Maadili

TAHADHARINI NA UHASIDI

Baada ya kumshukuru ALLAH (SW) kama anavyostahiki kushukuriwa sala na salamu zimfikie Mjumbe wake Sayyidina Muhammad (saw) pamoja na Masahaba zake na kila anayefuata njia yake kwa wema mpaka siku ya malipo.

Enyi Waja wa ALLAH :
Uhasidi ni maradhi mabaya ya nafsi, na ni kasoro kubwa inayokaa katika moyo wa mtu na ni asili na sababu ya kila matendo maovu, na ni tabia inayomuweka mtu mbali na uchamungu. Na maana yake ni kwa mtu kutamani neema au kheri alikuwa nayo mwenziwe imuondokee. Na hasidi huwa anachukia pale mwenziwe anapopata kheri na anafurahi pale mwenziwe anaposibiwa na shari.
Anasema ALLAH (SW) :
{ إِنْ تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُواْ بِهَا وَإِن تَصْبِرُواْ وَتَتَّقُواْ لاَ يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئاً
إِنَّ اللّهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ } ال عمران 120
“ Ikikupateni kheri huwasikitisha na ikikupateni shari wanaifurahia. Na mkisubiri na mkamcha ALLAH hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika ALLAH anayajua vizuri yote wanayoyatenda ”.

Vile vile, hasidi huwa haridhii vile ALLAH (SW) anavyogawa neema kwa waja wake na anapinga na kuchukia maamuzi ya ALLAH (SW) juu ya waja wake.
Imepokewa katika athari kuwa ALLAH (SW) anasema :
(( اَلْحَسُودُ عَدُوُّ نِعْمَتِي مُتَسَخِّطٌ لِقَضَائِي غَيْرُ رَاضٍ بِقِسْمَتِيْ ))
“ Hasidi ni adui wa neema zangu, ni mwenye kuchukia maamuzi yangu, na hauridhii ugawaji wangu ”.

Na yoyote atakaoujaza moyo wake kwa imani ya kweli na nuru ya yakini, akawa anaridhia maamuzi yote ya ALLAH (SW) katika ugawaji wa neema zake na maamuzi yake mengine, basi kamwe moyo hautokuwa na nafasi ya uhasidi, kwani imani na hasadi hazikai pamoja.
Amesema Mtume (saw) :
(( لاَ يَجْتَمِعَانِ فِيْ جَوْفِ عَبْدٍ الإِيْمَانُ وَالْحَسَدُ ))
“ Havikai pamoja katika katika kifua cha mja (muislamu), imani na uhasidi ”.

Anasema ALLAH (SW) :
{ أَمْ يَحْسُدُونَ النَّاسَ عَلَى مَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ } النساء 54
“ Au wanawafanyia watu husuda kwa yale aliowapa ALLAH kwa ukarimu wake ”.

Enyi Waislamu :
Hakika imethibi kuwa uhasidi husababisha madhara ya kidini na ya kidunia kwa mtu hasidi, kwa sababu daima huwa anaumia na kuhisi dhiki kubwa pale anapoona watu wameneemeshwa na Mola wao.
Amesema Mtume (saw) :
(( سَيُصِيْبُ أُمَّتِيْ دَاءُ الأُمَمِ . قَالُو : ياَ نَبِيَّ اللهِ وَمَا دَاءُ الأُمَمِ ؟ قَالَ : اَلأَشَرُ وَالْبَطَرُ وَالتَّنَافُسُ فِيْ الدُّنْيَا وَالتَّبَاغُضُ وَالتَّحَاسُدُ حَتَّى يَكُونَ الْبَغْيُ ثُمَّ الْهَرْجُ ))
” Utasibiwa umma wangu na maradhi ya umma. Wakasema Masahaba : Ewe Mjumbe wa ALLAH, ni yepi maradhi ya umma ? Akasema : Kiburi, na majivuno, na kushindana kwa ajili ya dunia, na kuchukiana na kufanyiana uhasidi, mpaka utaenea uovu na mauaji ”.

Na katika mapokezi mengine, amesema Mtume (saw) :
(( دَبَّ إِلَيْكُمْ دَاءُ الأُمَمِ قَبْلَكُمْ الْحَسَدُ وَالْبَغْضَاءُ ))
“ Yameingia juu yenu maradhi ya umma za kabla yenu; hasadi na kuchukiana ”.

Ndugu Waislamu :
Hasadi ndio dhambi ya mwanzo alioasiwa ALLAH (SW) katika mbingu na Bilisi pale alipokataa kumsujudia Adam baada ya kuona kuwa amepewa cheo kikubwa mbele ya Malaika na hatimae kutiwa katika pepo.
Anasema ALLAH (SW) :
{فَوَسْوَسَ إِلَيْهِ الشَّيْطَانُ قَالَ يَا آدَمُ هَلْ أَدُلُّكَ عَلَى شَجَرَةِ الْخُلْدِ وَمُلْكٍ لَّا يَبْلَى * فَأَكَلَا مِنْهَا فَبَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِن وَرَقِ الْجَنَّةِ وَعَصَى آدَمُ رَبَّهُ فَغَوَى * ثُمَّ اجْتَبَاهُ رَبُّهُ فَتَابَ عَلَيْهِ وَهَدَى} طه 120 – 122
“ Shettani alimtia wasiwasi akamwambia : Ewe Adamu, nikujuulishe mti wa milele na ufalme usiokwisha ? Basi wakaula wote wawili na uchi wao kuwadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya peponi, na Adamu akamkosa Mola wake na akapotea njia. Kisha Mola wake akamchagua, na akamkubalia toba yake na akamuongoa ”.

Na imepokewa kutoka kwa Ibnu Umar (ra) kuwa Bilisi kamwambia Nabii Nouh (as) :
(( اِثْنَتَانِ بِهِمَا أُهْلِكَ بَنِيْ آدَمَ الْحَسَدُ وَالْحِرْصُ ، وَبِالْحَسَدِ لُعِنْتُ وَجُعِلْتُ شَيْطَانًا رَجِيْمًا ))
“ Binaadamu amehilikishwa kwa mambo mawili, hasadi na pupa. Na kutokana na hasadi ndio mimi nikalaaniwa na nikajaaliwa kuwa ni shettani aliewekwa mbali na kila rehma ”.

Pia hasadi ndio dhambi ya mwanzo alioasiwa ALLAH (SW) katika ardhi na watoto wa Nabii Adam, baada ya wao kutoa sadaka na kukubaliwa sadaka ya mmoja wao na kukataliwa sadaka ya mwengine.

Anasema ALLAH (SW) :
{ وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ ابْنَيْ آدَمَ بِالْحَقِّ إِذْ قَرَّبَا قُرْبَاناً فَتُقُبِّلَ مِن أَحَدِهِمَا وَلَمْ يُتَقَبَّلْ مِنَ الآخَرِ قَالَ لَأَقْتُلَنَّكَ
قَالَ إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللّهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ } المائدة 27
“ Na wasomee khabari za watoto wawili wa Adamu kwa ukweli, walipotoa sadaka ikakubaliwa ya mmoja wao na ikakataliwa ya mwengine. Akasema :
( yule iliokataliwa sadaka yake) nitakuua. Akasema ( yule aliokubaliwa sadaka yake) : Hakika ALLAH huwapokelea wamchao tu “.

Na katika alama za mtu hasidi ni kujidai kumpongeza na hata kumuombea dua mtu aliepata neema huku moyo wake ukichukia, na kumsengenya anapokuwa hayupo hali ya kuwa anaona uchungu juu ya kile ambacho yeye hakimiliki.
Anasema ALLAH (SW) :
{قَدْ بَدَتِ الْبَغْضَاءُ مِنْ أَفْوَاهِهِمْ وَمَا تُخْفِي صُدُورُهُمْ أَكْبَرُ } آل عمران 118
“ Bughudha (yao juu yenu) inadhihirika katika midomo yao, na yanayofichwa na vifua vyao ni makubwa zaidi,

Enyi Waja wa ALLAH :
Ilivyokuwa hasidi ni mtu mbaya, basi ni lazima tujikinge kwa ALLAH (SW) kutokana na shari yake. Na katika njia za kujikinga na shari ya hasidi ni kusoma Suuratul Falaq ambayo ALLAH (SW) kwa rehma zake alimfunza kufanya haya Mtume wake na umma wake.

Anasema ALLAH (SW) :
{ قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ * مِن شَرِّ مَا خَلَقَ * وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ * وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ * وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ } الفلق 1 – 5
“ Sema : Najikinga kwa Mola wa walimwengu wote. Na shari ya alivyoviumba. Na shari ya giza la usiku liingiapo. Na shari ya wale wanaopulizia mafundoni. Na shari ya hasidi anapohusudu ”.

Enyi Waja wa ALLAH :
Hakika watu hugawika sehemu mbili wanapomuona mwenzao kaneemeshwa na ALLAH (SW). Wapo wanaochukia na kutamani neema ile imuondokee na hawa ndio mahasidi. Na wapo wanaotamani na wao waipate neema kama hiyo ili na wao washindane katika mambo ya kheri, na hii ndio sifa ya watu wema.
Amesema Mtume (saw) :
(( لاَ حَسَدَ إَلاَّ فِي اثْنَتَيْنِ رَجُلٌ آتاهُ اللهُ مَالاً فَسَلَّطَهُ عَلَى هَلَكَتِهِ فِيْ الْحَقِّ ، وَرَجُلٌ
آتاهُ اللهُ عِلْمًا فَهُوَ يَعْمَلُ بِهِ ويُعَلِّمُهُ النَّاسَ ))
“ Hakuna uhasidi (choyo) isipokuwa katika mambo mawili : Mtu kapewa mali na ALLAH akaitumia yote katika njia ya haki, na mtu kapewa elimu na ALLAH akaifanyia kazi na akawafundisha watu ”.

Enyi Waislamu :
Mcheni ALLAH Mola wenu Mtukufu, na jitengeni sana na tabia ya uhasidi, kwani kumbukeni kuwa uhasidi unafisidi mema yenu sawa na moto unavyokula kuni, na pia unaharibu imani kama vile shubiri inavyoharibu asali.

Amesema Mtume (saw) :
(( إِيَّاكُمْ وَالْحَسَدَ فَإِنَّ الْحَسَدَ يَأْكُلُ الْحَسَنَاتِ كَمَا تَأْكُلُ النَّارُ الْحَطَبَ ))
“ Jihadharini na uhasidi, kwani hakika uhasidi unakula mema kama vile moto unavyokula kuni “.

Na amesema Mtume (saw) :
(( اَلْحَسَدُ يُفْسِدُ الإِيْمَانَ كَمَا يُفْسِدُ الصَّبِرُ الْعَسَلَ ))
“ Hasadi inaharibu imani kama vile shubiri inavyoharibu asali ”.

Na pia amesema Mtume (saw) :
(( لَيْسَ مِنِّيْ ذُو حَسَدٍ وَلاَ نَمِيْمَةٍ وَلاَ كَهَانَةٍ وَلاَ أَنَا مِنْهُ . ثُمَّ تَلاَ : { وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَاناً وَإِثْماً مُّبِيناً } ))
“ Hayuko pamoja na mimi mwenye hasadi wala fitna wala mwenye kujidai kuwa anajua mambo ya ghaibu na mie si katika yeye ”. Kisha akasoma : “ Na wale wanaowaudhi Waislamu wanaume na wanawake bila ya wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi za dhahiri ”.

والسلام عليكم ورحمة الله تعالى وبركاته .

Share: