Makala/Tahariri

Miaka 26 ya kuzaliwa Chama cha Wananchi

By Juliua Mtatiro – Gazeti la Mwananchi
Sunday, May 3, 2018

Mei 28, 1992 (miaka 26 iliyopita), taasisi mbili za harakati za demokrasia – Kamahuru ya Zanzibar na Civic Movement kutoka Tanzania Bara – ziliungana na kutengeneza taasisi imara ya kisiasa ijulikanayo kama The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi).

Kamahuru ilikuwa ni taasisi ya harakati za kudai Demokrasia Zanzibar na Civic Movement ilikuwa ni taasisi ya kupigania haki za binadamu.

The Civic United Front (CUF) kilisajiliwa rasmi kuwa chama cha siasa nchini Tanzania Januari 21, 1993. Pamoja na kwamba kilikamilisha taratibu zote za usajili mapema sana, CUF kilipaswa kusubiri kwa zaidi ya miezi sita ili kusajiliwa kwa sababu ya mizengwe ya serikali.

Viongozi wengi waanzilishi wa CUF upande wa Zanzibar walikuwa ni wale waliochoshwa na uongozi wa CCM na vitendo vyake na kuamua kuondoka kwenye chama hicho au walifukuzwa kutoka CCM kwa sababu ya misimamo yao. Na viongozi wengi wa Bara walikuwa wanaharakati wa haki za binadamu na utawala bora.

CUF chachu ya chaguzi zote
CUF imeshiriki chaguzi zote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi; Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

Katika chaguzi zote hizo tano, CUF imekuwa na madai ya kudumu kwamba inashinda uchaguzi wa Zanzibar lakini inazuiwa na dola kupewa na kuongoza serikali.

Kwa upande wa Tanzania Bara, CUF ilikuwa ikisuasua sana kwenye chaguzi ilizoshiriki miaka ya nyuma lakini ikainuka kwa nguvu sana kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 kwa kupata wabunge 10 wa kuchaguliwa, halmashauri na manispaa tano na madiwani zaidi ya 300 nchi nzima.

Katika chaguzi za 1995, 2000, 2005 na 2010 CUF iliishia kupata wabunge wawili au kukosa, madiwani wachache na haikuwahi kuongoza halmashauri yoyote nchini (upande wa Tanzania Bara).

Nimeona nieleze hayo kabla ya kuanza kukukumbusha mwenendo wa CUF katika chaguzi zote kuu ilizowahi kushiriki Tanzania Bara na Zanzibar kwa usahihi.

Mwaka 1995 (Tanzania)
Mwaka 1995 CUF iliingia kwenye uchaguzi huku mgombea urais wake Ibrahim Lipumba alipata kura 418,973 sawa na asilimia 6.43.

Kwenye kura za urais CUF ilipitwa na CCM (Benjamin Mkapa) kura 4,026,422 (asilimia 61.82) na NCCR (Augustine Mrema) kura 1,808,616 (asilimia 27.77).

Katika uchaguzi huo wa mwaka 1995 CUF ikapata wabunge 28, ambapo 24 walichaguliwa wote kutoka Zanzibar na wanne wa viti maalumu.

Kwenye wingi wa kura za wabunge, mwaka 1995 CUF ilipigiwa jumla ya kura 323,432 (asilimia 5.02) ikizidiwa na CCM iliyopata wabunge 186 wakiwamo wa viti maalumu 26 na kura 3,814,206 (asilimia 59.22), NCCR iliyopata wabunge 16 wakiwamo wa viti maalumu watatu na kura 1,406,343 (asilimia 21.83), Chadema iliyopata wabunge watatu na mmoja wa viti maalumu na kura 396,825 (asilimia 6.16) na UDP iliyopata wabunge watatu na mmoja wa viti maalum na kura 213,547 (asilimia 3.325).

Mwaka 1995 (Zanzibar)
Katika uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 1995, CCM ilishinda urais ambapo mgombea wake Dk Salmin Amour alitangazwa kupata kura 165, 271 (asilimia 50.2) dhidi ya kura 163,706 (asilimia 49.8) za mgombea wa CUF, Seif Sharif Hamad.

CUF haikutambua matokeo ya uchaguzi huo kwa kutoa ushahidi wake kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

Kwa upande wa uchaguzi wa Baraza la Uwakilishi la Zanzibar, kati ya majimbo 50 ya yaliyoshindaniwa, CCM ilitangazwa kushinda majimbo 26 na CUF majimbo 24. Hata hivyo, CUF haikuridhishwa na kukubaliana na matokeo ya uchaguzi huo kwa sababu haukuwa huru na wa haki.

Mwaka 2000, (Tanzania)
Katika uchaguzi wa urais wa serikali ya Muungano mwaka 2000 ambao ulikuwa na matatizo makubwa hasa Zanzibar, mgombea wa CUF wakati huo, Profesa Ibrahim Lipumba alipata kura 890,044 sawa na asilimia 12.54 akizidiwa na mgombea wa CCM, Benjamini Mkapa aliyepata kura 5,863,201 (asilimia 71.74).

Uchaguzi huo wa mwaka 2000 CUF ilipata wabunge 21 ambapo 15 walichaguliwa kwenye majimbo ya Zanzibar na wawili wakachaguliwa kwenye majimbo ya Tanzania Bara (Kigamboni na Bukoba Mjini) na wanne walikuwa viti maalumu. Kwa jumla CUF ilijikusanyia kura 890,044 sawa na asilimia 12.54 ya kura za ubunge nchi nzima.

Kura za ubunge za CUF zilizidiwa na kura za wabunge wa CCM – 4,628,127 (asilimia 65.19) lakini CUF ikapata kura nyingi za ubunge kuvishinda vyama vingine vitano; TLP wabunge wanne na kura za ubunge 652,504 (asilimia 9.19), UDP wabunge watatu na kura za ubunge 315,303 (asilimia 4.44), Chadema wabunge wanne na kura za ubunge 300,567 (asilimia 4.23) na NCCR walipata mbunge mmoja na kura za wabunge 256,591 (asilimia 3.61).

Mwaka 2000, (Zanzibar)
Kwa mara nyingine tena mwaka 2000, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikamtangaza Salmin Amour (CCM) kushinda urais wa Zanzibar kwa kura 165,271 dhidi ya kura 163,706 za Seif Sharif Hamad (CUF). CUF haikuridhishwa pia na matokeo ya uchaguzi huo.

Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, CCM ikatangazwa kushinda majimbo 26 na CUF Majimbo 24 (CUF ilishinda majimbo yote Pemba na manne Unguja).

Mwaka 2005, (Tanzania)
Kwenye uchaguzi wa urais wa Tanzania wa mwaka 2005, mgombea wa CUF wa wakati huo, Profesa Ibrahim Lipumba alipigiwa kura 1,327,125 (asilimia 11.68) akizidiwa na mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete aliyepata kura 9,123,952 (asilimia 80.28) huku CUF ikimpita mgombea wa Chadema, Freeman Mbowe aliyepata kura za urais 668,756 (asilimia 5.88).

Kwenye ubunge mwaka huo 2005, CUF ilipata wabunge 30 kwa ujumla, 19 wakiwa wabunge wa majimbo (wote kutoka Zanzibar na Bara haikupata) na wabunge 11 wa Viti Maalumu huku wabunge wote wa CUF wakipigiwa kura 1,551,243 (asilimia 14.3).

CCM ikapata wabunge 206 wakiwamo 58 wa viti maalumu pamoja na kura za ubunge 7,579,897 (asilimia 70.0), Chadema ikapata wabunge watano na sita wa viti maalumu pamoja na kura za ubunge 881,133 (asilimia 8.2), TLP ikapata mbunge mmoja wa kuchaguliwa na kura za ubunge 297,230 (asilimia 2.7), NCCR ilikosa mbunge hata mmoja na ikipata kura za ubunge 239,452 (asilimia 2.2) na UDP ikipata mbunge mmoja wa kuchaguliwa pamoja na kura za ubunge 155,887 (asilimia 1.4).

Mwaka 2005, (Zanzibar)
Katika uchaguzi wa mwaka 2005 wa urais wa Zanzibar, CCM ilitangazwa kuwa mshindi kwa Dk Amani Abeid Karume kupata kura 239,832 (asilimia 53.18) na mgombea wa CUF, Seif Sharif Hamad (CUF) akatangazwa kupata kura 2017,773 (asilimia 46.07).

Uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi kwa mwaka 2005 ulishuhudia CCM ikitangazwa kushinda majimbo 30 na CUF ikishinda majimbo 19 huku matokeo ya uchaguzi wa mwakilishi wa jimbo moja yakibatilishwa.

CUF iliyakataa matokeo ya uchaguzi wa Rais ya mwaka 2005, baadaye mwaka 2010, busara za Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad zikawapeka mezani na hatimaye wakajenga maridhiano ili kuifanya Zanzibar iweze kuongozwa na vyama viwili vyenye nguvu kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Chama kinachozongwa zaidi
Ndiyo, tangu kuanzishwa kwake, CUF kimekuwa kinapitia kwenye matatizo mengi ambayo sitayaeleza kupitia katika makala hii, lakini inatosha kusema kuwa, tangu kuanzishwa kwake miaka 26 iliyopita, CUF imekuwa mhimili imara wa mageuzi nchini Tanzania ikishajihishwa na uimara na uwezo wake mkubwa kitaasisi kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Tunaweza kujifunza pia, CUF ni mshirika mkubwa wa siasa za Zanzibar, hakuna namna ambapo unaweza kuitaja Zanzibar na usiitaje CUF, na hata hali tete iliyomo Zanzibar kisiasa hivi sasa, ni kwa sababu hakukuwa na maelewano katika uchaguzi wa mwaka 2015 na ni jambo sahihi kuwa tangu mwaka 1992 CCM imekuwa hailali kwa sababu kipo chama kinaitwa CUF.

Katika kusherehekea miaka 26 tangu kuundwa kwake ni muhimu tukajikumbusha historia hizi. Jumapili ijayo nitamalizia sehemu ya pili ya makala haya.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com)

Share: