Makala/TahaririZenjiLikiz

Makamishna wa ZEC kubambikiziwa kesi feki za kuhujumu uchaguzi

Jabir Idrissa,

IDARA ya Mahakama Zanzibar inatumika kutekeleza mpango mchafu wa kuandaa na kuziamua kesi za jinai zinazokusudiwa kufunguliwa dhidi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa lengo la kutaka kuhalalisha madai ya kuvurugika kwa uchaguzi.

Madai ya kuharibika kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, yamekuwa yakipaishwa na viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinatajwa kumtweza nguvu Mwenyekiti wa Tume, Jecha Salim Jecha hadi kutangaza kufutwa kwa uchaguzi Oktoba 28.

Gazeti la MwanaHALISI limefahamishwa kuwa wanasheria kadhaa wakiwemo walioko Idara ya Mahakama wanashiriki katika mpango huo ambao wachambzi wanasema unalenga kuufanya uongo wa chama hicho uaminike kama ndio ukweli.

Zimepatikana taarifa za uhakika kuwa Mahakama ya Zanzibar itapokea kesi angalau mbili zinazohusu kilichoitwa “tuhuma za uzembe na ufisadi katika uchaguzi” walengwa wakiwa ni watendaji wa Tume waliosimamia uchaguzi majimboni.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, katika mnasaba huohuo, ndipo inafikiriwa hata Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, akamatwe na kutungiwa kesi.

Kesi inayotajwa sana katika vinywa vya viongozi wakubwa na wadogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), inahusu madai kuwa kiongozi huyo aliyegombea urais na kutangaza mwelekeo wa kushinda uchaguzi mkuu, alijitangazia “mshindi” Oktoba 26, siku moja baada ya upigaji kura.

Katika kesi ya watendaji wanaotuhumiwa kuharibu uchaguzi, ambao ulithibitishwa na waangalizi kuwa ulikuwa uchaguzi mzuri kuliko wa 2010, inadaiwa atakuwemo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Haijaelezwa hasa mashitaka gani yatamhusu Jecha, ambaye ndiye alitoa tangazo Oktoba 28, la kufutwa uchaguzi wote wa Zanzibar kwa alichodai ulikumbwa na matatizo mengi, yakiwemo machache aliyoyataja katika taarifa aliyoitolea ufichoni alikorekodiwa na taarifa kurushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Hata hivyo, inaelezwa katika mpango huo wa siri, Jecha atashitakiwa kama njia ya kulaghai ulimwengu, kwa kuwa wanaofadhili mpango huo, wamekuwa wakikiri “kunufaika na alichokifanya Jecha.”

“Hii kesi ya Jecha kama zilivyo nyingine, isipokuwa ya Maalim Seif, ni geresha tu kwa sababu wakati ya Jecha ni nzito ambayo ingeweza kuwa kesi ya kumfungisha jela, itakosa ushahidi kwa kuwa wenyewe hawako tayari aadhibiwe. Huyu wanasema hajatenda kosa,” amesema msiri wa gazeti hili ambaye ni mtumishi serikalini.

Kumekuwa na shinikizo nyingi kutaka Maalim Seif akamatwe na kushitakiwa kwa tuhuma za kujitangaza mshindi wa urais.

Taarifa zilizotangazwa hivi karibuni na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DDCI) wa Zanzibar, Salum Msangi, zimesema tayari maofisa wa Tume na makamishna wameanza kuhojiwa.

Kamishna Msangi ameripotiwa akisema Makamu Mweyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa tayari ameshahojiwa.

Mwenyewe Jaji Abdulhakim hajathibitisha kuhojiwa ingawa walio karibu nae wanasema baada ya kuwa ametekwa kwenye ofisi za Tume eneo la ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani, alidhibitiwa na Jeshi la Polisi Makao Makuu Ziwani kwa saa tatu hivi na kuachiwa kiasi cha saa 9 mchana Oktoba 28.

Jaji Abdulhakim mpaka sasa hajawa tayari kuzungumza kilichomtokea hasa siku hiyo. Jitihada za mwandishi wa habari hizi kupata kauli yake zimeshindikana. Simu haipokewi na meseji zinazouliza yaliyomsibu alipotekwa, hazijibiwi.

Siku hiyo alichukuliwa kwa nguvu na askari wawili waliovalia upolisi na kuongozwa kuingia kwenye gari ya vioo vya giza ambayo ni moja ya zinazotumiwa na Tume ya Uchaguzi zikiwa ni za mradi wa uchaguzi 2015 uliofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Wakati jaji huyo kijana akidhibitiwa na maofisa wa upelelezi wa Polisi makao makuu bila ya kuhojiwa lolote, ndipo kukasikika tangazo la Mwenyekiti Jecha la kufuta uchaguzi.

Siku hiyo Jecha alikuwa amesubiriwa na wenzake kuendelea na kazi ya kutangazwa matokeo ya urais akini hakutokea saa 4 kama alivyoahidi siku iliyotangulia ambayo shughuli zilisitishwa baada ya umeme kukatika Bwawani. Tayari alikuwa ametangaza matokeo zaidi ya asilimia 70.

Wasiri wa gazeti hili wanasema ndani ya Idara ya Mahkama Zanzibar, wapo majaji wasiopungua wawili wanashirikiana na wanasheria binafsi wa Zanzibar wanaohangaika maandalizi ya kesi hizo za kubabaisha.

Mwanasheria mmoja kati ya waliotajwa kushirikishwa, ameithibitishia MwanaHALISI kuwa mpango huo unafadhiliwa na baadhi ya wakubwa wa CCM.

“Vile ukiona baadhi ya watu wanatokeza kwenye teleivisheni kutetea alichokifanya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, ujuwe ni sehemu ya huo mpango unaoniuliza kama upo. Lakini mimi sijaingia sana labda kwa kuwa wanaamini siwezi kuwasaidia mambo yao,” amesema mwanasheria katika moja ya kampuni binafsi za uwakili hapa.

Imekuwa mtizamo wa watu wengi hapa kuwa baada ya Othman Masoud Othman, mwanasheria aliyefukuzwa kuwa mwanasheria mkuu wa serikali baada ya Bunge Maalum la Katiba, kutoa elimu kubwa kupitia programu ya Mada Moto ndani ya Channel Ten, kumetumwa baadhi ya watu kupotosha aliyoyaeleza.

Wakati watu hao wakisikika waziwazi kutetea uamuzi wa Jecha, na kuendeleza madai yaliyosikika kutolewa na viongozi waandamizi wa CCM mara tu tangazo la kufutwa uchaguzi lilipotolewa, wamekuwa wakieleza kwa hoja msisitizo kuwa Maalim Seif alivunja utaratibu kutangaza ushindi.

“Unaona hawa mara zote unaowasikia wakimsakizia tuhuma Maalim Seif, wanakwama unapouliza kama adhabu ya kosa lake inastahili uchaguzi ufutwe,” amesema ofisa ndani ya Tume ya Uchaguzi.

Imeelezwa kwamba mpango wenyewe ni kuzikabidhi kesi hizo kwa wanasheria hao binafsi ikiwemo kampuni ambayo baadhi ya wamiliki ni watoto wa viongozi wakubwa serikalini, watakaozisimamia chini ya mwamvuli wa serikali.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa taarifa wiki mbili zilizopita kupitia aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud kwamba wanaheshimu uamuzi wa Tume kufuta uchaguzi na kusihi wananchi watulie huku wakisubiri uamuzi mwingine wa kuitisha uchaguzi mpya.

Tangu Jecha atangaze uamuzi wa kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar wakati yeye mwenyewe alishatangaza hadharani matokeo ya kura za urais katika majimb 31, hajasikika yeyote katika tume hiyo kuzungumza lolote.

Hata hivyo, gazeti hili limethibitishiwa taarifa kuwa Jecha aliibuka Novemba mosi na kuwaita makamishna kwa ajili ya kikao.

Katika kikao hicho ambacho inasemekana hapakuwa na muandikaji kumbukumbu, Jecha alinukuliwa akisema “nimelazimika kusema uongo ili kuiokoa nchi na balaa.” Uongo wenyewe unatajwa kuwa ndio huo wa kudai taratibu nyingi za uchaguzi zilikiukwa ikiwemo kura zilizopigwa kukutwa mitaani, idadi ya kura kuzidi wapigaji katika baadhi ya vituo ambavyo hakuvitaja na kwamba katika kuyajadili matatizo hayo, makamishna walishikana mashati wakiwa wameacha jukumu lao la kuzidiwa na matakwa ya vyama vyao vya siasa.

Hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sasa, Said Hassan Said, hajajitokeza kueleza msimamo wake kuhusu madai ya kutokuwepo uongozi halali wa serikali akiweo Dk. Shein, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar. Imekuwa vigumu kumpata kwa simu na hata ofisini.

Jaji Mkuu Omar Othman Makungu naye hajapatikana. Simu yake imekuwa ngumu kupatikana. Mara nyingi inalia pasina kupokewa.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar inaundwa na mamishna saba – wawili kutoka CCM na wawili kutoka CUF; mwenyekiti na makamu mwenyekiti na mjumbe anayewakilisha vyama visivyo na wawakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Rais atamteua mwenyekiti wa Tume kwa kigezo cha mtu aliyekuwa au mwenye sifa za kuwa jaji katika Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufaa katika nchi yoyote iliyo mwanachama wa Jumuiya ya Madola au mtu anayeheshimika katika jamii.

Jecha amesomea Shahada ya Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akawa kiongozi mwandamizi serikalini ambaye alistaafu akiwa Katibu Mkuu wizara ya Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ.

Aliteuliwa kuongoza Tume mwaka 2013.

Kumetanda ukimya mkubwa hapa Zanzibar wakati Maalim Seif akiendeleza vikao vya majadiliano na marais wastaafu Amani Karume, Ali Hassan Mwinyi na Dk. Shein na Balozi Seif Ali Iddi.

Maofisa usalama wa taifa wanasema hwenda viongozi hao wakaendelea na vikao leo ambavyo hufanyikia Ikulu ya Zanzibar.

Vikao hivyo vimekuwa vya siri. Hakuna anayetaka kueleza kinachozungumzwa na lini majadiliano yatamalizika.

Hali inakuwa mbaya kwa umma kwa vile kinachosemwa ndani ya CCM ni maandalizi ya uchaguzi mpya kama ilivyoeleza taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Zanzibar, Waride Bakari Jabu.

Amesema “kwa mara nyingine tena tunaiomba Tume itangaze sik uya uchaguzi ili tufanye uchaguzi utakaokuwa wa huru na haki. Ni dhahiri, baada ya uchaguzi huo, CCM Zanzibar na wananchi wa Zanzibar watalazimika kufanya maamuzi mengine ingawa yatakuwa magumu.”

“… CCM inawaambia viongozi na wafuasi wa CUF kwamba suala la kuapishwa Maalim Seif Shariff kuwa Rais wa Zanzibar ni ndoto za mchana kwani Tume ya Uchaguzi tayari imetangaza kufutwa kwa uchaguzi huo, na kinachofanywa na wanaCUF ni kuwadanganya wananchi,” amesema Waride.

Taarifa hiyo imeanza na maelezo ya kulaani kitendo kilichofanywa na wabunge wa UKAWA kuwazomea “Viongozi wa SMZ waliohudhuria sherehe za uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano.”

Waride ametaka wanaCCM na wapenda amani watulie na kuvumilia (kwani) “dawa ya wapinzani iko njiani.”

Chanzo: MwanaHalisi

Share: