Makala/Tahariri

Lissu ni mtetezi, mpigania haki – ni kipenzi cha wazanzibari

KALAMU YA JABIR IDRISSA

MTU kutekeleza shambulio kwa silaha nzito, dhidi ya mwanaadamu, si jambo jepesi. Si jambo jepesi hata kama atatekeleza shambulio usiku. Ni jambo gumu ambalo asiye mwerevu wa matumizi ya silaha, si rahisi kujiingiza.

Nasema tena, si rahisi shambulio kwa mwanaadamu yeyote awaye silaha ikitumika. Na silaha yenyewe ikawa bunduki; na bunduki yenyewe ikawa ni Sub Machine Gun (SMG).

Lakini hata isiwe silaha hii ambayo inajuilikana kitaalamu kama moja ya silaha maridadi katika masuala ya kivita. Chukulia labda bastola ndiyo ilitumika kumshambulia mwanasheria na mwanasiasa hodari nchini, Tundu Antiphas Mugwai Lissu – bado ninaamini si rahisi hivo.

Si rahisi kama ambavyo haikuwa rahisi kumshambulia kwa silaha Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar. Aliuawa kwa kupigwa risasi saa moja hivi asubuhi tarehe 17 Februari 2013, akiwa anawasili katika Kanisa la Mtakatifu Teresa, Beit el Ras, nje kidogo ya mji wa Zanzibar kuongoza ibada.

Tofauti na shambulio kwa Lissu, lililohusisha zaidi ya mhalifu mmoja, hili la Padri Mushi, lilitekelezwa na mtu mmoja tu, kijana mbichi, kwa mujibu wa watu waliomshuhudia akishika njia na kutokomea kitongojini baada ya shambulio.

Lakini angalia tabia za wahalifu wa matukio haya mawili. Hawakuwa na hofu wala aibu. Walitekeleza uovu wao kwa utuo (utulivu), wakijua wanachokitaka. Walitekeleza katika hali hiyo kwa sababu hapana shaka kwa picha iliyokuwepo, waliagizwa na “watu wao.”

Wakati haikuwahi kufahamika taarifa za maandalizi ya mapema ya mpango wa kumuua Padre Mushi, ambaye uhai wake ulikatizwa kwa shambulio lililofanywa haraka lakini kwa uangalifu na utaalamu mkubwa, na mhusika kutoweka kiulaini, mazingira yanaonesha, na sasa taarifa zinasambaa, kuwa wahalifu waliotumwa kumuua Lissu, lakini wakashindwa kukamilisha utumwa, walijiandaa.

Padre Mushi alipigwa risasi na kijana aliyemvizia akiwa anawasili kwenye kanisa Jumapili ile, na alikuwa ndo kwanza anaelekea mlango mkuu wa jengo la kanisa. Alipigwa risasi chache tu akijiandaa kuteremka chini.

Taarifa zinadai kuwa “watu wasiojulikana” walionekana maeneo ya nje ya jengo la Bunge, mjini Dodoma, saa kadhaa kabla. Wakati huo wabunge wakiendelea na kikao ukumbini; Lissu akitoa hoja nzito kuhusu madhara ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokuwa makini katika utendaji wake, kwa kudhamiria au kujisahau tu, ukumbini.

Waliokuwa nje ya maeneo ya Bunge siku hii ya Alkhamis, tarehe 7 Septemba, wanasimulia kuwa kwa muda waliwaona watu wageni wakizunguka. Walipata hata kuagiza chai na vitafunwa. Walikula wakiwa ndani ya gari yao.

Lakini baadhi yao wanaamini waliona watu waliokuwa na undani – hawakuwa waliojishirikisha na maongezi na watu wengine pale, eneo ambalo wageni wa wabunge na wafanyakazi wa ofisi ya Bunge hukaa wakisubiri wenyeji wao.

Waovu wa Lissu walifanikiwa kutobainika. Lissu alipotoka nje ya Bunge, na kuingia kwenye gari na ikaondoka kwa safari iliyojulikana baadaye kuwa ya nyumbani kwake, waovu wakamfuata nyuma. Hii ndiyo siri anayoitoa dereva aliyekuwa na Lissu.

Waliomfikia wanaeleza kuwa akiwa safarini kwenda Area D, katika Manispaa ya Mji wa Dodoma, alibaini kufuatwa na gari fulani. Yumkini alimtanabahisha bosi wake, Lissu, kuhusu hilo. Sijui muitiko wake, lakini safari iliendelea ndio maana alishambuliwa akiwa anawasili nyumbani kwake.

Baada ya gari kufika, bado dereva aliona wanafuatwa na gari wasiyoijua. Wauaji wala hawakupata hofu. Watulivu kwelikweli kama vile walichotumwa kukifanya – kwa mantiki ya mjadala huu ninaamini walitumwa – kilikuwa kitu cha halali kisheria na kiutu.

Lissu na dereva wake walijua hawako salama. Lakini haieleweki kama walitafuta msaada wakaukosa. Walibakia ndani ya gari. Waovu ambao muda wote huo walikuwa wamesimama na gari karibu tu na nyumbani kwa Lissu, bila ya shaka wakisubiri uamuzi amri ya kutekeleza, walipoona muda unasonga, wakashusha kioo na kuchomozesha mtutu wa bunduki na kuanza kufyatua risasi wakilenga alipoketi Lissu.

Hawa watu walijiandaa, na kwa ukatili wakatekeleza walichotumwa. Si ubabaishaji kusema walikuwa waelewa hasa wa kutumia silaha. Mtu mjinga wa silaha hawezi kufyatua risasi nyingi vile pasina hofu, tena mchana kweupe.

Kama yule muuaji wa padre Mushi aliyefyatua risasi chache na zikaenda moja kwa moja kwenye paji la uso la kiongozi huyo wa kanisa, waliomtendea uovu Lissu, walikuwa wajuzi wazuri wa silaha.

Nimeanzia matukio haya mawili. Lakini tukio la kushambuliwa Lissu, linakumbusha matukio mengine kadhaa ya uhalifu dhidi ya Watanzania yaliyowahi kutendwa kwa staili ya watendaji kujua wanachokitenda na kama vile wakitekeleza amri za mabwana zao.

Wapo walioendesha mashambulizi ya kudhuru mwili dhidi ya wataalamu wa sheria na mawakili mashuhuri Profesa Jwani Mwaikusa na Dk. Sengondo Mvungi. Hawakushikwa bali vivuli vyao.

Profesa Mwaikusa alikuwa na kesi mkononi akimtetea mtuhumiwa uhalifu wa kivita raia wa Rwanda, katika Mahakama ya Uhalifu (ICTR) iliyoshughulikia kesi za mauaji ya kimbari ya nchi hiyo yaliyotokea mwaka 1994.

Akiwa mmoja wa mawakili katika Mahakama ya ICTR, iliyokuwa na makao yake jijini Arusha, Tanzania, alikuwa anajitahidi kumvua mtuhumiwa na hatari ya adhabu nzito. Alikamatwa na serikali ya Rwanda ambayo chini ya Rais Paul Kagame inatuhumu wanaopinga msimamo kuwa ni waasi tu waliohusika na mauaji yale. Kwamba wao waliokuwa askari wa msituni wakitaka kutwaa madaraka kwa vita, hawakuhusika.

Jitihada za kuwavua na makosa waliokamatwa na serikali ya Rwanda, zilikuwa ni kuwaudhi wakubwa. Hawakupendezwa na mawakili, na kwa Prof. Mwaikusa, ndo kabisa kwa vile hitimisho la utafiti wa kisomi alioufanya ndani ya Rwanda, lilikuwa “wote walioshiriki vita, walihusika na mauaji.”

Dk. Mvungi naye alikuwa wakili wa Mahakama Kuu. Miongoni mwa kesi alizosimamia ni pamoja na zilizohusu watu wa kawaida waliozuiliwa haki zao na serikali. Lakini Dk. Mvungi pia alikuwa guru katika kazi ya kuandaa rasimu ya katiba mpya. Ni mtafiti aliyekuwa mshauri wa utendaji wa tume.

Kazi ile ilikuja ikachukiwa na watawala. Hawakuipenda. Uthibitisho ni mwisho wa rasimu yenye maoni ya wananchi – kuvurugwa. Mpaka leo haieleweki hatima ya katiba iliyopitishwa na Bunge lililokuwa mateka wa matakwa ya CCM.

Yapo matukio ya kikatili yalitekelezwa dhidi ya wananchi wengine. Shida kubwa ni kwamba waliohusika hawakushikwa. Ndio kusema damu waliyoimwaga, haijalipwa. Kitu kibaya ni kwamba jitihada za kuwadhibiti hazikuonekana.

Nimejadili suala hili na hasa nikiashiria kubana utawala utende haki, kwa sababu nyingi; ila moja muhimu ni kuwa Lissu amekuwa na mchango hata kwa harakati za demokrasia za Zanzibar. Moja ya kesi zinazomkabili inahusu siasa za Zanzibar. Amekuwa kipenzi cha Wazanzibari, basi nao wameguswa na kudhuriwa kikatili.

Share: