Makala/Tahariri

Makala: Mama wajawazito Kisiwapanza, Makoongwe Pemba wanavyocheza kamari na maisha yao, kisa…..

March 21, 2018

Imeandikwa na Hababi Zarali, Pemba

MTUMWA Haji (35), mkaazi wa Kisiwa cha Makoongwe Mkoa wa Kusini Pemba hatasahau mkasa uliomkuta wakati wa wakati alipofikia hatuwa ya kujifunguwa katika ujauzito wake wa kwanza mwaka 2016.

Siku hiyo alijifunguwa mapacha wa kiume akiwa ndani ya mashua bandarini kabla kufikishwa hospitali kuu ya Abdalla Mzee na kwa bahati mbaya watoto wake hao walifariki baada ya muda mfupi tangu walipozaliwa.

Kufariki kwa watotowake kulichangiwa na kukosa huduma za wataalamu wa afya, ambalo ni tatizo kubwa kijijini kwao. “Nilipatwa na huzuni kubwa ambayo sitaisahau maishani mwangu, kupoteza watoto wangu wawili ni msiba mzito kwani familia yangu imekosa furaha,”anasema.

Ni dhahiri kuwa uchungu wakati wa kujifungua ni kipindi kigumu wanachopitia akinamama, ingawa jambo hili ni la kimaumbile kwao, lakini kwa dakika chache wanapokuwa katika harakati za kujifungua hali inakuwa ni kati ya mauti na kifo.

Hakuna binadamu mwenye akili timamu na hisia kamili, anayeweza kupinga kwamba uzazi ni njia ngumu kwa akina mama, ingawa kila jambo huwa jepesi mbele ya Mwenyezi Mungu ambaye ndie aliyejaalia hayo.

Katika hali kama hiyo, pale panapokosekana huduma bora kwa mama mjamzito tangu mimba inapotunga, kuilea hadi kujifungua, wapo waliopoteza maisha pamoja na watoto.

Aidha akinamama wengine hupata kifafa cha mimba na mara nyengine watoto huzaliwa kabla hawajatimiza umri wa kuzaliwa na hivyo kuitwa njiti.

Ingawa baba huona uchungu wa hali inayomkuta mwenza wake, lakini ni mama ndie anaebeba uchungu mwingi na unaouma bila kiasi.

Wanawake wa visiwa vya Makoongwe na Panza wanaposhikwa na uchungu kujifunguwa kulazimika kubebwa kwa vitanga vya mikono kutoka visiwani wanakoishi hadi bandarini na kuingia katika mashua kwa ajili ya kuwavuusha hadi ngambo ya pili na hapo ndipo hutafuta usafiri wa gari kuwapeleka hospitli ya Abdalla Mzee ilioko Mkoani

Mwandishi wa makala haya alifunga safari hadi kisiwa cha Makoongwe na Panza ambavyo vinaonekana kusahaulika kusogezewa huduma za afya ya uzazi.

MAENEO YALIYOSAHAULIKA

Visiwa vya Makoongwe na Kisiwa Panza, ni maeneo yanayokosa huduma za uzazi salama, ambavyo havijaguswa na sera ya Wizara ya Afya ya mwaka 2011.

Sera hiyo inasisitiza haja ya kuongeza kasi ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi hasa vijijini.

Lakini mambo ni tafauti kwa visiwa hivyo, ambapo vifo vinatokea kutokana na wakaazi wake kukosa huduma licha ya kuwepo vituo vya afya.

Kutoka Kisiwa cha Makoongwe chenye wakaazi 2,110,ni mwendo usiopunguwa dakika 45 hadi iliko hospitali kuu ya Abdalla Mzee inayotowa huduma hizo, wakati kutoka Kisiwa Panza chenye wakaazi 6,146, hadi hospitalini hapo ni mwendo usiopunguwa dakika 75.

Wahenga walisema, “Uchungu wa uzazi ni sawa na wingu la mvua” ambalo halijulikani lini na saa ngapi hutokea ili mama aweze kujiandaa na kuwahi hospitali.

Kutokana na ugumu wa usafiri majini wa kubadilika kwa hali ya hewa ya upepo usiokuwa wa kawaida unaoambatana na mawimbi makubwa husababisha wajawazito kupoteza maisha kabla ya kufikia hospitali.

Akina mama hao wa visiwani hupata kikwazo cha awali kabla ya kufika bandarini kwa kutokuwepo usafiri wa nchi kavu kwenye vijiji vyao na kulazimika kubebwa na familia zao mithili ya wagonjwa.

Siku niliyokwenda Makoongwe nilipanda mashua ya mwanzo saa 12.00, lakini nilipata hofu baada ya kuona mawimbi ya bahari yakiingia ndani ya mashua na nilipoulizia muda gani tutafika kisiwani nikaambiwa ni muda wa saa moja hivi

Nahodha, baada ya kuniona nimeingia hofu alinipa moyo kwa kuniambia nisijali nitafika salama na nilitulia kama maji mtungini hadi nilipofika baada ya nusu saa.

MASHUHUDA WENGINE

Mwanakhamisi Jamal Khamis (37) ni mama wa watoto wanne, ambaye simulizi zake za namna alivyokumbana na misukosuko ya uzazi, zinatia huzuni kwa yeyote atakayezisikia.

Almanusra apoteze maisha kutokana na kutokuwepo wataalamu wa afya ya uzazi katika kisiwa chao, hata hivyo, anasema mtoto wake aliyembeba tumboni miezi tisa alikufa.

Mimba hiyo ilimsababishia matatizo na hajui hatma ya uzazi itakuwaje kwa sababu tatizo la ukosefu wa wataalamu bado lipo.

Mwanahamisi, akikumbuka mateso aliyopata,anasema wakati huo alikuwa nyumbani kwa mkunga wa jadi alikofuata msaada wa kujifunguwa.

Siku hiyo ilikuwa ngumu kwake kwani mtoto alitanguliza mkono wakati akitoka kuja duniani kufuata majaaliwa yake na kusababisha bega kukwama hali iliyosababisha kifo chake.

Huku machozi yakimlengalenga, anasema mkunga wa jadi aliemewa na hakuwa na namna yoyote ya kumsaidia na ndipo ilipoamuliwa kuvuka bahari kupelekwa hospitali ya Abdalla Mzee akiwa hajitambui. “Nilichungulia kaburi, nilipoteza damu nyingi, nikapoteza fahamu na hata baada ya matibabu miguu yangu haikuwa na nguvu, kwa zaidi ya miezi miwili nilikuwa siwezi kusimama vizuri,” alibainisha.

Mzazi mwengine, Asha Haji Khamis (43) mkaazi wa Makoongwe, anasema tokea alipopata fahamu zake kisiwa hicho kina kituo cha afya lakini hakitumiki kwa huduma za uzazi.

Kutokana na hilo, wanawake wanapotaka kujifungua, hupata usumbufu kwa kutumia usafiri mgumu wa bahari kufuata huduma hospitali kuu ya Mkoani.

Akitoa ushuhuda wa matatizo aliyoyapata katika mimba yake ya kwanza mwaka 2003, mama huyo ambaye mimba zake zote tatu amejifungua kwa njia ya upasuaji, anasema alianza kuumwa na uchungu tokea saa 12.00 asubuhi

Siku hiyo hakukuwa na chombo cha uhakika cha kumfikisha ng’ambo ya pili ili kwenda hospitali hadi saa 1.45 alipobahatika kupata chombo.

Alipofika hospitali ya Abdalla Mzee akajifungua kwa upasuaji baada ya kuambiwa na wataalamu wa afya amechelewa kufika.

Mashaka hayakuishia hapo, kwani mikosi ilizidi kumuandama aliposhika mimba ya pili miaka miwili baadae.

Kilikuwa kipindi cha upepo na chombo alichopakiwa kukimbizwa hospitali badala ya kwenda mbele kilikuwa kinarudi nyuma huku maji ya bahari yakiingia ndani, hata hivyo, alijifungua salama lakini pia kwa upasuaji.

Mimba yake ya tatu, siku ya kujifungua, anasema alishikwa na uchungu saa 3.00 usiku, wakati ambao vyombo vyote vilikuwa juu baada ya manahoza kumaliza shughuli zao za uvuvi na usafirishaji na ikabidi wanakijiji kuitana ili kumpa msaada wa kumsafirisha.

“Sisi wanawake wa visiwani tuna tabu ya kupata huduma za uzazi na tunapokaribia siku ya kujifungua tunakuwa na hofu na mawazo tukifikiria jinsi hali itakavyokuwa,” anasema.

Tatu Makame Khamis (65) mkaazi wa Makoongwe, anaeleza jinsi mama mkwe wake alivyopata tabu katika harakati za kumpeleka hospitali kujifungua baada ya mkunga wa jadi kushindwa kumzalisha.

Alishawapeleka watoto wake kujifungulia hospitali ya Abdalla Mzee, lakini mkwewe alijifungulia bandarini walipokuwa wanasubiri usafiri wa kuwavusha ng’ambo ya pili. “Ilikuwa hatari, mtoto alitoka vibaya na mkunga hakuwa na uwezo tena wa kumsaidia, na pia pahala hapo hakukuwepo usafiri hatimaye mtoto alikufa na mama akawa taabani, hajiwezi baada ya kupoteza damu nyingi,” alisimulia.

Akisimulia matatizo wanayopata Juma Makame Haji kutoka Makoongwe alisema hulazimika kuwabeba akina mama kwa viganja vya mikono kuwapeleka katika kivuuko wanapotaka kujifunguwa.

Iwapo serikali haitochukuwa hatuwa kuwapeleka wataalamu wa afya katika vijiji hivyo wanawake na watoto wataenelea kupata matatizo ya uzazi siku zote.

Nahoza wa mashuwa inayoitwa Gema lao Hamad Chumu Hamad wa kisiwa Panza tayari ameshashuhudia akina mama wajawazito saba wakijifunguwa kabla ya kufika Hospitali kuu kutokana na kuharibikiwa na chombo ama kuishiwa mafuta. “Nimepata funzo sasa inanibidi kila muda mashine yangu iwe na mafuta ili kuwawahisha wajawazito hospitali kuu ya Mkoani na wala mimi kwa mjamzito simdai hata shilingi moja”anasimulia.

Mkuu wa kituo cha afya Makoongwe, Rajab Juma Seif, anakiri kituo hicho hakitoi huduma za uzazi kutokana na kutofikia darja hali inayowafanya wajawazito kwenda hospitali ya Abdalla Mzee. “kituo hichi cha afya hakiwezi kupokea wajawazito na kuwazalisha hata kwa bahati mbaya maana hatuna mtaalamu wa hilo, kitanda, dawa husika lakini hata chumba cha kujifungulia”alisema.

VIONGOZI WAKIRI

Moza Nassor Ali, ni muuguzi mkuu wa Wilaya ya Mkoani, anakiri kuwepo tatizo linalosababisha ongezeko la vifo vya mama na watoto wakati wa kujifungua.

Anasema, tatizo hilo linachangiwa na wajawazito kujifungulia nyumbani badala ya Hospitali kama wanavoelekezwa.

Aidha aliitaja changamoto ya kufuata huduma masafa marefu na uelewa duni wa elimu ya afya ya uzazi, kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la matatizo yatokanayo na uzazi.

“Muhudumu wa mama na watoto katika kitengo cha afya ya uzazi hospitali ya Abdalla Mzee, Amina Ali Mbarouk, anasema tatizo linalogharimu maisha ya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua ni kucheleweshwa kufika hospitali.

“Mara nyingi mama anapokuja hospitali hali huwa imeshakuwa mbaya,” anasema na kuongeza,

“Pamoja na juhudi tunazochukua, bado hujikuta tukimpoteza mama au mtoto na mara nyengine wote wawili.”

Uchunguzi unaonesha kuwa kwa mwaka 2015, wajawazito 30 walifika Hospitalini hapo kwa ajili ya kujifunguwa ingawa mwaka uliofuata idadi hiyo ilipunguwa 12, na kuripotiwa akina mama 18 tu kutoka visiwa vya Makoongwe na Panza pekee.

Ingawa kwa miaka hiyo miwili hakukuripotiwa kifo cha mama, na wanne kati ya 48 walifanyiwa upasuaji kuokowa maisha yao, na watoto wanne ndio waliofariki dunia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wazazi wao kutofika hospitali mapema.

Muhudumu mwengine wa afya ya uzazi, Rabia Mohamed Ussi, anasema bado elimu ya afya ya uzazi ni ndogo kwa hasa vijijini, ambako ndiko kwenye tatizo la kuzalia majumbani.

“Matatizo kama kukwama kwa zalio, kuchanika msamba, yote haya husababisha mama kutoka damu nyingi na mkunga wa jadi hawezi kumsaidia kwani haya yanataka wataalamu wa hospitali,” alieleza.

Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Hemed Suleiman Abdalla, anasema malengo ya serikali ya wilaya ni kuhakikisha vituo vya Makoongwe na Kisiwa Panza vinapatiwa wataalamu na vifaa ili viweze kutoa huduma za uzazi.

Kwa wakati huu ambapo wananchi hulazimika kwenda Hospitali ya Abdalla Mzee, alisema uongozi wa wilaya umewahamasisha wamiliki na manahodha wa vyombo vya usafiri baharini wasaidie kuwavusha wakati wowote wanapohitaji huduma.

Hemedi anakiri kwamba uhaba wa wataalamu wa afya ni tatizo katika visiwa hivyo lakini serikali inaajiri awamu kwa awamu na kwa sasa wameshirikiana na ofisi ya mganga mkuu wa wilaya kutoa elimu kwa wananchi kukimbilia hospitali mapema ili kupunguza matatizo.

Kila kituo kimoja kinahitaji wataalamu wa afya wasiopunguwa tisa (9) lakini kwa kituo cha makoongwe wapo wawili (2) na kisiwa panza wapo watatu(3).

Naibu Waziri wa Afya, Harusi Said Suleiman, anakiri kuwepo tatizo hilo lakini akasema serikali haikulala bali inapanga mikakati ya kuvijengea uwezo vituo hivyo ikiwemo kuongeza wataalamu na vifaa.

Anasema kwa kuwa kupanga ni kuchagua, suala la kuviimarisha vituo hivyo ni la muda tu na kuwaomba wananchi kuwa wastahamilivu.

“Mipango yetu ya baadae ni kuviimarisha vituo hivyo kwa kuvipelekea wataalamu wa uzazi na huduma za mama na watoto,” anasema.

Alisema kwa kuanzia serikali itaanza kukishughulikia kituo cha Kisiwa Panza na baadae Makoongwe.

Anasema hivi karibuni wizara iliajiri wataalamu lakini ikaviangalia zaidi vituo vinavozalisha na hawakutosha.

Katika kupambana na tatizo la uhaba wa wataalamu Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), limeweka mikakati na miongozo mbalimbali kuzitaka nchi zote kuhakikisha zinatenga bajeti za kutosha kwa ajili ya wizara za afya hasa kwa upande wa huduma za mama na mtoto.

WHO, linasaidia uimarishaji wa huduma hizo kwa kutoa misaada kuanzia fedha, vifaa na wataalamu hasa katika nchi zinazoendelea ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya, imekuwa mstari wa mbele kutekeleza mambo muhimu yanayohusu afya ya uzazi ikiwemo Kuhakikisha upatikanaji wa vifaa, zana za huduma za uzazi salama, huduma za mama na mtoto na huduma za uzazi wa mpango (family planning commodities)

Kwa upande huo, Zanzibar imefanikiwa kupunguza idadi ya wajawazito wanaozalia majumbani kwa asilimia 68.3 mwaka 2014, kutoka asilimia 56.6 mwaka 2013. Bajeti ya mwaka 2016/17 ya Wizara ya Afya imeweka wazi muongozo wa kutoa elimu kwa mama wajawazito kuhusu vidokezo vya hatari pamoja na lishe.

Wafanyakazi 70 wamepatiwa mafunzo ya kutumia muongozo huo ili kuhakikisha wajawazito wanajifungua katika vituo vya afya na hospitali ambapo wizara imeanzisha mpango maalumu wa ufuatiliaji kwa baadhi ya wilaya ikiwemo kaskazini ‘B’ Unguja.

Kupitia bajeti hiyo, dawa na vifaa tiba vimenunuliwa na kusambazwa katika vituo vya afya.

Hizo ni juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, lakini pamoja na mafanikio hayo, kuna maeneo yaliyoachwa nyuma.

MWISHO.

Pembatoday

Share: