Makala/Tahariri

Mabandia na vikaragosi kasuku katika enzi za udikteta

Ahmed Rajab

Na Ahmed Rajab

VIROJA vya hivi karibuni nchini Tanzania viliwahuzunisha wengi na watu kadhaa waliniuliza swali hilo hilo moja: “Tunaelekea wapi?” Jawabu yangu nayo imekuwa moja, kwamba hatuelekei popote kwani tumekwishafika tulipokuwa tukielekea tangu Awamu ya Tano ianze kwa vishindo.

Viashiria vilikuwa vingi vilivyoonesha tukielekea wapi. Kadhalika, baadhi yetu tukionya kwamba, muda si mrefu, tutafika hapa tulipofika sasa. Na hapa tulipofika si pazuri.

Katika nchi zenye tawala za kimabavu aghalabu matumizi ya nguvu huwa ya pande mbili: Ya upande wa wenye nguvu za dola na upande wa wenye nguvu ya haki. Hapo ndipo panapozuka mapambano. Ikiwa upande wa wenye haki pia unatumia silaha basi mapambano huwa ya silaha.

Tanzania haikuifikia daraja hiyo. Kwa sasa matumizi ya nguvu ni ya upande mmoja, upande wa wenye kuhodhi madaraka na vyombo vya dola. Mpambano au mgongano uliopo ni baina ya wenye nguvu na wasio na nguvu.

Walioanza kutumia nguvu ni wenye madaraka. Chambilecho mwanamuziki wa “Bongo flava” Emmanuel Elbariki, almaarufu kwa jina la “Ney wa Mitego”, anayeimba kuwa nchi inaendeshwa “kwa kiki.”

Mara nyingi tumekuwa tukionya kwamba watawala wetu si watu wenye insafu, wenye kutenda mambo kwa uadilifu na kwa nia safi. Tukitanabahisha kuwa hawakuwa wakweli walipokuwa wakisema watatenda haki. Tukisema kuwa haijuzu kuwaamini watu wasioaminika.

Sasa tunaiona hatari iliyotushukia. Akisimama mtu na akasema kweli mara mtu huyo hutumbukizwa gerezani au hufunguliwa mashitaka.

Hayo yanathibitisha kwamba wenye hatamu za utawala wanaendesha siasa za ubabe. Miongoni mwa watawala mna mabandia na vikaragosi. Mara nyingi utaona kuwa hawa ndio walio mbele kuzitekeleza siasa za ubabe.

Siasa aina hizo zina hatari kwa utawala mzima wa mabavu. Hatari yenyewe ni kwamba siasa hizo huwa kama ardhi yenye rutuba inayowezesha kuvunwa stihizai au tashtishi ya kisiasa (political satire).

Wakosoaji wa utawala wa kimabavu hutumia stihizai ya kisiasa kuwakebehi watawala na kuwaamsha wananchi.

Stihizai ya kisiasa dhidi ya watawala zaidi hutumiwa na waandishi pamoja na wasanii, waandishi, wachoraji, washairi na waimbaji. Nao hutumia medani mbalimbali ikiwa pamoja na majukwaa ya mawasiliano ya kijamii.

Tumeshuhudia hivi karibuni jinsi wachoraji wa vibonzo walivyohamasishwa na viroja vilivyomhusisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, shirika la utangazaji la Clouds Media, waziri wa zamani wa Habari, Nape Nnauye na Rais John Pombe Magufuli. Ubunifu wa wasanii hao ulizidi kuwa wa hali ya juu. Vivyo hivyo ubunifu wa mwanamuziki kama “Ney wa Mitego” na nyimbo yake mpya “Wapo”.

Hapa ningependa kukumbusha tu kwamba kadhia ya kuvamiwa Clouds Media jijini Dar es Salaam , haikuwa ngeni kwa wakazi wa Zanzibar ambao wamezoea kuona ugaidi kama huo ukifanywa na watu wanaosadikiwa kuwaunga mkono watawala. Usiku wa kuamkia Desemba 3, 2015, kwa mfano, stesheni maarufu ya redio Hits FM huko Unguja ilivamiwa na genge la zaidi ya watu 15 waliokuwa na silaha za moto na waliokuwa wamejifunika nyuso zao.

Mtangazaji mmoja wa steshini hiyo alijeruhiwa na studio za Hits FM zilimwagiwa petroli na kuchomwa moto. Hadi sasa hakuna aliyetiwa nguvuni kwa kuhusika na kitendo hicho cha jinai.

Kushindwa kwa vyombo vya ulinzi kuwachukulia hatua waliofanya unyama huo ndiko kunakozidisha dhana kwamba watawala wamezifikisha pahala pabaya nchi zote mbili zilizo katika Muungano wa Tanzania.

Dhana kama hiyo ndiyo inayowapa uwanja wasanii nao wazidi kuwafanyia watawala tashtishi za kisiasa na kuwaamsha wananchi.

Sidhani kama katika historia ya Tanzania kuna Rais aliyewahi kufanyiwa tashtiti au stihizai za kisiasa kushinda anavyofanyiwa Rais wa Awamu ya Tano. Rais anasema kwamba uhuru wa kutoa maoni una mipaka yake. Wasanii nao, kwa upande wao, hawachelei kumkumbusha kwamba hawezi kutawala atakavyo, kwamba madaraka nayo pia yana mipaka yake.

Nadhani unaweza kuzipima hatari za utawala wa kidikteta kwa kuangalia jinsi watawala wake wanavyowachukulia wenye kuwafanyia tashtiti za kisiasa. Ikiwa watakurupuka na kuwatia ndani wenye kuwacheka wanapowacheka au ikiwa watazipiga marufuku nyimbo zinazowafanyia stihizai basi ujue kwamba udikteta umekwishaanza kushamiri na hali ni ya hatari.

Iwapo mtawala hawezi kuyavumilia makombora ya tashtiti za kisiasa anayorushiwa na wasanii basi hiyo huwa ni ishara moja ya udhaifu wake wa kisiasa. Mtawala mwenye kujiamini ni yule mwenye ustahimilivu wa kuweza kubeba mambo mazito.

Watawala huiogopa stihizai ya kisiasa kwa sababu inaweza ikawa na nguvu hata zaidi ya upinzani wa vyama vya siasa katika kuchangia kwenye harakati za kuleta mageuzi.

Mengi hutegemea mazingira ya kisiasa yalivyo nchini. Katika nchi zenye tawala za kimabavu lakini zenye wananchi walioamka kisiasa na wanaharakati waliobobea, stihizai ya kisiasa inaweza kuchangia kwa haraka kuleta mageuzi ikitumiwa katika nyimbo au katika michezo ya tamthilia (drama).

Eugène Ionesco ni msanii, mtunzi wa michezo ya kuigiza aliyekuwa na asili ya Kiromania na Kifaransa. Tamthilia yake aliyoiita kwa Kifaransa Rhinocéros (Vifaru) ni mchezo wa stihzai ya kisiasa dhidi ya utawala wa mabavu. Katika mchezo huo wanadamu wanakusanywa pamoja na hatimaye wanageuka na kuwa vifaru.

Msanii mwengine maarufu wa tamthilia Mjerumani Bertolt Brecht akitumia sana stihizai dhidi ya watawala wa kimabavu katika michezo yake mingi. Brecht akiufokea ukatili na ukorofi wa utawala wa kimabavu. Tamthilia yake ilikuwa ni aina ya propaganda ya kisiasa kwa vile ilikuwa ikiziumbua hali za udikteta wa Hitler. Wakati huo huo Brecht akiziiga kwa kuzibeza dhuluma za utawala wa Hitler.

Si lazima tashtiti ya kisiasa iwe ya kuchekesha. Inaweza ikachekesha na inaweza isichekeshe. La muhimu ni kwamba itumiwe kwa kutaraji kwamba inaweza ikasaidia kuleta mageuzi ya kisiasa au ya kijamii. Ndio maana watawala huwa wanaiogopa. Wanayajuwa makali yake.

Jazanda (images) zinazotumiwa katika tamthilia za tashtiti ya kisiasa ni jazanda zinazoweza kuficha maana — kusitiri kile ambacho mtunzi wa tamthilia asichotaka kukiwadhihisha, kukiweka wazi, ama kwa kuwaogopa watawala au kwa kuunogesha mchezo.

Ali Attas, mwandishi wa Kenya mwenye kuishi Japani na ambaye tumewahi kumzungumza katika kurasa hizi, hivi majuzi ameitoa ukumbini tamthilia yake ya mwanzo inayoitwa “Mabandia” ambayo imechapishwa na Dafina Media Group, Nairobi. Kwenye kurasa za “Kauli ya Mwandishi” mwanzoni mwa mchezo huu mfupi wa kuigiza, Attas amemtaja Brecht kuwa ni mmoja wa waandishi wa tamthilia aliovutiwa nao kiasi cha kujifunza mawili matatu kutoka kwao.

Jumamosi iliyopita nilimuuliza nini hasa kilichompelekea atunge tathmilia hii ambayo ni aina ya stihizai ya kisiasa. Akanijibu kwamba labda majibu yanafanana kwa kiasi fulani na nia ya Profesa Ebrahim Hussein, msanii mashuhuri wa tamthilia wa Tanzania, alipotunga tamthilia yake maarufu iitwayo “Mashetani”.

Attas ameniambia kwamba aliusoma mchezo huo mara nyingi zama zake za ualimu alipokuwa akifundisha Fasihi ya Kiswahili katika skuli za Nairobi. Hiyo ilikuwa sababu moja.

Sababu nyingine ni kwamba Septemba mwaka jana siasa za Marekani zilimchochea alipoona dalili za wazi za kwamba Donald Trump ataitumia turufu kumpiku Hillary Clinton. Attas hakukosea kwa vile Trump kumbe alisaidiwa na joka, Vladimir Putin, Rais wa Urusi.

Hapa Attas ameonesha ustadi wa kucheza na lugha, tena mbili — za Kiswahili (joka, nyoka mkubwa) na Kiingereza (“joker”, jokari wa karata).

Binadamu – karibu wengi wetu tuna sura mbili, kwa maoni ya Attas. Za ujoka na za usamaria mwema. Hali kadhalika, tuna ubandia. Tunabandikizwa au wenyewe binafsi tunameza taaluma ambayo badala ya kutupa vigezo vya kuyatathmini maisha kwa usahihi, tunauachia ubandia huu utupotoshe.

Attas anasema asili yake haifahamu. Na ni shida kuung’oa kama mibuyu inayotumika katika mazingira ya jukwaa ya tamthilia ya “Mabandia” . Na kuna wengine wanaubugia ubandia kutoka majoka, kiasi cha athari yake kuwa sumu kali hata kuipindukia ile ya swila.

Attas anaamini kwamba nuru ya kuyamudu yote haya ni elimu mwafaka tunayoipata vyuo vikuu. Ila anasisitiza kuwa elimu hiyo isiwe kama “matambara ya watoto bali iwe elimu aali.”

“Mabandia” ni mchezo unaomulika hoja ambazo jamii mbalimbali zinaishi nazo. Gamba la nyuma la kitabu linauelezea mchezo huu kuwa “ni kioo kinachodundisha vitendawili vilivyojikita katika vipengere mbalimbali vya maisha.

Hali kadhalika, unagusia ubandia na ujoka unaojificha na kujifichua kwa sura tofautitofauti. Katika mchezo huu, kama ilivyo katika tawala nyingi, tunakutana pia na vikaragosi — vikaragosi-bandia na vikaragosi-kasuku.

Kadhalika, gamba la mwisho la kitabu linasema kwamba “maisha ni karata”. Kwa hivyo, si ajabu kumwona Attas akiwafanya wahusika wote sita wa “Mabandia” wawe njiani kuelekea barazani kwao kucheza “Wahedi wa Sitini’, mchezo wa karata ulio maarufu zaidi katika sehemu za pwani ya Afrika ya Mashariki na visiwa vyake.

Kabla ya karata kuanza Sungusungu, mmoja wa wahusika wakuu, auliza ushindi wapatikana kwa wingi wa duru au dinari? (Dinari ikiwa sarafu yenye kutumika.) Mjomba Kayaya anajibu: “Wingi wa dinari.” Hillary Clinton, alipokuwa anagombea urais wa Marekani, alichota milioni tatu zaidi ya kura lakini duru (yaani ule mfumo wa “electoral college”) ilimshinda. Mjomba Kayaya akajibu: “Ndio demokrasia halisi iliyoumuka.”

Attas hakufanikiwa tu kutunga tamthilia yenye maana na iliyo kama kioo cha jamii nyingi, hasa zile zenye tawala za kimabavu, lakini amefanikiwa pia kupandisha kiwango cha utunzi wa tamthilia ya Kiswahili kiwe cha hali ya juu zaidi maana siku hizi kuna wengi wanaojitosa kwenye fani hiyo ingawa hiyo si fani yao. Hakuna ubaya kufanya hivyo ikiwa kiwango kitakuwa cha juu.

“Mabandia” ni mchezo wenye vielelezo vingi vya kiistiara (allegory) na vitendawili — maana ya vitu na watu imefunikwa kwa maganda ambayo itakubidi uyamenye moja baada ya moja ili uufikie uhalisia wa hivyo vitu au hao watu.

Attas anatumai kwamba mada za vitendawili zilizo humo zitapepetwa kama vikaragosi kasuku na bandia wanavyonadi mchezoni: “Vitendawili zingatieni. Vidokezo vichambueni. Mafumbo yapepeteni.”

Share: