika. Mwalimu alijaaliwa kufanya kazi moja kubwa katika maisha yake, nayo ni kuupiganiya na kuupata uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Muingereza. Na katika hilo aliwasahau majasiri wa Kiislam ambao ndio chimbuko la harakati za kupiganiya uhuru Tanganyika na waliyoianzisha TANU hata kabla ya yeye kukaribishwa Dar es Salaam na wazee wanaharakati wa uhuru wa Tanganyika. Waislamu ndio waliokuwa wakiumizwa zaidi na ukoloni kuliko kundi au kikundi chengine chochote kile cha kidini Tanganyika. Waislamu wa Tanganyika walijipinduwa na wakapinduliwa kwa mapinduzi baridi ya mwaka 1954 baada ya kwa makusudi kumuachiya kwa makusudi, Mwalimu Nyerere achaguliwe kuwa kiongozi wa TANU.16

Miaka kumi baada ya hapo, 1964, ikawa zamu ya kupinduliwa Zanzibar kwa mapinduzi ya kumwaga damu. Ndipo ilipoandikwa makala mwezi wa Juni 1964 katika jarida maarufu la The Economist yenye kichwa cha maneno “Mashaka ya Nyerere” kuwa Mwalimu Nyerere “ameweza kuifanya nusu ya kazi ya chatu. Ameimeza Zanzibar sawa, lakini hakuziuwa nguvu zake za kujiteteya kwanza. Mnyama ambaye yungali hai anaendeleya kukila chakula chake, na mateke yake yanaendeleya kumuumiza [chatu] kwa maumivu makubwa, na pengine hata kuyahatarisha maisha yake, ndani huko kunako mwili wa kisiasa wa Tanganyika.”17

Katika hotuba yake muhimu kuliko zote aliyoitowa kwenye hoteli ya Kilimanjaro siku ya Jumaane, tarehe 15 Machi 1995, Mwalimu alianza kwa kuuzungumzia ufa mkubwa uliyoipasuwa nyumba ya Tanzania ni ufa mkubwa wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Mwalimu alitabiri kuwa ama mtikisiko utakwisha na nyumba ya Tanzania itakuwa imara, au utaendeleya na nyumba itabomoka hata ikiwa imara. Alisema lengo liwe mtikisiko usiendelee. Katika kuhamasika na kipaji cha kuzungumza alichojaaliwa Mwalimu Nyerere, kuna Mchungaji ameandika kunako blogi moja: “Hakika alikuwa nabii, zile nyufa alizoona ziliendelea na sasa naona zimekuwa mianya mikubwa kwenye kuta. Kama hatutaangalia, nyumba yetu itabomoka na kuanguka…”

Mwalimu kweli alikuwa “nabii” kwa maana aliweza kuzitabiri nyufa na mianya mikubwa inayoukabili Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ufa mkubwa kati ya nyufa zote alizozizungumzia Mwalimu ni ufa wa muungano ambao aliongeza kwa kusema kuwa uko katika “hatari ya kuvunjika [na] wala haijesha.”

Mwalimu pia alisema “ningependa mjadala wa sasa” uwe kuhusu kueleweka nyufa ziliopo na “tupate uongozi unaoelewa hivyo.” Ombi la Mwalimu halikujibiwa ipasavyo na wenye kutaka kuinusuru nyumba ya Tanzania kubomoka ingawa ndani na nje ya nchi tayari wapo watu na mataifa yenye kuanza kukubali kuwa pengine hilo ni jambo ambalo haliwezi kuepukika. Bahati mbaya Mwalimu alitaka mjadala uendelee bila ya kutoa sababu za chanzo au mzizi wa mtikisiko. Hilo asingeliweza kulifanya kwa sababu lilikuwa ni gumu sana kwake, maana kama angelizieleza sababu halisi za mtikisiko basi zingelimuondolea sifa ya kuwa kiongozi pekee katika bara la Afrika ambaye aliweza kuziunganisha kwa hiari nchi mbili huru za Kiafrika.

Tukirudi nyuma kwenye mizizi ya mitikisiko, na kwa mujibu wa ripoti ya mazungumzo ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Sir N. Pritchard yaliyofanyika Dar es Salaam tarehe 27 Februari 1963, Mwalimu Nyerere alisema:

Peke yao Wazanzibari hawatojaribu kufanya kitu dhidi ya Tanganyika lakini wanaweza wakawaleta marafiki ambao wataweza kuwafanya wawe wakorofi. Zanzibar ilikuwa ni kituo cha kwanza cha ubeberu Afrika Mashariki. Uingereza ilichukuwa jukumu la kuulinda utawala huu [wa Zanzibar] na mantiki inasema kuwa baada ya Uingereza kuondolewa Tanganyika, Waafrika wa Zanzibar huenda wakauondowa utawala wa Kisultani.18

Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 27 Februari 1963 chini ya mwaka mmoja kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nia ya Mwalimu Nyerere ya kuipinduwa Zanzibar ilikuwa imeshadhihirika kabla ya hapo lakini hilo lilikuwa kama tamko rasmi kwa Waingereza ambao hawakuonyesha kushituka au kukerwa na kauli hiyo. Jambo ambalo tutakuja kulieleza baadae kuwa ingawa Muingereza alichukuwa jukumu la kuilinda Zanzibar kabla ya uhuru alikataa kuilinda Zanzibar iliyopata uhuru na alipendekeza imezwe na Tanganyika ili awakomowe Wazanzibari walioupiganiya uhuru wao kwa kuungana na harakati za kikombozi dhidi ya Waingereza katika bara la Afrika.19

Upotoshaji mwengine mkubwa wa kihistoria ni kuwafanya watu waamini kuwa Waingereza, chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP), na Sultan Jamshidwalikuwa kitu kimoja na walipinduliwa pamoja tarehe 12 Januari 1964.

Msomaji anafaa pia akagutuka tena juu ya utumiaji wa neno “Muafrika” au “raia” na kadhalika, na ujasiri wa kujipa haki wageni katika nchi ya Zanzibar isiyokuwa yao na utumiaji wa neno “Muafrika” kuhalalisha haki za wageni Zanzibar na kuwaharimisha wenyeji. Utumiaji wa neno “Mwafrika” ni kiini hai ndani ya simulizi nyingi za wazee ambazo utakuja kuzisoma huko mbele kuwa Mapinduzi ya Zanzibar hayakuwashirikisha wenyeji wa Zanzibar ambao si “Waafrika wa Zanzibar” kwa matumizi ya Mwalimu Nyerere ingawa katika hotuba ya Mwalimu ya 1995 aliweka wazi kuwa “hatuwezi kuwahishimu makaburu hapa [Tanzania] kwa sababu ni weusi tu.”

Zaidi ya nusu ya jamii ya Zanzibar iliyokuja kuvipigiya kura vyama va Zanzibar Nationalist Party na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZNP na ZPPP) na kushinda kwa asilimia 46 ya kura na wingi wa viti 18 kati ya 31 katika uchaguzi wa Zanzibar wa Julai 1963 hawakuwa “Waafrika wa Zanzibar” kwa maana walikuwa ni Wazanzibari wa mchanganyiko wa damu na thakafa za Kiafrika na za Kiarabu na kwa mantiki hiyo haikutosha tu “Waafrika wa Zanzibar huenda wakauondowa utawala wa Kisultani” bali kuwauwa wale waliyoonekana kuwa si “Waafrika wa Zanzibar” yaani, Waarabu, Washirazi, nk. Mazungumzo ya Mwalimu Nyerere na Sir Pritchard yalikuwa tarehe 27 Februari 1963 na Mapinduzi yalifanyika tarehe 12 Januari 1964, yaani miezi sita kabla ya uchaguzi wa Zanzibar wa Julai 1963 na takriban mwaka mmoja kabla ya mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad anaelezeya kunako kitabu cha kumbukumbu ya maisha yake:

Julius Nyerere, Rais wa Tanganyika, ana sehemu ya lawama kwa mapinduzi ya Zanzibar. Aliamini kuwa Zanzibar ni sehemu ya Tanganyika na alianza kuyaingilia mambo ya Zanzibar mapema kuanzia katika miaka ya 1950…Mpaka sasa hivi, hadithi iliopo ni kuwa watu wa Zanzibar ndio walioyapanga mapinduzi, lakini kuna ushahidi kuwa Tanganyika ilihusika tena sana. Wengine wanaamini kuwa askari kutoka Tanganyika ndio waliyoyaongoza mapinduzi. Kwa kutumia ujanja, Watanganyika waliyagubika mavamizi kwa kuyafanya yaonekane ni mapinduzi, na ndio mwanzo wa matatizo ya Zanzibar kama ni dola.

Hisia yangu ni Nyerere alikuwa ndio kichwa nyuma ya mapinduzi. Ni vigumu kuziamini hadithi zenye kusema kuwa mwanzoni wanamapinduzi waliipinduwa serikali kwa mapanga tu; silaha walizozitumia zilitoka bara. Nyerere anabeba lawama pamoja na wanasiasa wa Kizanzibari kutoka pande zote mbili…Wanasiasa wetu wenyewe walimpa Nyerere fursa kuyaingilia mambo ya Zanzibar.20

Hisia za Maalim Seif zinalingana na matokeo ya utafiti na ushahidi kutoka kwa wazee wa ASP, TANU na CCM, kutoka Zanzibar na Tanganyika, waliohojiwa na mwandishi huyu na wenye kuufahamu uhakika wa mapinduzi ya Zanzibar. Hii ni dalili tosha kuwa uongozi na viongozi wa Kizanzibari na wa Kitanganyika ni kitu kimoja katika muelekeo na ufahamu wao wa kitendawili cha jinamizi lenye kuurusha usingizi Zanzibar kwa miaka arubaini na sita. Tafauti kubwa iko baina ya hisiya za Maalim Seif na “ushahidi” kutoka wazee wa ASP, TANU na CCM.

Kuanziya kupinduliwa kwa Dola ya Zanzibar; kudanganywa kwa marehemu Mzee Abeid Amani Karume na kutopewa fursa ya kushauriana na Wazanzibari wenzake kuhusu Hati za muungano; kujiuzulu kwa Mzee Aboud Jumbe; kuundwa kwa katiba ya CCM na kutiwa mnofu wa kisheria na Ilangwa Shahidi bila ya kuwashirikisha Wazanzibari; kufitinishwa marehemu Mzee Idris Abdulwakil na Maalim Seif Sharif Hamad; uingiaji madarakani wa Mzee Ali Hassan Mwinyi na kuondolewa kwa Idara ya Usalama ya Zanzibar wakati wa Urais wake; kuakhirishwa kwa Zanzibar kujiunga na OIC wakati wa uraisi wa Mwinyi na Dk Salmin Amour Juma; kugonganishwa Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe kupitiya vyama vya siasa ambavyo vimewekewa sheria za kutoweza kuihoji mihimili ya Dola—Mapinduzi na Muungano; kuzama kwa mkono wa Bara ndani ya mambo ya Zanzibar halafu waowao kuombwa na baadhi ya viongozi wa Zanzibar wawe wasuluhishaji; mpaka kufikia Uraisi wa Dkt. Amani Abeid Karume na utetezi wa kuirudishiya Zanzibar haki zake za kinchi; ni mtiririko wa matokeo ya uvamizi wa Zanzibar ambao kwa mujibu wa maadili ya Nuremberg “ni kikomo cha jinai ya kimataifa kwa sababu unakusanya maovu yote yanayofuatiya.”

Zanzibar ya leo imeshaelekeya kuwa kitu kimoja na ni hikma na uwezo wa Mwenye Enzi Mungu ndio uliowafanya wazee wa Mapinduzi wazungumze na kuielekeza Zanzibar izungumze kwa sauti moja ndipo mtikisiko aliokuwa akiukhofiya Mwalimu Nyerere utakaposita na umoja wa Waafrika wenye asili na dini mbali mbali ndipo utakapoimarika na neema ya utajiri wa bara la Afrika kuwafikiya watu wake. Kila wakati wa binaadamu unakwenda kwa dhamira yake na wakati tulionao ni wa kujikombowa kutokana na upotoshaji wa ukweli wa historia ya Zanzibar baada ya kuvifahamu vyanzo nyake.

Mapinduzi Ndani na Nje ya Afro-Shirazi Party

Sheria mbili kati ya saba za chama cha Afro-Shirazi zinasema:

1. Kutafuta uhuru na utawala kamili utaokuwa miongoni mwa Dola zilizomo katika Shirikisho la Udugu na Dola ya Kiingereza…

2. Kuifanya na kuiamirisha Serikali ya Kidimokrasi katika visiwa vya Unguja na Pemba chini ya utawala na utii kwa Bwana Seyyid Mtukufu.21

Maneno yenye kuongoza kunako sheria mbili za chama cha Afro-Shirazi ni maneno “Shirikisho” na “utii kwa Bwana Seyyid Mtukufu.” Hizo zilikuwa ni sheria rasmi za chama cha ASP ambazo zilikubaliwa na viongozi wake na kukubalika kwa mujibu wa sheria za wakati ule.

Msomaji anatakiwa awe makini kabisa na hata kabla hajaendeleya kusoma inampasa afahamu kuwa viongozi wakubwa wa chama cha Afro-Shirazi, kama marehemu Mzee Abeid Amani Karume, na marehemu Mzee Thabit Kombo Jecha, au Sheikh Aboud Jumbe, hawakushiriki katika mipango halisi ya mapinduzi ya Zanzibar. Amekiri Mzee Jumbe katika kitabu chake The Partner-ship: Tanganyika Zanzibar Union: 30 Turbulent Years pale alipoandika kwenye kurasa 9–10 kuwa “ijapokuwa nilikuwa Katibu wa Mipango wa chama cha Afro-Shirazi, sikujuwa vizuri [kuhusu Mapinduzi] asubuhi ya tarehe 12 Januari 1964. Ilikuwa ni siri iliyohifadhiwa vizuri ambayo ilifahamika na uongozi wake [Karume] tu. Mpaka hii leo hadithi kamili imefungwa ndani ya nyoyo na kumbukumbu zao.”22 Mzee Jumbe amemuingiza marehemu Mzee Karume katika uongozi wa mapinduzi bila ya kutowa dalili au ufafanuzi wa aina yoyote.

Marehemu Mzee Thabit Kombo ambaye alikuwa chini ya marehemu Mzee Abeid Amani Karume pia ndani ya kitabu Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha kilichoandikwa na Minael-Hosanna O. Mdundo na chenye Utangulizi aliouandika Mwalimu J.K. Nyerere, amekiri kwa maneno yafuatayo:

Usiniulize vijana wetu walioendesha mapinduzi walipata wapi mafunzo, au nani hasa alivamia mahali gani; mimi sijui. Nasikia hadithi tu kila mmoja akijinasibu baada ya kushinda, mengi ya kweli na mengine ya uwongo mtupu.23

Mpaka sasa hivi hakuna ushahidi wowote, mbali ya ule wa kinaga ubaga ambao unaweza kuthibitisha kuwa marehemu Mzee Abeid Amani Karume alikuwa jemedari wa Mapinduzi ya Zanzibar kama ilivyofanywa iaminike na kusadikiwa na wengi. Mara utasikia jemedari alikuwa Mzee Karume, na mara nyingine utasikia jemedari mkuu alikuwa ni “Field Marshall” John Okello. Mara nyingine utasikia mpishi mkuu alikuwa marehemu Abdulrahman Mohammed Babu na nadhariya iliozamishwa ndani ya bongo za kila Mzanzibari na asiyekuwa Mzanzibari ni Mapinduzi yaliongozwa na Kamati ya Watu 14 au 13 + 1.

Hili ni jambo muhimu kuweza kuufahamu undani wake kwa sababu hapa ndipo kwenye kizungumkuti cha Mapinduzi ya Zanzibar. Hapa ndipo penye guo zito ambalo linatakiwa angalau ligeuzwe liwe chandarua. Kuanguka kwa Kamati ya Watu 14 kwenye chati ya Mapinduzi ya Zanzibar ni njia pekee ya kulivuwa guo la khadaa na kuirudishiya jamii nzima ya Kizanzibari na ya Kitanganyika nuru ya kufahamu inakotoka na kujipangiya inakotaka kwenda na kufika. Suala ni jee, Kamati ya Watu 14 walikuwa ndio viongozi wa mapinduzi ya Zanzibar au walikuwa ni walinzi wa kulilinda paziya la uongozi khasa wa mapinduzi?

Kati ya memba wa Kamati ya Watu 14 waliokuwa hai na wenye siha ya kuzungumza ni wazee Hamid Ameir na Abdalla Saidi Natepe. Katika mahojiano ambayo alifanyiwa Mzee Hamid Ameir katika gazeti la Mwananchi la tarehe 11 Januari 2008, mwandishi Salma Said alimuuliza “ni kwa nini wewe uko kimya kiasi hicho na hadi vizazi vya sasa haviutambui mchango wako?” Alijibu Mzee Hamid Ameir, memba wa Kamati ya Watu 14 kwa kusema:

Mimi sipendi kujitokeza kwa sababu kuna vitabu vingi sana tayari vimeshaandikwa kuhusu historia ya Sultani na kufanyika kwa Mapinduzi lakini cha muhimu zaidi ni kuwa unapojitokeza na kuzungumza wanatokea watu wanajibu hoja ulizozungumza na kuweka listi kubwa ya watu waliofanya Mapinduzi, nami kwa kuwa sipendi mabishano na kwa kuwa nafahamu kwamba kuna mtu siku moja ataandika historia ya kweli, hivyo mimi nimeamua kukaa kimyaa.24

Tarehe 8 Septemba 2002, alizungumza marehemu Mzee Khamis Daruweshi, memba mwengine wa Kamati ya Watu 14, na gazeti la Johari ya Mwananchi katika habari yenye kichwa cha maneno “Hamis Daruweshi afichua siri ya Mapinduzi Zanzibar”. Katika sababu alizozitowa Mzee Daruweshi za kufanyika mapinduzi Zanzibar ni kuwa watu wa Zanzibar “walikuwa hawataki kujinasibu kama Waafrika. Hawapendi kuunga mkono Waafrika na walikuwa wakiwaita wakata maji.” Daruweshi pia alielezea kuwa:

Huyu Okello alikuwa miongoni mwa Afro Shirazi [Youth] League. Tulimchukua Pemba alikokuwa akichonga mawe ili kutoa matufali. Tulimchukua kwa kazi maalum kwa sababu baada ya mapinduzi, tulijua tulihitaji mtu ambaye atatangaza mapinduzi hayo kwa lafudhi ambayo ni tofauti kabisa na ya wenyeji wa Zanzibar.25

Mzee Daruweshi alijifahamisha kuwa:

Mimi ni Myao, mtu wa Ruvuma, Tunduru, kijiji cha Masuguru, kata ya Malumba. Lakini hapa Zanzibar nimekuja zamani kidogo tangu mwaka 1941, niko hapa ‘nimenationalize’ uraia wa Zanzibar. Nilipiga kura katika uchaguzi wa mwaka 1957. Lakini uchaguzi wa pili ikaja pingamizi kwamba wote waliozaliwa Bara hawatapiga kura. Ukijipanga kwenye mstari, wanakuja wakikuuliza, katika mstari walikuwapo mawakala wa Hizbu na wa ASP. Unaulizwa utamke ‘halua’, wengine hawawezi wanasema ‘haarua’ kwa hiyo wanakutimua kwenye mstari kwa kuwa wanajua kwamba wewe siyo Mzanzibari na kwa hiyo tuliotoka Bara wengi tukashindwa kupiga kura. Kwa hiyo nikaomba uraia wa Zanzibar Aprili 19 mwaka 1960 na kupewa kadi nambari 2020.26

La msingi katika mazungumzo ya Daruweshi ni kule kuelezea kwake bila ya kuweka ushahidi au vielelezo vyovyote vile kuwa: “Labda ni vyema ikajulikana tangu mwanzo kwamba kamati iliyoundwa na Karume ya kuongoza mapinduzi hayo, ilikuwa na jumla ya watu 14.”27

Walipotembeleya Cuba katika mwezi wa Mei 1964, Shirika la Habari la Cuba liliwafanyiya mahojiano memba wawili wa Kamati ya watu 14, Ramadhani Haji na Saidi Idi Bavuai yenye kutowa mwangaza mzuri juu ya maandalizi ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya kutowa historia fupi ya Afro-Shirazi kutokeya mwaka 1957 walielezeya matukio yaliofikiya kupinduliwa kwa Sultan Sayyid Jamshid bin Abdullah:

Uchaguzi ulipofanyika mwaka 1963 chini ya utawala wa kikoloni wa Kiingereza, chama cha Afro-Shirazi kilishindwa na kiliunda kamati ya kufanya mapinduzi. Baada ya uchaguzi kikundi kidogo cha chama cha Afro-Shirazi kiliungana na Chama cha Kizalendo (Nationalist Party).

Haya mapinduzi ya watu 14 hayakuungana wakati wowote ule na chama chochote chengine kikiwemo chama cha Afro-Shirazi…hata chama cha Afro-Shirazi chenyewe kilikuwa hakielewi kinachoendelea.28

Inaendelea ripoti ya Kiingereza juu ya ziara ya Bavuai na Haji:

Mchango wa kimapinduzi wa John Okello ulidharauliwa na Iddi na Haji na walisema kuwa mashirika ya habari yalikosea kumhusisha yeye kama ni kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar…Waliwaeleza Rais Karume na Waziri wa Mambo ya Nje Babu kuwa ni watu ambao hawakushiriki moja kwa moja katika harakati za mapinduzi, lakini hata hivyo, wanastahiki vyeo walivyokuwa navyo.

Inavyoonyesha, memba hao wawili wa Baraza la Mawaziri walishtukiwa na muungano wa Zanzibar na Tanganyika, na waliona haya kutamka chochote kuhusu maendeleo hayo huku wakieleza kuwa [muungano] umefanyika wakati wao wako nje ya Zanzibar.29

Mara nyingi imekuwa ikisikika kuwa Mzee Abdalla Saidi Natepe ameandika kitabu kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar lakini hakitotolewa mpaka kufariki kwake. Hapa panaonekana kuna dalili kuwa mwanamapinduzi Mzee Natepe amekosa ushujaa wa kuandika kuhusu mapinduzi ya Zanzibar katika uhai wake na kuweza kuingiya katika midani ya mazungumzo wakati yungali hai.

Fikra iliyozoweleka na kushindiliwa ndani ya bongo za Wazanzibari na wasiokuwa Wazanzibari ni kuwa Kamati ya watu 14 ndiyo kamati iliyokabidhiwa kazi ya kuyapanga mipango ya mapinduzi na Mzee Karume. Hapana shaka memba wa kamati hiyo walihusika na mapinduzi na kama alivyosema marehemu Mzee Thabit Kombo “Usiniulize vijana wetu walioendesha mapinduzi walipata wapi mafunzo, au nani hasa alivamia mahali gani; mimi sijui. Nasikia hadithi tu kila mmoja akijinasibu baada ya kushinda, mengi ya kweli na mengine ya uwongo mtupu.”30

Sasa inawezekana kuwa Mzee Karume alikuwa jemedari wa Mapinduzi na msaidizi wake Mzee Thabit Kombo asiwajuwe vijana wa mapinduzi na awe amesikia hadithi tu. Lakini hili la “uwongo mtupu” ndilo linalofaa kutushughulisha. Ni uwongo gani huo wenye kuupotosha ukweli wa Mapinduzi ya Zanzibar? Uwezekano unaoingiya akilini na msomaji akawa ana uhuru wa kupima baada ya kumaliza kukisoma kitabu ni mambo mawili. La kwanza ni kuna utata wa idadi na majina ya memba wa hiyo Kamati ya Watu 14. Pili, na muhimu zaidi, inamkinika sana kuwa Kamati ya watu 14 iliundwa na kukwezwa baada ya Mapinduzi kwa lengo la kuufunika ukweli wa chimbuko la Mapinduzi yenyewe.

Tukirudi kunako kitabu maarufu na muhimu cha Mzee Aboud Jumbe The Partner-ship utakuta anwani yenye kusema “siasa za Zanzibar kabla ya muungano.” Mzee Jumbe anaelezeya kuwa:

Hata kabla ya Mapinduzi, Uongozi wa Siasa [wa ASP] ulikuwa haujaungana sawasawa. Kulikuwa na mvutano wenye kukuwa, kati ya wale, nikiwemo mimi mwenyewe, tuliomuunga mkono Karume, na baadae tukapewa jina la “Karume-Yeka”; na wale waliokuwa wakimpinga; na waliobakia waliojaribu kuyakubali makundi yote mawili. Mpasuko huu nusura ukivunje chama mwaka 1961 kwenye mkutano mkuu wa chama uliofanyika Municipal Hall, Mji Mkongwe.31

Kwa mujibu wa mwandishi wa kitabu The Zanzibar Revolution and Its Aftermath, Anthony Clayton, “tarehe 2 Januari [1964] mivutano ndani ya A.S.P. ilikamilika pale walipojiuzulu Othman Sharif, Hasnu Makame, Idris Wakyl na Saleh Saadalla.”32

Bwana George Mooring, katika barua yake ya tarehe 29 Agosti, 1963, kwaW. B. L. Monson wa Ofisi ya Makoloni, London, ameandika kuwa:

Imeripotiwa kuwa Moshe Feinsilber, Yahudi mwenye kuendesha biashara ya samaki hapa [Zanzibar], amejishughulisha na siasa kwa kuiunga mkono A.S.P. na yumo kujaribu kuwavutia viongozi wakubwa wa chama waachane na Abeid Karume na waungane na Othman Shariff katika jitihada zake za kuungana na Z.P.P.P. Ijapokuwa kikawaida maoni yake huwa yana uzito ndani ya chama, yeye [Finsilber] pia ameshindwa kukipeleka chama kwa Othman Shariff.

Wakati huu viongozi wa A.S.P. wamekuwa wakitembelea Dar es Salaam mara kwa mara kwa kupata ushauri, ambapo imeripotiwa kuwa washauri wao wakubwa ni Kawawa na Kambona. Inasemekana kuwa Watanganyika wameshinikiza kuwa endapo Z.P.P.P. itakataa kujiengua kutoka Z.N.P. na kujiunga na A.S.P. basi A.S.P. iwe chama cha upinzani na isikubali kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na vyama vingine viwili [Z.P.P.P. au Z.N.P.]. Bahati mbaya ushauri huu umekubaliwa na A.S.P.; kwa vyovyote vile uwezekano wa kuundwa Serikali ya vyama vyote ya Umoja wa Kitaifa, umepotea.

Hapana shaka A.S.P. wameridhika kuwa mwisho wake, uzito wa kuungwa mkono na bara ndio utakaowaweka madarakani Zanzibar, na inawezekana ni imani hiyo kuliko kitu chengine chochote inayotuweka kwenye hali tuliyo nayo.33

Ripoti ya siri na kielelezo cha mukhtasari cha kitengo cha usalama cha Zanzibar cha tarehe 31 Julai–28 Agosti, 1963 kinamuelezeya:

MOSHE FINSILBER, mtu wa Israel Zanzibar, ambaye ni memba kamili wa A.S.P. Katika mikakati ilioelezewa katika kifungu kilichopita, [Finsilber] dhahiri amekuwa akimuunga mkono OTHMAN SHARIFF MUSA katika mkakati wake wa kuungana na Z.P.P.P. na amejaribu kwa uwezo wake wote kumvuta SALEH SAADALLA AKIDA na ABOUD JUMBE MWINYI kuachana na ABEID AMANI KARUME na kujiunga na OTHMAN SHARIFF MUSA. Lengo la FINSILBER, ni bila shaka, ni kukingowa chama cha Z.N.P. chenye kuongozwa na Waarabu ili kisiungwe mkono na walio wengi. Anatumia ushawishi wake mkubwa ndani ya chama [A.S.P.] kuondowa ushirikiano wowote ule wa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itaihusisha Z.N.P.34

Ni dhahiri baada ya kukamata khatamu za serikali marehemu Mzee Karume aliwabadilishia kibao Maisraeli kwa kule kuwaunga mkono makhasimu wake ndani ya A.S.P. Anaandika William Edgett Smith kwenye kitabu chake Nyerere of Tanzania:

Israel, kwa mfano, ilikuwa iwe rafiki wa kwanza na wa karibu wa serikali mpya, kwa sababu Maisraeli walikuwa wachangiaji wakubwa wa chama cha Afro-Shirazi katika miaka kabla ya uhuru. Lakini, baada ya mapinduzi, Maisraeli walipojaribu kuanzisha mahusiano na serikali ya Karume, walikutana na upinzani mkubwa usiofahamika.35

Kwa upande wake, Mzee Jumbe ameonyesha kuwa mvutano ulikuwa baina ya ujumbe kutoka Pemba ambao ulishikiliya kuwa Othman Shariff awe Waziri Mkuu baada ya uchaguzi mkuu wa kabla ya uhuru wa Zanzibar. Mvutano huo, anaendeleya kuelezeya Mzee Jumbe, uliendeleya kufukuta na ulijitokeza kwa nguvu katika mkutano wa pili wa kikatiba uliofanyika jijini London. Anaandika Mzee Jumbe:

Karume alikuja kujuwa kuwa baadhi ya wajumbe wa ujumbe wake walikuwa wanataka kufanya urafiki na ujumbe wa serikali kwa lengo la kutaka kujuwa wangeliweza kupewa nafasi gani za uongozi wakiamuwa kutoka kwenye chama cha upinzani [ASP]…Karume alifupisha mazungumzo ya London na akaweza kuuondowa uwezekano wa mpasuko ndani ya safu ya chama.36

Mpasuko ndani ya ASP ambao Mzee Jumbe amejaribu kuuonesha ni mpasuko baina ya ujumbe wa ASP kutoka Pemba na ule uliokuwa chini ya uongozi wa Mzee Karume. Hakuna mahala ambapo Mzee Jumbe ameutaja upinzani wa marehemu Abdalla Kassim Hanga, Abdulaziz Twala au Saleh Saadalla Akida dhidi ya uongozi wa Mzee Karume. Wala hakutowa maelezo yoyote kuhusu TANU kama ilikuwa ikimuunga mkono Mzee Karume au kundi lipi lililokuwa dhidi ya uongozi wake ndani ya ASP. Kwa mujibu wa Mzee Abbasi, “TANU ilikuwa imeshachoka na hayati Mzee Karume na khasa baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Julai 1963.”37

Katika kuthibitisha kutoelewana Mzee Karume na Mwalimu Nyerere, anaelezeya Profesa Issa G. Shivji, kuwa Mzee Aboud Jumbe anaelezeya kuwa baada ya daktari wa Kichina kumuambiya kuwa Mzee Karume alikufa palepale alipopigwa makao makuu ya A.S.P. Kisiwandui, Mzee Jumbe moja kwa moja alimpigiya simu Mwalimu Nyerere na kumwambiya:

Huku jambo kubwa limetokea. Yeye [Nyerere] akaniambia “Karume?” Nikasema “ndio.” Akasema “basi nitaitisha Baraza la Mawaziri.” …Sauti ya maelezo ya Mzee Jumbe ilitowa ujumbe kuwa Mwalimu Nyerere alikwishajuwa kuwa Karume ameshauawa Zanzibar kabla ya kuarifiwa na Mzee Jumbe.38

Kipindi cha kabla ya kuuliwa kwa Mzee Karume hali ya uhusiano baina yake na Mwalimu Nyerere ilikuwa mbaya kuliko wakati mwengine wowote ule.

Anaelezeya Shivji:

Kwa mujibu wa Jumbe [Karume na Nyerere] walikuwa hawazungumzi kwa mwaka mzima au kama hivyo kabla ya kuuliwa. Bhoke Munanka kwa upande wa Nyerere, na Jumbe kwa upande wa Karume, walikuwa wajumbe wa kupeleka na kurudisha habari. Salim Rashid amemuambia mwandishi [Shivji] kuwa alipokwenda kumuaga Karume baada ya kuwacha kazi serikalini siku moja kabla ya kuuliwa, Karume alimshauri kuwa asiwache kazi kwa sababu alikuwa anataka kuuvunja Muungano.39

Undani wa kuuwawa kwa marehemu Mzee Karume umeficha Mapinduzi kama kuundwa kwa Kamati ya Watu 14 kulivyolifunika kombe mwanaharamu apite. Nadhariya iliyopo ni kuwa waliyopanga kumuuwa marehemu Mzee Karume walikuwa wanafanya kazi ndani ya mpango ambao hawakuutambuwa undani wake. Maalim Seid Sharif Hamad ameandika kuwa “Baadhi ya watu wanafikiria kuwa Nyerere alimtumilia Babu na chama cha Umma kumuuwa Karume kwa sababu ikijulikana vizuri kuwa yeye [Nyerere] na Karume walikuwa hawana masikilizano mazuri.”40

Alipohojiwa Babu na mwandishi wa televisheni wa Kiingereza alikiri kuwa Balozi wa Cuba aliyekuwepo Dar es Salaam alikuwa hajui chochote kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar kama alivyokuwa hakuyajuwa yeye. Babu aliyarudiya maneno ya John Okello kwa kusema kuwa hakusaidiwa na nchi za kikoministi katika kuyapanga mapinduzi ya Zanzibar bali alisaidiwa na “Mungu wa Waafrika.”

Jee, Waingereza hawakumuona “Mungu wa Waafrika” alipokuwa akiandaa kupinduliwa kwa Dola ya Zanzibar na badala yake waliamua kuwanyosheya kidole wana-Umma Party kutokana na imani yao kuwa ASP haikuwa na uwezo wa kufanya Mapinduzi bila ya Tanganyika? Na si hivyo tu, Mzee Karume, Babu na viongozi wengi wengine wakaipokeya sifa ya kuyaongoza mapinduzi na kumfunikia kombe “Mungu wa Waafrika?” Kama John Okello alikuwa ni mtu aliyekuwa na nyota mbaya iliyochomoza na kuanguka papohapo, na marehemu Babu na Karume walikuwa hawayajuwi mapinduzi lakini walijaaliwa kupata vyeo, watakuwa wamebakiya nani na kwa ushahidi gani ambao walikuwa viongozi wa mapinduzi ya Zanzibar? Ni Waafrika waliowapinduwa Waarabu Zanzibar au ni Waafrika waliowapinduwa Wazanzibari?

Takwimu za Kikabila Zanzibar

Ukiiweka kando propaganda inayolinganisha Ubantu peke yake na Uafrika utakuta Marais wakubwa wa Kiarabu wa Kaskazini ya Afrika, marehemu Gamal Abdel Nasser, na Ahmed Ben Bella ambaye yuhai, walikuwa upande wa ASP na TANU katika kuyafanikisha mapinduzi ambayo kijuujuu yamekuwa yamefahamishwa na kufahamika kuwa yalikuwa mapinduzi ya “Waafrika” wanyonge dhidi ya “Waarabu” mabepari wa Zanzibar. Kana kwamba hao Waarabu wote wa Zanzibar walikuwa matajiri na mabepari.

Akitumiya takwimu za Michael Lofchie, Profesa Issa G. Shivji ameeleza yakuwa asilimia moja (1) tu ya jamii ya Kiarabu ilokuwa ikiishi Zanzibar kabla ya Mapinduzi ilikuwa katika tabaka la juu la kijamii, na asilimia 76 ya Waarabu walikuwa katika tabaka la chini. Kwa mujibu wa takwimu za kikabila za 1948 Waafrika Asilia (Washirazi) walikuwa asilimia 56.2, Waafrika kutoka bara walikuwa na asilimia 19.4, Waarabu asilimia 16.9, Wahindi asilimia 5.8, na Wangazija asilimia 1.2.41

La msingi si kutafautisha baina ya tabaka za Waarabu baina ya asilimia 1 na 76, bali kufahamu kuwa hawa Waarabu masikini za Mungu wa asilimia 76 waliokuwa wakiishi mashamba ndio walioubeba mzigo wa kifo na maangamizi katika mapinduzi ya 1964.42 Na hao hao Waarabu wa kawaida wa Kizanzibari waliokuwa wakulima, wavunjaji mbata na wazegazega hubebeshwa tuhuma za utumwa. Na katika hiyo asilimia 1 ya tabaka la juu na la kati la Kiarabu ipo haja pia ya kujiuliza Waarabu wa Zanzibar wakijiona kama raia au watawala? Kama watawala mbona hawajazijaza skuli za Kiarabu nchini? Mbona wengi wao walikuwa hawaijuwi lugha ya Kiarabu? Na nini mchango wa Waarabu katika kuijenga Zanzibar? Mlango wa Pili 30

Leo Mji Mkongwe wa Zanzibar una heshima ya Kimataifa (World Heritage Site) uliopewa na shirika la UNESCO la Umoja wa Mataifa (UN). Wakfu wa mwanzo wa maji ya mji wa Zanzibar ulianzishwa na Sayyid Barghash bin Said bin Sultan. Mchango wa Wahindi hauelezwi vya kutosha na khasa katika kuigharimiya misafara ya utumwa, au kuipa misaada ya kifedha chama cha Afro-Shirazi, au hata mchango katika kazi za udobi, ukataji nywele, au kuuza vifuu. Na huenda sababu ikawa kutaka kuonyesha pengo la kibaguzi baina ya Waafrika kutoka bara (asilimia 19.4) na Waarabu (asilimia 16.9). Takwimu hazisemi asilimia ngapi kati ya Waafrika kutoka Bara na Waarabu walikuwa Wazanzibari kisheria au kinyume na sheria.

Tagsslider
Share: