Makala/Tahariri

Maalim anamaanisha kuifuta CCM

Jabir Idrissa,

KAULI ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kuazimia kukifuta Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisiwani Pemba, ni nzito kuliko maelezo yaliyotolewa kumjibu.

Kwa mujibu wa mwandishi Haji Mtumwa wa gazeti la Mwananchi, Naibu Katibu Mkuu wake Zanzibar, Vuai Ali Vuai, anasema, “uwezo aliokuwa nao Maalim Seif ni wa kufukuza viongozi ndani ya chama chake, kazi ambayo anaifanya kila siku.”

Vuai anasema si rahisi Maalim Seif kuidhoofisha CCM kwani ni chama chenye “msingi imara na wananchi wake wanakikubali.”

Kwanza, kutokana na maelezo ya Vuai, kiongozi asiye historia ya kuchaguliwa kwa kura za wananchi, anaonesha alivyo kiongozi wa tofauti kubwa na Maalim Seif.

Tofauti ya haraka ninayoiona ni hii ya ukweli kwamba Vuai ameamua kumdhihaki Maalim Seif pamoja na kucheza na maneno katika namna ya kujifurahisha moyo tu. Kwa upande mwingine pia, amekusudia kufurahisha wanachama wenzake wa CCM.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo akiwa mbele ya kundi la wananchi walioamua kwa hiari yao kukihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na CUF, chama ambacho ni mwendawazimu tu anabisha kuwa kimeidhibiti CCM kisawasawa katika ufuasi kisiwani Pemba.

Mara nyingi imekuwa ni kauli ya kawaida kusemwa ya kwamba kwa CUF, Pemba ni ngome yake kisiasa isiyoshindika kwa namna yoyote ile.

Wakati anayasema maneno ya kuifuta CCM katika kuaminika na kuonekana na wananchi Pemba, Maalim Seif alikuwa moyoni amejaa furaha na tabasamu usoni la kuwakabidhi kadi ya CUF wananchi wapatao 2,240 wa vijijini vya Kiuyu Minungwini, Kilindini Mapofu na Tumbe, ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Katika risala yao kwake Maalim Seif, wananchi hao walisema wamebaini kwamba Civic United Front ndio chama makini na chenye dhamira ya kweli ya kuwainua wananchi na kujenga uchumi wa nchi.

Aidha, wananchi hao wamemwambia Maalim Seif kwamba wameshindwa kuendelea kustahmili kuona viongozi wa chama kile walichokuwa, wanatoa ahadi zisizotekelezeka.

Tafsiri ya maneno yao wananchi hawa, ni kwamba viongozi wa CCM hawaaminiki tena. Mtindo wao wa kuahidi umma mambo yanayoishia na kuwa hadithi na ahadi zinazofanana na zile za Abunuwasi. Ikumbukwe kuwa utimizaji wa ahadi ni moja ya hatua muhimu kwa mtu aliye muungwana.

Basi kwa wananchi kuhofia kuendelea kwa utamaduni wa viongozi wa CCM kutotimiza ahadi kwa wananchi, ina maana kuwa ndani ya chama hicho, hakuna ukweli na hakuna kuheshimiana miongoni mwa wanachama, bali badala yake, ni kuahidi mazuri yasiyokuwepo.

Historia ya kisiasa Zanzibar inayoanzia tangu enzi za harakati za kuiwezesha Zanzibar kujiongoza yenyewe, miaka ya 1950 mwishoni, uongozi uliopo serikalini haujawahi kuungwa mkono na wananchi.

Tena, ukija kuangalia mapokezi au kukubalika kisiasa kwa Mzee Abeid Amani Karume, kisiwani Pemba, unaona waziwazi namna ilivyopata uraia baada ya wazee wengine wa Pemba kulazimika kula kiapo cha kisheria ili kumwezesha kutambuliwa kuwa ni raia halali wa Zanzibar.

Simulizi za wakati huo zinatuambia kuwa alikuwa baba mzazi wa Mussa Haji Kombo, mwanasiasa mahiri ambaye alikuwa Afro Shirazi Party (ASP) na baadaye CCM, lakini akakumbwa na dafrau la kufukuzwa pamoja na kina Maalim Seif mwaka 1987, aliyemthibitishia uraia wake.

Wakati joto la siasa mpya za mageuzi likiongezeka miaka ya 1980 mwishoni, tayari kulikuwa na harakati za upinzani kupata nguvu Pemba. Hii ilikuja kuthibitika hasa baada ya CCM kutengeneza chuki dhidi ya Maalim Seif na wenzake baada tu ya kutumikia wananchi kwa nafasi ya Waziri Kiongozi wa Zanzibar.

Wananchi walipiga kura kwenye nafasi yake hata bila ya kuwa kweli iliandaliwa kuwa achaguliwe kuwa mgombea urais badala ya Mzee Idris Abdulwakil aliyekuwa rais madarakani.

Kilikuwa ni kipndi ambacho Maalim Seif alikuwa ametimiza mwaka mmoja wa wadhifa huo wa uwaziri kiongozi ambao ni wa kumsaidia Mzee Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Rais wa Zanzibar.

Hilo hasa liliongeza mvuto wa kiongozi huyu mbele ya umma na hususan Pemba ambako ni nyumbani kwao, ikiwa ndiko pia alikoanzia elimu yake ya awali hadi sekondari. Maalim Seif alizaliwa kijiji cha Nyali, Mtambwe Oktoba 22, 1943.

Akasomea elimu ya msingi skuli ya Uondwe, na sekondari ya wavulana ya Wete, ndipo akajiunga na King George VI sasa Lumumba Sekondari, Unguja. Alitakiwa kuingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini akiwa ameanza taratibu za kufanikisha hatua hiyo, aliitwa na Rais Aboud Jumbe Mwinyi (mwenyezi mungu amrehemu) asite kwenda chuoni na badala yake azibe pengo la upungufu wa walimu katika ngazi ya sekondari.

Hatua hiyo peke yake ilionesha ni kwa jinsi gani Maalim Seif alishabainika kijana hodari na mzalendo kwa nchi. Aliruhusiwa kwenda chuo kikuu cha Dar es Salaam baada ya miezi sita hivi na baadaye kuja kuteuliwa waziri wa elimu akiwa mmoja wa viongozi vijana werevu wakati huo.

Tangu hapo nyota yake ya kisiasa imekuwa ikizidi kung’ara na haijatokea hata mara moja akapunguza kupendwa na umma. Hii ilidhihirika siasa za vyama vingi ziliporuhusiwa mwaka 1992, chini ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kutungwa sheria na bunge.

Maalim Seif aliongoza kundi la wanasiasa machachari walioanzisha chama cha wananchi kwa kushirikiana na James Mapalala ambaye baadaye alikuja kufukuzwa chama kwa tuhuma za usaliti.

Kishindo cha Maalim Seif kilionekana katika uchaguzi wa kwanza wa Oktoba 1995, pale alipozoa ushindi lakini akazuiwa kiaina kuongoza baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza Dk. Salmin Amour Juma kuwa mshindi wa urais kwa kura za mkononi.

Mbinu za kumhujumu, bila ya shaka kwa ukakamavu wake kisiasa, hazijasimama tangu hapo; na huthibitika kila unapofanyika uchaguzi mkuu, fursa ya wananchi kuchagua wamtakae. Mwaka 2000 CCM ikapenyezwa kushinda tena kwa mizengwe iliyosaidiwa na vyombo vya dola kama ilivyokuwa mwaka 2005, 2010 na 2015.

Mara zote hizo, kura za Pemba zinaitesa CCM kwani haijawahi kufikisha asilimia 10. Akiongoza CUF, Maalim Seif amekuwa akidhibiti imani ya wananchi ambao nao wakiendelea kumpenda na kutumaini kuwa atawavusha kimaendeleo.

Ni dhahiri kwamba historia hiyo inamjenga Maalim Seif kuendelea kukubalika, na leo anatambulika kama mhimili muhimu wa matarajio ya uongozi mwema na wenye kuthibitisha mustakbali wa kweli wa Zanzibar na watu wake kwa kuwa amewashiba hata Unguja.

Basi Maalim Seif anaposema ataifuta CCM kisiwani Pemba, anamaanisha hasa kwani ndio hali halisi, tofauti na ubaraguzaji wa ukweli huo kama anenavyo Vuai. Hakika anajua CCM inatawala kwa kubebwa na dola.

Tagsslider
Share: