Makala/Tahariri

“Maguzuma” na suala la demokrasia

Na Ahmed Rajab

TUWACHUKUE marais wa nchi mbili za kirafiki barani Afrika, Tanzania na Afrika Kusini. Tuwatie marais hao katika chungu kimoja, tuwachanganye na tuwageuze wawe mtu mmoja, rais mmoja. Tumpachike jina la “John Jacob Maguzuma”.

Rais wetu “Maguzuma” amekuwa mtu mwenye sura mbili; ni wa kutafuna na kupuliza. Ana sifa zinazokinzana na ila chungu mbovu, baadhi hazifai kutajwa hadharani. Anajitia ubabe na kujifanya hamjali mtu.

Ingawa hutaka ulimwengu umuone kuwa ni mtu asiye na mchezo lakini mara akiusikia tu mdundo wa ngoma huwa wa mwanzo kujimwaga jukwaani au uwanjani akidengua na kuimba.

Sifa moja ya “Maguzuma” asiyoweza kuificha ni kuwa anajipenda. Ni jitu la anasa lisilo ona taabu kutumia fedha za umma kujijengea pandikizi la jumba. Hata hivyo, daima anasisitiza kwamba yeye ni mtu wa Mungu na muumini wa dhati wa dini ya Kikristo.

Anasema ni mpigania haki na amejitolea kuwatetea wanyonge. Wakati huohuo ana kibri kisichosemeka na ujeuri uliopindukia mpaka. Anajiona kuwa hakuna kama yeye. Si hayo tu bali pia anaamini kwamba taifa limebahatika kuongozwa naye.

Ukimuangalia “Maguzuma” kila anapopata nafasi ya kuwahutubia wananchi utaona jinsi anavyofurahi anaposhangiliwa.

Husema mambo ambayo ana hakika yatawahamasisha wananchi wazidi kumshangilia. Na kila wananchi wanapomshangilia huwa kama wanamtia ufunguo azidi kusema maneno ya kushangaza, maneno ambayo hujawahi kufikiria kuwa yanaweza kutamkwa na Rais mzima.

Au atachukua hatua za ajabu ajabu, kama kuwavuta mitajiri inayoshukiwa kuwa ni mifisadi na kuwa karibu nao.

“Maguzuma” anathubutu kusimama mbele ya halaiki ya watu na kusema kwamba si kazi ya serikali yake kuwalisha wananchi waliokumbwa na janga la njaa. Saa zote anapenda kukumbusha kwamba yeye ndiye Bwana Mkubwa kabisa nchini, kwamba anajua kila kitu na anaweza kuiendesha nchi bila ya kusaidiwa.

Anawataka viongozi wengine wa serikali wawe wanamyenyekea na kutekeleza alitakalo. Anahisi kuwa hiyo ni haki yake kwa sababu yeye ndiye aliyewateua na kuwapa nyadhifa walizo nazo.

Anavyoamini ni kuwa dhana ya demokrasia ni udhia mtupu wenye kumchelewesha asitimize lengo lake la kuipatia nchi maendeleo kwa haraka. Na akisema maendeleo anakusudia zaidi maendeleo ya reli, viwanja vya ndege, barabara na ya miundombinu mingine.

Kwa muda sasa amepata umaarufu kwa kujifanya jembe la kufyekafyeka kila anachohisi kuwa kina harufu ya ufisadi.

Wapinzani na hata wengine ndani ya chama chake wanasema kwamba hakuna fisadi mkubwa nchini kama yeye “Maguzuma”. Kila siku kuna malalamiko dhidi yake. Tangu ashike urais amekumbwa na kashfa za aina mbalimbali zinazomhusu yeye au watu walio karibu naye.

Ni wazi kwamba wananchi wenzake wamemchoka. Kwa sababu hiyo tunamchukua na kumrudisha chunguni ili ageuke tuwapate tena marais wawili halisi — John Magufuli wa Tanzania na Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini.

Kuna mengi ya uongozi wa Tanzania na wa Afrika Kusini yanayofanana. Unaweza kusema kwamba hadithi yao ndiyo ni ileile. Nchi zote hizo mbili zinaongozwa na vile viitwavyo vyama vya kihistoria, vyama ambavyo vinadhamiria kuhodhi madaraka kwa muda mrefu ujao.

Chama cha Mapinduzi (CCM) cha Tanzania kinasema kwamba kitatawala milele. Kwa upande wa Afrika Kusini, Zuma amesema zaidi ya mara moja kwamba chama chake cha African National Congress (ANC) kitatawala mpaka Nabii Issa (Yesu Kristo) atakaporudi tena duniani.

Hii shauku ya kutaka kutawala milele ni aina ya maradhi yaliyoviambukiza vyama kadhaa vinavyojiita vya kihistoria na vinavyoshika hatamu za utawala katika nchi kadhaa za Kiafrika.

Jingine tunaloliona Tanzania na vilevile Afrika Kusini ni kwamba vyama vilivyo madarakani vinaongozwa na watu wanaokabiliwa na upinzani mkubwa, nje na hata ndani ya vyama vyao. Viongozi hao wawili, Jacob Zuma na John Magufuli, ni watu wenye tabia na hisia tofauti.

Zuma hana kibri au jeuri kama Magufuli. Wala haripuki kwa mahamaki kama anavoripuka Magufuli. Kwa upande wake, Magufuli naye si mtu mwenye kupenda maisha ya kifahari kama Zuma. Ana mke mmoja wakati Zuma ameoa wake wasiopungua sita; nijuavyo ni mmoja kati ya hao aliyempa talaka. Inakisiwa kwamba ana watoto 24, aliozaa ndani na nje ya ndoa. Magufuli ana watoto watatu.

Wala Magufuli hakuwahi kushtakiwa kwa mambo ya ufisadi kama alivyoshtakiwa na kushtumiwa Zuma mara kadhaa.

Uzoefu wao wa kisiasa pia unatofautiana. Zuma ameleleka ndani ya ANC. Alizivaa siasa tangu alipokuwa mdogo. Aliingia ANC 1959, mwaka aliozaliwa Magufuli, na kuwa mwanachama wake akiwa na umri wa miaka 17. Alipotimu miaka 20 alikuwa amekwishajiunga na jeshi la ANC, Umkhonto we Sizwe (Mkuki wa Taifa). Alipokuwa na miaka 21, alijiunga na Chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini (SACP).

Mwaka huo aliojiunga na SACP, Zuma alikamatwa na wenzake 45 na akashtakiwa kwa kula njama za kutaka kuipindua serikali ya kikaburu ya Afrika Kusini. Alihukumiwa kifungo cha miaka kumi na akafungwa katika gereza kisiwani Robben Island, ambako Nelson Mandela na viongozi wenzake wengine wa ANC walikuwa wamefungwa. Alipofunguliwa Zuma alijitosa katika harakati za ukombozi.

Zuma hakuelimika rasmi kama alivyoelimika Magufuli lakini huwezi kumuelezea kuwa ni mtu mjinga au asiyejua mambo. Amejielimisha mwenyewe kwa njia mbalimbali.

Magufuli, kwa upande wake, aliyesomea mambo ya sayansi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliingia siasa 1995 alipochaguliwa mbunge wa Chato na halafu naibu waziri wa kazi baada ya uchaguzi.

Kuna tofauti mbili kubwa baina ya nchi hizo zenye kuongozwa na Magufuli na Zuma. Moja ni kwamba Afrika Kusini haijawahi kupitia utawala wa chama kimoja. Tanzania, kwa upande wake, haikuwahi kupitia utawala wa wachache na wa kibaguzi kama ule wa makaburu wa Afrika Kusini.

Kinadharia, nchi zote hizi mbili zinafuata mfumo wa kidemokrasia. Ukizisoma katiba zao utaona kwamba, kwa kiwango kikubwa, nchi hizo zinaelemea upande wa demokrasia. Lakini demokrasia hiyo si demokrasia iliyoumuka au iliyopevuka. Ni demokrasia iliyo changa.

Pamoja na kuwa changa mifumo ya kidemokrasia ya nchi hizi mbili ina mapungufu. La msingi tunalopaswa kulitia maanani kila tunapozungumzia demokrasia katika nchi kama hizi ni kwamba demokrasia inayofuatwa ni ile iitwayo “demokrasia ya kibwanyenye” (“bourgeois democracy”).

Huo ni utawala unaojikita juu ya mfumo wa kiuchumi wa kibepari na ni wenye kulitumikia zaidi tabaka la mabwanyenye na mabepari. Walio kwenye matabaka ya chini, kama la wafanyakazi au la wakulima wadogowadogo, huwa kama wametiwa ndani ya rikwama wakibururwa.

Hiyo pengine ndiyo sababu kubwa yenye kuwafanya baadhi ya wasomi, hasa wale wa itikadi za mrengo wa kushoto, waukebehi mfumo huo. Mara kwa mara wasomi hao husikika wakihoji kwamba afadhali pawepo na mfumo mbadala wa utawala wa kidemokrasia, hususan barani Afrika.

Ukiwauliza utapatikana vipi huo mfumo mbadala, hujibu kwa kuirukia mifumo asilia ya tawala za Kiafrika. Hoja yao ni kwamba tawala hizo za kale zilikuwa na aina ya, au aina za, mifumo ya kidemokrasia inayoweza kuifaa Afrika ya leo.

Nadhani ni kosa kuukebehi huo mfumo wa kidemokrasia uliopo sasa kwa sababu kama unafuatwa kwa dhati kuna mengi ya kuusifia. Ni kheri kuwa nao huo kuliko kuwa na utawala wa kimabavu, usioheshimu katiba za nchi au unaozikanyaga haki za binadamu.

Hapo ndipo palipo tofauti kubwa kabisa baina ya demokrasia iliyopo Afrika Kusini na ile watawala wa Tanzania wanaosema wanaifuata wakati ukweli ni kuwa tunachokiona ni demokrasia ya maneno matupu. Hayo yamedhihirika wazi kufuatia uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015.

Kuna mengi yanayoweza kufanyika Afrika Kusini ambayo ni taabu kufanyika Tanzania.

Hayo yanayowezekana kufanyika Afrika Kusini yanawezekana kwa sababu nchi hiyo inazo taasisi za kidemokrasia zenye kutekeleza wajibu wao. Kwa mfano, Rais anaweza akashtakiwa na wanaomshtaki wakashinda kesi. Zuma, hata akitaka, hawezi kujifanyia atakavyo.

Waandamanaji wanaweza wakakusanyika nje ya Ikulu ya Zuma wakapiga kelele na kumlaani bila ya kufikwa na kitu. Hayo ni muhali kutokea Tanzania. Hayawezekani asilan.

Ingawa katiba ya Tanzania inawaruhusu watu wawe na uhuru wa kukusanyika na kuandamana lakini wakijaribu watatiwa ndani au watatoweka. Vyombo vya dola vitasema watu hao hawana ruhusa ya “kumchezea” Rais. Wanasahau kwamba ni wao kwa kuichezea demokrasia ndio wenye kumchezea Rais.

Tofauti nyingine kubwa tukiziangalia siasa za nchi hizo mbili ni kwamba Rais Zuma wa Afrika Kusini akionekana kuwa amefurutu ada na analiabisha taifa, watu wenye na wenye kusikilizwa nchini hawakauki. Hawakai kimya. Husema kitu ama kwa kutoa indhari au kwa kulaani. Ndio tunamsikia Askofu Mkuu Desmond Tutu akionya kwa kutumia hekima yake na cheo chake katika jamii.

Na si wao tu bali hata vigogo wa chama kinachotawala cha ANC huthubutu kusimama na kumwambia kweli Zuma, kwamba afanyayo siyo na anastahiki ajiuzulu. Mmojawao alikuwa Ahmed Kathrada, mshauri wa zamani wa kisiasa wa Nelson Mandela, aliyefariki dunia Machi 28, mwaka huu.

Wengine walikuwa marais wastaafu Thabo Mbeki na Kgalema Motlanthe, aliyeushika urais kutoka Septemba 25, 2008 hadi Mei 9, 2009 baada ya Mbeki kujiuzulu Septemba 24, 2008. Wote wamethubutu kumkosoa Zuma, tena hadharani.

Aprili 11, Mbeki alitoa waraka akieleza wajibu na dhima ya wabunge wa ANC kwa mujibu wa mfumo wa Demokrasia ya Kikatiba unaofuatwa Afrika Kusini. Suala hilo lilizuka baada ya wabunge wa upinzani kuamua kwamba watawasilisha Mswada bungeni wa kutokuwa na imani na Rais Zuma.

Katika hali hiyo, wabunge wa ANC wamuunge mkono Zuma, mwanachama mwenzao wa ANC, au wawe na uhuru wa kuunga mkono Mswada dhidi ya Zuma? Yaani wajibu wao ni kwa ANC au kwa umma wa Afrika Kusini? Wanakitumikia chama bungeni au wanawatumikia wananchi?

Mbeki amesema kuwa katiba imesema wazi ya kuwa wabunge wote wanawatumikia wananchi sio vyama vyao. Mbeki na Motlanthe hawakukauka kama wafanyavyo marais wastaafu wa Tanzania.

Kimya chao hatimaye kitaweza kuwafanya Watanzania wajikute wanaomboleza kwenye magofu ya kisiasa yatayoachwa na wenye kutawala kimabavu bila ya kuzizingatia sheria za nchi na utawala bora.

Share: