Makala/Tahariri

MAALIM SEIF – HAZINA TUNAYOIPOTEZA

Rushyd Ahmed

NIMEKUWA pamoja na Maalim Seif Sharif Hamad tangu alipokuwa Waziri Kiongozi, Februari 1984 hadi nilipohama Zanzibar, mwezi wa Machi 1996.

Maalim Seif ni Waziri Kiongozi wa pili kwa Serikali ya Zanzibar, tangu kubuniwa kwa cheo hicho. Waziri Kiongozi wa Kwanza alikuwa Ramadhani Haji Fakih, aliyeondoka madarakani Januari 29, 1984 baada ya kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar.

Nimekuwa na Maalim Seif katika ziara zake za ndani ya Zanzibar katika kujenga Chama cha Wananchi (CUF), kila alipokwenda. Niliondolewa kazini Novemba mwaka 1993 kwa sababu za kisiasa.

Maalim Seif ni kiongozi wa uhakika, ni hazina ya kuijenga Zanzibar, ni turufu iliyoachwa bila kutumika, bila kufanyiwa kazi katika kujenga heshima ya Taifa la Zanzibar na watu wake.

Maalim Seif ni aina ya vingozi adimu na adhimu kupatikana katika mataifa mengi masikini na dhaifu katika kuyarejeshea utu na heshima ya binadamu. Maalim Seif lulu iliyoachwa kutumiwa sawasawa kwa maslahi ya Zanzibar.

Maalim Seif ni lulu inayotutoka bila wenyewe (sisi) kujitambua. Hajawahi Zanzibar, kutokea kiongozi aliyepata misukosuka kwa ajili ya Wazanzibari anayeweza kulinganishwa na Maalim Seif.
Hotuba zake zote anazozitoa ndani na nje ya Zanzibar, zimejaa utu, busara na maslahi mapama kwa raia wote wa Zanzibar, bila kuwa na chembechembe za ubaguzi na ubinafsi.

Tangu niishi nchini Uingereza takriban miaka 20 na kidogo sasa viongozi wengi wa Zanzibar na Tanzania (Tanganyika), wanaofika hapa hotuba zao ni za ovyo ovyo zimejaa unafiki na ulaghai.
Jana, hotuba ya Maalim Seif, aliyoitoa katika hafla ya kumuaga baada ya ziara yake ya wiki moja hapa, nilimvulia kofi nikiamini kuwa ndani ya Zanzibar na Tanzania (Tanganyika), hana mfano wake. Maalim Seif ni mjuzi na mtaalamu ni shujaa mwenye dira.

Maalim Seif, anapendwa. Anapendwa kwa sababu anazo sifa zote za kupendwa. Ana akili na upeo (vision), busara na ndoto za kuibadilisha Zanzibar na watu wake katika kuwajengea mfumo mzuri wa maisha, uchumi na utawala.

Maalim Seif, ameamua kujitenga na viongozi wanaojenga utawala wa kiadui dhidi ya raia. Inakuwaje rais wa nchi anakuwa adui kwa raia wake au niseme raia anamuona rais ni sehemu ya adui wa maisha yake na mali zake.

Hayo ndiyo yanayoendelea kufanyika sasa Zanzibar. SMZ imekuwa ni sehemu ya kuwafanyia raia vitendo vya kijambazi, kama kuwapiga, kuwakamata na kuwafungia vituo vya polisi na kuwanyang’anya mali na mifugo yao.

Serikali inayotawala kwa niaba ya raia inayosimamia haki, misingi ya utawala bora na sheria za nchi haisubutu kufanya vitendo vya dhulma dhidi ya raia wake wasiyokuwa na hatia kama yanayotokea Zanzibar. SMZ, imejaa ubaguzi na uonevu.

Mwenyezi Mungu ‘Jallah Jalal tunakuomba kwa utukufu wako umpe uzima, mzidishie afya nzuri na mzidishie umri Maalim Seif Sharif Hamad, Rais wa Wazanibari katika uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 kwa mujibu wa waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa..

FB

Share: