Makala/Tahariri

M.Seif na turufu ya Urais

Na Jabir Idrissa

RAIS anayesaka ridhaa ya kuendelea kuongoza, Dk. Ali Mohamed Shein, anatumia jukwaa la kampeni kutetea mapinduzi ya Januari 12, 1964, kama vile kuna ubishani kwamba mapinduzi yale ni halali au haramu.

Kwa hakika, jambo hili halijawahi kuwa la kubishaniwa hata kuwa ajenda wakati wa uchaguzi.

Halikuwa mwaka 1995 ulipokuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, wala halina nafasi kwa uchaguzi huu ambao kura itapigwa tarehe 25 mwezi ujao.

Lakini mwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), amelishadidia. Anajua anachokilenga, lakini nasisitiza halina maana katika siasa za maridhiano zilizokusudiwa.

Hafanyi kwa bahati mbaya. Yeye ni CCM na ametamba si kada aliyeibuka tu, bali alianzia utotoni akiwa Afro-Shirazi Youth League (ASPYL).>

Naona ameridhika kuwa asipothibitisha, wenzake hawatamuelewa. Lazima ashikilie kamba ya Mapinduzi Daima. Ukweli, ametoka nje ya mstari katika kulea mfumo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ingawa aliapa kuutetea alipoapishwa 2010.

Mara mbili-tatu daktari ametamka majukwaani umuhimu wa mfumo huu uliokuja kwa ridhaa ya wananchi kupitia kura Julai 2010, na kuuridhia kwa asilimia 66.

Si mara moja wala mbili, akiwa Ikulu akikutana na wageni mbalimbali, ametaja alichoita “mafanikio ya serikali anayoongoza” na kueleza wazi yamechangiwa na utulivu uliotokana na serikali ya mfumo huu.

Kwenye uzinduzi wa kampeni yake wiki iliyopita, viwanja vya Kibandamaiti au uwanja wa Demokrasia, Dk. Shein aligusia umoja, amani na utulivu, akisema ni nguzo ya maendeleo ya taifa lolote.

Akaahidi serikali yake itahakikisha Zanzibar inaendelea kuimarisha hayo matatu.

Kwa bahati mbaya sana, kauli yake siamini kama amedhamiria. Si kauli thabiti kwa sababu uongozi wake umepuuza usimamiaji hayo.

Hivi anaposimama jukwaani kuomba ridhaa ya kuendelea kuongoza, yote hayo yamedhoofika. Hakuna amani ya kweli, utulivu ni wa bandia na umoja umetikiswa.

Ushahidi: Dk. Shein ameshindwa kuzuia wahuni kujeruhi wananchi. Askari wa serikali wanapita mitaani na gari za serikali wakitisha wananchi.

Wanafanya unyama huu mchana wakiwa wamevalia sare rasmi, mikononi wamebeba silaha; wanarandaranda mitaani kama nchi ipo kwenye tahadhari ya kushambuliwa. Uhuni wa kijinga.

Hapo najadili amani. Hakuna amani ya kweli Zanzibar, hasahasa kwenye mji wa Zanzibar na vitongoji vyake, pande zote za Unguja – magharibi, kati, kusini na kaskazini.

Wahuni hawa wanaostahili kuitwa “maharamia” wanafika mpaka miji midogo ya maeneo ya shamba, Makunduchi kwa mfano, wakishambulia wananchi waliokuta wanashughulika kisiasa au kazi nyinginezo halali.

Wamefika Kizimkazi, jirani na Makunduchi, na Chwaka ambako walidiriki kubaka msichana mchana kweupe. Kijiji hicho, kama ilivyo vingi vya Zanzibar, kinasifika kwa watu watulivu wakiwemo walioilimika kidini. Msononeko huko haujamalizika.

Maharamia wamefanya vitimbi vingi Tumbatu, ambako waziri mgombea uwakilishi amejenga ngome akitaka awe rais kule na asiguswe.

Huyu ni Haji Omar Kheri, waziri mwenye dhamana ya vikosi hivi vinavyotesa na kudhalilisha wananchi – Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Idara Maalum), jina lililolenga kuzuga wananchi wanaoamini vikosi vya SMZ vinawadhalilisha kwa maslahi ya kisiasa.

Makumi ya watu wamepewa vilema (rudia picha ya toleo lililopita). Unapomuumiza mwananchi namna ile, anabaki na kilema. Askari wa serikali wanajeruhi wananchi na kuwapa ulemavu?

Maelfu wananyimwa haki ya kushiriki uchaguzi kwa kukataliwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, ambacho kwa kukihusisha na masuala ya kisiasa, ndio leseni ya Mzanzibari kuandikishwa kuwa mpigakura.

Kwa kuwa siku zote haki huitangulia amani, kumkosesha mwananchi haki hii ya kikatiba, kuchagua, kunavuruga amani. Amani na haki hwenda pamoja; pasipo haki hakuna amani.

Kuwanyima baadhi ya wananchi haki ya kikatiba ni kuwatenga katika kuwahudumia. Ni kuendesha serikali kibaguzi – kubagua. Dk. Shein aliapa kuongoza kwa mujibu wa katiba, kwamba hatobagua kwa namna yoyote – si dini, kabila, rangi wala asili ya mtu atokako.

Kama tunasimama kwenye haki, basi rais amevunja Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kuwatenga baadhi ya wananchi kwa kuwanyima haki za msingi na kikatiba, ni kuwaambia kuwa wao ni hawana maana, hawahesabiki. Kama hawahesabiki, hawatakiwi katika nchi.

Hapo wanaotengwa wanajisikia watu wanaoonewa na matokeo yake ni kuubomoa umoja na mshikamano wa nchi.

Sijagusia maeneo mengine ya ubaguzi wanaofanyiwa wananchi. Yapo malalamiko ya ubaguzi katika ajira, fursa za kusoma vijana na wakubwa zao walioko kazini tayari. Wasiokuwa “wenzetu” hawachaguliwi.

Nina rafiki amehilikishwa vya kutosha asitimize ndoto zake za kujiendeleza kwa sababu tu asili yake ni Pemba na yeye haabudu CCM. Kutoabudu chama hiki ni dhambi kwa siasa za Zanzibar.

Amenyimwa msaada na hata mkopo wa kusoma Shahada ya Uzamili. Alipopata mfadhili binafsi, akanyimwa ruhusa ya kuondoka kazini ili akasome. Wala si ughaibuni, D’Salaam.

Rafiki yangu ni mhasibu, kada muhimu katika utumishi wa serikali, na ambayo mpaka sasa haina wataalamu hata nusu ya mahitaji, kwa mujibu wa utafiti wa kitaalamu.

Wahasibu siku zote ni wataalamu mahsusi popote pale duniani. Lakini kwa sababu amechukiza kwa mkuu wa wahasibu, anakandamizwa.

Chini ya uongozi wa Dk. Shein aliyeingia Ikulu Novemba 2010, yale yaliyokuwa yamelengwa kupungua, yanaishi na kuimarika.

Umoja na mshikamano unayumba. Ubaguzi unashamiri katika ajira, fursa za kusoma na haki ya mwananchi kupata huduma za jamii.

Ni mambo yanayoudhi wananchi, yanagusa mioyo yao na matumaini yao kiasi cha kujaa hisia kuwa hwenda kusiwe na uchaguzi huru, wa haki na uliosimamiwa kwa uwazi. Na uchaguzi mzuri hukuza imani.

Katika hali hii, unapomsikia kiongozi anaomba tena ridhaa ya kuongoza, na ukashuhudia hatabiriki kidhamira, huku ikishuhudiwa pia wapambe wanaompigia kampeni ni wabobezi wa matusi, mipasho, dhihaka na wapotoshaji wa mambo, lazima ushuku uadilifu wa mtaka urais.

Serikali ya umoja imeishia Baraza la Mawaziri. Haijasogea kwa hata inchi kuzama katika mfumo wa utumishi wa umma. Ninavoandika, ikiwa imepita miaka mitatu, SMZ imegoma kuipa kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL) kibali cha kuchapisha gazeti jipya.

Kiongozi akishindwa kusimamia jukumu muhimu la kuimarisha mshikamano wa kitaifa, na kuzuia uhuru wa kujieleza kushamiri, amekosa maono kimaendeleo.

Wala simuonei daktari. Ninaeleza ninachokiona ambacho wachambuzi wengine wajitokeze kunikosoa, ninakosoleka.

Mgombea mshindani wake, Maalim Seif Shariff Hamad, hajawahi kuwa rais, bali anazo rekodi za utendaji uliotukuka akiwa tu msaidizi wa rais awamu iliyokuwa na rais aliyetandika uongozi mwema.

Sishangai kuona CCM wakitumia nguvu kubwa kupotosha historia ya mgombea huyu ambaye amejaaliwa imani ya wananchi, turufu nzito ya kutarajia ridhaa kuongoza Zanzibar.

Chanzo: Mawio

Tagsslider
Share: