MaadiliMakala/TahaririMaoni

Makala: Wamelishwa nini?

Habari za wakati huu mpenzi wa mtandao huu wa kijamii wa mzalendo net, natumai muwazima wa afya, nakutakieni nyote siku njema, na nakutakieni mabadiliko mema ya uongozi ambao umependekezwa na wengi.
Leo nimewaletea makala hii maalumu ambayo itaangalizia ni kwa nini chama tawala cha CCM ambacho ni chama ambacho hakionekani kwa sura nzuri miongoni mwa wanachi wengi wa Pemba bado kuna watu ambao wanakipigia debe na kukichagua? Makala hii imeandaliwa na mimi mzalendo mwenzenu, Moh’d Khamis Songoro.
Nimechukua takriban wiki mbili hivi kukamilisha makala hii.
Chama cha Mapinduzi, bila ya shaka ni Chama ambacho hakimo katika mioyo ya watu wengi wa Zanzibar hususan wakaazi wa kisiwa cha Pemba, ila cha kushangaza ni kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanasema kuwa CCM imo ndani ya damu yao, nimechukua siku kadhaa kukaa na familia moja ambayo tuna uhusiano wa kidamu kwa kiasi kikubwa nikitaka kujua haswa ni nini sababu inayofanya chama tawala cha CCM kubaki katika mioyo yao? Pia katika makala haya nitaunganisha baadhi ya matokeo ambayo nimeona kuwa ni ya muhimu kuweka.
Katika utafiti wangu niliofanya, niligundua kuwa Chama cha Mapinduzi kinabaki kutetewa tu na baadhi ya wafanyakazi wa Serikali na kupigiwa debe, Takriban wiki mbili kabla ya uchaguzi nilipokuwa shule, kabla ya dakika kadhaa kuruhusiwa kuondoka shule, tuliitwa katika paredi ya kawaida, kulikuwa na mgeni wa heshima kutoka katika Wizara ya elimu, kwa sababu ya kiusalama sitotaja jina na cheo chake. Alikuja shule kwa ajili ya kuongea na wanafunzi juu ya suala zima la amani na kutoshiriki katika vurugu lolote la kisiasa, aliongea mengi ila baada alijitia hamnazo na kujitia kupigia kampeni chama cha CCM kwa siri, hakutaja halisi kuwa mchagueni fulani, ila alilosema ni kuwa kwa wanafunzi ambao mumeshakuwa munajua cha kufanya, na kutoa methali yake ya kuwa mkono unaokulisha … usiitemee mate, hili ni kwa maana ya kuwa kwa sasa tunasomehswa na serikali ya mapinduzi ambayo inaongozwa na CCM hivyo tuifanyie hisani CCM, pia alipokuwa anaongelea kuhusu wanafunzi wasishiriki chochote kuhusu vurugu kama litatokea aliuliza kuwa kwani serikali imewakosa nini wanafunzi, kwa kuwajengea jengo kusoma ama kwa kuwaletea waalimu ambao wanasomesha?
Siku ya Jumatatu tarehe 19 october 2015, takriban muda wa saa 11 za jioni, nilikuwa katika nyumba ya bi. Aisha Ali Hussein (sio jina lake, nimempa jina hilo kwa sababu za kiusalama), nilikuwa nao kama familia, mara aliwalalamikia watoto wake kuhusu mama mmoja ambae amekuja kumpiga kampeni ili apigie UKAWA, bi Aisha alisema kuwa anamshangaa yule mama kwa kuwapigia kampeni C.U.F wakati mama mwenyewe hana alilo nalo na ni maskini kama yeye. Maneno yale yalinigusa moyoni mwangu na nikaanza kuyafanyia uchambuzi moyoni mwangu. Bi Aisha ni mama kizuka, ni mwaka wa pili sasa tokea mume wake afariki, mume wake alikuwa ni mwanachama mwenye msimamo wa dhati kwa chama cha CCM, Mama huyu kwa sasa anao watoto wanne ambao wanamtegemea kwa kula, mavazi na malazi; ni mama asie na kazi yoyote na maisha yake yanategemea kilimo kidogo amabacho mavuno yake hayawezi kumchukua hata nusu mwaka, huishi kwa kilimo hiki na visaada vidogo vidogo ambavyo anavyopewa na ndugu jamaa na marafiki. Mume wake aliifanyia kazi CCM tokea zama za Idi amini na baadae aliacha kazi ya uwanamgambo, akawa naibu wa sheha na alikufa bado akiwa ni naibu wa sheha. Kitu pekee ambacho serikali kinafanya kwa mama huyu ni kuwa kila mwezi hupewa shilling elfu tano, elfu tano ambayo pia hukatwa tena shilingi elfu moja na katibu wa CCM wa kijiji chao, hivyo hupewa shilingi elfu nne tu za kitanzania, katibu ambaye anajua haswa kuwa mama huyu ni kizuka, na kazi ndogondogo ambazo hutokea kupitia kwa katibu huyu, huchukuwa wanawe na hajawahi kumchukua mtoto wa mzee huyu, ijapokuwa anae mtoto mmoja ambae anao uwezo wa kufanya kazi hizo ambazo hutoka. Nilishangaa ninini chama tawala kimempa mama huyu, ameshatekwa kimawazo, huku akili yake ikizidi kudidimia bila ya kutafakari mustakbali wa maisha ya baadae ya watoto wake. Nilifikiri na kuwaza kuwa Chama tawala kinawasaliti watu ambao wametoa muhanga kwa ajili yao, hivi kama chama hicho kimewasaliti watu hao kama kitapendwa na kuendelea kuenziwa na kila mwanamchi wa Zanzibar basi kitakachozidi kuvunwa ni umasikini na matatizo badala ya yale yanayoitwa eti ni matunda ya mapinduzi.

Kwa upande mwengine, sio kuwa ni wafanyakazi wote wa serikali ambao hufanya kazi chini ya CCM wanayo mapenzi ya dhati na chama tawala, bali mambo ni tofauti, Mmoja ya waalimu wangu wa shue ambae nimempa jina la Ahmed Abdallah kwa sababu binafsi, sasa ni mfanyakazi wa wizara ya elimu, wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu, nilipata nafasi ya kuongea nae, tuliongea mengi kibinafsi, ila mwishoe alinipa wasia ya kuwa, usidanganywe na kampeni za CCM, wewe mtu akikujia akikwambia atakusomehsa, atakufanyia hivi, atakufanyia vile, wewe itikia tu, hawana watakalo fanya, ni nusu karne sasa, siku zote wanarudia sera zile zile na hawana wanachokifanya, wewe waitikie tu, siri yako unayo moyoni.
Siku ya Ijumaa 23 October 2015, niliongea na binti ambae nae nimempa jina la Leluu, niliongea nae kama mzaha huku nikijua kuwa mwisho utatumbuka usaha, niliongea nae na nilianza kukiponda chama cha Mapinduzi kwa kusema kuwa hakina sera na hakifai kuongoza tena, alijaa na kujaa hadi akamwagika, alisema kuwa kama C.U.F wakipata nchi waarabu watarudi na watu watafanywa kuwa watumwa, mwaka 2010 ilikuwa teari waarabu washajitayarisha kuja lakini aliposhinda sheni wakapigiwa simu wasije. Binti alienda mbali na hadi kufikia kuangusha matusi, naomba radhi kwa lugha nitakayotumia hapo chini.
Alichosema binti ni kuwa nyinyi unaotaka C.U.F ni wasenge nyote, kwa sababu waarabu watakaporudi watatembea na wanawake na mwisho wanawake watamaliza mutageukiwa nyinyi wanaume.
Kwangu lilikuwa ni jambo la kiajabu sana, nilidhania kuwa maneno hayo yalikuwa yamo katika akili za watoto tu, nilishangaa sana kuona binti ambae miaka yake ni takriban miaka 19 akiongelea jambo hili na nilijua tu kuwa si bure, ni propaganda za uongo na hofu walizotiwa tokea utoto.
Pia nilikuja kugundua kuwa wanachama wa CCM hupewa vipao mbele juu ya upatikanaji wa vitambulisho, mmoja miongoni mwa madada wa Leluu ambae nimempa jina la Aziza, nilifanikiwa kuona kitambulisho chake ambacho pia alitumia kupigia kura mwaka 2010, kitambulisho hicho kilitengenezwa kienyeji kwani aliandikiwa amezaliwa mwaka 1998 ili apate kupiga kura uchaguzi wa mwaka ule hali ya kuwa tarehe yake ya ukweli ni mwaka 1993. Dada huyu nilijaribu kuongea nae ila alinambia ya kuwa mara hii hana mpango kabisa wa kupiga kura.
CCM ni chama ambacho pia kimekosa kutengeneza wanachama wazalendo, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa CCM ilikuwa inakodi gari kwa ajili ya kuwapeleka watu katika kampeni zao, mambo yalikuwa tofauti kwa ukawa, wanachi walijitolea wao wenyewe kwa kuonesha uzalendo wa chama chao.

Na siku ya uchaguzi mkuu, nimekuja kugundua kuwa wazee pia huwalazimisha watoto wao kuingia katika siasa na kuwatilia CCM kura, muda wa mchana nikiwa eneo la bi Aisha, nilipoenda bi Aisha alikuwa hayupo, nilimkuta Leluu na Aizaza, Aziza alinilalamikia kwa kuwa mama yao aligomba sana na kaondoka na hamaki kwa sababu wao hawajataka kuenda kutia kura. Baada muda si mrefu, mzee mmoja ambae ni naibu wa sheha na ana uhusiano mkubwa na bi Aisha, alikuja kuwaita Leluu na Aiziza na kuwambia kuwa kuna gari imekuja kuwachukua ili ikawapeleke kupiga kura huko maeneo ya Vikunguni, Chake Chake, Pemba. Leluu alijificha lakini mzee alizidi kuwakazia na kupiga kelele, ndipo Leluu alipoamua kutoka na kuenda kwenye gari, ni gari ambayo ilikodiwa na CCM kwa ajili ya kupeleka na kutafuta watu wa kuwapigia kura. Ni gari ya Haisi ya abiria ishirini ila ndani yake mulikuwa na watu wawili mbele, nyuma alikuwa Leluu, Yule mzee na pamoja na konda wa gari ile. Nami niliamua kuingia kwenye gari ile ili niende nao, niliingia katika gari ile, wakati tupo njiani, mzee alianza kulalamika juu ya Aziza na kusema kuwa yeye asimwambie lolote kwa sababu hajaenda kupiga kura, alisema kuwa kura moja ina thamani kwa CCM, kama haina thamani isengelitolewa gari mbali ikafuate mtu mmoja tu.
Tulipofika kituo cha kupigia kura Yule mzee alimtafuta sheha wa shehia na kumweleza kuwa amepata watu watatu na kuwa mmoja (ambae ni Aziza labda) hakutaka kuja. Nilijaribu kutaka kuongea na Aziza kule kituoni na kumuuliza haswa ni nani anaetaka kumpigia kura? Ila juhudi zangu zilikwama kwani alikuwa amechukia sana kuenda katika kituo cha kupigia kura.
Hivyo basi CCM inabaki kutetewa na vibaraka wao wanaowatumia madarakani, wazee na vijana wanaolazimishwa kuichagua CCM pamoja na watu duni amabo wamejazwa uongo mioyoni mwao.
Na hapa ni mwisho mwa makala haya fupi.

Share: